UTANGULIZI
Ndugu zangu popote
Tanzania na nje ya Tanzania. Nawapa salamu za upendo na furaha kubwa.
Tarehe 7 September,
2017, ni siku iliyobadilisha maisha yangu na, pengine, maisha yetu kama jamii
ya Watanzania.
Majira ya saa saba
mchana wa siku hiyo, nilitoka kwenye maeneo ya Bunge mjini Dodoma, nilikokuwa
nahudhuria vikao vya Bunge, na kuelekea nyumbani kwangu kwenye Eneo D la mji wa
Dodoma, kwa ajili ya kupata chakula cha mchana.
Bila mimi kujua, gari
yangu ilifuatiliwa kwa nyuma na gari iliyokuwa na vioo vyeusi hadi ndani ya
eneo la nyumba za viongozi wa umma. Eneo hili limezungushiwa ukuta na nyaya za
miba (barbed wire) na hulindwa na walinzi wenye silaha usiku na mchana.
Na nje ya kila jengo
pia, kuna ulinzi usiku na mchana. Mchana wa siku hiyo, walinzi wote, wa geti
kuu la kuingilia na wa katika kila jengo, hawakuwepo kabisa.
Nje ya jengo
ninamoishi, watu wawili wanaume walishuka wakiwa na bunduki za kijeshi na
ghafla waliishambulia gari yangu kwa risasi nyingi. Dereva wangu alifanikiwa
kuruka nje na kujificha chini ya magari yaliyokuwa jirani.
Mimi sikuweza
kuwatoroka. Kwa sekunde chache nilipigwa risasi 16 katika sehemu mbali mbali
miguu, kiuno na mikono.
Nilipigwa risasi mbili
kwenye paja la kushoto zilizotoka nje upande wa pili. Nilipigwa risasi tatu juu
kidogo ya kiuno upande wa kushoto zilizopita chini kidogo ya ngozi. Hizi
hazikusababisha majeraha makubwa.
Nilipigwa risasi mbili
mkono wa kushoto chini ya kiwiko na kwenye kiwiko chenyewe; na risasi moja
kwenye mkono wa kulia chini ya kiwiko. Mikono yote miwili ilivunjika.
Kwa upande wa kulia,
nilipigwa risasi moja kwenye mfupa wa juu ya goti la kulia ambayo iliuvunja
mfupa huo vipande vipande. Risasi nyingine ilivunja mfupa wa nyonga.
Baadae hospitalini
Dodoma na Nairobi, madaktari walifanikiwa kutoa risasi sita tumboni na moja
kwenye kiwiko cha mkono wa kushoto. Risasi moja imebaki chini ya uti wa mgongo
juu kidogo ya kiuno.
Majeraha yaliyotokana
na risasi hizo yalikuwa makubwa na ya hatari. Kwa mujibu wa Dr. Vincent
Mutisso, aliyeongoza jopo la madaktari bingwa wa Nairobi Hospital nchini Kenya
walionitibu baada ya kusafirishwa Nairobi kwa ndege ya dharura, nilipoteza
sehemu kubwa ya nyama (blocks of muscle) katika sehemu zilizopigwa.
Aidha, nilipoteza mara
tatu ya ujazo wa kawaida wa damu yangu, kwa maana kwamba niliongezewa damu tatu
ya ujazo wa kawaida wa damu yangu.
Hadi hapa nilipo,
nimekwifanyiwa jumla ya operesheni 21, Nairobi Hospital operesheni 17, na
Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg, hapa Ubelgiji operesheni 4.
Tumboni na kwenye mguu wa kulia pekee, nimefanyiwa operesheni 14.
Hata hivyo, kama
wasemavyo Waswahili, Mungu sio Athumani. Na kama mwanaharakati wa Kenya, Koigi
wa Wamwere, alivyosema kwenye kitabu chake 'I Refuse to Die', na mimi pia
'nilikataa kufa.' Mwenyezi Mungu hakuruhusu mipango ya wauaji na wale
waliowatuma kufanikiwa.
Leo ni mwaka mmoja
kamili tangu niumizwe kiasi kile, na nimeweza kusimama kwa miguu yangu tena,
hata kama ni kwa msaada wa magongo.
Majeraha ya sehemu
zote za mwili, isipokuwa mguu wa kulia, yamepona. Na madaktari wangu
wamesema mguu wa kulia nao utapona, na nitarudi Tanzania tofauti na
nilivyoondoka: nikiwa natembea mwenyewe bila msaada wa mtu mwingine au kifaa.
Safari bado ni ndefu kiasi, lakini mwisho wake sasa unaonekana.
Lakini mwaka huu mmoja
umeshuhudia mjadala mkubwa, ndani na nje ya Bunge, juu ya mazingira ya
shambulio hilo. Kumekuwa na mvutano na mabishano makubwa baina ya watu na
taasisi mbali mbali. Leo ni muda muafaka kuyatolea ufafanuzi baadhi ya masuala
haya.
Nilitakiwa kufa kwa
sababu ya msimamo wangu wa kisiasa, hasa kwa kumpinga Rais Magufuli na kumkosoa
hadharani tangu aingie madarakani.
Mapema kabisa katika
utawala wake, wakati kila mtu anampigia vigelegele, mimi nilimsema, ndani na
nje ya Bunge, kwamba ataiingiza nchi yetu kwenye janga kubwa la ukiukaji wa
haki za binadamu.
Nilipinga kauli zake
tata kuhusu tetemeko la ardhi Mkoa wa Kagera na kuhusu tatizo la njaa mahali pengi
nchini.
Nilikemea tabia yake
ya kubeza na kudhalilisha majaji wetu na kutisha wanasheria na mawakili wa
kujitegemea.
Nilipinga vikali
vitendo vyake vya kukamata mali za wawekezaji wa kigeni bila kujali sheria
zetu, mahusiano yetu ya kiuchumi na jamii ya kimataifa na hatari ya kushtakiwa
katika Mahakama za kimataifa na kuingizwa hasara kubwa zaidi.
Nilipinga vikali
ukiukaji wa haki za binadamu uliokithiri chini ya utawala wake, sio tu kwa
kupiga kelele lakini pia kwa kutoa msaada wa uwakilishi mahakamani kwa wale
waliokamatwa na kushtakiwa kwa sababu ya kukosoa serikali yake na vyombo
vyake.
Serikali ya Magufuli
ilipoanza kuingilia masuala ya uendeshaji wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika
(TLS) kwa kuingilia uchaguzi wa viongozi wake, nilisimama kidete na
nikachaguliwa kwa kura nyingi kuwa Rais wa TLS.
Nilikuwa wa kwanza
kutoa taarifa juu ya kukamatwa nchini Canada kwa ndege ya Bombardier
iliyonunuliwa na Serikali yake kwa ajili ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania
(ATCL), baada ya Magufuli kuvunja mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo na
kusababishwa Serikali kushtakiwa na kushindwa kesi katika Mahakama ya Kimataifa
ya Usuluhishi.
Kwa sababu ya msimamo
wangu kwenye masuala haya, nilianza kutiwa misukosuko mingi. Magufuli
hakumaliza hata mwaka mmoja nilianza kusakamwa na Jeshi la Polisi na Idara ya
Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS).
Ndani ya takriban
mwaka mmoja, nilikamatwa mara nane na kufunguliwa kesi za jinai sita
mahakamani. Walifikiri watanitisha na kuninyamazisha kwa manyanyaso ya mapolisi
na tishio la magereza.
Walipogundua hayo
hayanitishi, wakaamua kuninyamazisha milele kwa risasi za bunduki za
Kalashnikov. Mungu sio Athumani. Na hilo halikufanikiwa.
Walichofanikiwa ni
kunivunja vunja viungo vya mwili wangu. Moyo wangu haujavunjika. Nafsi yangu
iko vile vile. Na msimamo wangu haujatetereka.
Ernest Hemingway,
Mwanafasihi wa Kimarekani na Mshindi wa Tuzo ya Fasihi ya Nobel, aliandika -
katika fasihi yake ya 'The Old Man and the Sea' - kwamba 'mtu anaweza kuuawa
lakini asishindwe.'
'Kushindwa' kwa maana
ya Hemingway ni kukata tamaa, na kubadili msimamo, na kukubali kumtumikia
kafiri ili upate mradi wako. Nimeumizwa vibaya kimwili, lakini bado niko imara
kichwani na moyoni. Sijashindwa.
KUHUSU BUNGE NA
MATIBABU YANGU
Kumekuwa na mvutano
mkubwa kati ya familia yangu na uongozi wa Bunge chini ya Spika Ndugai na
Katibu wa sasa wa Bunge, Steven Kagaigai. Mvutano huu unahusu utaratibu wa
kulipia gharama zote za matibabu yangu.
Huu ni mgogoro wa
kutengenezwa na ni aibu kubwa kwa Bunge kama taasisi na kwa Spika Ndugai kama
kiongozi wake.
Msimamo wa uongozi wa
Bunge chini ya Spika Ndugai na Katibu Kagaigai ni kwamba Bunge haliwajibiki
kulipa gharama za matibabu yangu kwa sababu nilikiuka au viongozi wa chama
changu bungeni walikiuka taratibu za matibabu ya Wabunge kwa kulazimisha
nipelekwe Nairobi badala ya kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
kwanza.
Kufuatana na maelezo
ya Spika Ndugai, Hospitali ya Muhimbili ilitakiwa kutoa mapendekezo ya mimi
kupelekwa nje kutibiwa kwa Katibu wa Wizara ya Afya ambaye naye angeunda jopo
la madaktari watatu kuchunguza mapendekezo ya Muhimbili.
Endapo mapendekezo ya
Muhimbili yatakubalika, basi jopo la madaktari litamshauri Katibu Mkuu ambaye
akiridhika, itabidi Bunge liombe idhini kwa Rais Magufuli ambaye naye
akiridhika basi pesa ya matibabu itatolewa.
Tatizo liko wapi???
Kwanza, utaratibu huu hautambuliki kisheria. Sheria inayohusika na matibabu ya
Wabunge ni Sheria ya Uendeshaji wa Bunge, 2008. Sheria hiyo imesema kwa kifupi
kwamba kila Mbunge atakuwa na haki ya kutibiwa ndani au nje ya Tanzania kwa
gharama ya Bunge.
Utaratibu wa kupata
kibali cha Muhimbili, au cha Katibu Mkuu Afya, au cha Rais haupo kwenye Sheria
hiyo.
Pili, utaratibu
unaozungumzwa na Spika Ndugai na watu wake unaliweka Bunge, mhimili huru wa
dola na wenye bajeti yake inayojitegemea, chini ya mamlaka ya mhimili wa
Serikali, yaani Wizara ya Afya na Ikulu.
Hii inaingilia moja
kwa moja uhuru, hadhi na heshima ya Bunge na inakiuka kanuni kuu ya Katiba ya
mgawanyo wa madaraka.
Tatu, hata kama
utaratibu huo ungekuwepo kisheria, haukidhi na usingeweza kukidhi mahitaji ya
dharura iliyotokana na kushambuliwa kwangu.
Kwa majeraha
nikiyokuwa nayo na kwa hali ya kiusalama iliyokuwepo, hakukuwa na uhakika
kwamba nikipelekwa Muhimbili nitakuwa salama dhidi ya watu
walionishambulia.
Na hakukuwa na muda
mrefu wa kusubiri hali itulie ndio taratibu zinazosemwa zifuatwe. Ilibidi
uamuzi ufanywe haraka ili nikapatiwe matibabu katika hali ya dharura ya kiafya
na kiusalama iliyokuwepo.
Uamuzi wa kunipeleka
Nairobi Hospital haukuwa wa Mwenyekiti Mbowe peke yake, hata kama ni kweli
kwamba yeye ndiye aliyesisitiza umuhimu wa kwenda Nairobi Hospital badala ya
Muhimbili.
Baada ya kukimbizwa
Hospitaliya Mkoa wa Dodoma nikiwa nimejeruhiwa vibaya, kilifanyika kikao cha
viongozi wa CHADEMA, Bunge na Serikali kuhusu hatua za kuchukua.
Upande wa CHADEMA
uliongozwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mwenyekiti Mbowe na
wabunge kadhaa.
Upande wa Bunge
uliongozwa na Spika Ndugai, Naibu Spika Tulia na Katibu wa Bunge wakati huo,
Dr. Thomas Kashililah.
Kwa upande wa Serikali
alikuwepo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu wake Dr. Ulisubisya Mpoki na
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.
Kikao hicho ndicho
kilichoamua nipelekwe Nairobi. Ndio maana katika msafara ulionipeleka Nairobi
Hospital, alikuwepo pia Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Na ndio maana ndege
iliyonipeleka Nairobi iliruhusiwa kuruka Uwanja wa Ndege wa Dodoma saa sita
usiku.
Ningekuwa nimepelekwa Nairobi
kwa utaratibu binafsi, kama inavyodaiwa sasa, nisingesindikizwa na Mganga Mkuu
wa Mkoa na wala Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) isingeruhusu ndege kuondoka
Dodoma saa sita usiku.
Na wala maafisa wa
uhamiaji wasingegonga muhuri passport zetu na kuturuhusu kutoka nje ya
nchi.
Baada ya kuwa
nimeshapokelewa Nairobi Hospital na maisha yangu kuokolewa, Spika Ndugai na
Katibu wa Bunge Kashililah walikutana na ndugu zangu kwenye Ofisi ya Bunge Dar
na kuwashauri waandike barua rasmi ya maombi ili Bunge liweze kutoa fedha za
matibabu yangu.
Waziri wa Afya Ummy
Mwalimu naye alishauri hivyo hivyo, tena hadharani kwenye mkutano na wandishi
habari. Waziri Mwalimu alisisitiza jambo hilo kwa kutoa mfano wa Spika wa
zamani wa Bunge, marehemu Samuel Sitta, ambaye inasemekana aliomba msaada wa
kutibiwa na Bunge wakati hakuwa Mbunge tena, na tayari alikuwa hospitalini
London, Uingereza.
Barua zikaandikwa na
ndugu zangu kama walivyoelekezwa na uongozi wa Bunge. Lakini mara Katibu wa
Bunge Kashililah akaondolewa madarakani na Rais Magufuli, na Steve Kagaigai
akateuliwa kushika nafasi hiyo.
Inaelekea Steve
Kagaigai alikuja na maelekezo ya Rais Magufuli: Tundu Lissu asipewe pesa yoyote
ya matibabu na Bunge.
Spika Ndugai mwenyewe
amethibitisha hivyo, tena ndani ya Ukumbi wa Bunge. Spika Ndugai aliliambia
Bunge mwezi Juni kwamba sitatibiwa na Bunge kwa sababu Rais Magufuli hajatoa
idhini hiyo.
Hiyo ndiyo sababu ya
mvutano huu. Spika Ndugai amekubali kuingiliwa na kupokwa madaraka ya Bunge
kuendesha shughuli zake kama mhimili huru wa dola na mhimili mwingine,
Serikali.
Sasa Rais Magufuli
ndiye anayeamua nani atibiwe na nani asitibiwe na Bunge. Hii haijawahi kutokea
tangu Bunge letu lianzishwe wakati wa ukoloni!!! Kwa upande wetu, njia pekee
iliyobaki sasa ni kulipeleka suala hili mahakamani ili Mahakama Kuu itoe
tafsiri sahihi ya jambo hili. Maandalizi ya kwenda mahakamani
yanaendelea.
UCHUNGUZI WA POLISI
UMEISHIA WAPI???
Shambulio dhidi yangu
limethibitisha jinsi ambavyo Jeshi la Polisi la Tanzania linavyotumika
kutekeleza matakwa ya kisiasa ya walio madarakani.
Kwa vile
aliyeshambuliwa ni mbaya wa Serikali ya Magufuli, Jeshi la Polisi
halijahangaika na kufanya upelelezi wa kijinai wa kitendo hiki cha
kihalifu.
Hadi ninapoandika
haya, hakuna mtu yeyote anayeshukiwa kunishambulia. Hakuna yeyote
anayetuhumiwa. Hakuna yeyote aliyehojiwa na wapelelezi wa polisi kama shahidi.
Hata wahanga wa shambulio lenyewe, mimi na dereva wangu,
hatujahojiwa.
Lakini ndugu zangu na
viongozi wangu wa chama walisema tangu mwanzo: Jeshi la Polisi la Tanzania
haliwezi kuchunguza shambulio hili.
Linafahamu mpango
mzima. Linawafahamu 'watu wasiojulikana' na mtu aliyewatuma kuja kuniua.
Linawafahamu walioamuru walinzi wote wa majengo nilipokuwa naishi waondolewe
ili 'watu wasiojulikana' wafanye kazi yao ya mauaji bila ushahidi.
Linafahamu aliyeamuru
kamera ya CCTV iliyokuwepo kwenye jengo la makazi yangu iondolewe na wanafahamu
ilikofichwa hadi sasa, kama haijaharibiwa ili kupoteza ushahidi.
Marehemu Sipho
Sepamla, mshairi maarufu wa Soweto, aliandika shairi linaloitwa 'At the Dawn of
Another Day', yaani 'Mawio ya Siku Nyingine': 'Tungeweza kuuliza mashahidi,
lakini mashahidi wa nini kwa risasi zilizopigwa wakati jua linaangazia macho
kitendo chenyewe.'
JE, DEREVA WANGU AMEFICHWA
WAPI???
Kuna wajinga
wanaoelekea wametumwa na 'watu wasiojulikana' kueneza maneno ya kijinga kwamba
dereva wangu anafahamu siri za kushambuliwa kwangu. Kwamba alitoroshwa na sasa
amefichwa na CHADEMA na Mwenyekiti Mbowe, n.k.
Nimekuwa na dereva huyu
tangu mwaka 2002, akiwa kijana wa miaka 19. Katika miaka yote hii, amekuwa ni
sehemu ya familia yetu.
Ninamfahamu fika.
Ninafahamu alivyo mwaminifu kwangu. Hawezi na asingeweza kufahamu njama za
kuniua mimi halafu asiniambie.
Mara baada ya kushambuliwa
kwangu, 'watu wasiojulikana' walianzisha minong'ono ya chini chini kwamba
wakimpata dereva wangu basi 'wamemaliza maneno' juu ya kushambuliwa
kwangu.
Watu wetu waligundua
hatari kubwa aliyokuwamo dereva kutokana na minong'ono hiyo. Wakaamua kumtoa Tanzania
na kumleta Nairobi nilikokuwa nimelazwa mimi.
Hakutoroshwa.
Aliondoka na Mh. Godbless Lema na alipitia mpaka wa Namanga. Alipatiwa hati ya
muda ya kusafiria na maafisa wa uhamiaji Namanga.
Na wala hakufichwa
Nairobi. Alikaa na mimi Nairobi Hospital kwa miezi minne.
Jeshi la Polisi la
Tanzania lilimjulisha kaka yangu, wakili Alute Mughwai, kwamba litatuma
wapelelezi wake kuja Nairobi kutuhoji mimi na dereva wangu. Tuliwasubiri
mapolisi hao. Hawakuonekana mpaka wakati tunaondoka Kenya kuja Ubelgiji tarehe
6 Januari ya mwaka huu.
Dereva wangu
hakutoroka Kenya kuja Ubelgiji. Ili aweze kusafiri kutoka Kenya kuja Ubelgiji,
alihitaji passport ya Tanzania na visa ya Ubelgiji. Hakuwa navyo.
Hivyo, Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Serikali ya Ubelgiji ilimpatia hati maalum ya kusafiria na kuingia
Ubelgiji. Wakati mimi na mke wangu tulisafiri kwa passport za Tanzania; dereva
wangu alisafiri kwa passport maalum ya Serikali ya Ubelgiji.
Hapa Ubelgiji anaishi
mji mmoja na mimi. Amekodishiwa nyumba na anaishi kwa gharama za Serikali ya
Ubelgiji, sio za CHADEMA au Mwenyekiti Mbowe au za kwangu mwenyewe. Anasomeshwa
na Serikali ya Ubelgiji.
Bado anaweza kuhojiwa
na wapelelezi kuhusiana na jaribio la mauaji dhidi yangu. Utaratibu wa kufanya
hivyo upo kisheria, kwa mujibu wa Sheria ya Kusaidiana Katika Masuala ya Jinai
iliyotungwa na Bunge la Tanzania.
Lakini Jeshi la Polisi
la Tanzania halitaki kufanya hivyo. Linafahamu mpango mzima wa 'watu
wasiojulikana.'
Huu ujinga
unaosambazwa na vijigazeti vya Jamvi la Habari na Tanzanite ni kazi ya 'watu
wasiojulikana' wanaofamika vyema. Ni aibu kubwa kwa nchi yetu, kwa Jeshi la
Polisi na kwa Serikali ya Magufuli.
HITIMISHO
Naomba nimalizie
ujumbe huu mrefu. Nataka niwe muwazi. Huu mwaka mmoja umekuwa mrefu na mgumu
sana kwangu sio kwa sababu ya majeraha ya mwili. Ni kwamba pia nimei-miss sana
Tanzania na nimewa-miss Watanzania.
Nime-miss sana Bunge,
licha ya matatizo yote ya Bunge la Spika Ndugai. Nimewa-miss sana watu wangu wa
Jimbo la Singida Mashariki na mikutano yetu ya hadhara.
Nime-miss sana kazi
zangu za chama na nimewa-miss viongozi wenzangu, wanachama wetu na wafuasi wetu
katika mamilioni yao.
Nime-miss sana
mapambano ya utetezi wa haki za watu wetu ndani na nje ya Mahakama.
Nimewa-miss mawakili
wa Tanzania Bara walionipa heshima ya kuwaongoza katika kipindi kigumu sana
katika historia ya TLS.
Mshairi Sipho Sepamla
aliandika shairi lingine liitwalo 'The Exile', yaani 'Uhamishoni.' Shairi hilo
linaelezea machungu ya kuishi uhamishoni kwa kulazimishwa wakati wa utawala wa
kibaguzi wa makaburu wa Afrika Kusini.
Katika huu mwaka mmoja
wa kulazimishwa kuwa nje ya nchi; wa kutokuonana moja kwa moja na watu wetu,
familia, ndugu, jamaa, majirani na marafiki zangu; wa kufuatilia mapambano ya
kudai haki na demokrasia mitandaoni badala ya kuwa mshiriki kwenye uwanja wa
mapambano, sasa ninaelewa maana hasa ya kuwa 'uhamishoni.'
Baada ya
kushindwa na Wajapan kwenye Mapigano ya Bataan nchini Ufilipino mwaka 1942
wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kamanda wa majeshi ya Marekani katika
Bahari ya Pacific ya Magharibi, Jenerali Douglas MacArthur, alitamka: 'I Shall
Return.' 'Nitarudi.'
Na mimi nawatamkia
Watanzania: 'Nitarudi!!!'
No comments:
Post a Comment