BARUA YA WAZI YA TUNDU
LISSU KWA RAIS
Mheshimiwa John Pombe
Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
Ikulu, Dar Es
Salaam
Agosti 30, 2018
UTANGULIZI
Mheshimiwa Rais,
Nakusalimu kutoka
Leuven, Ubelgiji ninakoendelea na matibabu. Naomba pia upokee salamu zangu za
rambi rambi na pole kwako wewe binafsi, mama yako mzazi, ndugu, jamaa, marafiki
na majirani zenu wa Chato, kwa kufiwa na mpendwa dada yako hivi karibuni.
Mheshimiwa Rais,
Nimewiwa kukuandikia
barua hii ya wazi baada ya kusikiliza kipande cha hotuba yako ya leo tarehe 30
Agosti, 2018, wakati ukizungumza na viongozi wa ngazi mbali mbali wa Wilaya
yako ya Chato, Mkoa wa Geita. Aidha, nimepitia taarifa rasmi kuhusu hotuba yako
iliyotolewa na Mkurugenzi wako wa Mawasiliano, Gerson Msigwa
Ni barua ya wazi kwa
sababu masuala uliyoyazungumzia kwenye hotuba yako, na nitakayoyajadili hapa,
ni masuala yenye umuhimu mkubwa kwa umma wa Watanzania, hasa katika kipindi
hiki katika historia ya nchi yetu. Kwa umuhimu wake, na kwa njia uliyoitumia
kuyazungumza, haya ni masuala ya umma yasiyohitaji kufungwa kwa viapo vya siri
vya Ikulu.
Mheshimiwa Rais,
Umezungumza vizuri
sana, na kwa upole ambao wengi wetu hatujauzoea kutoka kwako. Kwa mujibu wa
taarifa ya maandishi ya Mkurugenzi wako wa Mawasiliano, umewataka viongozi wote
nchini kutekeleza majukumu yao "kwa kuzingatia sheria sambamba na
kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya
wananchi."
Kwa kifupi, Mheshimiwa
Rais, umezungumzia umuhimu wa viongozi wote kuheshimu Katiba na Sheria za nchi
yetu katika utekelezaji wa mamlaka yao ya umma. Hiki ndicho kinachoitwa, kwa
lugha ya kitaalamu, Utawala wa Sheria. Yaani kila mtu, bila kujali cheo, nasaba
au nafasi yake ya kiuchumi au kijamii, anapaswa kuheshimu Katiba na Sheria za
nchi.
Mheshimiwa Rais,
Ijapokuwa imekuchukua
karibu miaka mitatu kutambua umuhimu wa Utawala wa Sheria kwa nchi yetu, hasa
kwa "viongozi wote", kwenye suala hili mimi ninakuunga mkono.
Sina shaka, Mheshimiwa
Rais, kwamba kwa matendo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam ambayo leo
umelazimika kuyakiri hadharani, umeanza kutambua hatari ya viongozi wetu wa
umma kuendesha shughuli za umma kwa amri, matamko na utashi wao binafsi, badala
ya kuongozwa na utashi wa Katiba na Sheria za nchi yetu.
Kwa uzoefu wetu
wenyewe wa miaka mingi kama Taifa, viongozi wa aina hii huwa hawachelei kugeuza
ofisi na dhamana zao za umma kuwa 'pango la walanguzi', kwa kauli maarufu ya
Baba wa Taifa.
Aidha, kwa uzoefu wetu
huo, viongozi wa aina hii hutumia mamlaka yao hayo kuonea wananchi, kuwadhulumu
haki zao na kuwanyanyasa ama kudhalilisha utu wao. Haya yote, Mheshimiwa Rais,
tumeyashuhudia sana katika awamu hii ya utawala wa nchi yetu.
YA MKUU WA MKOA PAUL
MAKONDA
Mheshimiwa Rais,
Mkuu wa Mkoa wa Dar Es
Salaam ni kielelezo sahihi na cha wazi cha viongozi wasiozingatia, nay
wanaopuuza Utawala wa Sheria. Naomba na hili la makontena yaliyoko bandarini
ambalo umelizungumzia wewe mwenyewe.
Umesema kwamba kama
Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam anadaiwa kodi kutokana na yaliyomo kwenye
makontena yale basi ailipe kodi hiyo.
Lakini papo hapo,
Mheshimiwa Rais, umeibua maswali kadhaa. Je, kilichopo ndani ya makontena yale
ni madawati ya shule tu au kuna masofa ya kupelekwa kwenye shopping
malls!!!
Je, ni marafiki au watu
gani waliomtumia Mkuu wa Mkoa makontena yale!!!
Je, kama ni zawadi kwa
Mkuu wa Mkoa, kiongozi wa Serikali, kwa nini zawadi hizo kwa Serikali
hazijapelekwa Waziri wa Fedha ambaye, umetuelimisha, ndiye mwenye mamlaka
kisheria ya kupokea zawadi zote za Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Misaada,
Mikopo na Dhamana za Serikali ya mwaka 1974.
Mheshimiwa Rais,
Maswali uliyoyaibua
yanaonyesha dhahiri kwamba hata wewe mwenyewe huamini hii hadithi ya makontena
ya vifaa vya elimu kwa ajili ya shule za Dar Es Salaam.
Na kwa sababu wewe ni
Mkuu wa Nchi na Kiongozi Mkuu wa Serikali pia, sisi wananchi wako wa kawaida
hatuwezi kutilia shaka msingi wa mashaka yako juu ya makontena haya na mwenendo
wa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam kuhusiana nayo.
Ninachotaka kuelezea
ni kile ambacho wewe hujakisema kuhusiana na maswali uliyoyaibua juu ya Mkuu wa
Mkoa wa Dar Es Salaam.
Moja, kama ni kweli
kwamba makontena ya Makonda yana mizigo mingine ambayo hajaitangaza bandarini,
basi Mkuu huyo wa Mkoa atakuwa ametenda kosa la jinai la kutoa taarifa ya uongo
(false declaration) kwa mujibu wa Sheria mbali mbali za kodi za nchi
yetu.
Hilo ni kosa la jinai
pia kwa mujibu wa Sheria yetu kuu ya jinai, yaani Kanuni ya Adhabu, na kwa
Sheria yetu ya TAKUKURU.
Pili, kama Mkuu wa
Mkoa Makonda hajawataja hao marafiki au wafanya biashara anaodai wamempa zawadi
ya makontena hayo, hilo ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya TAKUKURU na
Sheria ya Mapato ya Udhalimu (Proceeds of Crime Act).
Tatu, kama Mkuu wa
Mkoa Makonda amepokea zawadi zinazodaiwa kuwa kwenye makontena kinyume na
Sheria ya Misaada, Mikopo na Dhamana za Serikali uliyoitaja wewe mwenyewe, basi
sio tu amekiuka masharti ya lazima ya Sheria hiyo. Atakuwa pia amekiuka
masharti ya lazima ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu zawadi kwa
viongozi wa umma.
Mheshimiwa Rais,
Kwa makosa yote haya,
haitoshelezi na haitatosheleza kwa Mkuu wa Mkoa Makonda kuambiwa alipe kodi
anayodaiwa tu halafu yaishe.
Kama wasi wasi wako ni
wa kweli, na hatuna sababu za kukukanusha juu ya hilo, basi Mkuu wa Mkoa wa Dar
Es Salaam ni mhalifu anayetakiwa kufukuzwa kazi mara moja, kuchunguzwa kijinai
na kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria kulingana na makosa yake.
Sisi raia wako wa
kawaida tunatarajia kwamba, kwa vile na wewe mwenyewe umeanza kutambua hatari
ya viongozi wa aina hii kwa maslahi ya umma, hutafumbia macho vitendo vya
kihalifu ambavyo inaelekea vimefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam.
Vinginevyo, Mheshimiwa
Rais, sisi wananchi wako wa kawaida tutakuwa na sababu halali ya kuamini hii
minong'ono tunayoisikia chini kwamba Mkuu wa Mkoa Makonda ana ubia mkubwa
katika Urais wako.
RAIS KAMA MFANO WA
UONGOZI
Mheshimiwa Rais,
Kama Rais, Mkuu wa
Nchi na Kiongozi Mkuu wa Serikali, wewe ni 'First Citizen' (Raia Nambari Moja),
kama Wamarekani wanavyopenda kusema. Kwa sababu hiyo, unatakiwa kuongoza kwa
kuonyesha mfano.
Kwa hoja ya kuzingatia
sheria uliyoizungumza kwenye hotuba yako, wewe mwenyewe ndiye unayetakiwa
kuonyesha mfano wa kuheshimu Utawala wa Sheria.
Viongozi wengine wote
hufuata kwanza mfano na msimamo unaowekwa na Kiongozi Mkuu wa Nchi. Kama Mkuu
wa Nchi anaendesha nchi kama mali yake binafsi na anaona wananchi wake kama
watwana wake wa kutii amri na maagizo yake bila mjadala, basi viongozi wote wa
chini yake nao wataendesha ofisi au idara zao kama mali zao binafsi, na
watawaona walio chini yao kama punda wa kubebea mizigo yao.
Nchi inayotawaliwa
namna hii haiwezi kuwa tofauti na Zaire ya Mobutu Sese Seko, na haiwezi
kuchukua muda mrefu bila kuingia kwenye machafuko na hata kuparaganyika.
GHARAMA ZA
KUTOZINGATIA SHERIA
Mheshimiwa Rais,
Madhara ya viongozi
wetu wa umma kutokuzingatia Utawala wa Sheria yamekuwa, na yanaendelea kuwa, na
gharama kubwa kwa nchi yetu. Ni wiki hii tu, kwa mfano, tumepata taarifa ya
Serikali ya Tanzania, kupitia Shirika letu la Ugavi wa Umeme (TANESCO),
kushindwa kesi katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya
Uwekezaji (ICSID).
Sasa, kwa sababu ya
kushindwa kesi hiyo, Serikali yako inatakiwa kuilipa Standard Chartered Bank
Hong Kong, dola za Marekani milioni 170 au takriban shilingi za Tanzania
bilioni 425.
Na wala sihitaji
kukukumbusha madhara ya kupuuza kulipa deni hili jipya na kwa wakati muafaka.
Serikali yako isipolipa deni hilo sio tu kwamba litaongezeka kwa sababu ya riba
na faini nyinginezo, bali pia mali za Serikali yako zitakuwa halali kukamatwa
popote zitakapokutwa nje ya nchi yetu.
Yaliyotokea Canada kwa
Bombardier yetu mwaka jana, yanaweza kutokea tena kwa Dreamliner ya sasa endapo
itafanya safari nje ya Tanzania, na jitihada zako za kufufua ATCL zitakuwa ni
kazi ya bure.
Mheshimiwa Rais,
Hasara hii kwa Taifa
letu ilikuwa inajulikana na tungeweza kuiepuka, kama viongozi wetu wa Serikali
ya Awamu ya Nne wasingekula njama za kuiba na kulipana zaidi ya shilingi
bilioni 309, zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki
Kuu ya Tanzania.
Mimi mwenyewe, na
Wabunge wengine, tulitoa tahadhari bungeni Dodoma kwamba Serikali na TANESCO
ilikuwa inakabiliwa na kesi ICSID kuhusu fedha hizo za Tegeta Escrow Account,
na kwamba tukishindwa kesi hiyo tutatakiwa kuzilipa kwa wanaotudai. Tulijibiwa
kwa kejeli na viongozi wa serikali kwamba sisi ni nchi huru na hatuwezi kuogopa
kushtakiwa na taasisi au mtu yeyote. Matokeo ya kiburi hicho ndio haya ambayo
yametokea wiki hii.
Katika suala hili, na
kama sehemu ya utekelezaji wa kauli yako ya leo, tunatarajia, Mheshimiwa Rais,
kwamba utaelekeza kuwa faili la Kesi ya Tegeta Escrow Account liangaliwe upya
na mamlaka zenye wajibu huo, ili wale wote waliohusika kuliingizia Taifa letu
hasara hii wachukuliwe hatua stahiki za kijinai.
Haiwezekani, na
itakuwa ni doa kubwa kwako na kwa Serikali yako, kwamba watu pekee ambao
wamechukuliwa hatua kutokana na 'kuchotwa' kwa mabilioni ya Tegeta Escrow
Account hadi sasa ni Mzee James Rugemalila na Harbinder Singh Sethi peke
yao.
Viongozi wa umma wa
ngazi zote walioruhusu pesa hizo kutolewa Benki Kuu, au 'waliochotewa'
mabilioni hayo, wameepukaje mkono mrefu wa sheria??? Tafadhali tuonyeshe kwa
vitendo sisi wananchi wako kwamba kauli yako ya leo sio maneno ya bure.
HAKI ZA VYAMA VYA
SIASA
Mheshimiwa Rais,
Kwa vile sasa
umetambua umuhimu wa viongozi wote kuheshimu Utawala wa Sheria, sisi raia wako
wa kawaida tunatarajia kwamba utatembelea kwenye utambuzi huu kwa kutengua
makatazo yako kwa vyama vya siasa vya upinzani kuendesha shughuli zao kwa
mujibu wa Katiba na Sheria na Kanuni husika.
Katiba yetu inatamka
wazi kwamba "Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia... yenye kufuata
mfumo wa vyama vingi vya siasa."
Aidha, "mambo
yote yahusuyo uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini yatasimamiwa
kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa
ajili hiyo."
Kwa kuzingatia
masharti haya ya Katiba, Bunge lilitunga Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka
1992. Sheria hiyo imevipa vyama vya siasa haki ya kufanya mikutano ya hadhara
na maandamano, baada ya kutoa taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya
(OCD).
Na, kwa mujibu wa
Sheria hiyo, ni OCD peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuratibu na kudhibiti
mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa na wafuasi wao.
Aidha, Sheria hiyo
imeweka utaratibu na masharti ya vyama vya siasa kupatiwa ruzuku kutoka kwa
Serikali ili kuendeshea shughuli zao za kisiasa, ikiwapo mikutano ya hadhara na
maandamano.
Sasa, Mheshimiwa Rais,
ni karibu mwaka wa tatu tangu upige marufuku mikutano halali ya vyama vya
siasa. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, mamlaka yako kama Rais
yanaishia kwenye kuteua Msajili wa Vyama vya Siasa.
Huna mamlaka yoyote
juu ya uendeshaji wa vyama vya siasa kama vile kufanya mikutano ya hadhara na
maandamano. Umepoka mamlaka ya kisheria ya maOCD wakati wewe sio OCD.
Sasa kwa vile
umetambua makosa ya kutozingatia sheria zetu, tunatarajia utatengua na kufuta
makatazo ya mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa vya
upinzani.
Kama ilivyowahi kusema
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mojawapo ya taarifa zake za
uchunguzi, sio haki na ni ukiukaji wa sheria za nchi na misingi ya utawala
bora, kwa Jeshi la Polisi kutumika kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya
vyama vya siasa vya upinzani wakati mikutano ya hadhara na maandamano ya CCM
hayazuiliwi.
HAKI ZA BINADAMU
Mheshimiwa Rais,
Tangu mwaka 1984,
Katiba yetu imeweka hifadhi ya Haki za Binadamu kama sehemu muhimu ya Katiba.
Sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba imefafanua haki na wajibu wetu kwa
kirefu.
Kwa takriban miaka
mitatu sasa, Serikali ya Awamu ya Tano imeleta janga kubwa sana la kukithiri
kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi yetu.
Kwa mfano, wakati
Katiba inapiga "... marufuku mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa
adhabu ya kumtweza au kumdhalilisha", Watanzania wengi wameteswa,
kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu za kuwatweza au kuwadhalilisha katika vituo
vya polisi au sehemu nyingine za kutesea watu.
Wengi wameumizwa
vibaya kimwili na kisaikolojia, wengine wamepata vilema vya maisha. Mambo haya
yamefanywa na vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo wewe ndiye Amiri Jeshi Mkuu
wake.
Wakati Katiba imeweka
haki ya kila mtu "kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha
yake...", watu wengi wameuawa na vyombo vya ulinzi na usalama na makundi
ya wahalifu wanaoelekea kupata ulinzi wa vyombo vya dola.
Alfons Mawazo
aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita hayuko peke yake; wala aliyekuwa
diwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero; au Katibu wa
CHADEMA Kata ya Hananasif, Dar Es Salaam, au mwanafunzi Aquilina Aquiline wa
Chuo cha Usafirishaji Dar Es Salaam.
Wapo pia mamia ya
wananchi wa maeneo mbali mbali ya Wilaya za Mkuranga, Kibiti, Rufiji na Kilwa,
ambao wanadaiwa kukamatwa kwenye makazi, mashamba au hata nyumba za ibada na
kupotezwa na vyombo vya dola, na baadae miili yao kuokotwa kwenye fukwe za bahari
au ikielea kwenye Mto Rufiji.
Wakosoaji wa Serikali
yako nao wamekiona cha mtema kuni, kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere. Sio
Ben Saanane wa CHADEMA au mwandishi Azori Gwanda tu ambao wamepotea kwa zaidi
ya mwaka sasa.
Ni pamoja na Roma
Mkatoliki aliyeponea chupu chupu baada ya Watanzania wengi kupiga kelele; na
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ambaye naye amepotezwa na vyombo
vya ulinzi na usalama.
Ni pamoja na mimi
mwenyewe ambaye wiki ijayo nitamaliza mwaka nikiwa kitandani, baada ya
kumiminiwa risasi 16 na wanaoitwa 'watu wasiojulikana', ndani ya eneo la nyumba
za viongozi wa umma linalolindwa muda wote.
Ninaamini unafahamu
kwamba siku ya tukio hilo walinzi wote waliondolewa kwenye maeneo hayo na 'watu
wasiojulikana' pia.
Mheshimiwa Rais,
Vitendo hivi vimeacha
wajane na watoto yatima wengi sana. Kilio cha wajane na yatima hawa; na cha
wazazi au ndugu, jamaa na majirani wa wote ambao wamepotezewa uhai wao, au
wamefanywa vilema wa maisha, ni kikubwa.
Wote hawa wanastahili kufutwa
machozi. Njia mojawapo bora ya kuwafuta machozi yao ni kuweka ukweli wote wa
mateso yao hadharani. Ukweli utatuweka huru, kama yanavyosema maandiko
matakatifu. Ninakushauri uunde Tume huru na thabiti ya kijaji (Judicial
Commission of Inquiry) kuchunguza matukio yote haya na kuweka ukweli wote
hadharani.
Njia nyingine bora ya
kufuta machozi ya wote ambao sasa wanalia, ni kuhakikisha kwamba vitendo vya
ukiukaji wa haki za binadamu vinakomeshwa kabisa; au endapo vitatokea,
kuhakikisha vinachunguzwa kwa ukamilifu na mamlaka huru za kiuchunguzi na
wahusika wanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
Ukimya wako mwenyewe
na wa Serikali yako kuhusu matukio haya umekuwa na kishindo kikubwa. Watu wengi
wanaamini, kwa halali kabisa, kwamba Serikali yako inahusika na mambo haya
mabaya. Ndio maana umekuwa kimya sana, na matukio haya hayachunguzwi wala
wahusika kujulikana na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria zetu.
Baada ya hotuba yako
ya leo, huu sasa ni muda muafaka kwa wewe kuchukua hatua stahiki na za wazi
wazi kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa kama ilivyoamriwa na Katiba.
HITIMISHO
Mheshimiwa Rais,
Mambo yanayohitaji
kufanyiwa kazi ili kurejesha Utawala wa Sheria katika nchi yetu ni mengi sana.
Niliyoyasema ni baadhi tu.
Kuheshimu Uhuru wa Mahakama
na wa wanasheria; kutokuingilia uhuru na uendeshaji bora wa shughuli za Bunge;
kuacha utamaduni wa sasa wa kuwarubuni wabunge, madiwani na viongozi wa vyama
vya siasa vya upinzani kwa kuwapa rushwa ya vyeo vya kiserikali ili wahame
vyama vyao; kurekebisha mfumo mzima wa kikatiba, kisheria na kiutendaji kuhusu
usimamizi wa chaguzi zetu, n.k., ni maeneo mengine yanayohitaji kufanyiwa kazi
ili kujenga Utawala wa Sheria na kuliepusha Taifa letu na hatari ya kuwa 'a
failed state.'
Yote haya, Mheshimiwa
Rais, yanahitaji uongozi wako. Ukiwa jasiri na kuyarekebisha historia
itakukumbuka na utasifiwa na sisi wote tuliopo sasa, pamoja na vizazi vyetu
vijavyo.
Ukiyanyamazia au
kuyaendeleza, kwa ukimya au kwa matendo yako, historia pia itakuhukumu vikali
na kukuweka katika kundi moja na watesi wengine wa Bara letu na wa kwingineko
duniani.
Uamuzi ni wa kwako.
Ninatarajia utachagua upande sahihi wa historia.
Nakutakia kila la
kheri.
Tundu AM Lissu, MB
Leuven, UBELGIJI
No comments:
Post a Comment