Monday, September 10, 2018

JESHI LA POLISI LIWAACHIE WENYEVITI WA VIJIJI WALIOKAMATWA ZIARA YA RAIS MAGUFULI, MKOANI MARA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

JESHI LA POLISI LIWAACHIE WENYEVITI WA VIJIJI WALIOKAMATWA ZIARA YA RAIS MAGUFULI, MKOANI MARA

Wenyeviti wawili wa Serikali za Vijiji, Jijini cha Natta, Kata ya Natta, Serengeti na Kijiji cha Kewanja, Kata ya Kemambo, Tarime Vijijini ambao wote wanatokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waliokamatwa wakati wa ziara ya Mhe. Rais John Magufuli mkoani Mara, wiki iliyopita, hadi sasa bado wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, kinyume cha sheria za nchi.

Mwenyekiti wa Kijjiji cha Natta, Mossi Magoto alikamatwa na jeshi hilo Septemba 6 mwaka huu kijijini hapo baada ya kutuhumiwa na Mwenyekiti wa CCM aliyepewa nafasi ya kuzungumza na Rais Dkt. Magufuli kwenye mkutano wake kijijini hapo.

Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, Mwenyekiti huyo wa CCM katika eneo hilo la Natta kwa maneno matupu, alimtuhumu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kijiji Ndugu Magotto kuwa anahusika na matumizi mabaya ya mamilioni ya pesa za kijiji hicho.

Katika hali isiyotarajiwa hapo hapo, bila kupewa haki ya kusikilizwa, ilitolewa amri mbele ya Rais Magufuli, ya kumkamata Mwenyekiti Magotto na kushikiliwa na Jeshi la Polisi tangu siku hiyo hadi sasa, ambapo hajapewa dhamana wala hajafikishwa mahakamani.

Siku iliyofuata, Septemba 7, mwaka huu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kijiji cha Kewanja, Mtanzania Omtima naye alikamatwa na hadi sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mara kwa amri iliyotolewa mbele ya Rais Magufuli, baada ya kutuhumiwa kuhusika na matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha.

Kama ilivyokuwa katika Kijiji cha Natta, vivyo hivyo katika Kijiji cha Kewanja, aliyetoa tuhuma alikuwa ni Mwenyekiti (mstaafu) wa CCM katika eneo hilo aliyepewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano wa Rais Magufuli uliofanyika kijijini hapo. Tangu akamatwe, amenyimwa haki yake ya dhamana wala hajafikishwa mahakamani. Ndugu Omtima amekuwa akiandamwa na Serikali ya CCM na jeshi hilo Tarime kwa miaka mingi sasa kutokana na misimamo yake thabiti dhidi ya Mgodi wa North Mara.

Tangu walipokamatwa, viongozi hao wamekuwa wakihamishwa kupelekwa maeneo tofauti tofauti kwa madai ya kufanyiwa mahojiano huku wakinyimwa haki ya kupata msaada wa kisheria kutoka kwa wanasheria wao.

Hadi taarifa hii inatolewa, ambapo muda wa kisheria kwa Jeshi la Polisi kumweka mtu yeyote chini ya ulinzi bila kumwachia kwa dhamana au kumfikisha mahakamani ukiwa umeisha (tangu Magoto na Omtima wakamatwe), na kwa kuzingatia uzoefu wa utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli, haijajulikana nini itakuwa hatima ya Wenyeviti hao na haki yao itaamriwa mikononi mwa Jeshi la Polisi au Waziri wa Mambo ya Ndani au Rais Magufuli mwenyewe kwa sababu amri hizo zilitolewa kwenye mikutano yake ya hadhara au itaamuriwa mahakamani.

Kupitia taarifa hii, tunazitaka mamlaka zinazohusika kutambua kuwa;

1. Viongozi hao wamekamatwa kwa tuhuma zilizotolewa kwenye mikutano ya hadhara ya Mheshimiwa Rais, kinyume cha sheria za nchi yetu, kwa sababu:

(a) Jeshi la Polisi halina mamlaka kumkamata mtu yeyote kwa sababu ya tuhuma iliyotolewa kwenye mkutano wa hadhara wa kisiasa, hata kama ni wa Rais. Kama kuna kosa, sheria zinaelekeza mlalamikaji apeleke malalamiko yake kwenye kituo cha Polisi kwa ajili ya hatua za kisheria;

(b) Hata kama kuna mazingira ya maagizo ya rais katika ukamatwaji wa viongozi hao, ieleweke kuwa bado ni ukiukwaji wa sheria vile vile. Kwa mujibu wa sheria zetu, Rais hawezi kumkamata mtu yeyote kwa kosa lolote isipokuwa kwa vitendo vinavyotishia usalama wa taifa, ambapo amepewa mamlaka hayo kwenye Sheria ya Kuweka Watu Kizuizini ya 1962.

2. Kutokana na ukiukwaji huo wa sheria wakati wa kuwakamata, viongozi hao wanatakiwa kuachiliwa huru bila masharti yoyote. Vinginevyo wanasheria wa chama watalazimika kuchukua hatua zaidi za kisheria kwa kufungua maombi ya *habeas corpus* Mahakama Kuu ili OCD wa Tarime au RPC wa Mara au IGP, waitwe na kujieleza mahakamani kwa nini wanawashikilia watu hao kinyume cha sheria.

Imetolewa leo Jumatatu, Septemba 10, 2018 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment