(1) Ni muhimu kutambua
kwamba kipindi tunachopitia hakijawahi kuwepo katika historia ya mfumo wa vyama
vingi vya siasa nchini na hata wakati wa chama kimoja.
(2) Hatujawahi kuwa
utawala wa kikatili wazi wazi kama huu. Hatujawahi kuwa na utawala usioheshimu
Katiba na Sheria za nchi yetu wazi wazi kama huu. Hatujawahi kuwa na utawala
unaokandamiza haki za binadamu na haki za kisiasa kama huu.
(3) Hatujawahi kuwa na
utawala uliojiapiza wazi wazi kuwa utaangamiza vyama vya upinzani kama huu.
Kutekeleza kiapo chake hicho, baadhi ya mbinu anazotumia Magufuli na watu wake
ni hizi:
(a) Kukandamiza
wapinzani thru mauaji, kuwapiga na kuwaumiza, kuwafunga kwa kesi za
kubambikiza;
(b) Kuwarubuni kwa
rushwa ya fedha au ya madaraka wale wote wanaoweza kurubuniwa;
(c) Kuwashindisha kwa
nguvu wagombea wa CCM katika chaguzi za marudio.
(4) Magufuli na watu
wake wanafanya yote haya kwa sababu wanajua kwamba upinzani dhidi ya CCM ni
mkubwa na una nguvu kuliko pengine tunavyojifahamu sisi wenyewe. Ya 2015
yamewatisha sana na hawako tayari kuyaona tena 2020. Ndio maana ya yote haya
yanayoendelea.
(5) Tufanyeje???
(a) Tuyaelewe
mazingira haya mapya ya kisiasa na sababu zake kama nilivyoelezea hapo juu;
(b) Tujielewe sisi
wenyewe. Chama chetu kimekuwa kikubwa sana na hivyo kimeingiza watu wa kila
aina:
(i) Wapo ambao
wameingia kwenye chama kwa sababu wanaamini katika haja ya kulikomboa taifa
letu na kujenga mfumo bora zaidi wa kikatiba na kiutawala. Hawa tutakuwa nao
katika milima na mabonde tutakayopitia kwenye safari ya ukombozi;
(ii) Wapo walioingia
ili kupata madaraka ya udiwani au ubunge au Urais au mengineyo. Wamegundua
kwamba maisha ya upinzani ni magumu na ya hatari sana. Hawa sio wetu na
hatutaweza kuwazuia kununuliwa au kuondoka kwa hiari yao wenyewe.
(iii) Wapo walioingia
kwa sababu halali kabisa lakini kwa imani kwamba safari ya ukombozi itakuwa
fupi na rahisi. Wamegundua katikati ya safari kwamba njia ya ukombozi ni ndefu
na imejaa miba na mawe na kila aina ya ugumu.
Wapo watakaokimbia sio
kwa sababu wamehongwa, bali kwa sababu ya ugumu wa safari. Na wapo watakaobaki
na kuendelea na mapambano.
(iv) Wapo walioingia
kwa sababu hawaoni njia nyingine yoyote ya kujikwamua na mfumo tawala uliopo.
Hawa ni wetu vile vile through thick and thin, lakini tuhakikishe hawakatishwi
tamaa na haya yanayoendelea.
(v) Wapo
waliopandikizwa ili watuhujumu kwa ndani. Hawa nao sio wetu na hatuwezi
kuwazuia kujiondoa au kununuliwa.
Tunachohitaji kufanya
ni kuweka utaratibu bora zaidi wa kuchuja kila anayeingia kwenye chama chetu;
na hasa kila anayetaka au anayepewa dhamana ya uongozi wa chama wa nafasi za
kiserikali kama madiwani na wabunge.
(c) Tuhakikishe chama
chetu kinaendelea kuwa salama. Tusije tukafanya jambo lolote litakalompa
Magufuli na watu wake sababu ya kukipiga marufuku chama chetu.
Hii haina maana
tusiendelee kupigania haki na demokrasia katika nchi yetu. Ina maana tu kwamba
tusifanye yale ambayo Sheria na Katiba ya nchi kwa sasa imeyakataza.
Tufanye yale ambayo
Sheria na Katiba zimeyaruhusu na ni mengi. Matope ya kukiuka Katiba na Sheria
za nchi yetu yabakie kwa Magufuli na watu wake, yasihamishiwe kwetu.
(d) Tuwalinde viongozi
na wanachama wetu dhidi ya maonevu wanayofanyiwa. Tuweke utaratibu wa kuwatetea
wanapokamatwa na wanapofunguliwa mashtaka ya uongo. Utaratibu huu uwe wa nchi
nzima na tuache kutegemea kila kitu kifanywe na Makao Makuu ya chama.
(e) Tuendelee
kujitolea kufanya kazi za chama. Hatuna mjomba au shangazi wa kututatulia
matatizo yetu bali sisi wenyewe. Tuache kunyoosha vidole vya lawama kwa
viongozi wakati sisi wenyewe hatutimizi wajibu wetu.
(f) Tujifunze kuwa na
nidhamu ndani na nje ya Chama. Tuna migogoro mingi ya bure kabisa; tuna vichuki
na vijiwivu visivyokuwa na msingi. Tuna vitabia vibaya vya kufikiria kwamba
kila kitu lazima kitolewe nje hadharani na kujadiliwa as if hakuna taratibu za
kichama za kuyajadili na kuyatatua. Lazima tuwe na nidhamu.
(g) Tuache visingizio
na tufanye kazi za chama kwa bidii na maarifa. Kuna mengi ambayo yanatufanya
tushindwe chaguzi kwa sababu zetu wenyewe. Haya tuyatambue na kuyarekebisha,
kabla hatujakabiliana na ya Magufuli na watu wake na ya kimfumo.
Mwisho, Magufuli na
watu wake wanajua hawana jawabu la matatizo ya kimsingi ya nchi yetu na ya watu
wetu.
Wanataka kutuharibu
ili kusiwe na sauti mbadala itakayowaambia wananchi kwamba Magufuli
ameshindwa.
Tutambue kwamba vita
dhidi ya CHADEMA na vyama vya upinzani ni sehemu tu ya vita kubwa dhidi ya
Watanzania.
CHADEMA iko mstari wa
mbele wa vita hii. Tukishindwa sisi hakuna mwingine atakayeweza kusimama na
kupigana na utawala huu.
Tuna wajibu mkubwa
sana.
No comments:
Post a Comment