Thursday, August 16, 2018

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU ZIARA YA KAMPENI YA MKUU WA WILAYA YA ILALA JIMBONI UKONGA KABLA YA MUDA WA KAMPENI

CHADEMA MKOA WA ILALA

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU ZIARA YA KAMPENI YA MKUU WA WILAYA YA ILALA JIMBONI UKONGA KABLA YA MUDA WA KAMPENI 

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Ilala tunamtaka Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Sophia Mjema asitishe mara moja ziara anayofanya hivi sasa katika kata mbalimbali za jimbo la Ukonga. Ziara hii ina kila dalili ya kuanza kufanyia kampeni Chama cha Mapinduzi (CCM) kabla ya muda wa kampeni kuelekea uchaguzi mdogo wa ubunge kwenye Jimbo hilo utakaofanyika tarehe 16 Septemba 2018.

Ratiba ya mchakato wa uchaguzi mdogo katika Jimbo la Ukonga imetolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambapo kampeni za vyama zimetangazwa kuanza tarehe 21 Agosti 2018 hadi 15 Septemba 2018.

Lakini wakati ratiba hizo zikiwa zimeshatolewa kama ilivyoonyeshwa, Mkuu wa Wilaya ya Ilala ameamua kupanga na kufanya ziara katika kata mbalimbali za jimbo la Ukonga ambapo, pamoja na mambo mengine, anafanya mikutano ya hadhara ya wananchi. Sisi CHADEMA tunaona wazi kwamba ziara hizi za Mkuu wa Wilaya zimepangwa kimkakati kwa ajili ya kufanya kampeni kwa ajili ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwani kwa kauli na aina ya maneno yanayotolewa na Mkuu huyo wa Wilaya na watendaji wengine wa Serikali na CCM wanaoongozana naye kwenye ziara hizo ni wazi Mkuu wa Wilaya anafanyia CCM kampeni katika Jimbo la Ukonga kabla ya tarehe ya kuanza kampeni kufika kinyume na kanuni na sheria za uchaguzi. Ushahidi mwingine wa dhahiri wa madai yetu haya ni kabrasha analozunguka nalo DC huyo lilioandikwa "KERO ZA WANANCHI WA UKONGA KUELEKEA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA UKONGA".

Aidha CHADEMA inaitaka Tume ya Uchaguzi imwagize Mkuu wa Wilaya ya Ilala asitishe mara moja ziara yake inayoendelea katika Jimbo la Ukonga lenye lengo la kufanya kampeni za CCM kabla ya muda wa kampeni uliowekwa na Tume.

Jeromin W. Olomi
KATIBU WA CHADEMA ILALA
16 Agosti 2018

No comments:

Post a Comment