Tuesday, August 14, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA KUHUSU DC ILALA KUMWEKA NDANI MASAA 48 DIWANI WA KITUNDA

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA KUHUSU DC ILALA KUMWEKA NDANI MASAA 48 DIWANI WA KITUNDA 

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinalaani na kukemea vikali vitendo vya wateule wa Rais John Magufuli kuendelea kukiuka sheria za nchi, kama alivyofanya Mkuu wa Wilaya ya Ilala dhidi ya Diwani wa Kata ya Kitunda, huku mamlaka yao ya uteuzi ikikaa kimya bila kuwachukulia hatua za kuwawajibisha.

Jana majira ya mchana wakati wakiwa kwenye kikao cha pamoja kwa ajili ya kukagua shughuli za maendeleo katika kata hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alitoa amri ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu ya polisi kwa masaa 48 Diwani wa Kata ya Kitunda, Nice Gisunte bila kosa lolote.

Mjema alifika katika kikao hicho akiwa ameambatana na wanachama wa CCM waliokuwa wamevalia sare za chama hicho, ambapo wakati akihutubia kikao hicho kilichohusu uzinduzi wa kisima cha maji, DC huyo alianza kwa kutoa salaam za CCM kisha akasema kisima hicho ni matokeo ya utendaji kazi wa mzuri CCM hivyo wanaCCM wanapaswa kujivunia kwa sababu ndiyo inayoongoza sehemu zote. Naye katika kutambua wajibu wake pia, Diwani Gisunte aliposimama alitoa salaam za CHADEMA kisha akawaeleza wananchi kuwa kisima hicho kimeanza kufanya kazi baada uchaguzi wa 2015 chini ya uongozi wa diwani (wa kata hiyo) na Meya (Manispaa ya Ilala) wa CHADEMA.

Baada ya Diwani Gisunte kushangiliwa na wananchi kwa maelezo yake hayo, ndipo inadaiwa DC Mjema aliamuru Gisunte akamatwe na kuwekwa ndani masaa 48.

Hadi tunapotoa taarifa hii Diwani Gisunte bado yuko mahabusu katika Kituo cha Polisi Stakishari, Wilaya ya Kipolisi ya Ukonga, ambapo jitihada za wanasheria wa chama kufika kituoni hapo jana jioni kumpatia msaada wa kisheria na kusaidia Jeshi la Polisi nalo lisifanye kosa kwa kutekeleza amri hiyo batili, hazikufanikwa.

Mbali na kulaani na kukemea vikali kitendo hicho, CHADEMA kinamtaka DC Mjema kutoa maelekezo mengine haraka ya kutengua amri yake batili ya kumweka ndani masaa 48 mwakilishi huyo wa wananchi ili Jeshi la Polisi Wilaya ya Ukonga limwachie diwani huyo aendelee na uhuru wake kama raia asiyekuwa na hatia pia akaendelee kutekeleza majukumu kwa wananchi wake. Vinginevyo mamlaka za juu ya DC zione hatari ya kunyamazia au kubariki amri hiyo inayokiuka misingi ya sheria na zichukue hatua ya kuibatilisha na kumwajibisha mkuu huyo wa wilaya.

Ikumbukwe kuwa mojawapo ya tahadhari iliyotolewa na Viongozi Wastaafu nchini dhidi ya utawala wa serikali ya awamu ya tano, walipoitwa na Rais Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam, ilikuwa ni kuhusu ukiukwaji wa sheria za nchi unaofanywa na wateule wa Rais, ambapo Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta alisisitiza kuwa kila juhudi inayofanywa na Serikali lazima izingatie sheria na kutenda haki, pia akaongeza kwa kuhoji uwepo wa amri zinazotolewa na ma-DC kinyume cha sheria.

Imetolewa leo Jumanne, Agosti 14, 2018 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment