Wednesday, August 8, 2018

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimebaini uwepo wa hila na njama za wazi katika uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika Jumapili, Agosti 12, mwaka huu, kwenye jimbo moja na kata 77, hali ambayo inahitaji hatua za haraka kabla uchaguzi huo haujazidi kuvurugwa na kuharibika.

Mathalani katika Jimbo la Buyungu, hadi leo Agosti 7, zikiwa zimebaki siku 4 kabla ya siku ya kupiga kura, Msimamizi wa Uchaguzi hajatangaza orodha ya majina ya watu anaokusudia kuwateua kuwa Wasimamizi na Wasimamizi Wasaizidi wa Vituo vya Kupigia Kura, kinyume na Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 (Sura ya 343), kifungu cha 56 na Maelekezo ya NEC Kifungu cha 10.1 (ii). Kitendo hicho kimevinyima haki vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo kuweka pingamizi kwa wanaokusudiwa kuteuliwa siku 4 tangu kutangazwa kwa orodha hiyo.

Aidha, zikiwa zimebaki siku 4 kabla ya siku ya kupiga kura, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Buyungu hajatangaza orodha ya wapiga kura vituoni, kinyume na Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 (Sura 343) kifungu cha 47(i) (c) ambayo inaagiza majina hayo yanapaswa kubandikwa siku 8 kabla ya siku ya kupiga kura ili wananchi wapate rusa ya kuhakiki majina na vituo vyao.

Kama hiyo haitoshi, CHADEMA imebaini kuwa msimamizi huyo wa uchaguzi hadi sasa, kinyume na Sheria ya Uchaguzi Sura ya 343, kifungu 57(2) na kanuni zake kifungu cha 42(i) na Maelekezo ya NEC, kifungu 10.2, ameendelea kupokea majina ya mawakala kutoka CCM huku hakimu akiwaapisha nje ya utaratibu ulioelekezwa kisheria, ambao unaelekeza vyama vyote vinatakiwa kuwasilisha majina hayo siku 7 kabla ya siku ya kupiga kura.

Wakati msimamizi huko Buyungu, akiendelea kupokea majina ya CCM kinyume taratibu za uchaguzi, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Songoro amegoma kumuapisha Wakala wa CHADEMA, baada ya aliyekuwa kwenye orodha kupata ajali akiwa njiani kwenda kuapishwa.

Tunaitaka NEC, itimize majukumu wake kwa mujibu wa sheria, kuchukua hatua za kuzuia njama na hila hizo zinazofanywa na mawakala wake (wasimamizi wa uchaguzi), zenye nia ya kukwamisha ushindani ulio sawa kwa vyama vyote na wagombea wote na kuwanyima wapiga kura haki yao ya msingi ya kuchagua wagombea wa chama wanachokitaka.


Ratiba ya Viongozi Wakuu kuhitimisha kampeni

Wakati huo huo, kuanzia Agosti 7, mwaka huu, Viongozi Wakuu wa Chama wataanza ziara, wakiongoza timu zitakazokwenda kuongeza hamasa ya kampeni na kuzungumza na wananchi kwenye maeneo yatakayokuwa na uchaguzi wa marudio hapo Agosti 12, mwaka huu, kama ifuatavyo;

Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mhe. Freeman Mbowe (Mb) ataongoza timu itakayokwenda Kata ya Bugalama (Shinyanga), Kata ya Kibare na Bugoloma (Kagera) na Jimbo la Buyungu (Kigoma).
Katibu Mkuu wa Chama, Mhe. Dkt. Vincent Mashinji; Kata ya Mwanganyanga ((Mbeya), Kata ya Isapulano (Njombe) na Kata ya Mwangata (Iringa).
Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mhe. Salum Mwalim; Kata ya Unyambwa (Singida), Kata ya Itobo (Nzega), Kata ya Turwa (Mara), Kata ya Kiyungi na Kabila (Tabora mjini).

Imetolewa leo Jumanne, Agosti 7, 2018 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA 

No comments:

Post a Comment