Leo ni mwezi wa tatu tangu kufanyika kwa jaribio la kuniua la tarehe 7 September.
Tangu siku hiyo, nimetembelewa na mamia ya Watanzania na watu wengine kutoka nchi mbali mbali duniani.
Nimeombewa sala na mamilioni ya Watanzania na watu wengine wengi kutoka nchi nyingine walioguswa na tukio hili.
Nimetembelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na viongozi wengine wa serikali ya Kenya na taasisi zake; pamoja na wabunge wa Tanzania na wa Kenya, majaji na wanasheria wa nchi mbali mbali, n.k.
Hata hivyo, hadi sasa Jeshi la Polisi la Tanzania halijataja linamshuku nani kuhusika na kitendo hicho cha kigaidi.
Hadi sasa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania hajamwomba Mwanasheria Mkuu mwenzake wa Kenya ruhusa ya mimi kuhojiwa na Polisi wa Kenya juu ya shambulio hilo kama inavyotakiwa na sheria husika za nchi yetu.
Polisi wa Tanzania hawana mamlaka ya kunihoji nikiwa Kenya au kwingineko nje ya mipaka ya Tanzania.
Hadi sasa Bunge la Tanzania na uongozi wake haujachukua hatua yoyote ya kunitembelea hospitalini nilikolazwa wala kunihudumia kwa namna yoyote ile.
Sheria ya Uendeshaji wa Bunge inasema ni wajibu wa Bunge kumhudumia mbunge kwa matibabu na huduma nyingine anapokuwa hospitalini ndani au nje ya Tanzania.
Kwa kila namna, ninauguzwa na chama changu, Watanzania na watu wengine kutoka sehemu mbali mbali duniani kwa michango yao, sala zao na mapendo yao kwangu. Nawashukuruni sana na Mungu wetu awabariki sana.
Mambo yote haya yanatilia nguvu hoja yetu juu ya ulazima wa uchunguzi huru wa shambulio hili la kigaidi. Likiachiwa kwa serikali ya Tanzania peke yake ukweli hautakaa ujulikane.
Ninaendelea vizuri na matibabu na madaktari watakaposhauri nitaanza hatua nyingine ya matibabu yangu.
Mungu ni mwema, nitasimama na kutembea tena. Nitarudi nyumbani ili kuendelea na kazi ambayo imempendeza Mungu kuokoa maisha yangu ili niweze kuitenda.
Kumekuwa na matukio mengi ya kutisha kama hili na mengine mbaya zaidi. Nchi yetu inahitaji ukombozi ili maovu haya yakomeshwe kabisa. Hili ni jukumu letu sote tunaojiona kuwa wazalendo halisi wa Tanzania.
Nawashukuruni sana na Mungu wetu awabariki sana.
Tundu AM Lissu (MB)
The Nairobi Hospital, Kenya
No comments:
Post a Comment