Friday, December 8, 2017

CHADEMA YAJITOA KWENYE TIMU YA BUNGE INAYOSHIRIKI MICHEZO YA EALA

CHAMA KUWAAGIZA WABUNGE WAJITOE KWENYE TIMU YA BUNGE MICHEZO YA EALA

Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inayokutana jijini Dar es Salaam tangu jana Jumatano, katika kikao cha dharura, pamoja na masuala mengine, imeendelea kutafakari kwa kina mwenendo wa hali ya kisiasa nchini.

Kipekee katika agenda hiyo, Kamati Kuu baada ya kupokea taarifa na tathmini ya kina ya uchaguzi wa marudio katika kata 43 uliofanyika hivi karibuni, ambao ulitawaliwa na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, vitendo vya kinyama dhidi ya ubinadamu na ukandamizwaji mkubwa wa misingi ya demokrasia na utawala bora, kinyume cha sheria za nchi yetu, vyote hivyo vikilenga kuharibu uchaguzi na kupora matokeo tofauti na matakwa ya wapiga kura;

Na baada ya kujiridhisha kuwa vitendo hivyo vimefanyika kwa makusudi, vikilindwa au kunyamaziwa na mamlaka za kiserikali zenye wajibu wa kusimamia taratibu za uchaguzi, vikiwemo vyombo vya dola, lengo ikiwa ni kutaka kuua siasa za ushindani wa vyama vingi na kipekee kuishughulikia CHADEMA, wanachama, wafuasi, mashabiki na viongozi wake;

Kwa kuzingatia pia misimamo ambayo imekuwa ikioneshwa na chama kilichoko madarakani, wakiwemo viongozi wake na hata wabunge katika matukio ya kinyama yanayofanyika wazi kwa nia ya kuwadhuru wanaChadema, mathalani tukio la kushambuliwa kwa nia ya kuuwawa Mwanasheria Mkuu wa Chama na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili nchini (TLS), Kamati Kuu ya Chama imetoa azimio kwa kauli moja kuwa;

1. Wabunge wote wa CHADEMA ambao ni sehemu ya Timu ya Michezo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoshiriki michezo ya Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waondoke mara moja kwenye kambi ya timu hiyo.

2. Wajitoe rasmi kushiriki mashindano hayo ambayo mwaka huu Tanzania ndiyo nchi mwenyeji, yakifanyika jijini Dar es Salaam.

3. Kwamba maagizo hayo yanaanza kutekelezwa mara moja kuanzia usiku wa Jumatano, Desemba 6, mwaka huu, baada tu ya kupitishwa kwa azimio hilo, ambapo Kamati Kuu ilimwagiza Katibu wa Wabunge kuwafikishia wabunge husika maagizo hayo mara moja kwa ajili ya utekelezaji.

Maazimio mengine ya kikao cha Kamati Kuu ambacho bado kinaendelea jijini Dar es Salaam, yatatolewa katika hatua ya baadae kwa njia ambayo umma utataarifiwa rasmi.

Imetolewa leo Alhamis, Desemba 7, 2017 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment