MSIMAMO WA VYAMA VYA CUF, NCCR -MAGEUZI, CHAUMMA, NLD NA CHADEMA KUHUSU
MWENENDO WA HALI YA KISIASA NCHINI NA KUSHIRIKI UCHAGUZI MDOGO WA MARUDIO WA TAREHE 13 JANUARI, 2018.
UTANGULIZI
Serikali ya awamu ya tano imeonyesha wazi kuwa haiko tayari kufuata Katiba na Sheria za nchi katika utendaji wake wa kazi. Iimejipambanua wazi kuwa haiheshimu demokrasia. Haki za Binadamu zimeendelea kuvunjwa na serikali na vyombo vyake. Hakuna hatua zozote zinazoonekana kuchukuliwa kudhibiti hali hii.
Baadhi ya vitendo ambavyo vimeonyesha wazi kuwa kuna ukiukwaji wa Katiba na Sheria za Nchi ni pamoja na vifuatavyo;
i. Kupiga Marufuku Mikutano ya Vyama vya Siasa:
Serikali ilipiga marufuku vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa mpaka mwaka 2020. Huu ni uvunjaji wa Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, katazo hilo linakiuka Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 ambayo imetoa haki kwa vyama vya siasa kufanya kazi ya siasa.
ii. Mauaji, unyanyasaji na uonevu unaofanywa dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani:
Uonevu na unyanyasaji dhidi viongozi wa kisiasa wa vyama vya upinzani unaendelea kufanywa kwa kuwakamata, kuwaweka rumande na kuwafungulia mashtaka mbalimbali ya kubuni na kubambika viongozi hao, huu ni mkakati wa kuwafunga midomo wapinzani wanapotekeleza jukumu lao la msingi la kuikosoa Serikali. Aidha wapo ambao wameshambuliwa kwa lengo la kuuwawa (Tundu Lissu), wengine wamepotezwa na mpaka sasa hawajulikani walipo (Ben Saanane) na wengine wameuawa kikatili (Alphonce Mawazo) na wengine wanaendelea kushambuliwa maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
iii. Uchaguzi kugeuzwa uwanja wa vita, badala ya kushindanisha hoja na sera za vyama na wagombea
Tumeshuhudia chaguzi za marudio zilizopita kwenye kata 43 zikiendeshwa bila kufuatwa kwa sheria, taratibu, kanuni na maadili ya uchaguzi, bila hatua zozote kuchukuliwa kwa wahusika. Badala yake viongozi wa vyama vyetu wameendelea kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwenye mahakama mbalimbali na wengine wapo mahabusu za Polisi mpaka sasa.
Aidha, viongozi wetu kwenye kata hizo walishambuliwa kwa mapanga na wengine mbele ya Polisi na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahalifu hao, badala yake walikuwa wanalindwa na Polisi ili kutimiza uhalifu wao huo.
iv. Mauaji na watu kupotezwa
Kumekuwa na utamaduni mpya ambapo sasa wananchi wanauawa na miili yao inaokotwa ikiwa ama inaelea baharini au maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwa imewekwa kwenye sandarusi na hatuoni Serikali ikitoa taarifa yeyote rasmi kuhusu mauaji hayo.
Aidha kumeibuka utamaduni wa watu kutekwa, kuteswa na kupotezwa na watu wanaoitwa ‘wasiojulikana’. Ahadi ya Serikali kuwabaini watu hao ‘wasiojulikana’ hadi sasa hazionekani kuzaa matunda, hali inayopelekea kujenga imani kuwa ‘wasiojulikana’ hao, wanajulikana kwa baadhi ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na kwamba kuna mkakati maalum wa kuwalinda.
v. Vyombo vya habari kuminywa
Tumeshuhudia vyombo vya habari nchini vikiendelea kuminywa na vingine kufungiwa kwa sababu tu vimekuwa na ujasiri wa kuikosoa serikali. Hali hii imeenda mbali zaidi sasa tunashuhudia waandishi wa habari wakitekwa na kupotezwa (mf; Azory Gwanda) na hakuna taarifa rasmi za kufuatilia kwa kina jambo hili.
vi. Matukio ya aibu katika uchaguzi kata 43
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza uchaguzi mdogo wa marudio katika majimbo ya Longido,Singida Kaskazini , Songea Mjini na Kata sita ambao utafanyika tarehe 13 Januari,2017.
Itakumbukwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi wa marudio katika kata 43 mnamo tarehe 26 Novemba ,2017. Uchaguzi huu ulifanyika bila ya kufuata misingi ya sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi,baadhi ya matukio hayo ni kama ifuatavyo;
• Mawakala walitolewa nje ya vituo vya kupigia kura; hili lilifanywa kwa ushirikiano baina ya polisi na wasimamizi .
• Vituo kuvamiwa wakati wa kuhesabu kura; vituo vya uchaguzi vilivamiwa na watu wa CCM na kuharibu zoezi la kuhesabu kura. Matokeo katika baadhi ya vituo yalibadilishwa kwa nguvu.
• Fomu za malalamiko; mawakala wetu walikataliwa kujaza na wale wachache waliojaza hawakupewa kabisa nakala za fomu husika
• Umwagaji wa damu; Viongozi na wanachama wetu kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya kwa silaha mbalimbali yakiwemo mapanga, marungu na fimbo.
• Viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Wilaya; kuingia kwenye vituo vya kupigia kura wakati hawaruhusiwi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi
• Wasimamizi wa uchaguzi; walifanya hujuma za wazi kama vile kuwanyima barua za viapo mawakala wetu,kuwazuia wagombea wetu kufanya kampeni na kuwaengua wengine bila kufuata taratibu.
• Matokeo halisi kutokutangazwa; wasimamizi wa uchaguzi waliamua kutangaza matokeo ya uongo na kuipa CCM ushindi pamoja na fomu zote kuwepo zinazoonesha kuwa vyama vya upinzani vimeshinda.
MAANA YA MATUKIO HAYA
1. Hakuna tena uchaguzi utakaofuata sheria ,kanuni na taratibu zilizopo.
2. Tume ya Taifa ya uchaguzi imekosa uhalali wa kuendelea kusimamia chaguzi .
3. Jeshi la polisi wameonyesha wazi kuwa wapo upande wa CCM na hata tuliporipoti matukio mbalimbali hawakuchkua hatua.
4. CCM kwa kushirikiana na serikali yake hawako tayari kutangazwa kuwa wameshindwa kwenye uchaguzi.
5. Wasimamizi wa uchaguzi wameonyesha dhahiri kuwa wao ni CCM.
6. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeshindwa kusimamia kikamilifu haki ya vyama vyote vya siasa na sasa ni dhahiri imeegemea upande mmoja wa kulinda CCM na Serikali yake dhidi ya vyama vya upinzani!
HITIMISHO.
Itakumbukwa kwamba, kwa nyakati tofauti kabla ya uchaguzi wa marudio wa Novemba 26, tayari kumekuwepo na kauli za maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa ya kwamba hatamwelewa Mkurugenzi atakayemtangaza mgombea wa chama cha upinzani kuwa mshindi. Kauli hiyo imethibitika katika uchaguzi huu wamarudio wa kata 43 uliomalizika hivi karibuni.
Uchaguzi unapokosa kuwa huru, wa haki na halali, unajenga chuki na mfarakano mkubwa katika taifa. Kuendelea kushiriki chaguzi zenye viashiria vyote vya ubatili ni kujenga misingi ya ubatili katika Taifa.
Vyama vya siasa hujengwa na kuimarika pale vinapofanya shughuli zake za kisiasa wakati wote. Kufungia/kuzuia vyama kufanya shughuli zake kihalali na kisha kuviruhusu tu kushiriki uchaguzi ni sawa na kuingiza timu katika mashindano bila mazoezi.
Umoja wetu unaamini kuwa uchaguzi uliotangazwa kufanyika Januari 13, 2018, hauna sifa kuendelea bila kwanza wadau wote, kwa maana ya Vyama vya Siasa, Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa, Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wadau wengine wowote, kukaa meza ya pamoja na kutafakari njia bora zaidi ya kuendesha chaguzi katika awamu hii ya tano.
Ni rai yetu kwamba uchaguzi huu UAHIRISHWE ili kutoa nafasi hii. Kama Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) na Serikali hawatakubaliana na RAI hii, umoja wetu wa vyama tajwa, HAUTASHIRIKI uchaguzi uliopangwa kufanyika Januari 13, 2018.
Kwa upande mwingine, umoja wetu utaendelea na jitihada za kudai TUME HURU, KATIBA MPYA na UTAWALA UNAOHESHIMU KATIBA, SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU, kupitia majukwaa mbalimbali. Ndani nan je ya nchi, ikiwemo mahakama.
….……………………..
MHE.JULIUS MTATIRO
M.KITI KAMATI YA UONGOZI –CUF
…………………….
MHE. FREEMAN MBOWE
M.KITI –CHADEMA
……………….
MHE. HASHIM RUNGWE
M.KITI –CHAUMMA
…………………..
MHE. DANDA JUJU
KATIBU MKUU –NCCR –MAGEUZI
…………………….
MHE. TOZY MATWANGA
KATIBU MKUU –NLD
No comments:
Post a Comment