Sunday, August 28, 2016

KAULI YA TUNDU LISSU JUU YA SABABU YA KUANZISHA UKUTA

"Makamanda tunahitaji kufahamu namna mbali mbali za mapambano. Kuna mapambano ya mapanga na kuna mapambano ya kisiasa na kiitikadi.

Kuna mapambano ya kivita na kuna mapambano ya kidiplomasia. Mifano ni mingi. Ili Wamarekani waweze kuzungumza na Wacuba baada ya miaka zaidi ya hamsini ya uhasama, ilibidi Barack Obama akutane na kushikana mkono na Raul Castro kwenye mazishi ya Nelson Mandela.

Ili Marekani irudishe uhusiano na China ya Mwenyekiti Mao, ilibidi kuwe kwanza na 'ping pong diplomacy', timu za table tennis za Marekani na China zilitembeleana na kucheza ping pong. Chini ya hiyo ping pong, mazungumzo ya kisiasa yalikuwa yanafanyika yaliyopelekea kurudishwa kwa mahusiano ya kibalozi kati ya Marekani na China.

Chini ya salamu za Obama na Raul kulikuwa na mazungumzo yaliyopelekea kurudishwa kwa mahusiano ya kibalozi kati ya Marekani na Cuba. Na ili Mandela aachiliwe huru na mfumo wa kibaguzi kuondolewa Afrika Kusini ilibidi Mandela mfungwa akutane na Rais de Klerk kwenye Gereza la Pollsmoor na kuzungumza.

Kwa nini tumeanzisha UKUTA?......
Ni kwa sababu tunataka demokrasia ya vyama vingi kama ilivyo kwenye Katiba na Sheria zetu iheshimiwe. Turuhusiwe kufanya shughuli za kisiasa za aina zote zinazotambuliwa na sheria zetu, yaani mikutano ya ndani na nje ya kisiasa, maandamano ya amani, uhuru wa vyombo vya habari, Serikali iwajibike kwa Bunge na sio kuligeuza Bunge kuwa extension ya Ikulu ya Magufuli, wafungwa na mahabusu wote wa kisiasa na kesi za kijinga jinga tulizofunguliwa zikome n.k.

Kama yote haya yanawezekana kupatikana baada ya Magufuli na Lowassa kukutanishwa na Kardinali Pengo kwenye Jubilei ya Mkapa litakuwa jambo jema. Kwa vyovyote vile ni lazima tufahamu kwamba Magufuli amekubali kukutana na Lowassa kwa sababu ya joto kali la UKUTA.

Kwa vyovyote vile, ni lazima tufahamu kutumia silaha ya ulimi wa mazungumzo na diplomasia pale mazungumzo na diplomasia vinapohitajika. In the meantime, kama kuna chochote kilichozungumzwa kwenye Jubilei ya Mkapa kuhusu UKUTA, tutakiambiwa. Tuvute subira ili tupate kheri. Lakini vile vile tuendelee na maandalizi ya Septemba Mosi.

Tundu Lissu (Mb).

No comments:

Post a Comment