Tuesday, June 28, 2016

TAARIFA KWA UMMA​ KUHUSU SINTOFAHAMU YA ALIPO MAKAMU MWENYEKITI WA BAVICHA TAIFA NDG. SOSOPI

TAARIFA KWA UMMA​
KUHUSU SINTOFAHAMU YA ALIPO MAKAMU MWENYEKITI WA BAVICHA TAIFA NDG. SOSOPI

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) taifa, Tanzania Bara, Ndugu Sosopi hajulikani aliko tangu jana Jumapili majira ya saa 3 usiku alipopakiwa ndani ya gari linaloaminika kuwa la Jeshi la Polisi wilayani Iringa kwa ajili ya kupelekwa Ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Iringa (OCD) Afande....

Siku ya jana Jumapili, Juni 26, 2016, Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Sosopi baada ya kuhudhuria mahafali ya Shirikisho la Wanafunzi walio wanachama wa CHADEMA (CHASO) Mkoa wa Iringa ambako yeye alikuwa Mgeni Rasmi akiambatana na Wabunge Peter Msigwa (Iringa mjini) na John Heche (Tarime Vijijini), Mratibu wa Uhamasishaji na Uenezi BAVICHA Taifa, Edward Simbeye na makamanda wengine, aliitikia wito wa Jeshi la Polisi mkoani humo kufika Kituo Kikuu kwa ajili ya mahojiano.

Mkuu wa Kituo Kikuu, Afande Thadei alidai kuwa alikuwa amepewa amri na RPC Sakamba Peter ya kumfikisha Sosopi kituoni hapo kutokana na kosa alilodaiwa kulifanya nje ya Mkoa wa Iringa na kwamba polisi walikuwa wakimtafuta kwa muda mrefu.

Akiwa Kituo Kikuu cha Polisi Mkoani Iringa, RPC aliwaambia kuwa Sosopi anatakiwa kwenda kujibu tuhuma za kauli za uchochezi alizotoa akiwa Dar es Salaam. Hivyo polisi Mkoa wa Iringa wao wanasubiri maagizo tu ya kumsafirisha kwenda huko anakotuhumiwa kufanya kosa ambako angefanyiwa mahojuano.

Viongozi wa chama, wabunge na wanachama wengine walikuwa pamoja nae kituoni, walikuwa tayari kumdhamini ili aondoke kisha arejee leo Jumatatu, Juni 27, kuripoti na kusubiri maelekezo yoyote yatakayokuwepo kuhusu hizo tuhuma.

RPC Kakamba amedaiwa kujibu kuwa yeye hakuwa na tatizo iwapo tu OCD wa Iringa ambaye ndiye mwenye wajibu wa kumshikilia na kumsafirisha Sosopi ataridhia ombi la dhamana hiyo.

Wakati viongozi hao wakijiandaa kuambatana na RPC na OCS kwenda kwa OCD, ilifika gari moja yenye namba za kiraia T 134 CJX RandCruiser, ikiwa na askari 6, wanne wakiwa nyuma ya gari, wawili (pamoja na dereva) wakiwa mbele. Wote 6 walikuwa na silaha.

Sosopi akaamriwa kuingia ndani ya gari hiyo. Tayari kwa safari iliyodhaniwa kuwa ni kwenda ofisini kwa OCD.

Katika hali iliyowashangaza viongozi wenzake aliokuwa nao ambao walikuwa wako kwenye gari jingine, gari ile iliyombeba Sosopi iliondoka kwa kasi ya ajabu ambayo haikutarajiwa hivyo haikuwa hata rahisi kuifuatilia na kujua ilikoelekea.

Hadi taarifa hii inaandikwa muda huu saa 11 jioni ya Jumatatu, Sosopi hajulikani aliko tangu jana saa 3 usiku alipochukuliwa na gari hilo kuelekea kusiokujulikana. Jitihada za Uongozi wa BAVICHA taifa kuwasiliana na Jeshi la Polisi kupitia ZCO kujua kama kiongozi huyo amefikishwa Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na pengine kupelekwa mahakamani hazijazaa matunda ya kujua hasa Sosopi yuko wapi hadi muda huu.

BAVICHA inalitaka Jeshi la Polisi kumleta Dar na kumhoji kwa mujibu wa sheria au kumuachilia huru kwa kuwa ni wazi hakuna sababu ya kuendelea kumshikilia kwa siku ya pili mfululizo.

Kama hadi kesho haitajulikana alipo, mawakili wetu kwa kushirikiana na wale wa chama watapeleka maombi ya Habeas Corpus dhidi ya RPC na RCO Iringa alikokamatiwa na ZPC na ZCO Dar es Salaam, wanaoonekana kufahamu alipo.

Imetolewa leo Jumatatu, Juni 27, 2016

Ofisi ya Katibu Mkuu BAVICHA

No comments:

Post a Comment