Tuesday, June 28, 2016

TAARIFA KUHUSU KUFUNGULIWA KWA KESI MBILI; KUOMBA KUTENGULIWA KWA ZUIO LA JESHI LA POLISI NA BUNGE LIVE

TAARIFA KUHUSU KUFUNGULIWA KWA KESI MBILI; KUOMBA KUTENGULIWA KWA ZUIO LA JESHI LA POLISI NA BUNGE LIVE 



Taarifa inatolewa kwa umma kuwa Baraza la Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Katibu Mkuu wa Chama, wamefungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam (main registry) kuiomba mahakama hiyo itengue uamuzi wa Jeshi la Polisi nchini kupiga marufuku, mikutano na maandamano ya vyama vya siasa nchi nzima.

Katika shauri hilo la madai namba 43, 2016, wadai hao wanaiomba Mahakama Kuu kufuta/kutengua zuio la mikusanyiko/mijumuiko ya kisiasa ya vyama vya siasa kwa kipindi kisichojulikana lililotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), kwa sababu;

Halikuwashirikisha.
Halikuwapatia haki ya kusikilizwa.
Ni uonezi.
Linaua demokrasia nchini.
Halina mipaka wala sababu za msingi kisheria na kimantiki.
Limezidi mamlaka ya polisi kisheria.

Shauri hilo limetajwa leo Juni 27, 2016, mbele ya Jaji Kiongozi Prof. Ferdinand Wambali ambapo upande wa Serikali utatakiwa kuleta hati ya kiapo kinzani, Juni 30, mwaka huu, kabla mahakama hiyo haijakaa kuanza kusikiliza maombi madogo (leave) Julai 1, saa 8 mchana mbele ya Jaji Kiongozi ambapo uamuzi unatarajiwa kutolewa Julai 4, mwaka huu.

Wakati huo huo, Chama kinapenda kutoa taarifa kwa vyombo vya habari na umma wa Watanzania kwa ujumla kuwa katika jitihada za kuhakikisha nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya katiba na sheria, kimewatafutia mawakili wananchi walioamua kufungua kesi ya Kikatiba, Mahakama Kuu wakipinga kuminywa kwa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya bunge (Bunge Live).

Wadai hao; Azizi Himbuka, Perfect Mwasilelwa, Moza Mushi, Hilda Newton, Penina Nkya, Rose Moshi, Kubra Manzi, Andrew Mandari, Ben Rabiu Saanane, Juma Uloleulole na Ray Kimbito, wamefungua kesi hiyo ya Kikatiba namba 13, 2016 wakidai kuwa;

Wanayo haki ya kikatiba kupata habari na kushiriki moja kwa moja au kupitia wawakilishi wao katika shughuli zote za uongozi na kuisimamia serikali. Kutokana na kuwepo kwa mminyo huo wa matangazo ya bunge, wananchi hao wanashindwa kuona moja kwa moja namna ambavyo Serikali inawajibika ili waweze kutoa maelekezo stahiki kwa wabunge wao.

Katika kesi hiyo iliyotajwa leo Juni 27, mbele ya Jaji Kiongozi Ferdinand Wambali, wadai hao wanasema kuwa kutokana na mminyo huo wa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya bunge, wanashindwa kujua wabunge wao wanasimamia vipi serikali ili waweze kujua na kutathmini uwakilishi wao bungeni.

Aidha wadai hao wanasema kuwa kwa kuangalia mahitaji ya utawala bora na uwazi katika zama za maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, matangazo ya moja kwa moja ni sehemu muhimu ya haki ya kupata habari ambayo ni haki ya kikatiba.

Kesi hiyo nambari 13 ya mwaka huu itasikilizwa mbele ya Majaji watatu; Jaji Kiongozi Wambali, Jaji Kihiyo na Jaji Munisi, ambapo Julai 15, mwaka huu asubuhi, ndipo itaamriwa siku ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, baada ya upande wa serikali kuwa umeleta hati ya utetezi Julai 11 kama ulivyotakiwa na Mahakama hiyo leo.

Hatua hiyo ya CHADEMA kuwasaidia wananchi hao kupata mawakili ni mwendelezo wa juhudi za chama kuchangia mapambano ya demokrasia na kulinda utawala bora unaozingatia katiba na sheria za nchi ili kuwapatia wnaanchi haki na matumaini katika nchi yao ambayo ndiyo msingi imara ya amani na utulivu wa kweli katika jamii.

Imetolewa leo Jumatatu Juni 27, na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment