Wednesday, December 16, 2015

Kesi ya Kubenea, Makonda yaahirishwa

KESI iliyofunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda dhidi ya Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea katika Mahakama ya Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo, imeahirishwa. Anaandiaka Yusuph Katimba … (endelea).

Akiahirisha kesi hiyo, hakimu anayesimamia kesi hiyo Thomas Simba amesema uchunguzi umekamilika na kwamba upande wa mashitaka na kwamba imepangwa kuanza kusikilizwa tarehe 29 Desemba mwaka huu.

Kwenye mahakama hiyo, Makonda amefungua madai matatu dhidi ya Kubenea ambayo ni lugha ya matusi, kuitwa mpumbavu, mjinga pamoja na cheo cha kupewa.

Kubenea ameweka mawakili sita katika kesi yake ambao ni Peter Kibatara, Rugemereza Nshara, Nyaronyo Kicheere, Frederick Kihwelo, Teremia Ntobesya pamoja na Omary Msemwa.

Hata hivyo, Kubenea yupo nje kwa dhamana, waliomdhamini ni Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest na Mbunge wa Kinondoni, Maulidi Mtulia ambapo kila mmoja aliweka dhamana ya Sh. 300,000.

Kesi hiyo imefunguliwa ikiwa ni siku moja baada ya Makonda kuagiza askari wa Jeshi la Polisi kumkamata mbunge huyo kwa madai ya kushindwa kutii agizo lake kama Mkuu wa Wilaya.

Tukio la kukamatwa Kubenea lilitekelezwa jana jijini Dar es Salaam, baada ya viongozi hao kukutana katika mgogoro wa wafanyakazi wa Kiwanda cha nguo cha Tooku Tanzania.

Kwenye mgogoro huo, Kubenea alikuwa wa kwanza kufika ili kukutana na wafanyakazi hao na kuangalia namna ya kutatua mgogoro wa wafanyakzi na viongozi wa kiwanda hicho.

Katika mgomo huo Kubenea, alisikiliza kero za wafanyakazi ambao walikuwa wakivutana na menejimenti ya kiwanda hicho na baada ya makubaliano yaliyohusisha pande mbili, walikubali kuendelea na kazi.

Hata hivyo, wakati mbunge huyo pamoja na viongozi wa kiwanda hicho wakiwa katikati ya mazungumzo, Makonda aliwasili katika eneo hilo la kiwanda kilichopo ndani ya Mamkala ya Uwekezaji EPZ, Mabibo External.

Baada ya kufika, Makonda hakutaka kuhoji kuhusu kilichoendelea kwenye mgomo huo wa wafanyakazi na kutaka kuanza upya kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi licha ya Kubenea kuupatia ufumbuzi kwa mazungumzo yaliyohusisha pande zote.

Kutokana na hatua hiyo, Kubenea hakupinga hatua hiyo ingawa Makonda alipomaliza kuzungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho, alifunga mkutano bila kuruhusu hoja yoyote kutoka kwa mbunge huyo.

Hali hiyo ilimfanya Kubenea kuhoji sababu ya kutopewa nafasi ya kuzungumza wakati ndiye alikuwa wa kwanza kufika katika eneo la tukio saa nne asubuhi na kulimaliza suala hilo.

Pamoja na hali hiyo Makonda, alipinga hoja ya Kubenea kuzungumza na wafanyakazi hao na kusema kwamba tayari amekwisha kufunga mkutano, hivyo haruhusiwi mtu mwingine kuzungumza kwa kuwa ndiye alikuwa mzungumzaji wa mwisho na tayari alikuwa amefunga.

Hatua hiyo ilizua mabishano makali baina ya Kubenea na Makonda kwa kila mmoja kusimamia kile anachokiamini.

Wakati hayo yakiendelea, Kubenea aliendelea kuwasihi wafanyakazi hao watulie, lakini Makonda akasisitiza hatozungumza hali iliyosababisha polisi waliokuwapo katika eneo hilo na baadhi ya viongozi wa kiwanda kuingilia kati kusuluhisha mzozo huo.

“Huwezi kufunga mkutano nisiongee na wafanyakazi ambao ni wapiga kura wangu, nimekuja hapa tangu asubuhi nimepambana hadi tukafikia hapa na niliwaahidi nikitoka kwenye kikao cha utawala nitawapa mrejesho (yaliyojiri).

“Inakuwaje wewe umekuja sasa hivi unazungumza na kufunga mkutano kwa ubabe?,” alihoji Kubenea huku Makonda akiendelea kusimamia msimamo wake kwamba tayari amefunga mkutano.

“…mimi hawa wamenipigia kura, wewe umepata kura ngapi, huwezi kunifanya lolote wewe,” alisema Kubenea. Baada ya mabishano hayo, Makonda aliamuru Kubenea akamatwe pamoja na kuamuru mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Star TV kunyang’anywa kamera yake.

Polisi walimtaka Kubenea kupanda kwenye gari lao la polisi (Defender) lakini kukatokea mabishano makali, kwani Kubenea alipinga kupanda gari lao umuazi waliokukubali na hatimaye askari wawili wenye silaha na mmoja ambaye hakuwa na silaha waliingia kwenye gari la mbunge huyo hadi Kituo cha Polisi cha Magomeni.


MwanaHalisiOnline

No comments:

Post a Comment