Wednesday, December 16, 2015

MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA KUFANYA ZIARA YA KUWASHUKURU WAPIGA KURA

KUHUSU ZIARA YA MH. EDWARD LOWASSA KUSHUKURU WATANZANIA



Taarifa inatolewa kwa vyombo vya habari na umma wa Watanzania kwa ujumla kuwa aliyekuwa Mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Ndugu Edward Lowassa atazungumza na wananchi wa Tanga katika mkutano wa hadhara utakaofanyika mjini Tanga, siku ya Alhamis, Desemba 17, 2015.

Mkutano huo ni sehemu ya ziara ya viongozi waandamizi wa Chama na UKAWA kwa ujumla ambao watakwenda maeneo mbalimbali nchi nzima kuwashukuru wananchi kwa namna walivyounga mkono upinzani na agenda nzima ya MABADILIKO katika uchaguzi mkuu uliopita na wanavyoendelea kuweka matumaini yao kwa upinzani kuwa ndiyo nguzo imara wanayoweza kuitegemea kuwaletea mabadiliko ya kweli kwa ajili ya maendeleo yao na ustawi wa taifa kwa ujumla.

Itakumbukwa kuwa mbali ya Watanzania kupiga kura za ushindi katika nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu uliopita, wananchi waliwachagua wabunge wengi wa upinzani wanaotokana na UKAWA na kuongeza nguvu kubwa ndani ya bunge hususan kupitia Kambi ya Upinzani Bungeni ambayo itakuwa serikali yao mbadala huku wakiviamini vyama hivyo kusimamia na kuongoza halmashauri zipatazo 34 nchi nzima, ikiwa moja ya misingi imara katika kupigania mabadiliko ambayo Watanzania wanayataka.

Wananchi wanastahili shukrani kwa imani hiyo kubwa ambayo ni ishara ya wazi kuwa matumaini yao kwa miaka mingine mitano yatasimamiwa na kuongozwa na upinzani imara kupitia UKAWA.

Katika ziara hiyo ya Tanga, Ndugu Lowassa ataambatana na viongozi wengine waandamizi wa UKAWA ukiwa ni mwanzo tu wa ziara kubwa itakayokwenda nchi maeneo mbalimbali nchi nzima.

Imetolewa leo Jumanne, Desemba 15, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment