Sunday, July 19, 2015

Tundu Lissu 'aichana' CCM.

Matatizo na manyanyaso yanayolalamikiwa na Watanzania yanadaiwa kutokana na mfumo mbovu wa serikali iliyopo madarakani inayotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kushindwa kutetea maslahi ya wananchi wanyonge.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kamachumu wilayani Muleba jana, mjumbe wa Kamati kuu na mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, aliwataka Watanzania kutomchagua mgombea aliyepitishwa na CCM kugombea urais Jonh Magufuli, maana hatakuwa na utendaji tofauti na viongozi waliomtangulia.

“Matatizo na changamoto zinazowakabili Watanzania zimetokana na mfumo mbaya wa CCM sio mtu, kwa hiyo wananchi wasimchague Magufuli wakidhani atatenda maajabu au mapya yatakayowafanya kuondokana na changamoto hizo,” alisema Lissu.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alisifiwa sana wakati anachaguliwa lakini ameshindwa kutetea maslahi ya wananchi na badala yake umekuwapo mfumuko wa bei na kuongezeka kwa michango inayowaongezea maumivu wananchi.

“Wizi wa fedha za EPA, Richmond na Escrow, mbunge wenu (jimbo la Muleba Kaskazini) Charles Mwijage na Magufuli mbona hawakuwa na mtazamo tofauti na CCM ili muweze kuwaamini wapo tofauti na viongozi wengine wa chama hicho,” alihoji.

Alisema ili kudhihirisha CCM wanafanya maamuzi ya kuwaumiza wananchi makusudi, maamuzi yaliyofanyika bungeni ya kuletwa na kupitishwa kwa miswada ya dharura haikuwa mara ya kwanza maana miaka 18 iliyopita, serikali ya CCM ilileta muswada wa madini kwa dharura na sasa matokeo yake yanaonekana ya kuibwa kwa madini ambayo yangekuwa mkombozi kwa Watanzania.

Katika mkutano huo ambao pia ulitumika kumpigia debe mgombea ubunge katika jimbo la Muleba Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Ansbert Ngurumo, diwani wa kata ya Kamachumu, Danstan Mutagahywa, alitangaza rasmi kuhama CCM na kuhamia Chadema.

No comments:

Post a Comment