Friday, July 3, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KONGAMANO LA WAZEE WA DAR ES SALAAMCHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)BARAZA LA WAZEE WA CHADEMA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

KUHUSU  KONGAMANO LA WAZEE WA DAR ES SALAAM

Taarifa kwa vyombo vya habari.

CHADEMA inajivunia Mabaraza yake katika shughuli zake za kila siku za ujenzi wa Chama. Kama mtakumbuka mwaka jana Oktoba tulifanya uchaguzi wa ndani ya Chama na kupata viongozi wa baraza letu katika ngazi zote.

Toka tuingie madarakani tumefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuzindua caucas za wazee katika Mikoa mbalimbali, kushiriki katika siku ya Wazee duniani na utatuzi wa migogoro ndani ya Chama ambalo ndio jukumu kuu la baraza hili.

Ndugu waandishi wa habari itakumbukwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu. Wazee tuna jukumu kubwa katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa amani, ndio maana Baraza linaandaa kongamano lenye ujumbe wa “Wazee na mustakabali wa Taifa letu tunapoelekea uchaguzi mkuu.” Lengo ni kuwakumbusha wazee majukumu yao ya msingi yaani kusimamia maadili na hasa ya uongozi.

Kwa muda mrefu, marais ambao kimsingi ni wenyeviti wa CCM wamekuwa na tabia ya kuongea na wazee wa Dar es salaam na kila mara wamekuwa ni wazee wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hivyo CHADEMA imeamua kuvunja mwiko huu kwa kuwa kina amini kuwa wazee wa Dar es salaam wapo walio wanachama na wasiokuwa wanachama wa vyama vya siasa.

Kwa kutambua umuhimu wa wazee na changamoto zinazowakabili tumeona ni busara kuwa na kongamano hili litakaloeleza wajibu wa wazee tunapoelekea uchaguzi mkuu.

Wote tunajua binadamu anapitia hatua nne muhimu za maisha nazo ni utoto, ujana, utu uzima na uzee. Wazee wengi hapa nchini wanakumbwa na matatizo mengi hususani ya kutotambuliwa na kutengwa na jamii. Serikali imeshindwa kuongeza pension ama kuwapatia makao yenye hadhi. Tumeshuhudia wazee wengi wakiuawa kikatili katika maeneo mengi.

Hitimisho.

Tunapoelekea uchaguzi mkuu, wazee tuna jukumu kubwa la kuhakikisha tunashiriki kikamilifu katika zoezi zima la kuandikisha na kupiga kura. Lakini pia kuwashawishi watoto,wake zetu, waume zetu, wajukuu zetu kushiriki kikamilifu.

Tuna jukumu la kutatua migogoro, kushawishi na kusimamia maadili, kubwa zaidi ni kuwa na uthubutu wa kukemea viongozi wanaopata madaraka kwa njia ya rushwa na ufisadi.

Tunahitaji wazee watakaosimama kidete na kupaza sauti zao kukemea maovu na watenda maovu. Tunasikitika sana kuona wazee ambao wangepaswa kuwa na msimamo wa kukemea kama alivyofanya baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakishindwa na badala yake kuwa sehemu ya maovu kwa kuwatetea

Mgeni rasmi katika kongamano hilo litakalofanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 4 Julai, 2015, atakuwa ni Katibu Mkuu wa Chama, Dk. Willibroad Slaa, ambapo litatangazwa moja kwa moja kupitia Kituo cha Televisheni cha ITV.

Imetolewa leo Ijumaa, 3 Julai, 2015 na;
Hashimu Juma Issa
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee CHADEMA.

No comments:

Post a Comment