Wednesday, July 29, 2015

Kwanini naunga mkono kwa Mh Edward Lowassa kukaribishwa UKAWA : Ismail Jussa

Mjadala mkubwa umezuka kuhusu mwelekeo wa ushirikiano wa vyama vikuu vya upinzani vinavyounda UKAWA na hatua ya kumkaribisha Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli, Mhe. Edward Lowassa, ili kushirikiana kuiondosha madarakani CCM pamoja na mfumo wake wa kikandamizaji na kifisadi ulioambatana na kiburi kikubwa cha watawala.

Baada ya kusoma maoni na mitazamo ya watu mbali mbali, nataka na miye nieleze mtazamo wangu kuhusiana na masuala hayo lakini zaidi nikirudi nyuma katika miaka ya 1991 na 1992 ambapo kulikuwa na vuguvugu zito la kudai mabadiliko ya mfumo wa utawala katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa baada ya kuangushwa Ukuta wa Berlin na kuporomoka kwa dola kandamizi za kikomunisti na washirika wao zilizokuwa zikijitambulisha na Kambi ya Mashariki zama za Vita Baridi (Cold War). Tanzania haikusalimika. Na mimi nikiwa kijana mdogo wa miaka 19 nilikuwa katikati ya vuguvugu hilo.

Sote tunajua kwamba demokrasia ya vyama vingi inastawi pale nchi inapokuwa na uwanja wa ushidani ulio sawa (level playing field).

Mwaka 1991, Tume ya Jaji Francis Nyalali iliyopendekeza kurudishwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ilipendekeza pia, kupitia Taarifa yake iliyokuwa na vitabu (volumes) vitatu, haja ya kwanza kubadilisha Katiba, Sheria na misingi ya Utawala katika maeneo mengi ili kuondoa nafasi ya CCM kudhibiti hatamu zote na pia kudhibiti taasisi zote kuu za nchi pamoja na rasilimali nyingi ambazo kimsingi zilipatikana kupitia michango ya lazima iliyokamuliwa kwa wananchi ambao wengi wao hawakuwa hata wanachama wa CCM.

Kwa mukhtasari ni kwamba Tume ya Nyalali ilitaka kwanza CCM kiondolewe nguvu hizo kubwa ambazo haikuzipata kutokana na kazi ya kisiasa iliyofanya au kukubaliwa kwake kwa hiyari na wananchi bali kutokana na kuhodhi kwake kwa mabavu mamlaka makubwa chini ya dhana ya "Chama kushika hatamu" (Party Supremacy), dhana iliyokifanya kisiwe chama cha siasa bali ni chama dola (state party) ambacho kilikuwa siyo tu chama pekee cha siasa lakini zaidi ilikiweka juu ya mamlaka na taasisi nyengine zote za dola tena kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi.

Kwa kutumia dhana hiyo ya "Chama kushika hatamu" (Party Supremacy), Katiba na Sheria za Nchi ziliiweka CCM kuwa juu ya Serikali, Bunge, Mahkama na hata Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Tume ya Nyalali kwa usahihi kabisa iliona hali hiyo itaondoa kabisa dhana nzima na maana ya kuruhusu demokrasia ya vyama vingi nchini na itapelekea CCM kuwa juu ya vyama vingine si kwa sababu ya kukubalika kwake na wananchi bali kwa sababu ya mfumo wa kikatiba, kisheria na Utawala unaokilinda.

Kwa sababu hizo, ndiyo Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji aliyeheshimika sana Francis Nyalali ikaja na mapendekezo mengi ya hatua ambazo kama zingetekelezwa zingeuweka uwanja sawa wa ushidani kwa vyama vyote vya siasa. 

Tume hiyo ilikuja na mapendekezo ya ratiba kamili ya utekelezaji wa hatua hizo. Lakini kwa sababu CCM ilijua kuwepo kwa ushidani ulio sawa kutakipa wakati mgumu kushindana na vyama vipya ILIYAKATAA mapendekezo hayo yote. Hiyo ndiyo hali tunayoendelea nayo hadi leo.

Hali ya namna hiyo haikuwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tu bali ndivyo ilivyokuwa kwa nchi takriban zote za Afrika ambazo kwa miaka mingi tokea Uhuru zilikuwa na tawala za chama kimoja vilivyohodhi mamlaka zote za nchi.

Katika hali kama hiyo, kuwa na uchaguzi huru na wa haki linakuwa ni jambo gumu na kukishinda chama dola (state party) kuwa takriban jambo lisilowezekena.

Njia pekee inayobaki ya kuweza kujenga mfumo imara wa ushindani huru na wa haki ndani ya demokrasia ya vyama vingi katika nchi kama hizo ni kwanza kuhakikisha kuwa chama dola (state party) kinaondolewa madarakani ili kutoa nafasi ya ujenzi wa mfumo mpya wa demokrasia iliyojengwa juu ya misingi imara ya haki na inayorudisha mamlaka ya kuendesha nchi na hatamu zake kwa wananchi wenyewe.

Ili kufikia hapo, uzoefu wa nchi nyingi umeonesha kwamba hatua mbili ni lazima zifanyike. Kwanza, vyama vya upinzani viunganishe nguvu zake; na pili, chama dola kigawike. 

Hatua hizo ndizo zilizoving'oa vyama vya KANU nchini Kenya, UNIP na hata MMD nchini Zambia pamoja na MCP nchini Malawi. Hata Zimbabwe katika uchaguzi wa mwanzo ambao ulikipa ushindi MDC dhidi ya ZANU-PF cha Robert Mugabe, hali ilikuwa hivyo hivyo kabla ya Mugabe kuamua kuitia nchi katika machafuko makubwa ili aendelee kubaki madarakani. Mfano wa karibuni kabisa ni wa Nigeria pale chama cha APC cha Rais Muhammad Buhari kilipofanikiwa kukin'goa chama cha PDP cha Goodluck Jonathan na watangulizi wake. Tukio la Olesagun Obasanjo kuchana kadi yake ya PDP ndiyo iliyohitimisha safari ya chama hicho kuondoka madarakani.

Ni katika muktadha huo, naona kwamba njia pekee ya kukiondoa madarakani CCM na mfumo wake dhalimu na kandamizi, ambao ndiyo unaolea ufisadi na rushwa, kuua uwajibikaji hapa nchini na hatimaye kuwaingiza Watanzania katika umasikini wa kutupwa wakati nchi yenyewe imejaa utajiri wa kila aina, ni kuunganisha nguvu za vyama vya upinzani na kugawanyika kwa CCM yenyewe.

Kuundwa kwa UKAWA na sasa kupasuka kwa CCM kwa hatua ya Mhe. Edward Lowassa na kundi kubwa linalomuunga mkono ndani ya chama hicho kukihama na kujiunga na UKAWA ni fursa ya kihistoria ambayo tunapaswa kuikumbatia ili CCM ifuate mkondo wa vyama dola vyengine vya Afrika na kuipa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nafasi ya kupata MWANZO MPYA utakaotukwamua katika mkwamo huu tuliokwamishwa na CCM.

Viongozi wakuu na wakongwe wa siasa za CCM wanapoliona ANGUKO LA CCM tujue sasa zama zake zimefikia kikomo na TANZANIA MPYA INAKARIBIA KUZALIWA.

* Karibu Edward Lowassa
* Ahsante UKAWA

1 comment:

  1. Asante sana mheshimiwa Freeman Mbowe na Mheshimiwa Dr. W. Slaa kwa uongozi wenu uliotukuka. Mungu awaongoze katika kutafuta haya mapi ndugu ya haki ya kila mtanzania kuishi tena kwa uhuru uliopiganiwa na mababu zetu.

    CCM kama vyama vingine vingi africa, k inafikiriwa nchi ya Tanzania ni yao wenyewe. Kwanza wamejichukulia majengo mengi ya serikali, viwanja vingi vya Jamie na kuvifanya vyote ni mali zao. Eeh Mungu baba wasimamoe viongozi wetu wa Chadema na ukawa ili tupate ukombozi na uhuru wa kweli ndani ya nchi yetu.

    Kama sio kujitolea muhanga nyie viongozi wetu wa Chadema sijui tungekuwa wapi leo. Wamejaribu kuwamaliza kwa mabomu wameshindwa. Nilifurahi kumsiliza Mwenyekiti FM (Freeman Mbowe) akisema hivi, ninanukuu "hata mkiniua mimi FM, CDM itaendelea mbege kwa mbele" mwisho wa kunukuu. Hakika huu ni ujasiri na nakupongeza kwa hili na mengine uliyojitolea kwa nchi yetu.

    Mimi, EM

    ReplyDelete