Wednesday, July 8, 2015

Chadema yakutana Dar kwa dharura

KAMATI Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),leo wamekutana Jijini Dar es Salaam kwa dharura kwa ajili ya kujipanga ili kukabiliana na changamoto za kisiasa wanazokabiliana nazo kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu. Anaandika Deusdedit Kahangwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu amesema kwamba kikao hicho ni kwa ajili ya kupokea, kujadili na kutolea mamuzi taarifa kadhaa.

Amesema kuna Taarifa ya Utekelezaji wa Mkakati wa Chadema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015 mpaka sasa, Taarifa ya Zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR nchini, Hali ya Kisiasa huko Zanzibar, Taarifa ya Wabunge Kuhusu Yaliyojiri Bungeni kuhusiana na miswada tata ya gesi na mafuta, na Taarifa nyingine kuhusiana na utendaji wa kazi za kila siku za chama.

Mwalimu amesema Zanzibar watu wanapigwa hovyo wakiwa katika vituo vya kujiandikisha. Serikali ya Mapinduzi ikiulizwa amesema vitendo hivyo vinafanywa na genge wahuni wanaomiliki silaha

Kuhusu zoezi la Kuandikisha wapiga kura nchi nzima, Mwalimu amesema kwamba, kuna taarifa za vurugu kutoka sehemu mbalimbali nchini kote; kwamba magari ya serikali yanasemekana kukosa mafuta na hivyo kushindwa kubeba mashine za BVR katika baadhi ya maeneo.

“Mambo haya yanatokea katika maeneo ambako ni ngome ya Ukawa kisiasa. hivyo kuwa kikao cha leo kitapokea taarifa kamili kutoka kila mkoa na hatimaye kufanya maamuzi stahiki kuhusu zoezi hili.”amesema.

Nae Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, John Mnyika, amesema katika mkutano alipinga vikali taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la serikali ya CCM likidai kwamba wabunge wa ukawa wanakwepa kujadili miswada ya gesi na mafuta kwa kuwa ni vibaraka wa makampuni ya kigeni yaliyowekeza katika sekta hii.

Kwa mujibu wa Mnyika, “wabunge wa CCM wanaoshirikiana na Spika Makinda kupitisha miswada husika kinyemelea ndio wanapaswa kuhesabiwa vibaraka wa wawekezaji hao.” Mnyika aliwaomba waandishi wa habari kutafuta habari za kiuchunguzi kuhusu jambo hili kusudi hatimaye walisaidie taifa kuujua ukweli wote kuhusu ukibaraka huu wa wabunge wa CCM na serikali yao.

Mnyika alitumia nafasi hiyo kutoa msimamo wa Chadema kuhusu hukumu iliyotolewa na Mahakama dhidi ya Aliyekuwa Waziri wa Fedha Basil Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Daniel Yona amesema adhabu ya miaka mitatu waliyopewa ni ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa hasara waliyolisababishia taifa.

Hata hivyo, Mnyika ameipongeza hukumu hiyo kwani imethibitisha tuhuma zilizotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa, mnamo 15 Septemba 2007 huko Mwembeyanga jijini Dar es Salaam, alipowataja mafisadi wakuu 11, wakiwemo Yona na Mramba.

Mnyika alitumia nafasi hiyo kuikumbusha serikali kuendeleza zoezi hili la kuwaburuza mafisadi wote mahakamani bila kujali sura zao. Kwa upekee aliiomba serikali kuwaburuza mahakamani watuhumiwa wote katika sakata la EPA, Escrow, na kashfa nyingine kubwa zilizolikumba taifa hili mpaka sasa.

Hata hivyo viongozi hao wamesema wataweka wazi kwa waandishi wa habari yale yote yatakayojadiliwa katika kikao na maazimio waliyoyaweka baada kumalizika .

No comments:

Post a Comment