Saturday, June 6, 2015

Lema: Wabebeni wagonjwa kujiandikisha daftari la kudumu

Mbunge wa Arusha, Godbless Lema (Chadema) amewataka wakazi wa hapa, kuwabeba wagonjwa na kwenda nao kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni ya kuwahamasisha watu kujiandikisha katika daftari hilo, Lema aliwaomba kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji huo.

“Kila mmoja aende lakini usiende peke yako, mchukue na rafiki yako na hata wagonjwa waliolazwa, wabebeni wakajiandikishe,”alisema.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imepanga kuanza kuandikisha watu kwenye daftari la kudumu la wapiga kura mkoani hapa kesho.

“Habari ya mjini sasa hivi ni kujiandikisha kupiga kura, waamsheni vijana wenu, masela nanyi msiende klabu, nendeni kujiandikisha tuing’oe CCM kwa kura,” alisema.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel Natse, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Karatu, alisema watu waliojitokeza kutangaza nia kupitia CCM hawawezi kuoshwa hata kwa waya za chuma za kuoshea sufuria.
“Hata wakioshwa kwa ‘still wire’ hawawezi kuosheka kwa sababu wote ni wachafu.

“Tazama wanavyoumbuana, mara utasikia huyu ni kibaka, mla rushwa….” Alisema.
Aliwataka wananchi wa Arusha kuanza safari ya uhakika na sio safari ya matumaini.

Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, ambaye pia ni mwenyekiti wa kanda, Amani Golugwa, alisema uchaguzi wa mwaka huu ni wa kurudisha utawala wa Mungu.

Alisema kila mgombea wa Chadema anatakiwa kusema huu ni mwaka wa mwisho kwake kuwa kiongozi wa upinzani baada ya Oktoba 25, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment