Tuesday, June 2, 2015

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI MHE. SUSAN ANSELM JEROME LYIMO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU BAJETI YA WIZARA HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016

Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Aprili, 2013
_______________________
1.   UTANGULIZI
Mheshimiwa spika, napenda kuchukua fursa hii adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia afya njema na kuweza nkusimama hapa kusoma hotuba hii.   Kipekee namshukuru sana Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mhe. Freeman Mbowe kwa kuendelea kuniamini katika kusimamia Wizara hii nyeti kwa maendeleo ya Taifa. Aidha, nawapongeza kwa dhati wenyeviti wenza wa UKAWA; Mhe. Dkt. Emanuel Makaidi wa NLD, Mhe. Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF na Mhe. James Mbatia wa NCCR Mageuzi kwa kazi kubwa sana na nzuri  wanayofanya  ya kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na UKAWA kwa kuwa ndio tumaini pekee  lilobaki la kuwakomboa na ndio njia pekee ya kuiondoa serikali  ya CCM madarakani ifikapo 25/10/2015. Hivyo naomba wananchi wote wanaokerwa na kuporomoka kwa shilingi yetu, ufisadi, rushwa na hali mbaya ya maisha watumie fursa hii ya maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kujitokeza kwa wingi na kuwahi kujiandikisha mapema daftari litakapopita katika maeneo yao kwani ndio njia pekee ya kuiondoa CCM madarakani kidemokrasia.
Mheshimiwa Spika,  napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa wanawake wa Mkoa wa Kinondoni kichama kwa ushirikiano wao, kipekee nawashukuru viongozi wa CHADEMA na wanachama wa Jimbo hilo kwa ushirikiano mnaonipatia katika kutimiza nia na ndoto zangu. Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maisha ya  Bunge hili la  kumi yatafikia ukomo wake hivi karibuni, hii itakuwa ni hotuba yangu ya mwisho kama Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  itakumbukwa kwa kwa jitihada zake za kuikosoa na kuishauri Serikali juu utekelezaji wa majukumu ya Wizara hii kwa lengo na nia nzuri ya kuboresha elimu hapa nchini. Ni imani yangu kwamba niliitumikimia nafasi hii ya Waziri Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa uaminifu na weledi mkubwa. Na ni furaha yangu vilevile kwamba wananchi na wadau wote wa elimu waliridhika  na mchango wa kazi za upinzani katika wizara hii.

Inaendelea.......


2.   SERIKALI YA CCM ILIVYOSHINDWA KUTEKELEZA ILANI YAKE KUHUSU ELIMU
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya awamu ya nne ya  CCM imeshindwa kutekeleza Ilani yake ya Uchaguzi kuhusu Elimu kwa mihula yote miwili ya utawala wake.  Ibara ya 85 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 inasema kwamba: “Serikali itachukua hatua za kuboresha, kuimarisha elimu ya awali hadi ya Chuo Kikuu na kuhakikisha kwamba elimu ya ngazi zote itakayotolewa nchini tangu sasa iwe na ubora utakaowawezesha vijana wetu kuchukua nafasi zao stahiki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla”.

(a)  Elimu ya Awali
Mheshimiwa Spika, Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliwaahidi watanzania kupitia Ilani yake ya uchaguzi kufanya yafuatayo katika Elimu ya Awali endapo kitapewa ridhaa ya kuongoza Serikali.
                    i.            Kuhakikisha kwamba kila shule ya msingi ina darasa la Elimu ya Awali  lenye madawati yanayolingana na hali ya watoto wa elimu hiyo.
                  ii.            Kujenga vyoo kwa ajili ya watoto wa Elimu ya Awali ili wasiingiliane na wale wa shule ya msingi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuwaambia wananchi wote kwamba walitapeliwa na  CCM kwani Serikali ya CCM haikutekeleza ahadi hiyo hata japo kwa asilimia 50. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge wananchi kama imetekeleza ujenzi wa madarasa ya elimu ya awali katika kila shule ya msingi nchini  na kuweka madawati yanayolingana na watoto hao, sambamba na ujenzi wa vyoo vya watoto wa elimu ya awali katika kila shule ya msingi ili wasiingiliane na wale wa shule ya msingi kama ilivyoahidi.


Mheshimiwa Spika, mazingira ya elimu ya awali bado yako duni sana ambapo asilimia kubwa ya watoto bado wanakaa chini. Aidha kumekuwa na ongezeko la matatizo ya kukosa matundu ya vyoo, kukosa chakula jambo linalowafanya watoto kukosa hamasa ya kujifunza kutokana na njaa, na vifaa duni vya kufundishia na kujifunzia.

Mheshimiwa Spika, Uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi kwa elimu ya awali nao umekuwa ni tatizo. Japo lengo la kitaifa ni mwalimu 1 afundishe wanafunzi 25, hali ya uwiano wa kitaifa ni mbaya sana ambapo takwimu za BEST  za mwaka 2013 zinaonesha uwiano hivi sasa ni mwalimu 1 anafundisha wanafunzi 199 na kila mwaka unaongezeka ambapo mwaka 2010 ulikuwa 1:73 ukaendelea kukua na kufikia 1:124 mwaka 2012, na sasa umefika 1:199


(b) Elimu ya Msingi
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha elimu ya msingi, Chama cha Mapinduzi pia kiliwaahidi wananchi kufanya yafuatayo endapo kingepewa ridhaa na wananchi kuongoza Serikali:
                                                 i.            Kuendelea kuyaboresha maslahi ya walimu ili kuhakikisha mishahara itolewayo inazingatia hali halisi ya maisha na soko.
                                               ii.            Kuendelea kuimarisha ukaguzi wa shule na kuhakikisha kila shule inakaguliwa angalau mara moja kwa mwaka na taarifa ya ukaguzi kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, wananchi waliamini, wakaichagua CCM kuongoza dola. Lakini baada ya kushika dola wamesahau kabisa yote waliyoahidi. Wote tunajua madhila yanayowapata walimu wetu.  Kilio chao cha malimbikizo ya mishahara na stahili zao nyingine   ni cha muda mrefu sana. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba hata mishahara ya walimu imekuwa  haifiki kwa wakati. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imebaini kwamba baadhi ya walimu walioajiriwa tarehe 1 Mei, 2015 hawajalipwa fedha yao ya kujikimu (settling in allowance) hadi leo.

Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema walimu ndio nyenzo kuu katika elimu lakini cha ajabu walimu wa Tanzania wamekuwa wakionewa na  kudhalilishwa kila leo.  Mfano Serikali imetoa muundo mpya wa  mishahara ya walimu Julai,  2014 unaojulikana kama TGTS ambapo zaidi ya walimu laki moja (100,000) walipaswa kutoka E kwenda F.  Walimu hawa kwa makisio ya chini wanahitaji zaidi ya bilioni mia moja (100,000,000,000/=) kwa wastani wa nyongeza ya shilingi 100,000/= kwa mwezi.  Kwa mahesabu rahisi kama ni walimu 100,000 x 100,000/= kwa miezi 12 kwani muundo huu umeanza toka Julai, 2014. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuonyesha fedha zilizotengwa kwa ajili ya nyongeza ya mishahara ya walimu katika bajeti hii. Msingi wa hoja hii ni kuepuka mwendelezo wa malimbikizo ya madeni ya walimu ambayo licha ya kuwa kero kwa walimu sasa pia yameanza kutumiwa kama kete ya kisiasa nyakati za chaguzi.  Nathubutu kusema hivyo kwa sababu Rais Kikwete akizungumza na chama cha walimu hivi karibuni alisema kabla hajaondoka madarakani atahakikisha walimu wamelipwa madeni yao kana kwamba hakuyaona madeni hayo tangu 2005 alipoingia madarakani. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali pia kulieleza Bunge hili kama lile deni ambalo Serikali ilisema inalihakiki na kwamba sasa ni bilioni 10 lipwa lini na tengeo lake katika bajeti hii liko wapi? Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua wale walimu zaidi ya 37,000/= waliopandishwa madaraja lakini hawajarekebishiwa mishahara yao watalipwa lini?

Mheshimiwa Spika, kuhusu ukaguzi; ni wazi kuwa bila ukaguzi ubora wa elimu hauwezi kupatikana. Licha ya majigambo na ahadi hewa ya Serikali hii kupitia Ilani ya CCM; kwamba kila shule itakuwa inakaguliwa mara moja kwa mwaka, takwimu za wizara zinaonesha kwamba, ukaguzi wa shule umefikia asilimia 37 tu.  Hii ina maana kwamba zaidi ya asilimia 63 ya shule za Msingi na sekondari hazikukaguliwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM ni ya ajabu sana kwa kuwa imechoka, inajichanganya na imefikia hatua ambayo hata haina kumbukumbu ya mambo iliyowahi kuahidi. Nasema hivi kwa sababu  tarehe 29 Aprili,  2013, Rais Jakaya Kikwete aliwaahidi wananchi kupitia mazungumzo yake na Wakuu na Wamiliki wa Shule za Sekondari binafsi huko Mbeya kwamba “Serikali ingeanzisha Wakala wa Ukaguzi anayejitegemea na kwamba Serikali ingemwezesha Wakala huyo kwa rasilimali fedha /watu na vitendea kazi ili kimarisha utendaji kazi ya ukaguzi na matokeo yake yataonekana kwa muda mfupi”,

Mheshimiwa Spika, jambo hilo halijafanyika, lakini mbaya zaidi ni kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani imesikitishwa sana na utendaji wa serikali hii baada ya ofisi ya Waziri Mkuu kuandika  barua ya kumbukumbu No: CBC/10/348/05/10 ya tarehe 13 Oktoba, 2014 inayositisha agizo la Rais la kuanzisha wakala wa ukaguzi wa shule. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kutoa maelezo juu ya mkanganyiko (confusion) huu ndani ya Serikali kuhusu uanzishwaji wa wakala wa ukaguzi wa shule. Swali la kujiuliza tuna serikali ngapi??

Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia sehemu hii kwa kuwaambia wananchi kwamba, Elimu haijawahi kuwa kipaumbele katika sera za CCM kwa awamu zote nne za utawala wake ndio maana haitekezi hata ilani yake yenyewe .  Sera ambayo CCM imepigia upatu kwa miaka yote 53 ya uhuru na ambayo pia imeshindwa kutekeleza ni Kilimo. Ndio maana tangu enzi za uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere sera zilizosikika ni Siasa ni Kilimo, Kilimo cha Kufa na Kupona , Kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa, na sasa Kilimo Kwanza.  Hatujawahi kusikia Elimu Kwanza kwa utawala wa CCM kwa miaka yote 53 ya uhuru.

Mheshimiwa Spika, Sera ya Elimu Kwanza ni Sera ya Upinani. Ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA ya 2005, na 2010 na imepewa kipaumbele cha kwanza, cha pili na cha tatu.  Na kwa kuwa sasa hivi tupo katika ushirikiano wa UKAWA, sera hii imekuwa ni Sera ya UKAWA. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawaonya wanaotangaza nia ya kugombea Urais wa Tanzania kupitia CCM kuacha kuwawadanganya wananchi kwamba Elimu itakuwa kipaumbele namba moja ikiwa watachaguliwa, kwa kuwa walikuwa Serikalini kwa miaka yote tangu uhuru na wakashindwa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kwamba CHADEMA iliposema elimu itakuwa bure kama ingechaguliwa kuunda Serikali mwaka 2005 na 2010, CCM iliendesha propaganda chafu na kuwapotosha wananchi kwamba haiwezekani kutoa elimu bure. Lakini ili kuthibitisha ile methali isemayo kwamba njia ya mwongo ni fupi, CCM sasa hivi imekubali kula matapishi yake na kusema katika kipengele cha 3.1.5 cha Sera Mpya ya elimu ya mwaka 2014 kwamba Elimu ya Msingi itakuwa bure.   Huu ni uthibitisho kwamba CCM imebobea katika wizi hadi kufikia hatua ya kuiba sera za upinzani waziwazi bila aibu!!! Lakini inathibitisha kwamba Sera za Upinzani zinatekelezeka, na kwa maana hiyo, UKAWA ukitwaa madaraka ya dola katika uchaguzi wa Oktoba, 2015 Elimu ya Msingi mpaka Chuo Kikuu itakuwa BURE KWELI KWELI.


2. SERA  MPYA YA ELIMU 2014
Mheshimiwa Spika, Sera ya Elimu ilizinduliwa kwa mbwembwe nyingi lakini ukiisoma vizuri sera ile ni vituko vitupu.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilidhani kwamba, baada ya Sera ya Elimu ya 1995 kuwa na mapungufu mengi yaliyopelekea mambo mengi kuharibika basi ingekuwa somo tosha kwa maboresho ya sera hii, lakini   kwa masikitiko makubwa sera hii imekuwa ni ya  matamko tu.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunashindwa kutekeleza sera zetu kwa kuwa zimekuwa ni sera bainishi (substantive policies) na hivyo kubainisha mapungufu tu  na kuacha sehemu ya pili ya utekelezaji. Hivyo kilichobainishwa kinashindikana kutekelza kwa kuwa nyenzo za utekelezaji haziwekewi mkazo. Kimsingi,  ili sera hii itekelezeke ni lazima  iwe na ngazi hizi mbili yaani sera bainishi na sera namna. Sera nyingi hapa nchini zimekuwa  dhaifu na kutokutekelezwa  kwa kukosa ngazi ya pili yaani sera namna.

Mheshimiwa Spika,   Ili sera hii ya elimu iweze kutekelezeka inahitaji kutafutiwa ufumbuzi wa mambo matatu la sivyo hakutakuwa na jipya. Mambo hayo ni pamoja na walimu bora, zana bora za kufundishia, na walimu wenye motisha. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili imetenga fedha kiasi gani katika bajeti hii kwa ajili ya zana bora za kufundishia na motisha kwa walimu ili kurahisisha utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu?

Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa inasifika sana kwa kuandika vizuri sera zake lakini utekelezaji wake ni Shiidaa!!!  Mfano sera hii haielezi ni kwa kiasi gani itaondoa ubaguzi au matabaka ya elimu hasa viwango vya elimu.  Aidha, haielezi nini maana ya kufuta ada ikiwa kuna michango ni mingi kuliko ada yenyewe.

Mheshimiwa Spika,  Sera ya Elimu inasema serikali itahakikisha  kuwa elimu ya msingi  katika mfumo wa umma inatolewa bila ada. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulithibitisha Bunge hili kama elimu bila ada itaanza kutolewa kwa mwaka wa fedha 2015/16, au tamko hili la sera lilikuwa ni la kisiasa kwa ajili ya kuendelea kuwahadaa watanzania?

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatiaka Serikali kutoa majibu kwa swali hili kwa sababu asa hivi wazazi wengi wana mkanganyiko wa suala hili   kwa kuwa  wanafahamu kuwa kwa kuwa sera hii  imezinduliwa mwezi Februari 2015 na matarajio yao ni kwamba utekelezaji wa elimu bure utaanza mwaka wa fedha 2015/2016.

Mheshimiwa Spika, Katika kujibu hoja hii, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka  serikali ikumbuke kuwa changamoto kubwa za mazingira ya kufundishia na kujifunzia zinatokana na ufinyu wa bajeti na pia serikali kutotoa fedha za kutosha shuleni. Mathalani  katika utekelezaji wa MMEM I na MMEM II ni wastani wa shilingi 5,000  hadi shilingi 6,000  kati ya shilingi 10,000 kwa kila mwanafunzi ndio zilitolewa na serikali na hata katika MMEM III bado serikali imeshindwa kutoa fedha hizi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2014/2015 serikali imetoa wastani Shilingi 860 tu,  kwa kila mwanafunzi badala ya shilingi  10,000.  Kambi Raasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ni kwa kiwango gani changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi katika bajeti ya 2015/2016 au ndio kusema Bussiness as Ussual.

3.   SHULE BINAFSI
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko mengi sana kuhusu gharama za shule za binafsi kuwa kubwa mno kiasi kwamba ni wananchi wachache wanaweza kuwalipia watoto wao ada na gharama nyingine katika shule hizo.  Na kwa kuwa shule hizo zinatoza ada kubwa zinakuwa na uwezo wa kuwapa motisha walimu na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunza hivyo kuonekana kwamba zinatoa elimu bora kuliko zile za Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo hili limeleta matabaka katika utoaji wa elimu kwani sasa inaonekana kwamba shule za Serikali ni kwa ajili ya watu masikini na shule binafsi ni kwa ajili ya watoto wa matajiri. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili imefanya jitihada gani katika kuwianisha gharama za elimu kati ya shule binafsi na shule za Serikali ili kuondoa matabaka katika utoaji wa elimu? Kwa kuwa wenye shule binafsi wanadai gharama zao ziko chini kama tutaangalia Student’s Unit Costs. Je pamoja na malalamiko hayo ni kwa nini serikali haijafanya utafiti kujua kama hili ni kweli Ili wananchi wajue gharama halisi za elimu? .

4.   SERIKALI YA CCM ILIVYOSHINDWA KUWAPATIA WANAFUNZI MADAWATI MASHULENI TANGU UHURU

Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha na ni aibu kwa Serikali hii ya CCM inayojigamba kuwa imeleta maendeleo kushindwa kuwapatia wanafunzi madawati licha ya utajiri wa rasilimali za misitu tulizo nazo, na licha ya ujuzi na nguvu kazi iliyopo katika magereza yetu ambapo wafungwa na mahabusi wangeweza kutumika kutengeneza madawati hayo.

 Mheshimiwa Spika, ni aibu kubwa kwa Serikali hii ya CCM kujigamba katika Sera Mpya ya Elimu  na Waziri Mkuu kujibu swali hapa Bungeni na kukazia kwamba wanafunzi wa shule za msingi watapatiwa Kompyuta Mpakato (Laptops) ilhali sehemu kubwa ya watoto wetu bado  wanakaa chini na wengine wanakalia mawe kama nyani kwa miaka 54 sasa ya uhuru. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapata tabu kuelewa kama Serikali hii imechanganyikiwa au iko serious kwamba itawapa kompyuta wanafunzi wambao hawana pa kukaa shuleni na shule hizo hazina umeme. 

Mheshimiwa Spika,   wenzetu wa Kenya na Rwanda wameweza kuwapa watoto wao kompyuta mpakato (Laptops). Katika bajeti ya elimu - Kenya toka 2013 walitoa laptops kwa wanafunzi wote wa shule za msingi lakini hapa kwetu  ni porojo tu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuonesha bajeti ya kununua laptops kwa wanafunzi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu na ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu akijibu swali hapa Bungeni kwamba wanafunzi wote wa shule za Msingi watapatiwa kompyuta mpakato.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji, hivi Kamati Kuu ya CCM iliyokaa zaidi ya mara 212 (x4 kila mwaka) ukiacha vile vikao vya dharura kwa miaka yote 53 na nusu ya uhuru huwa inajadili nini ikiwa hali ya upatikanaji wa madawati ni tete kiasi hiki huku magogo yetu yakiuzwa China na kwingineko? Kambi Rasmi ya Upinzani imeshawishika kuamini kwamba Serikali hii ya CCM si kwamba imechoka tu bali pia imefikia ukomo wa kufikiri na kwa maana hiyo kuiruhusu kuendelea kutawala ni kuruhusu anguko kuu la nchi au waswahili wanasema ni janga la Taifa na  ni shiiida.


5.   ELIMU YA UALIMU
Mheshimiwa Spika, Elimu ni mwalimu, kwani unaweza kuwa na madarasa mazuri sana, maabara ya viwango vya juu lakini bila mwalimu mwenye motisha na aliyepewa mafunzo vizuri hakuna chochote tutakachofanikiwa. Elimu ni sawa na kiwanda ambapo mwanafunzi ni malighafi, walimu na vitabu ndio mashine za uchakataji na usindikaji.  Hivyo kama ilivyo kwa malighafi inapopita kwenye mashine tunachopata ni kitu kipya kama pamba kuwa nguo. n.k.  Hivyo mtoto anaingia hajui chochote lakini anategemewa atoke amebadilika kwa kujua kusoma, kuandika na kubwa zaidi kujitambua na   kujua kuchambua mambo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili kama Elimu ya Ualimu inayotolewa ina ubora wa kutosha  kwa kuwa mwalimu bora ndiye anayegemewa katika kuwafundisha watoto wetu

Mheshimiwa spika. Kulingana na mtaala wa mafunzo ya ualimu, mafunzo kwa vitendo kwa walimu (Block Teaching Practice) yanapaswa kutolewa kwa wiki 8 kila mwaka wa masomo.  Kwa miaka miwili 2013/14 na 2014/15 mafunzo yametolewa kwa wiki 2 tu yaani wiki 4 badala ya wiki 16. Kupunguza muda wa mafunzo kwa vitendo kunapunguza pia weledi na uwezo wa mwalimu husika. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili sababu za kupunguza muda wa mafunzo kwa vitendo na athari zitakazotokana na muda huo kupunguzwa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia inahoji, Serikali inategemea kuwapata walimu wa kiwango gani cha weledi ikiwa inapunguza muda wao wa mafunzo?

Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu kwa kutambua umuhimu na ubora wa waalimu lilipitisha bajeti ya shilingi 7,210,370,000/= (2014/2015). Serikali kwa kutothamini fani hii ilipunguza kiasi hicho kwa shilingi 5,165 006, 020, sawa na 72%, hii ina maana kwamba fani ya Elimu ya Ualimu wamepata shilingi bilioni 2 tu sawa na asilimia 28% ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa mwaka huo hadi April 2015.

Mheshimiwa Spika, inasikitisha na inatia hasira kusikia kwamba Serikali inasema mkakati Iliyo nao ili kuhakikisha walimu hawa waliokosa mafunzo kwa vitendo, “watakuwa chini ya uangalizi wa wakaguzi wa shule kwa kipindi cha  mwaka mmoja pindi watakapoajiriwa ili kupata muda wa kutosha wa mazoezi ya ufundishaji” Kambi Rasmi ya Upinzani inaihoji Serikali itatekeleza vipi mpango huo wa ukaguzi na kwa bajeti ipi ikiwa ukaguzi uliofanyika ni asilimia 30 tu?


6.   ELIMU YA JUU
Mheshimiwa Spika, elimu ya juu ndio inayomfunza kijana jinsi ya kuchambua mambo na kujenga weledi katika fani mbalimbali.  Mwl. Nyerere, katika kitabu chake cha Uhuru na Maendeleo,  alisema:  “Intellectuals have a special contribution to make to the development of our nation,  and their knowledge and greater understanding that they should posess,  should be used for the benefit of the society of which we are all members”

Mheshimiwa Spika, Kinyume na maneno ya Hayati Baba wa Taifa, mchango wa wasomi wetu katika maendeleo ya jamii na taifa kwa jumla umewekewa vikwazo na mfumo wa utawala wa Serikali hii ya CCM. Wasomi wenye elimu ya juu kokosa ajira limekuwa ni jambo la kawaida, na wasomi pia  kukosa fursa na mazingira bora ya kujiajiri nayo ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kueleza imewasaidiaje wahitimu wa elimu ya juu kama vile wahandisi, kilimo, wanasheria, katika kuanzisha Kampuni zao za uhandisi, Kampuni za huduma za kisheria (Law firms), Kampuni za ushauri nasaha kwa waliohitimu fani za Saikolojia nk. Nauliza hivi kwa sababu kodi za wananchi zimetumika kuwasomesha wahitimu hao lakini mwisho wa siku wanabaki mitaani bila tija yoyote. Hii inamaana kwamba Taifa limeingia hasara kuwasomesha watu ambao hatimaye hawana mchango wowote katika uchumi wa nchi na badala yake wanakuwa tegemezi na kuongeza kiwango cha umasikini nchini. Na haya yote yamesababishwa na mitaala mibovu ya elimu ambayo imeshindwa kuwajengea uwezo wa kujiajiri pale wanapokosa ajira za moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili, nchi hii inafuata falsafa gani ya elimu kwa sasa? What is our current education philosophy?  Nauliza hivi, Mhe. Spika, kwa sababu wakati wa utawala wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nchi hii ilikuwa ikifuata falsafa ya “Elimu ya Kujitegemea” yani Education for Self Reliance, ambapo msingi wa elimu ulikuwa ni kumwezesha aliyenufaika na elimu kujiajiri katika sekta mbalimbali za uzalishaji mali. Lakini kwa hali ilivyo sasa, elimu yetu haionekani kuwa na msingi wa kumsaidia mhitimu kujiajiri. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama ile falsafa ya elimu ya kujitemea imefutwa, na kama imefutwa sasa hivi taifa lina falsafa gani ya elimu au tupo tupo tu?.


7.   MATATIZO YA ELIMU YA JUU
Mheshimiwa Spika, elimu katika ngazi zote nchini imepanuka kwa kasi isiyozingatia ubora. Hii inadhihirishwa na utafiti uliofanywa na The Global competitiveness Index (GCI) mwaka  2013/14  kuangalia ubora wa vyuo vikuu kwa nchi 148 duniani. Matokeo yanaonesha Kenya ikishika nafasi ya 44, Uganda ya 82,    huku Tanzania ikishika nafasi ya 100. 

Mheshimiwa Spika, pamoja na tafiti kuonyesha Tanzania tulivyo nyuma katika ubora wa elimu ya Juu, sasa hivi kumezuka tatizo kubwa la utofauti wa mitaala ya Vyuo Vikuu hususan vile vya binafsi hali inayopelekea migomo na sintofahamu miongoni mwa wanafunzi. Mfano mzuri ni vyuo vya St. Joseph na Kampala International University (KIU). Kwa muda mrefu tatizo hili limefikishwa kwa wahusika na bado ufumbuzi wa kina haujajulikana.  Tunaitaka serikali itueleze uswahiba uliopo kati yake na Vyuo hivi.  Na ni kwa nini wanafunzi wakitanzania wateseke kwa manufaa ya wamiliki?

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hapo awali, kumekuwa na tofauti kubwa ya mitaala ya Elimu ya juu kati ya vyuo vya elimu ya juu vya Serikali na vyuo binafsi. Tofauti hii kubwa kwa upande mmoja  imesababishwa na kuongezeka  kwa kasi kwa vyuo vya Elimu ya juu nchini kutokana na ongezeko la watu wanaohitaji elimu lakini kwa upande mwingine tofauti hii imesababishwa na ukweli kwamba elimu hasa kwa vyuo binafsi inatolewa kibiashara zaidi kuliko huduma. Kutokana na hali hii ya vyuo vya elimu ya juu (hasa vya binafsi) kuwa katika mkakati wa kufanya biashara zaidi kuliko kutoa huduma ya elimu, imesababisha baadhi ya vyuo kuongeza muda wa programu zake kutoka miaka minne hadi minne na miezi sita, na miaka  hadi mitano na miezi sita bila kuzingatia utaratibu wa bodi ya mikopo. Tunataka serikali itueleze hili ongezeko la miezi sita litagharamiwa na  nani huku wataalamu wa bodi wakidai kutotambua muda huo wa nyongeza?.

Mheshimiwa Spika, hali hii imesababisha pia baadhi ya vyuo kujitengenezea mitaala yake kwa lengo la kuwavutia wanafunzi kwa kile kinachoitwa “bridging courses”na hivyo kutanua wigo wa  kujipatia faida zaidi bila kuzingatia ubora wa elimu inayotolewa na bila kujali namna elimu iliyotolewa inavyoendana na mazingira ya nchi yetu. Kutokana na hali hii, vijana wengi wanaohitimu ngazi mbalimbali katika elimu ya juu wamekuwa wakishindwa kuingia katika soko la ajira kwa kuwa masomo waliyofundishwa hayaendani na mahitaji halisi ya soko la ajira; Mfano ni wahitimu wa Astashahada ya famasi ya Kampala International University.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa  kumekuwa na utofauti mkubwa wa mitaala katika vyuo vya elimu ya juu jambo linalosababisha  kukosekana kwa ubora  linganifu  wa elimu ya juu katika ngazi mbalimbali; na kwa kuwa  kukosekana kwa ubora linganifu wa elimu ya juu unaozingatia mazingira ya nchi yetu kumesababisha vijana wengi wanaohitimu elimu ya juu katika ngazi mbalimbali kukosa sifa za ushindani katika katika soko la ajira na hivyo kukosa fursa mbalimbali za ajira; na kwa kuwa udhaifu wa mitaala katika elimu ya juu umesababisha mara kadhaa migogoro kati ya wanafunzi na watawala wa vyuo husika na hivyo kusababisha baadhi ya wanafunzi kusimamishwa masomo na kufukuzwa kabisa; na kwa kuwa Tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza ubora wa elimu hapa nchini zilibaini kuwa elimu ya Tanzania imekuwa ikiporomoka mwaka hadi mwaka; na kwa kuwa  kati ya sababu zilizotajwa za kuporomoka kwa elimu ni kukosekana kwa mitaala thabiti inayoeleweka na inayozingatia ubora wa elimu katika mazingira mahalia; na kwa kuwa Tume ya Elimu ya Juu (TCU) ina mamlaka ya kuratibu na kusimamia  mitaala ya vyuo vya Elimu ya Juu;
HIVY0 BASI, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kufanya yafuatayo:
                                i.             Kuiagiza Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kutoa ndani ya kipindi cha siku sitini, mwongozo mpya kwa vyuo vya elimu juu nchini kuhusu ya vigezo vya kuzingatia wakati wa kuandaa mitaala ya elimu ya juu.
                              ii.            Kuvifungia mara moja vyuo vyote vya Elimu ya Juu  vinavyoendeshwa kwa maslahi ya kibiashara zaidi bila kuzingatia mitaala na ubora wa elimu mpaka hapo vitakapojirekebisha;
                            iii.            Kuiagiza Tume ya Vyuo vikuu nchini (TCU) kusitisha mara moja kutoa ithibati kwa vyuo vya Elimu ya Juu ambavyo vitakuwa havina mitaala iliyozingatia vigezo vitakavyowekwa na Tume ya Elimu ya Juu.
                          iv.            Kuhakikisha muda wa Provisional Accredation ni wa kipindi cha mwaka mmoja tu ili kuondoa athari kwa wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuleza ni kwa nini Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) ilitoa ithibati kwa Chuo Kikuu cha Kampala International University huku wakijua baadhi ya program hazijasajiliwa na Board mbalimbali kama ile ya Pharmacy hivyo kusababisha hasara kwa Chuo na wanafunzi? Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa majibu kwa maswali yafuatayo:
                                i.            Ni kwa nini baadhi ya program zinazofanana mfano Medical Laboratory na Pharamacy kwa Chuo Kikuu cha Kampala Internationa University (KIU)  zitofautiane kwa kiasi kikubwa hivyo na Vyuo Vikuu vingine kama Muhimbili, KCMC nk?  Mfano wakati KIU wana kozi 14 wenzao wana 7 – 8 tu?
                              ii.            Ni kwanini TCU na Wizara wanapopata taarifa za matatizo haya hawajali na kuacha jambo hilo liote mizizi na kuleta athari kubwa kama ilivyotokea  KIU, St. Joseph na IMTU?
                            iii.            Ni kwa nini inapotokea tatizo na kuonyesha wazi Serikali ndio yenye makosa wanafunzi ndio wanakuwa wahanga badala ya Serikali kuwajibika?

8. BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU
Mheshimiwa Spika, tangu sheria ya Bodi ya Mikopo kuanzishwa, bado kumekuwa na changamoto nyingi kuhusu mikopo ya elimu ya juu hadi Rais  alipoteua Tume chini ya Prof.  Maboko Makenya kushughulikia matatizo ya mikopo ya Elimu ya Juu.  Kinachotushangaza ni kwamba ripoti ya Tume hiyo haijawekwa hadharani na bado matatizo ya mikopo kwa wananafunzi wa elimu ya juu yako pale pale. Wanafunzi wengi hawapati fedha kwa wakati hali inayoleta adha kubwa kwa wanafunzi kwani wengi wao wanatoka kwenye familia duni. Kwa mfano wanafunzi wanaosoma kozi ya ualimu katika Chuo Kikuu cha  St. Joseph,  hawajalipwa fedha zao za mkopo tangu mwezi Machi 2015  jambo linalowafanya waishi maisha ya dhiki na hivyo kushindwa kusoma. Kinachoshangaza ni kwamba wenzao wa Uhandisi wamelipwa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza ni kwa nini inatoa mikopo kwa ubaguzi?   Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo ni kwa nini Chuo cha St. Joseph kiliwafukuza  wanafunzi hao waliokosa mikopo na kuvumilia zaidi ya siku 50, na ni nini hatima ya wanafunzi hao?

Mheshimiwa Spika, kuhusu urejeshwaji wa mikopo ya elimu ya juu, imebainika kwamba urejeshaji ni mdogo sana kwa kuwa hakuna mfumo mzuri unaoratibu zoezi la ukopeshaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu. Kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikishauri kazi hiyo kufanywa na mabenki yetu lakini mpaka sasa ushauri huo haujatekelezwa.  Tunaitaka Serikali kulieleza bunge hili kama Bodi ya Mikopo ina wataalamu wa mikopo kwa ajili ya kazi hiyo. Ili kuyapatia ufumbuzi matatizo ya mikopo ya elimu ya juu, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka vilevile Serikali kutoa ripoti ya tume ya Profesa Maboko ambayo ilipewa jukumu la kutafuta vyanzo vya matatizo na kupendekeza namna ya kukabiliana na matatizo ya mikopo ya elimu ya juu.

Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa tumeshauri mara kadhaa kuhusu matatizo ya mfumo wa mikopo ya elimu ya Juu na kupuuzwa. Serikali Mpya ya UKAWA italipa kipaumbele suala la mikopo ya elimu ya juu kwa kutambua kwamba mikopo ni haki ya wanafunzi na bila mikopo hiyo hawataweza i kusoma kwa utulivu na kuzifikia ndoto zao.

Mheshimiwa Spika, Kama Serikali  haitaki ushauri wa UKAWA basi basi walau ijifunze kutoka nchi jirani ya Rwanda  inavyofanya kuhusu mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza yafuatayo:
        i.            Ni kwanini haitoi fedha ya mikopo hadi wanafunzi wagome na kuandamana?
      ii.             Ni wapi fedha hizo zinakwenda hasa ukizingatia 100% ni za ndani?
    iii.             Ni kwa nini ndani ya masaa 12 tu ya mgomo wa UDSM 19/5/2015 fedha zikatoka?  Au ni sera ya CCM kuwajengea wanafunzi tabia ya kupata haki zao kwa migomo na baadaye kusema ni UKAWA wanachochea migomo vyuoni?




9.   UWEKEZAJI KATIKA ELIMU NA MPANGO  MATOKEO MAKUBWA SASA (BRN).
Mheshimiwa Spika, Takwimu mbalimbali za ripoti ya utekelezaji wa BRN ya Presidential Delivery Bureau na Jarida la HakiElimu la hali ya utekelezaji wa BRN zinaonesha kuwa mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa BRN ulikuwa na changamoto nyingi za kiutekelezaji na mambo mengi yanayohusiana na fedha hayakutekelezwa. BRN ya Elimu ilibaninisha wazi kutoa ruzuku ya asilimia 100 yaani shilingi 10,000/=  kwa kila mwanafunzi shule za msingi na shilingi 25,000/=  kwa shule za sekondari lakini utekelezaji umekuwa kwa asilimia 42 tu  kwa msingi na asilimia 48 tu kwa sekondari.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miundombinu haukutekelezeka pia ambapo kati ya shule 792 zilizopangwa kufanyiwa ukarabati hadi ifikapo mwezi March 2014, ni shule 56 tu zimekarabatiwa. Lengo la utoaji mafunzo ya usimamizi kwa walimu wakuu halikutekelezwa ipasavyo ambapo kati ya walimu 19,035 waliotarajiwa kupata mafunzo ifikapo September 2013, ni walimu 3,469 tu sawa na asilimia 18 ndio wameshapatiwa mafunzo.

Mheshimiwa Spika, dhamira ya BRN kutatua mgogoro wa walimu na kufanya walimu wafundishe ipasanyo ilikuwa ni nzuri hasa kwa kutoa motisha kwa walimu na kulipa madeni ya walimu. Wakati BRN inaanza asilimia 53 ya walimu walikuwa hawapo darasani yaani hawafundishi. Utafiti wa Shirika la Twaweza kwenye kijarida namba 13 cha mwaka 2014 unaonesha kuwa hivi sasa ni asilimia 34 tu ya walimu ndio wanaingia na kufundisha muda wote wa kipindi na idadi iliyobaki ama wanaingia kwa muda mfupi tu au hawaingii kabisa. Kwa takwimu hizi za utekelezaji,  Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni  inauliza:  ni mambo gani yaliyofanya sekta ya elimu hadi kuipatia sekta hiyo alama 81 katika utekelezaji ilihali katika malengo yote ya BRN ya elimu hakuna hata lengo moja ambalo limetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 20? .

Mheshimiwa Spika, ni wazi Serikali haijawekeza vya kutosha katika elimu. Hii inadhihirishwa na bajeti zetu.  Kwa mfano mwaka 2014/15 Kenya ilitenga sh Bilioni 294.6 sawa na asilimia 27.3% ya bajeti yake kwenye elimu huku Tanzania ikitenga shilingi 3.46 bilioni sawa na asilimia 17 ya bajeti kuu kwenye elimu.  Lakini ieleweke hata hizo zilizotengwa ni asilimia kidogo zilizokwenda kwa wastani wa 50 au chini hadi Machi 2015.  Lakini takwimu zinaonesha kuwa katika nchi za Afrika Mashariki Kenya imetumia 7.8% ya GDP katika  elimu huku Tanzania ikitoa 1.49 % ya GDP, Uganda 5.8% na Rwanda 4.8%.  Haiwezekani usiwekeze halafu utegemee mavuno mazuri.  Ni sawa na mimea inahitaji kuwekwa mbolea na kupaliliwa na hata kumwagiliwa.  Ni jambo linalosikitisha kuona watoto wakikaa darasani kwa miaka saba na kutoka bila chochote.  Watoto hawapati chakula shuleni jambo linalowafanya watoroke shule Jirani zetu Kenya toka 2013 walianza program ya kula shuleni ambayo  kimsingi ni motisha hasa kwa watoto wa familia maskini.

Mheshimiwa Spika, Jambo linalochekesha ni pale Serikali hii ya CCM inapotamba kuwa elimu imefanikiwa kwa 81% katika mpango wa matokeo makubwa sasa.  Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu atajiuliza ni uwekezwaji gani umefanyika hadi tukapata matokeo haya.  Je walimu ambao ndio watendaji wakuu wamefanyiwa nini?  Je maslahi yao, motisha na mazingira yao yameboreshwa?  Ni jambo la kusikitisha kuona uwekezaji ukipungua lakini matokeo yakiwa mazuri zaidi.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji;  “kuna miujiza gani kama si  mbinu chafu na za ujanja ujanja kama tuliovyosema mwaka juzi?  Ukweli kilichofanyika ni kubadili alama na madaraja jambo ambalo  kimsingi ni mbinu chafu na hauoneshi  uhalisia wa uwezo wa mtoto.  Ieleweke kuwa Tanzania sio kisiwa na kwamba ukosefu wa ajira unachangiwa na ubovu wa wahitimu wetu kutokana na mfumo wetu wa elimu na hasa mfumo mpya wa madaraja na alama.

 Mheshimiwa Spika Ni lazima tuelewe kila mtoto wa kitanzania anahitaji elimu bora kwani elimu ni kwa ajili ya kujikomboa na kujibadili (liberation and transformation). Ni vibaya sana kuwajaza watoto wa maskini kwenye shule za viwango vya chini.  Kama Mwalimu Nyerere alivyosema mwaka mmoja kabla ya  kifo chake (5/3 1998)  akiwa Open University “Not all of us will have the same concept of community, but all of us have a need to belong ….. nobody is asking us to love others more than we love ourselves but those of us who have been lucky enough to receive a good education have a duty also to help to improve the well being of the community to which we belong, is part of loving ourselves”

Mheshimiwa Spika, ni kwa kiasi gani wasomi wa nchi hii na wenye  madaraka mnapenda watoto wa watanzania kupata elimu bora? Au sisi wenyewe watoto wetu wako nje ya nchi? Je tunaboreshaje  jamii/elimu yetu  kwa kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya kupendana? Tumeshindwa kwa kuwa tunashuhudia wasomi wetu waliopata elimu bora wamekuwa chanzo cha kuharibu elimu yetu kwa kuruhusu akili ndogo kutawala akili kubwa. Haiwezekani Profesa aliyepewa kuongoza sekta ya elimu ashindwe kutoa ushauri kuhusu uboreshwaji wa elimu. Inawezekanaje maprofesa wasajili/ watoe ithibati kwa vyuo vikuu vyenye maabara yenye kiwango cha shule za kata? Mnategemea wahitimu wa vyuo  hivi waajiriwe wapi? 

10.               UCHAMBUZI WA BAJETI
Mheshimiwa Spika, pamoja na bajeti ya sekta nzima kuendelea kuongezeka kutoka Trilioni 3.46 mwaka  2014/15 hadi trilioni 3.88, sawa na takribani asilimia 10 tu ya fedha iliyopangwa mwaka jana, si ongezeko linaloweza kuleta mabadiliko yanayoonekana katika sekta ya elimu. Tunasema hivi kwa kuzingatia kuwa thamani ya shilingi imeshuka na mfumuko wa bei umeongezeka. Inawezekana ongezeko hili ni matokeo ya urekebishaji mfumuko wa bei badala ya ongezeko halisi katika matumizi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo uchambuzi unaonesha kuwa bado kiwango cha fedha za bajeti ya sekta kinachopangwa ni asilimia kati ya 15 – 17 cha bajeti nzima ya serikali. Tanzania hatujaweza  hata kufikia kiwango kilichokubaliwa cha azimio la Darkar Senegal chini ya EFA, cha kuwekeza hadi walau aslimia 20 ya bajeti ya taifa katika elimu. Wakati tunaamini kuwa kiwango cha asilimia 17 si kibaya, lakini ni muhimu kujua kuwa bado Tanzania inawekeza asilimia kati ya 10-11 tu ya bajeti ya sekta ya elimu kwenye miradi ya maendeleo ukilinganisha na majirani zetu Kenya, Rwanda, na Uganda ambao wamefikia walau asilimia 20 -25.

Mheshimiwa Spika, ni wazi sekta ya elimu imeendelea kupewa kipaumbele kwa maana ya kuwa sekta inayopokea fungu kubwa zaidi la bajeti ya serikali. Wakati ikipangiwa trilioni 3.46 mwaka jana sekta ya miundombinu ambayo ilifuatia ilipokea takribani trilioni 2.3 wakati mwaka huu sekta ya elimu imepangiwa trillion 3.88 wizara inayofuatia ambayo ni miundombinu imeshuka zaidi hadi takribani Trilion 1.9.

Hatahivyo bado kuna mapungufu makubwa ambayo inabidi yafanyiwe kazi;

Ø Kiwango cha fedha zinazokwenda kwenye matumizi ya kawaida bado ni kubwa sana kuliko kinachokwenda kwenye matumizi ya maendeleo ambayo ni muhimu zaidi. Mathalani katika makadirio ya Trilioni 3.88 yanayopendekezwa mwaka huu wa fedha kwenye sekta ya elimu, 84% zimeelekezwa katika matumizi ya kawaida huku asilimia 16 pekee (bilioni 604) ndizo zinaombwa kwaajili ya maendeleo. Pia kati ya Tsh bil 604 zilizopangwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo asilimia 50 ya fedha hizi zimepangwa kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na hivyo fedha zinazobaki kwa ajili ya miradi halisi ya maendeleo ni ndogo sana kulingana na changamoto zinazokabili sekta ya elimu hasa elimu ya msingi na sekondari. Tunatoa rai kwa Wizara kuongeza fedha zaidi kwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali za mitaa.

Ø Tunatambua, Wizara ya Elimu imegatua madaraka na sasa hivi shughuli nyingi za elimu ya msingi na sekondari zinatekelezwa na serikali za mitaa na Wizara ya Elimu imebaki na jukumu la ushauri, utengenezaji wa sera na ufuatiliaji wa utekelezaji wa sera. Cha kushangaza katika makadirio ya bajeti ya maendeleo ya sekta ya Elimu, kati ya Sh billion 604 zilizopangwa, sh bilioni 478.7(asilimia 79) zimepangwa wizara ya ya Elimu na Tsh bilioni 126 tu ndio zimepangwa serikali za mitaa. Swali la kuuliza inakuwaje tunapanga fedha nyingi kwenye kazi za ushauri,utungaji wa sera na ufuatiliaji na kupanga fedha kiasi kidogo kwenye serikali za mitaa ambazo ndio zinatekeleza shughuli nyingi za maendeleo? Unawezaje kutatua changamoto za miundombinu elimu ya msingi na sekondari kwa kupanga shilingi  bilioni 126 tu.

Ø Changamoto nyingine ambayo imekuwapo na imeendelea kujitokeza katika bajeti ya mwaka huu, ni utegemezi wa bajeti ya maendeleo kwa wahisani. Uchambuzi unaonesha bado takribani aslimia 50% ya bajeti ya maendeleo sekta ya elimu inatarajiwa kutoka kwa wahisani. 

Ø Changamoto ya mwisho ambayo ni lazima tuiseme, ni kutokuwepo kwa uwiano kati ya bajeti inayopangwa, fedha ambazo hutolewa na hazina au wahisani na kiwango ambacho hasa kinatumika katika utekelezaji wa mipango na bajeti. Kwa miaka mingi wizara, halmashauri na taasiasi zimekuwa zikitekeleza bajeti pungufu kutokana na kutopatiwa kiwango sahihi kilichopangwa katika bajeti, na hata kinachotolewa hakitolewi kwa wakati. Hivyo wakati mijadala ikiendelea juu ya elimu ni muhimu serikali ifikirie upya suala hili na ikiwezekana kupunguza kiwango cha bajeti kama utekelezaji utaonekana kuwa na shida. Uchambuzi wa shirika la HakiElimu unaonesha kuwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, matumizi halisi ya bajeti ya maendeleo ya wizara imekuwa asilimia kati ya 50-65 tu ya bajeti iliyopangwa.Na hii ndio imekuwa sababu kuu kwa miradi mingi kudorora na kusababisha sekta ya elimu kubaki na changamoto nyingi na mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

11.               HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, hakuna nchi yoyote iliyoendelea hapa duniani bila kuwekeza kwenye elimu. Malaysia inajivunia maendeleo yake kwa kuwa iliwekeza kwa vitendo katika elimu.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuwaarifu  wananchi wote kwamba, kwa kuwa Serikali hii ya CCM haina nia ya dhati ya kuboresha elimu yetu kutokana na kushindwa hata kutekeleza ilani yake kuhusu elimu, Serikali ya Mpya ya  UKAWA itakayoingia madarakni baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015  itayashughulikia matatizo yafuatayo katika sekta ya elimu na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu:

                                            i.            Kutokuwa na malengo yakinishi ya kielimu ya jumla na katika ngazi mbalimbali
                                          ii.            Uhafifu na uduni wa elimu inayotolewa katika ngazi mbalimbali, na hasa katika ngazi ya msingi na sekondari yanayodhihirishwa na:
                                        iii.            Kuongezeka kwa idadi ya watu wasiojua 3K (kusoma, kuandika na kuhesabu)
                                       iv.            Uduni wa shule za sekondari: ni asilimia nne tu ya shule za sekondari nchini ndizo zinazokidhi vigezo vya chini kabisa vya hadhi ya sekondari-hizi takribani shule 160 tu kati ya shule za sekondari zaidi ya 4000 zilizopo nchini.
                                         v.            Uduni wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi mbalimbali za elimu.
                                       vi.            Walimu wasio na motisha na kada ya ualimu kutelekezwa kwa ujumla
                                     vii.            Kutokuwa na uwiano kati ya walichojifunza wahitimu na kinachoendelea katika ulimwengu wa kazi, kutokana na udhaifu wa mitaala na ufundishaji. Matokeo yake: Wahitimu wetu walio wengi hawaajiriki wala hawawezi kujiajiri.
                                   viii.            Kutokuwa na mfumo thabiti kuhusu ugharamiaji wa elimu, na hasa elimu ya juu
                                        ix.            Usimamizi dhaifu wa elimu inayotolewa na taasisi zinazomilikiwa na watu na mashirika yasiyo ya kiserikali au ya umma. Matokeo yake: tuna mifumo zaidi ya mmoja katika nchi moja
                                          x.            Kutokupewa kipau umbele kwa elimu ya awali (miaka 3-6) ambayo ndiyo msingi wa kujifunza katika ngazi za baadaye
                                        xi.            Mkanganyiko wa lugha ya elimu (kufundishia na kujifunzia).


 Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, na watanzania wote wanaopenda kuona taifa letu likisonga mbele kwa kasi ya kumwondoa adui ujinga  jambo lililoshindwa kutekelezwa na Serikali ya CCM, ni UKAWA tu wanaoweza kubadili hali hii kwa kuboresha mfumo wa elimu na kuwekeza kwa vitendo katika elimu, naomba kuwasilisha.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nawatakia wabunge wote kila la heri wanapoelekea uraiani baada ya bunge hili kuvunjwa, lakini pia nawatia ushindi wa kishindo wagombea wote wa udiwani, ubunge na urais watakaopendekezwa na UKAWA kugombea nafasi hizo, ili Serilali ya awamu ya tano itokane na UKAWA.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

________________________________
Susan Anselm Jerome Lyimo (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA WAZIRI KIVULI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

Tarehe 1 Juni, 2015

No comments:

Post a Comment