Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza safari ya kwenda mikoani kuwajengea uwezo wanawake ili mafisadi wanaotumia mianya ya rushwa kuwashawishi wawapigie kura wawaogope.
Mkurugenzi wa Wanawake Band, Lilian Wasira, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia uzinduzi wa bendi ya wanawake na operesheni ya Amsha Wanawake Tanzania, itakayofanyika Kanda ya Pwani, viwanja vya Tanganyika Parkers leo.
Katika uzinduzi huo wasanii kama Christian Bella, Profesa J na Flora Mbasha wanatarajia kutumbuiza siku hiyo.
Lilian alisema bendi hiyo pamoja na operesheni ya Amsha, malengo yake ni kuwahamasisha wanawake kujitambua kuwa mabadiliko ya taifa yataletwa na wao ikiwa watakataa rushwa za vitenge, khanga na hela ya chumvi.
“Wanawake iwe mwiko kuhongwa khanga, kofia hatupo tayari kuona wanawake vijijini wanaendelea kuwa masikini mwaka hadi mwaka kwa sababu tu wanauza kura zao kwa mafisadi, tunaenda kuwaamsha wajitambue,” alisema.
Pia alisema wanaenda kuwahamasisha wanawake kutambua kuwa uuzaji wa kura zao unasababisha rasilimali ambazo ni urithi wa watoto wao unahodhiwa na wachache.
Aliongeza kuwa uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, wanaenda kukiangusha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) inaenda kuchukua dola.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake jimbo la Kawe, Janeth Rithe, alisema mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo atakuwa ni Katibu Mkuu wa chama, Dk. Wilbroad Slaa.
Kaimu Mwenyekiti wa mkoa wa Kinondoni, Rose Moshi, alisema kuwa, mwanamke ni miongoni wa wale walioleta mabadiliko ya Taifa hivyo wanapaswa kuheshimiwa.
No comments:
Post a Comment