Saturday, June 27, 2015

Chadema wafurika kurudisha fomu za ubunge

Katibu wa Chadema Ofisi ya Kanda ya Pwani, Halfan Milambo akipokea fomu za mtangazania ya kugombea nafasi ya ubunge katika Jimbo la Ilala kupitia chama hicho, Joyce Charles (katikati) huku akimpongeza kwa kurudisha fomu hizo Dar es Salaam jana. 

Makada mbalimbali wa Chadema jana walirudisha fomu za kuwania kuteuliwa na chama hicho katika nafasi ya ubunge katika majimbo ambayo yanashikiliwa na CCM.
Mchakamchaka huo wa kurudisha fomu hizo ulifanyika katika maeneo mbalimbali nchini jana ambayo ilikuwa siku ya mwisho.

Katika Jimbo la Monduli linaloshikiliwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa tayari makada watatu wamerudisha fomu. Waliorudisha fomu ni Mwenyekiti wa Chadema wa wilaya hiyo Josephat Sironga, Mwenyekiti Baraza la Wanawake (Bawacha) Mkoa wa Arusha, Cecilia Ndosi na Katibu Mwenezi wa chama hicho Monduli, Patrick Ngala ole Mong’i.

Akizungumza jana Mong’i alisema: “Tumechukua fomu sisi watatu na tumerejesha ili kupisha vikao vya maamuzi.”

Mkoani Mbeya makada lukuki wa Chadema mkoani humo walimiminika kurudisha fomu katika muda uliotakiwa huku wengine wengi wakitajwa kucheleweshwa na kazi ya kuweka fedha benki.

Katika Jimbo la Mbarali linaloshikiliwa na Modestus Kilufi (CCM), makada saba walirudisha fomu hadi saa 10.00 jioni muda ambao ulikuwa wa mwisho.

Katibu wa chama hicho wilayani hapo, Nicolaus Lyaumi aliwataja waliorudisha fomu kuwa ni Jidawaya Kazamoyo, Grace Mboka, Dick Baragasi, Tazan Ndingo, Liberatus Mwang’ombe, Rajab Kilemile na Machami Kasambala.

Katika Jimbo la Mbozi Mashariki, linaloshikiliwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi, wanachama 27 wa Chadema walichukua fomu, lakini hadi saa 10.00 jioni, Katibu wa chama hicho, Michael Mwamlima aliwataja waliorudisha kuwa ni Happness Kwilabya, Abraham Msyete, Anastazia Nzowa, Abdul Nindi, Gerald Silwimba, Eliud Msongole, Zablon Nzunda na Eliud Kibona.

Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Wilaya ya Vijijini, Jackson Mwasenga alisema jimbo la wilaya hiyo ambalo linashikiliwa na Mchungaji Luckson Mwanjale (CCM), waliorudisha fomu ni Daud Mponzi, Edson Jisandu, Adam Zela, Anthony Mwaselela Hadson Sheyo, Benson Mwamengo, Stephano Mwandiga, Frank Mwaisumbe Christina Kalisoto, William Msokwa, Elias Songela na Jeremiah Mwaweza.

Katika jimbo la Kwela linaloshikiliwa na Ignas Malocha (CCM), Daniel Ngogo pekee amerudisha fomu jana huku akitaja vipaumbele vinne ambavyo ni elimu, afya, kuboresha miundombinu ya barabara na ajira jimboni kupitia kilimo.

Pia katika jimbo la Sumbawanga Mjini linaloshikiliwa na Aeshi Hilal(CCM) tayari mfanyabiashara wa mjini Sumbawanga, Casiano Kaegele, maarufu kwa jina la Upendo alirudisha fomu ya kuomba kuteuliwa na Chadema kuwania jimbo hilo.

Kaegele alisema amesukumwa na mambo kadhaa kugombea ubunge katika hilo ikiwamo kuanzisha miradi ya wajasiriamali, kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana na wanawake, sambamba na miundombinu hususan uwanja cha ndege.

Katika jimbo la Morogoro Mjini linaloshikiliwa na Mohammed Abood, makada wa 11 walijitokeza kuomba kuteuliwa baadhi yao ni Marcussy Albaine, James Pawa Mabula, Batromeo Tarimo, Esther Tawete, Steven Daza, Doris Kweka, Gerard Temba, Robert Mruge.

Katika jimbo la Kibaha Mjini linaloshikiliwa na Sylivestry Koka (CCM) wanachama sita kati ya saba waliochukua fomu waliorudisha.

Katibu wa Chadema Kibaha Mjini, Michael Nkobi aliwataja waliorudisha kuwa ni Michael Mtally, Joachim Mahenga, Frank Mzoo, Henry Msukwa, Bosco Mfundo na Isihaka Omari.

Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Khalfan Mirambo alisema Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, waliorudisha fomu za Ubunge jumla yao ni 60 na kati ya hao, 56 ni viti maalumu. Hata hivyo alisema bado majimbo matatu ya Mkuranga, Rufiji na Chalinze.


No comments:

Post a Comment