Kauli ya Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Nape Nnauye, kudai chama chake kitaendela kuongoza nchi hata kama ni kwa kura za wizi, chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibuka na kumjibu kuwa hizo ni ndoto za mchana.
Akizungumza na NIPASHE kwenye ofisi za Chadema Wilaya ya Chato, Katibu wa Baraza la Vijana Chadema Taifa (Bavicha), Julius Mwita, alisema chama chake kipo kwenye maandalizi kamili ya kuingia Ikulu na kwamba mbinu za CCM kuendelea kuiba kura mwisho wake umefika.
Alisema kila mbinu chafu za CCM zilizoandaliwa kuhujumu Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu zimeshabainika ikiwamo kuagiza magari 700 ya kutawanya wananchi kwa maji ya kuwasha, badala ya kujikita kubuni mbinu bora za kudhibiti mauaji ya walemavu wa ngozi (albino) pamoja na vikongwe wanaouawa bila hatia.
"Nikuhakikishie kuwa mwaka huu Chadema kupitia Ukawa tunaingia madarakani...hivi sasa CCM wanaweweseka tu wasijue la kufanya ndiyo maana wamekuwa na foleni kubwa ya wagombea urais kana kwamba ni taasisi ya kuchezewa hadi na wasomi wa darasa la saba," alisema.
Alisema tathmini ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu imejionyesha kwenye uchaguzi mdogo uliomalizika ambapo Ukawa ulikishusha CCM katika viwango vya ushindi kutoka aslimia 95 hadi kufikia asilimia 64 na kwamba hatua hiyo ni wazi kwamba Ukawa wanakwenda kuchukua dola.
Akizungumza hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara wilayani Chato mkoani Geita, Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdurahman Kinana, aliwataka wafuasi wa chama hicho kuikosoa serikali ya CCM inapofanya mambo yasiyopaswa na ikiwezekana wafanye maandamano kupinga badala ya kusifia kila kitu.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida Nnauye, alisisitiza kuwa CCM kitaendelea kuongoza nchi kwa kuwa ni chama makini na kwamba hata kama itakuwa kwa kura za kuiba na kudai kuwa bao ni bao hata kama ni la kidole iwapo kama mwamuzi hataweza kuona.
Kauli ya Nape ilipokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo huku wakidai ameamua kutoa siri inayowafanya CCM kupata ushindi katika chaguzi zilizopita huku wengine wakisifia kuwa ni wakongwe wa siasa na kwamba mbinu zote za ushindi wanazo.
No comments:
Post a Comment