KATIKA kuendeleza harakati za kumkomboa mwanamke kwenye vishawishi na rushwa mbalimbali kutoka kwa viongozi wa kisiasa, Balaza la Wanawake Chadema (BAWACHA) limegundua mbinu mpya.
Mbinu hiyo inalenga kushawishi wanawake kuchukia na kukataa rushwa ili kuweza kuchagua viongozi wenye maadili. Harakati hizo zitafanywa kati ya BAWACHA na Wanawake Bendi.
Imefahamika kuwa, wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wanawake wanaoonekana kuwa na ushawishi kubwa, hutumia kuwapotosha wanawake wenzao na hata kupokea rushwa kutoka kwa viongozi.
Lakini pia wanawake huchukuliwa kama watu wa mwisho ambapo hufanyiwa maamuzi na wanaume hasa kipindi cha uchaguzi.
Kwa kuliona hilo, BAVICHA kwa kushirikiana na Wanawake Bendi imeanzisha oparesheni maalumu iliyolenga kuhamasisha wanawake wote nchini kuchagua viongozi bora.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa bendi hiyo ambaye ni Kada wa Chadema, Lilian Wasira amesema, lengo kuu la kuanzisha bendi hiyo ni kuchochea mori ndani ya wanawake ili watambue umuhimu wao.
“Wanawake wanatakiwa kuutambua uthamani wa kipekee walionao, hivyo wasikubali kurubuniwa na kuuza haki zao za msingi kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema Wasira.
Aidha, bendi hiyo pamoja na “Operesheni Amsha Wanawake Tanzania” vinatarajiwa kuzinduliwa kesho katika viwanja vya Tanganyika Parkers, Kawe saa 7;00 mchana, ambapo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kuongoza uzinduzi huo.
Na kwamba, uzinduzi huo utahudhuriwa na wanachama mbalimbali kutoka mikoa mingine, pamoja na wadau mbalimbali wapenda maendeleo ya wanawake.
Wasira ameeleza, mara baada ya kuzinduliwa bendi itaanza ziara zake za kuhamasisha wanawake. “tutaanza kanda ya Dar es Salaam na baadaye tutasambaa mikoa mingine Tanzania nzima.”
Katibu BAWACHA Jimbo la Kinondoni, Rose Moshi amewataka viongozi wote wa chama kuhudhuria uzinduzi huo ili kuleta hamasa zaidi.
“Wanawake muda wa ukombozi umefika tujitokeze kwa wingi. Na sisi kama BAVICHA tutashirikiana vizuri na bendi hii kuhakikisha inaleta mabadiliko makubwa ndani ya nchi yetu, huku tukijiandaa kuipokea serikali mpya,” amesema Moshi.
Mwanahalisi Online
No comments:
Post a Comment