1.0 Utangulizi
Mheshimiwa Spika,
Kwanza napenda kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na kunitunza ili niweze kutumikia Taifa
langu. Napenda kuishukuru familia yangu kwa msaada mkubwa na uvumilivu hasa
ninapokuwa katika shughuli zangu za kisiasa.
Mheshimiwa Spika,
Napenda kutumia fursa hii, kuwashukuru
watanzania wote kwa kupokea na kulea harakati za mabadiliko nchini.Shukrani
hizi za pekee ziwafikie wenyeviti wenza wa vyama vinavyounda UKAWA,Mh. Freeman
Mbowe, Mh. Prof. Ibrahimu Lipumba, Mh. James Mbatia na Mh. Dr.Emanuel Makaidi.
Vile vile, shukurani zangu ziwafikie Makatibu wakuu viongozi wa UKAWA; Mhe.
Wilbrod P. Slaa, Mhe. Seif Shariff Hamad, Mhe. Masena Nyambabe na Mhe. Tozi
Matwange. Sambamba na hao, shukurani zangu ziende kwa timu ya wataalamu wa
UKAWA, viongozi, watendaji, wanachama na wapenzi wa vyama vyote vinavyounda
UKAWA. Mwisho japo si kwa kumaliza shukurani zangu ziwaendee wabunge wote wa
Kambi ya Upinzani bungeni wanaounda UKAWA kwa kazi nzuri ya kutetea na kusimamia
maslahi ya wananchi wa Tanzania. Aidha,
bila kuwasahau watendaji wa Kambi ya Upinzani ambao wamekuwa ni msaada mkubwa
katika utekelezaji wa shughuli zetu.
Mheshimiwa, Spika,
Napenda kuwashukuru kwa nafasi ya pekee
wananchi wa wilaya ya Karatu na wananchi na wote wa mkoa wa Arusha kwa
ushirikiano na imani kubwa kwangu wakati nikitekeleza majukumu kama mwakilishi
wao. Niliahidi daima nitakuwa “Mtumishi
wa watu, kwa Maslahi ya watu na kwa Maendeleo ya watu” na daima nitabaki
kuwa hivyo. Ninawashukuru na nawaomba wazidishe imani hiyo kwangu kwani haiwezi
kupotea bure.
Baada ya Shukrani hizo napenda kuanza hotuba
yangu kwa kunukuu maneno machache kutoka kwa Baba wa Taifa, ningependa
watanzania kuyatafakari hususan kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi oktoba
2015;
“Na hakutakuwa na watu wa
kizazi hiki na karne hii ambao watatakiwa kujitoa muhanga kwa ajili ya maisha
bora katika siku zijazo wakakubali, wakati wanawaona watu wachache wakiendelea
kuneemeka machoni pao bila kujali wakati ujao, wakati wananchi na watoto wao
wakiendelea kuishi katika maisha duni na dhalili.”
UKOSEFU WA AJIRA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Kwa muda mrefu tumekua tukionesha jinsi ambavyo Serikali imekua haina
mikakati endelevu ya kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini. Aidha, Serikali
ya CCM imekuwa ikitumia mikakati ya ‘kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa’ kama nadharia
iliyozoeleka kwa nia yenye kuwapumbaza wananchi kwa kuwapa matumaini yasiyo na
matokeo chanya juu suala zima la utengenezaji wa ajira hapa nchini na hivyo
kulifanya tatizo la ajira kuwa ni wimbo uliozoeleka ndani ya masikio ya
watanzania. Hili ni jambo la aibu kwa nchi iliyojaliwa utajiri mkubwa wa
maliasili na rasilimali.
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere amewahi kutamka maneno yafuatayo;
“Amini nawaambieni enyi waswahili wachache mnaotawala; mnategemea kweli
kuwa mtawaongoza watanzania kwa lazima wakati wamepoteza matumaini, na mtegemee
kuwa wanasalia wamekaa kimya kwa amani na utulivu?”(Reflections
on Leadership in Africa -VUB –University Press, 2000)
Mheshimiwa Spika,
Mwelekeo wa uongozi wa mazoea na wa kuongoza na kuamua mambo kwa matukio
ni kuonesha jinsi gani Serikali ya CCM ilivyochoka na kwamba inahitaji kukaa
pembeni na kujifunza namna ya kuongoza nchi kwa viwango vya uwajibikaji wenye
maslahi mapana kwa jamii ya watanzania. Serikali ya CCM imeshindwa kuzioanisha
Sera, Sheria, Mikakati na mipango mbalimbali ambayo kwa pamoja ingeweza kutatua
matatizo sugu ya ukosefu wa ajira nchini. Ni Serikali hii ambayo, imeua falsafa
ya kujitegemea ‘self reliance’ ambayo Baba wa Taifa aliipigania kwa ajili ya
watanzania wote. Je, ni kiongozi yupi wa CCM atakayeweza kusimama na kusema
kuwa Serikali ya CCM imekua mdau nambari moja wa azimio la Arusha? Je ni nani
kati yenu anayeweza kusema mfumo wa elimu tulionao leo unampa mhitimu uwezo wa
kujitegemea? Ni nani anaweza kusimama na kueleza mafanikio ya Serikali ya CCM
kuhakikisha kuwa kilimo alichokipigania Baba wa Taifa kinatoa ajira kwa makundi
yote? Je, ni nani kati yenu atakayeweza kusimama na kujinasibu kuwa vyuo vikuu
mlivyojenga kwa fedha za wachangiaji ambao wengi ni wafanyakazi na wakulima wa
nchi hii vimemuandaa mtanzania kukabiliana na changamoto za ajira?
Mheshimiwa Spika,
Serikali yoyote katika hali halisi ya kiutendaji na utawala, itakuwa na
walakini kama itaangalia tu utawala au mfumo bila kujielekeza kuangalia pia
mchakato mzima katika utawala na mfumo wake. Ni wazi kwamba, Tanzania inahitaji
kufanya mageuzi makubwa kwa sababu nchi inahitaji mabadiliko na hii ni kwa kuwa
serikali hii inayoongozwa na CCM ina mambo ambayo hayaendani na kasi ya
mabadiliko ya sasa ya kidunia.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kwamba Serikali ya Tanzania inayoongozwa na CCM kuwa na utaratibu wake, hakika huu ni
utaratibu wa kushindwa kuendana na mahitaji ya kiuchumi na kijamii ya watu wake,
utaratibu wa kushindwa kuleta maendeleo kwa watu wake, utaratibu wa kushindwa
kuleta maendeleo ya amani kwa watu wake na taratibu nyinginezo zenye kunyonya
nguvu za watu wake.
Hivyo basi, Serikali ya UKAWA itakapoingia madarakani imekusudia kudhibiti na kuondoa changamoto
hizi kwa kuhakikisha kuwa wananchi wa taifa hili la Tanzania wanatengenezewa
ajira za kutosha na wanaishi na kufanya
kazi kwa amani na utulivu na kuondoa umaskini, kuhakikisha kuwa watu wanaishi
kwa uhuru na wanafurahia haki za msingi za kidemokrasia na kwa ufanisi mkubwa, kuhakikisha kuwa mfumo wa
uendeshaji serikali kiutawala na kisiasa unaleta maendeleo endelevu ya
kiuchumi, na zaidi, mabadiliko hayo ya kiuchumi yanafikiwa katika nchi hii
yenye utajiri mkubwa wa rasilimali.
Mheshimiwa Spika,
Katika historia ya sasa; Tanzania imekuwa chini ya utawala wa sheria
uliovaa koti la shari, vitisho na mabavu chini ya CCM, na sasa watanzania wanatambua
juu ya matokeo ya utawala wa namna hiyo. Hata hivyo, tangu uhuru, watanzania
wamekuwa wakiishi kwa pamoja na kujenga
urafiki na ushirikiano baina yao, serikali na
watu wa nchi nyingine katika msingi wa amani.
Mheshimiwa Spika,
Kauli hiyo ya utawala wa sheria uliovaa koti la shari, vitisho na mabavu
unadhihirishwa pia na kauli za Kiongozi wa nchi alizowahi kuzitoa huko nyuma
Mwezi Mei 2010 alisema:
“.....wafanyakazi wanaotaka kugoma waache
kazi.....kwa kuwa kuna watu wengi wanahitaji kazi....”
Mheshimiwa Spika,
Ni
ukweli usiopingika kwamba “soko la ajira” Tanzania limefurika wanaotafuta kazi;
lakini si kweli kwamba watu wote wanaotafuta kazi wanasifa stahiki kwa kila
kazi. Kiongozi yeyote awaye mwenye mamlaka ya juu ya kiutendaji ana wajibu wa
kuchagua maneno yenye hekima; kwa kuwa “hekima ni uhuru”. Wafanyakazi wanapodai
haki zao ni vema wasijione wanyonge mbele ya “Mwajiri Mkuu”
Mheshimiwa Spika,
Naomba pia nitumie fursa hii kunukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius K. Nyerere aliyoyatoa Dar es Salaam kwenye sherehe za Mei mosi mwaka
1974:
“......tulipoanzisha vyama wafanyakazi, na halafu
baada ya uhuru kwa uamuzi wa serikali ya TANU, wafanyakazi wa Tanzania
wamelindwa wasinyonywe na matajiri wao, watu binafsi, na hata mashirika ya
umma. Na ulinzi huo umezidishwa siku hata siku. Kima cha chini cha mishahara
kimewekwa na kimekuwa kikiongezwa mara kwa mara. Sasa ni vigumu sana kumfukuza
mfanyakazi, na kila mfanyakazi apate heshima yake kama binadamu......” (Julius
K.Nyerere (1974): UHURU NI KAZI, National Printing Company Ltd, Dar es Salaam,
ukurasa 15)”
Inaendelea.......
Mheshimiwa Spika,
Kauli ya Baba wa taifa inatufundisha msimamo wa viongozi wanaojali
maslahi ya wafanyakazi na watu wao kwa ujumla na kuwahakikishia wafanyakazi
:(1)ulinzi wa ajira zao dhidi ya unyonyaji unaofanywa na matajiri, watu
binafsi, na mashirika ya umma; (2) kuweka kima cha chini cha mshahara na kukiongeza
kila mara kuendana na mwenendo wa uchumi;(3) kuondoa vitisho vya wafanyakazi
kufukuzwa na waajiri;(4)kuwapa wafanyakazi heshima yao kama binadamu[ibara ya
12(2), Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977(2005)]
Mheshimiwa Spika,
kauli za viongozi zisizokidhi matarajio ya wafanyakazi zinazotolewa katika siku
za dhama hizi zinaonesha wazi kuwa leo wafanyakazi wa Tanzania si kama “Enzi za
Mwalimu.” Soko la ajira limewapa nafasi matajiri, watu binafsi, mashirika ya
umma na serikali (yenyewe) kunyonya jasho la wafanyakazi, kuendesha vitisho,
kulipa mishahara isiyokidhi maisha (na mafao duni ya uzeeni na/au kiinua
mgongo), vitisho vya kufukuzwa kazi, na ukosefu wa heshima kwa wafanyakazi!
Inawezekana haya ni matunda ya kuliua Azimio la Arusha na mahala pake kuliweka
“Azimio la Zanzibar”
Mheshimiwa Spika,
Utawala usiozingatia maslahi ya wafanyakazi wake kwa kiwango cha juu kwa
jinsi unavyoendeshwa na CCM, unazuia amani na maendeleo ya pamoja.Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na washirika wake (UKAWA) wanatambua kuwa
amani na utulivu katika nchi yoyote hujenga na kuleta maendeleo ya kitaifa na
hatimaye maisha bora kwa watu wake, hali kadhalika amani katika dunia inalinda
maendeleo ya pamoja na ustawi wa watu wote na mgawo halali katika mafanikio ya
maendeleo yao. Katika njia ya kujenga jamii yenye demokrasia yenye mpangilio mzuri
na wa kuridhisha,UKAWA watakapotwaa mamlaka ya kuongoza nchi hii watachukulia
umuhimu wa kwanza masuala ya maendeleo na ushirikiano na wananchi wa Tanzania
na kutambua kuwa ajira na ujira wenye staha ni njia muhimu ya kujenga jamii
yenye ustawi wa kisasa.
UKUAJI WA SEKTA YA AJIRA
Mheshimiwa Spika,
Mwalimu Nyerere aliwahi kusema:
“To measure a country’s wealth by its gross
national product is to measure things, not satisfaction.”[1]
Kwa maana isiyo rasmi ya Kiswahili anasema:
“Kupima
utajiri wa nchi kwa kutumia pato lake (yaani maana ya namba ya GNP), ni kupima
vitu na si mahitaji toshelezi ya wananchi wake”.
Mheshimiwa Spika,
Ukuaji wa Uchumi na Uzalishaji wa
Ajira (Economic growth and Employment creation) ni vitu viwili ambavyo haviwezi
kutenganishwa katika mahusiano yake. Katika hotuba ya Waziri Mkuu, inaeleza
kuwa ‘kwa mwaka 2014, uchumi ulikua kwa
asilimia 7.0 ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 2006, ukuaji ambao ni mzuri
ikilinganishwa na nchi nyingi zinazoendelea’. Lakini ni vizuri kujua kuwa
umekuwa ukikua bila kuzalisha ajira nyingi na bila kupunguza umaskini. Hii
inatokana na aina ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Sekta zinazokua kwa kasi ni
zile zinazotumia mashine na mitambo ambazo ukuaji wake kwa asilimia katika
mabano ni ujenzi(14.1), usafirishaji na uhifadhi(12.5), fedha na bima(10.8) na
nyinginezo.Sekta zinazotumia mashine na mitambo haziajiri wafanyakazi wengi
kama zile zinazotumia misuli mfano kilimo, uvuvi, na ufugaji. Kilimo kilikua
kwa asilimia 3.4 tu. Pia Sekta zilizokua kwa kasi hazina mwingiliano na sekta
zisizokua. Jambo lingine linaloweza kufanya ukuaji wa uchumi usipunguze
umaskini ni mgawanyo mbovu wa wa sehemu ya uchumi iliyokua.
Mheshimiwa Spika,
Kimsingi, bajeti lazima zizingatie si tu kukua kwa uchumi bali pia
kuhakikisha kuwa ukuaji huu unakuwa shirikishi, unazalisha ajira na kupunguza
umaskini. Ni muhimu pia kusisitiza ukuaji wa kijani (green production growth)
ambao ni ukuaji usioharibu mazingira (ikolojia).
Mheshimiwa Spika,
Maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji ni muhimu sana katika ukuaji wa
sekta ya ajira na kujenga ustawi wa maisha ya watu. Japokuwa Bajeti ya Waziri
Mkuu imezungumzia mambo mengi kuhusu maendeleo ya sekta binafsi, ingekuwa
vizuri kutambua mambo ya msingi katika sekta binafsi, Uchambuzi katika sekta
binafsi unaonesha kuwa sekta hii si kitu kimoja, ina vipande vingi. Hivi ni
pamoja na: sekta binafsi ya nje na ya ndani; sekta binafsi kubwa, ya kati na
ndogo na sekta binafsi isiyo rasmi.Hatua za kibajeti lazima zitambue ukweli huu
kuhusu sekta binafsi. Aina zote za sekta binafsi zikiwekwa katika kapu moja
haitakuwa sahihi kwa maendeleo ya sekta hii hasa ile ya ndani, ndogo na isiyo
rasmi. Ni vema CCM wakajiuliza maswali na kuachana na mazoea ya utengenezaji
hotuba za bajeti kwa namna ambayo haitoi taswira halisia tena kwa fikra zile
zile, za miaka ile ile na kwa ujanja ule ule.
Mheshimiwa Spika,
Aidha hatuwezi kupigia kelele ukosefu wa ajira bila kujielekeza katika kuangalia
sekta ya uwekezaji. Suala kuu katika sekta ya uwekezaji ambayo CCM imekuwa
ikipata ganzi kulifanyia kazi na kuchukua hatua makini za makusudi ni
uboreshaji wa mazingira kwa wawekezaji wa ndani na nje, wakubwa kwa wadogo.
Hatua mahsusi za kibajeti zinatakiwa katika kuleta na kuboresha mazingira
rafiki na wezeshi ya uwekezaji ili kuongeza ajira na ustawi wa maisha ya
watanzania.
Mheshimiwa Spika,
eneo lingine ni maboresho katika
sekta ya utalii yanaweza kujenga ajira nyingi kwa watanzania. Tayari sekta ya
utalii ni mchangiaji mkubwa kwa uchumi wa Tanzania. Chapisho la Hali ya Uchumi wa Tanzania linalochapishwa Na Benki ya
Dunia libainisha kwamba sekta ya utalii inaweza kukua na kujenga ajira
zaidi, hususan katika ajira zinazolipa vizuri, pia inaweza kuunganisha biashara
na wana jamii wa maeneo husika. Ili kutumia fursa hii, serikali inapaswa
kupitia upya wajibu wake kwa kurahisisha mfumo wa kodi na ushuru, na kufanya
mgawanyo wa mapato kuwa wazi zaidi.
Mheshimiwa Spika,
sekta ya utalii huajiri moja kwa moja taktribani watanzania nusu milioni
na huchangia karibu asilimia 20 ya bidhaa zinazouzwa nje. Huwakilisha takribani
asilimia 3.4 ya Pato Ghafi la Tanzania(GDP), lakini kiwango hiki kinaweza
kufikia makadirio asilimia 10 unapochukuliwa mchango wake ambao si wa moja kwa
moja katika sekta nyingine kama kilimo na uchukuzi. Pamoja na kwamba sekta ina
lengo la kuongeza mapato yatokanayo na utalii mara nane ifikapo mwaka 2025, au
kuongeza kiwango cha ukuaji wa sekta mara dufu kwa kila mwaka kama
inavyoonekana katika miaka hivi karibuni, Lengo hili litafikika endapo tu kutakuwa
na mabadiliko katika sera na mitazamo
miongoni mwa wadau wote.
Mheshimiwa Spika,
kama nilivyokwisha sema awali, bila kujenga uwezo wa kitaasisi katika
sekta zetu mbalimbali hapa nchini ni vigumu kuzalisha ajira na kuleta maisha ya
ustawi kwa watu wetu. Katika kuboresha sekta hii ya utalii ambayo ni moja ya
sekta zenye mchango mkubwa wa ajira katika nchi yetu mambo kadhaa yanahitajika.
Serikali itakayoundwa na UKAWA imejipanga (1) kupanua shughuli za utalii kuwa
anuai tofauti na msisitizo wa sasa ambao unatoa umuhimu kwa watalii wa gharama
kubwa katika kanda ya kaskazini na kuzunguka Arusha na Zanzibar ambako asilimia
90 ya shughuli za utalii ndiko ziliko sasa;(2)kuongeza juhudi za kuwaunganisha
wana jamii wa maeneo husika na wafanyabiashara wadogo wa utalii katika shughuli
za utalii, kupitia michakato ya kugawana faida.
Aidha, Serikali itakayoundwa na UKAWA itaandaa programu za mafunzo na
kuunganisha jamii baina ya sekta za umma na binafsi, hii italeta viwango vya
juu vya ubora wakati huo huo ikiongeza ushiriki wa wafanyabiashara na
wafanyakazi wa maeneo hayo katika shughuli za utalii; na (3) Serikali yetu itafanya
mapitio ya mfumo wa sasa wa kodi na ushuru ambao ni mgumu kuuelewa, mapitio
hayo pia yatagusa usimamizi wa matumizi yasiyo ya wazi ya mapato yaliyokusanywa
kutoka utalii. Vilevile, mfumo wa kodi na ushuru utafanywa kuwa rahisi na
kutekelezwa kwa usawa zaidi kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa
biashara na kuziba mianya ambayo inatoa nafasi kufanya malipo haramu. Aidha,
mgawanyo wa mapato utarasimishwa ili uwe rahisi kufuatilia na kuongeza manufaa
kwa wananchi walio wengi.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 7
bado hakiakisi maendeleo halisi ya watu kwenye kaya zao. Hivi sasa maisha yako
juu. Bei ya bidhaa na huduma mbalimbali za jamii, ziko juu. Kwa kifupi hali ya
maisha ni ngumu. Kambi rasmi ya upinzani inaona kuwa tatizo kubwa la viongozi
wa CCM ni kuona kuwa “wizara husika inapaswa kufa kivyake” bila kutambua na kuona
pia jitihada za makusudi zinatakiwa kuchukuliwa ili kuwepo na “mfumo unaounganisha wizara, idara, wakala za
serikali, na uongozi wa sekta binafsi kufanya kazi kwa umoja” utakaoweza
kusaidia kujenga uwezo wa uelewa wa jinsi gani ajira zinaweza kutengenezwa
katika nchi.
Serikali ya UKAWA inaahidi kuifanya Wizara ya Kazi na Ajira kuwa bunifu
na kuioanisha na vitengo vingine vya utawala pamoja na wataalamu mbalimbali wa
wizara zingine katika kufikia lengo la kuongeza ajira kwa watanzania.
Mheshimiwa Spika,
UKAWA tutakapopewa ridhaa ya kuongoza nchi hii tutahakikisha kuwa
masuala ya kisera, kisheria na ya udhibiti yaliyo rafiki yanazingatiwa, kwa
kuwa na bajeti zinazojikita katika maendeleo ya miundo mbinu kwa upana wake,
kuondoa urasimu serikalini na kukuza rasilimali watu inayohitajika kwa sekta
binafsi kuwa na ushindani wa kimataifa. UKAWA tutaweza kujenga mfumo imara
utakaoweza kujenga uwezo katika utengenezaji wa ajira hapa nchini na kuipaisha
Tanzania katika modeli za ukuzaji wa ajira ukilinganisha na hali ilivyo ya sasa
ya kufanya kazi kwa mazoea bila kuendana na mabadiliko ya dunia ya sasa.
AJIRA KWA VIJANA
Mheshimiwa Spika, Kwa
mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu milioni 200 miongoni mwa wakazi wa
Afrika ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24. Hii ni katika hali ambayo
Umoja wa Mataifa unasema kuwa, idadi ya vijana wasio na ajira barani Afrika ni
mara mbili zaidi ya watu wazima. Ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana
unawafanya washawishike kujiunga na makundi yenye misimamo mikali tena kwa
ujira mdogo tu au hata kwa hasira za kukata tamaa na maisha. Mfano wa hali hiyo
unashuhudiwa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria na Mali. Inaonekana
kuwa, vijana wasio na ajira ni mawindo mazuri kwa makundi yenye kutishia amani.
Leo hii siku za karibuni tumeshuhudia kijana wa kitanzania Rashid Charles
Mberesero (21), akituhumiwa kuwa mmoja wa wanamgambo wa Al-Shabaab ambao
walifanya mauaji katika Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya na kuua wanafunzi
148. Haya ni matokeo ya kushindwa kwa mfumo wa utawala katika sekta ya elimu
unaosimamiwa na Serikali ya CCM ambao ndio msingi wa kumuandaa kijana kifikra
na hata kimtazamo.
Mheshimiwa Spika,
Ajira kwa vijana ni suala nyeti katika uchumi wa Tanzania.Ni bahati
mbaya kuwa vijana wengi hawajaajiriwa katika sekta rasmi. Katika Hotuba ya
Waziri Mkuu aliyoiwasilisha mnamo tarehe 12 Mei 2015 katika bunge hili ni kwa
masikitiko makubwa haikueleza kabisa hali ilivyo hivi sasa. Hotuba ya Waziri
Mkuu ingepaswa kueleza kwa nini hali iko hivi na nini kinafanyika kupambana na
hali hiyo. Zipo sababu nyingi za vijana kutoajiriwa na kujiajiri ikiwa ni
pamoja na upungufu wa nafasi za ajira na kukubalika katika soko la ajira. Upungufu
huo na kutokubalika katika soko la ajira vina sababu zake ambazo bajeti
ilipaswa kuelezea lakini imekaa kimya. Pia uwezo mdogo wa vijana kujiajiri
ungepaswa kuelezewa pamoja na hatua zinazochukuliwa na ambazo zimeshachukuliwa
miaka ya nyuma.
Mheshimiwa Spika, wakati wa majadiliano ya bajeti ya wizara ya
kazi na ajira mwaka jana tarehe 24 Mei 2014, Waziri Kabaka alielezea kuwa
vijana wa kitanzania hasa wahitimu wanategemea kuajiriwa serikalini na
mashirika binafsi na hawako tayari kujiajiri. Haya ni ghiriba kwa watoto wa
masikini na waziri anapaswa kufuta kauli yake kwa kuwa inavyoonekana leo hii
kuwa ni watoto wa vigogo pekee ndio wana haki ya kupata ajira serikalini na
watoto wa kimasikini ndio wajiajiri.
Mheshimiwa Spika,
Ajira 200 za uhamiaji zilitangazwa Februari 17, mwaka 2014 ambapo watu
15,707 walijitokeza kuwania nafasi hizo 200, miongoni mwao, waombaji 1,005
waliitwa kwenye usaili na 200 waliothibitishwa waliitwa kazini. Hata hivyo,
baada ya tangazo la kuitwa kazini malalamiko yaliibuka kupitia vyombo vya
habari na baadhi ya mitandao ya kijamii, kwamba baadhi ya walioitwa katika
ajira hizo walikuwa ni watoto, jamaa na ndugu wa maofisa wa Idara ya Uhamiaji.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na kuwa si kosa kwa ndugu na jamaa kuajiriwa katika nafasi yoyote iwapo
wanakidhi vigezo vyote, lakini inapotokea kwamba hakuna uwazi(transparency) ni
dhahiri kwamba kunakuwa na upendeleo kama ilivyotokea.Hii inatokana na ukweli
kuwa idara hiyo haichukui watumishi
kutoka Sekretarieti ya Ajira, kwa kuwa wanaohitajika ni askari. Lakini hii ni
mojawapo ya ushahidi kuwa nafasi za kazi nchini zimeendelea kutolewa kwa
upendeleo na wanaonufaika na nafasi hizo ni vigogo na ndugu zao au watu wenye
mahusiano ya karibu na wenye mamlaka hayo.
Mheshimiwa Spika,
Kukosekana kwa takwimu sahihi na taarifa za nguvu kazi nchini kunaleta
sintofahamu kubwa katika kutatua matatizo ya ajira nchini. Kukosekana huko kwa
taarifa sahihi ndio kunakofanya CCM itake kuwaaminisha watanzania kuwa
Mabilioni ya Rais Kikwete yameweza kutatua changamoto za ajira nchini.Tukiwa
tunamaliza miaka 10 ya utawala usio wa kimkakati, vijana na nguvukazi ya Tanzania
inawakumbuka watawala wa CCM kama wazee wa ahadi, ahadi zenye mashaka! Leo hii tuna Serikali inayokiri
kutokua na takwimu za ajira nchini, ni vipi mikakati na sera hizi zitapimwa
utekelezaji wake ikiwa takwimu sahihi zinakosekana?
Mheshimiwa Spika,
Mabilioni ya Kikwete ni mojawapo
ya mikakati iliyoshindwa kwa kuwa haikua na nia ya dhati ya kumfundisha
mtanzania kuvua bali kuwapatia samaki wa siku moja na ililenga kuwadumaza
watanzania kwa kuwaaminisha kuwa Rais Kikwete ana mahela ambayo yanaweza
kutatua shida zao na si kuwainua kiuchumi. Kwa bahati mbaya sana Serikali za
CCM za Awamu ya Pili, Tatu na hata hii ya
Nne, zimekuwa siku zote zikisema zinafufua uchumi. Kila uongozi unaokuja
hauishi kutamba kuwa unataka kufufua uchumi.Swali la kujiuliza ni kwamba, ni
nani aliyeua uchumi na kuuzika? Na ni nani anayetaka kuufufua? Jibu la haraka
ni serikali hiyo hiyo, tena ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) toka Baba wa Taifa
akabidhi madaraka kwa marais waliomfuatia.
Mheshimiwa Spika,
Mkazo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na washirika wake
(UKAWA) watakapopewa ridhaa ya kuongoza nchi hii Oktoba mwaka huu ni kwamba,
pamoja na kiwango cha mchango wa pato letu kwenye kaya za jamii zetu kuwa ni
kidogo, tunaweza kupunguza utegemezi na mgawanyo wa ovyo wa rasilimali na
kupiga hatua katika utafiti na uendelezaji (Research and Development) na kuweka
jitihada kubwa ili kuhakikisha kuwa rasilimali tulizonazo zinatumika kwa kiwango
cha juu. Utawala wa UKAWA utajenga uwezo mkubwa wa viwanda vyake vya malighafi,
vifaa vya uzalishaji(capital goods) na uzalishaji wa bidhaa za mlaji ili
kutosheleza mahitaji ya walaji wa Tanzania na kutoa bidhaa na huduma bora katika
soko la kimataifa. Kwa kufanya hivyo pia kutaongeza ajira kwa watanzania.
Mheshimiwa Spika,
Uchumi wa taifa hili unaongozwa
na CCM na CCM ndiyo yenye jukumu la kuua au kukuza uchumi. Serikali ya Awamu ya
nne baada ya kuingia madarakani, ilikuja na mkakati mahususi wa kuleta maisha
bora kwa kila Mtanzania. Ili kuondoa umaskini, mbali ya kutoa ahadi ya ajira
milioni moja kila mwaka kwa vijana, Rais Jakaya Kikwete pia alikuja na mpango
wa kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya kukopesha vikundi vya ujasiriamali.
Fedha hizo zilisemekana kuwa zingetolewa kupitia benki, vyama vya akiba na
mikopo (SACCOS) na taasisi nyingine za fedha zilizoruhusiwa na Serikali
kupitishia mikopo hiyo.Chini ya mpango huo, kila mkoa uliahidiwa kumwagiwa sh
bilioni moja.
Mheshimiwa Spika,
Hivi karibuni wakati akijibu
swali la msingi la Mbunge wa Viti
Maalumu, Faida Mohamed Bakari (CCM) ambaye alitaka kufahamu ni wafanyabiashara
wangapi wenye ulemavu walipatiwa mikopo kupitia fedha hizo. Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Uwekezaji na Uwezeshaji, Christopher Chiza alisema kuwa mpango
huo ulikuwa na madhumuni ya kuwezesha wananchi kiuchumi na kuongeza ajira kwa
wanawake na vijana vijijini na mijini kwa kuwapatia mikopo bila kujali maumbile
yao. Alisema chini ya mpango huo, mikopo ilitolewa katika awamu mbili kupitia
benki na asasi za kifedha, zilizoteuliwa na serikali baada ya kukidhi vigezo
ambapo jumla ya Sh bilioni 43.69 zilitolewa na kunufaisha wajasiriamali 74,593.
Vilevile, cha kusikitisha zaidi ni kuwa Waziri Chiza alieleza kuwa mikopo hiyo
haikuwa na kipengele cha utambuzi cha watu wenye ulemavu. Hii inaonesha ni
jinsi gani Serikali ya CCM imeshindwa kuwapa vipaumbele walemavu katika
mikakati yake ya kuwawezesha kiuchumi na kukuza ajira. Ni hatari kuona kuwa,
walemavu kwa muda wa miaka 10 ya utawala wa Kikwete hawajapewa kipaumbele cha
kujiajiri wala kuajiriwa bali Serikali imekua ikiwakumbuka kipindi cha uchaguzi
pekee. Ndio maana Serikali siku zote hutoa idadi ya walemavu walionufaika na
nafasi za kiuongozi na kisiasa na wala si walionufaika na fursa za ajira
nchini. Kambi rasmi ya Upinzani
inaendelea kuwa mtetezi nambari moja wa haki za walemavu katika masuala ya
ajira kwa kuwa watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii yetu na wana haki sawa na
watu wote.
Mheshimiwa Spika,
Sasa inatosha! Kambi ya Upinzani Bungeni inapenda kuwaambia watanzania
kuwa kwa muda wa miaka 10, matatizo yao yametumika kama mtaji wa Serikali ya
CCM na hivyo utatuzi wa matatizo hayo ni sawa na ahadi hewa. Ikumbukwe kuwa
Mheshimiwa Kikwete pia katika muendelezo wa ahadi zake zilezile, alitoa agizo
mahsusi kwa Wizara hii Jumatano, Aprili 10, 2013 baada ya kuwa ameelezwa na
kuonyeshwa video ya Mpango wa Kuwawezesha Wajasiriamali Vijana Wahitimu wa Chuo
Kikuu cha Kilimo cha Sokoine cha Morogoro katika shughuli iliyofanyika Ikulu,
Dar es Salaam. Mpango huo unaogharimiwa na Benki ya CRDB na kuendeshwa kwa
pamoja kwa kushirikiana na SUA pamoja na Ushirika wa Wahitimu Wajasiriamali wa
Chuo Kikuu cha Sokoine (SUGECO).
Mheshimiwa Spika,
Rais Kikwete aliitaka Wizara ya Kazi na Ajira kuwasilisha haraka
iwezekanavyo kwenye Kikao cha Baraza la Mawaziri mapendekezo ya kuboresha na
kupanua mpango mpya wa uwezeshaji na ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu
ambao unalenga kupanua fursa za ajira kwa kutoa mitaji kwa vijana ili waanzishe
shughuli zao za uzalishaji. Hii ni kauli ya Kiongozi Mkuu wa Serikali kukubali
kuwa mikakati yake dhidi ya tatizo la ajira imekosa vipaumbele vya muda mfupi
na mrefu.
“Huu mpango nimeupenda sana. Huu ni bora zaidi
kuliko hata ule mwingine wenye mafanikio wa Mabilioni ya Bwana Fulani kwa
sababu huu unamwandaa vizuri mjasiriamali ili aweze kukopeshwa. Huu ndiyo aina
ya mpango ambao nimekuwa nauzungumzia na kutaka uanzishwe ambako wasomi na
wasio wasomo wanajiunda katika vikundi kulingana na ujuzi na elimu ili Serikali
iweze kuwawezesha.”
Ikiwa imepita mwaka mmoja toka Rais atoe ahadi ya utekelezaji wa wazo
hilo, wizara ina majibu gani?
Aidha, Rais Kikwete aliendelea kusema kuwa
“Serikali yangu iko tayari kuchangia kiasi cha sh.
bilioni tano katika mfuko wa kuunga mkono mpango huu.Hii ni modeli nzuri ya
kuwezesha vijana, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu. Tuendelee
kuwezesha vijana katika sekta ya kilimo lakini sasa tuanze kufikiria namna ya
kupanuka na kuingia katika maeneo mengine ili kusudi anayetaka kukopa kufanya
biashara ya mitumba na ya teknolojia ya habari naye aweze kukopeshwa.’
Mheshimiwa Spika,
Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa Rais anakubali kuwa modeli
aliyooneshwa ni bora kuliko mabilioni yake ambayo anashindwa kutaja hata jina
lake kwa kuwa, mpango wa Mabilioni ya Kikwete si tu umeshindwa kuwa na matokeo
mazuri lakini pia umeshindwa kutatua tatizo la ajira nchini na kuwainua
wananchi kiuchumi.
MISHAHARA YENYE STAHA KATIKA SEKTA MBALIMBALI
NCHINI
Mheshimiwa Spika,
kwa miaka yote mitano ya uhai wa Bunge hili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
imekuwa ikiwatetea watumishi wa umma katika nyanja mbalimbali lakini cha
kusikitisha ni kwamba Serikali hii ya CCM inayojiita sikivu mara zote imekuwa
ikipuuza na kubeza mapendekezo mazuri yanayotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni.
Mheshimiwa Spika,
Miongoni mwa masuala muhimu tuliyopendekeza na serikali kuyapuuza ni
kama ifuatavyo:
1.Kima cha Chini cha Mshahara:
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani kwa muda
mrefu imekua ikiishauri Serikali kupandisha kiima cha chini cha mshahara kwa
watumishi wa umma kufikia shilingi 315, 000/= kwa mwezi lakini Serikali imeamua
kuziba masikio na mpaka sasa haijatekeleza pendekezo hilo. Inashangaza sana
kuona Serikali ikijigamba kuwa imepandisha kima cha chini cha mshahara kutoka
shilingi 240,000/= hadi shilingi 265,000/= sawa na ongezeko la shilingi 25,000
tu.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na matumaini ambayo Rais
Kikwete aliwapa wafanyakazi mwaka 2005 na 2010, leo hii anapoondoka madarakani
hata walimu ambao waliamini Rais kwa nafasi yake kama mkuu wa nchi atawapa
alichowaahidi, leo wanambebea bango na kumuuliza kwa machungu ‘Shemeji unatuachaje’? hii inasikitisha
sana .
Mheshimiwa Spika,
Leo hii Rais anaondoka madarakani watu wakiwa hawana shauku tena na Mei
Mosi zaidi ya Taasisi za Serikali kwa kuwa maadhimisho haya hayana maana tena
kwao. Maadhimisho haya kwa muda wa miaka 10 hayajakata kiu ama shauku ya
mfanyakazi kupunguziwa kodi ya mapato wala kusikia ongezeko la mshahara wenye
staha. Je ni nani kati yetu anayeweza kuishi kwa shilingi 265,000 kwa mwezi,
akalipia kodi ya nyumba, ada ya watoto, huduma za umeme, maji na afya na
kujikimu kwa chakula kwa kiasi hicho? Ipo hapi azma ya baba wa Taifa ya kujenga
Taifa la wafanyakazi? CCM inaondoka madarakani ikiwa imeharibu misingi
iliyojengwa na Mwalimu, ni nani wa kusimama na kujivunia hayo?
Pamoja na kuahidi kuwa Serikali itaongeza mshahara, Mhe. Raisi
anashindwa kutamka hadharani iwapo ongezeko la mshahara litafikia 315000, na
hata kama halitafikia bado anatoa matumaini kwa watanzania kuwa ataongeza. Hii
ni mbinu ya kudaka kura za watanzania kwa mara nyengine.
KODI YA PATO LA MSHAHARA (PAYE)
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa utaratibu wa kodi ya mapato ya wafanyakazi ni kati ya asilimia 12 na
35 ya mshahara wa mfanyakazi. Kwa mujibu wa CAG katika mwaka 2013/2014 mamlaka
ya kodi ta Tanzania ilikusanya jumla ya trilioni 15 kama kodi itokanayo na
mapato (PAYE). Aidha, mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali alionesha kwamba
katika kipindi hicho, serikali ilitoa msamaha kwa walipa kodi wakubwa na
makampuni ya nje liliyofikiwa kiasi cha shilingi trilioni 1.5 sawa na kodi
iliyokusanywa na Serikali kutoka kwa wafanyakazi. Hii ina maana kwamba kama
Serikali isingetoa misamaha hiyo ya kodi, mapato ya serikali kutoka kwa walipa
kodi wakubwa nchini yangeongezeka maradufu na hivyo kumpunguzia mfanyakazi
mzigo wa kodi.
Mheshimiwa
spika,
Kutokana na ukuaji mbaya wa uchumi,
mfumuko wa bei pamoja na kupanda kwa gharama za maisha, kodi itokanayo na
mapato ya wafanyakazi imekuwa mzigo mkubwa na maumivu kwa wafanyakazi wa
Tanzania waliopo katika ajira rasmi. Katika maoni yake ya mwaka toka kuanza kwa
Bunge lako la 10, Kambi rasmi ya Upinzani, imekuwa ikipendekeza kwamba viwango
vya kodi ya mapato ya wafanyakazi vipunguzwe kufikia asilimia 9 hadi 27
respectively. Pendekezo hili bado lina nguvu mpaka leo. Leo Rais anaondoka madarakani akiacha kiwango
cha asilimia 12 huku akiwa hana uhakika wa kutekeleza ahadi zake za kupunguza
kodi kwa wafanyakazi. Akihutubia Maadhimisho ya Mei Mosi, Rais Kikwete alisema:
‘Na mwaka
huu tutapunguza sijui tutafikia asilimia 9 kama mnavyotaka ila tutakapofikia si
pabaya’
Haya ni maneno ya Rais ambayo si tu
hayatoi mwelekeo bali hayajibu njaa ya miaka mingi ya punguzo la kodi ili
Tanzania iwe sawa na nchi nyingine za Jumuia ya Afrika Mashariki. Ni ahadi yetu
kwa wafanyakazi wote nchini ambao Mwalimu Nyerere aliwapigania kwa moyo wake wote
bila kujali itikadi zao kuwa, UKAWA itayatekeleza haya kwa kuwa maoni ya CAG
kwa mwaka 2013/2014 yalieleza dhahiri kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza
misamaha ya kodi bila kuathiri mapato ya Serikali kwa namna yoyote ile.
WAKALA BINAFSI WA AJIRA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Kwa muda mrefu sasa Kambi ya upinzani imekua ikiwasilisha malalamiko ya
watanzania ambao wamekua wakinyonywa nguvu zao na makampuni binafsi yenye kutoa
huduma za wakala wa ajira huku wakala hawa binafsi wakinufaika. Katika hotuba
yetu ya mwaka 2014/2015 tulielezea kuwa mawakala hawa binafsi wamekua wakitumia
kampuni zao kuwaajiri watafuta kazi na si kuwaunganisha watafuta kazi na
mwajiri.Hali hii imewakosesha wafanyakazi wanaounganishwa na wakala hawa haki
zao za msingi ikiwemo likizo, huduma za matibabu, huduma za mifuko ya hifadhi
za jamii na kuwanyima mishahara na posho zao pamoja na stahiki zao nyingine.
Mheshimiwa Spika,
Kwa muda mrefu tumeelezea ni jinsi gani wizara imezembea kuchukua hatua
madhubuti za kiutawala ili kuhakikisha wakala hawa wa ajira wanafanya kazi kwa
kuzingatia sheria na kanuni za nchi yetu ikiwemo Sheria ya Huduma za Ajira Na.
9 ya mwaka 1999. Aidha, wakala hawa binafsi wengi wameendelea kufanya kazi zao
bila kulipa kodi na hivyo kulikosesha Taifa mapato. Mojawapo ya makampuni
yaliyokuwa yakiendesha huduma za ajira ni pamoja na Erolink ambayo kwa mujibu
wa Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Gaudensia Kabaka alieleza kuwa iliikosesha
Serikali mapato ya takribani Bilioni 3 kwa muda wa miaka mitatu. Na katia kipindi hiki, makampuni takribani 56
ya wakala binafsi wa ajira yalituma barua za kuomba kibali mara baada ya
Serikali kupiga marufuku makampuni ambayo hayana kibali kujihusisha na kazi za
huduma za ajira. Ikiwa kampuni moja ya Huduma za ajira imeikosesha Serikali
kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni 56 kwa miaka mitatu, je makampuni 56 ambayo yalituma maombi ya vibali yatakuwa
yameikosesha Serikali kiasi gani cha mapato?
Mheshimiwa Spika,
Ikumbukwe kuwa wakala binafsi wa
ajira pamoja na kuendelea kufanya kazi bila kibali pia zimeendelea kuwanyima
haki za msingi wafanyakazi wanaowamiliki kinyume na Sheria na utaratibu uliowekwa.
Mheshimiwa Spika,
Kampuni ya Uwakala wa Ajira inayojulikana kwa jina la ISON BPO (zamani
SPANCO BPO) imelalamikiwa kwa muda mrefu kutotoa haki kwa wafanyakazi wapatao
500 wa kitengo cha huduma kwa wateja wa Airtel waliopo jengo la Quality Plaza
na Makao Makuu ya Airtel, Morocco jijini Dar Es Salaam. Kampuni hii (ISON BPO),
ni kampuni ya uwakala wa ajira inayotokea nchini India, na imepewa jukumu la
kusimamia kitengo cha Huduma kwa Wateja na kampuni ya mawasiliano ya Airtel,
tangu mwaka 2011 katika mambo yanayohusu voice (sauti), data (internet), na
Airtel Money (huduma za kibenki kwa njia ya simu).
Mheshimiwa Spika,
Mnamo mwaka 2013, kupitia Wizara ya Kazi na Ajira, Serikali iliagiza na
kutoa maelekezo kuwa wafanyakazi katika Sekta ya Mawasiliano wanatakiwa walipwe
kiima cha chini cha Tshs. 400,000/- (laki nne) kama mshahara (basic salary).
Lakini la ajabu, la kushangaza na la kusikitisha, ni kuwa kampuni hii ya kigeni
imekuwa ikipuuzia maagizo na maelekezo hayo ya Serikali kwa kuendelea kuwalipa
wafanyakazi wake mishahara kati ya 150,000/- na 270,000/- kinyume na agizo la
Serikali. Aidha, ISON BPO, wamekuwa wakilipa kiwango hicho kwa madai kuwa wao
(ISON BPO) hawaendeshi kampuni inayojihusisha na mambo ya mawasiliano, vilevile
kwa dai lao lingine ni kuwa hawana hela za kuwalipa wafanyakazi kwa kiwango
hicho cha 400,000/- (laki nne) kama ilivyoelekezwa na Serikali. Lakini wakati
wakidai hayo kuwa hawana pesa ya kuwalipa wafanyakazi kwa kiwango hicho cha
laki nne (400,000/-), wafanyakazi wenye asili ya India wamekuwa wakilipwa
mishahara minono ya kati ya milioni tano na milioni kumi.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa Airtel waliopo chini ya Kampuni ya
ISON BPO uliotokea siku mbili kati ya tarehe 17 na 18, Aprili, 2015 ili
kushinikiza wafanyakazi hao wa Airtel kulipwa malimbikizo yote na mshahara
stahiki kama ilivyoagizwa na Serikali kupitia Wizara ya Kazi na Ajira; kwa
kuamini watu wa Wizara ya Kazi na Ajira kuwa wangeweza kutatua mgogoro huo
ambao umedumu kwa takribani miaka miwili sasa, wafanyakazi hao waliwasiliana na
maafisa kazi (labour officers) ili kupata msaada. Maafisa hao wa Wizara ya Kazi
walipofika, kwanza waliongea na wafanyakazi, na baadae waliongea na uongozi wa
ISON BPO, baada ya mazungumzo ya pande mbili kufanyika katika nyakati tofauti,
walikaa wote meza moja ya majadiliano na katika kuhitimisha, maafisa kazi
walimpa ISON BPO (mwajiri) njia mbili;
1.
ISON BPO awalipe mshahara wa laki nne (400,000/-)
na kama hawezi kulipa kiwango hicho cha fedha, basi ISON BPO wasitishe mkataba
na Airtel ili idara au kitengo cha huduma kwa wateja kirudishwe Airtel.
au;
2.
ISON BPO kama mwajiri ajadiliane na wafanyakazi ili
angalau awalipe laki tatu na nusu 350,000/-; na wakamalizia kwa kusema wao kama
Wizara hawana mamlaka ya kumlazimisha ISON BPO alipe kiwango hicho cha
mshahara, na huo ukawa mwisho wa kazi yao kama Wizara.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani tunataka kupata majibu ya malalamiko ya wafanyakazi hao wapatao 500 kama
ifuatavyo;
1. ISON BPO, ilisajiliwa kwa leseni na sheria ipi
ya nchi? 2. ISON BPO, kwa nini wanaendelea kukaidi agizo la Serikali kwa
kukataa kulipa mishahara stahiki na iliyopendekezwa na Serikali yaani 400,000/-
TZs. na badala yake wanalipa mishahara kwa kiwango wanachojua na kutaka
wenyewe? 3. Wizara ya Kazi na Ajira, kwa nini inakuwa na kigugumizi na
kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya ISON BPO katika mgogoro huu ilhali
inajua kinachoendelea kufanywa na hawa ISON BPO ni ukiukwaji wa sheria za nchi
na kuisababishia Serikali kupoteza pato la Taifa kupitia P.A.Y.E. ya
wafanyakazi hawa?
USALAMA MAHALI PA KAZI (OSHA)
Mheshimiwa Spika, kwa
muda mrefu katika hotuba zetu tumekua tukionesha wasiwasi wetu juu ya masuala
yanayohusu usalama na afya mahali pa Kazi. Ieleweke kuwa, kwa muda mrefu
tumekua tukiwasilisha malalamiko mbalimbali yanayoletwa na wafanyakazi lakini Serikali
imeendelea kuyapuuza.Maeneo mbalimbali ya kazi yamekua hayazingatii usalama na
afya za wafanyakazi wake na hivyo kuhatarisha maisha yao. Leo hii kuna
watanzania wengi waliopoteza maisha, watanzania waliopata ulemavu na matatizo
makubwa ya kiafya kutokana na kukosa usalama makazini. Lakini watanzania hawa,
hawajapewa fidia kutokana na madhara waliyopata na mbaya zaidi wengi wamekua
wakiachishwa kazi hasa pale wanapokua wakidai haki zao dhidi ya waajiri.
Mheshimiwa Spika,
Sehemu za migodini, viwanda pamoja na sekta ya ujenzi ndio maeneo
yanayoongoza kwa ajali mbaya na za kusikitisha zinazotokea mahala pa kazi.
Ikumbukwe kuwa mpaka leo hii Serikali yako baada ya kupokea malalamiko ya
wafanyakazi 79 walioachishwa kazi na kampuni ya uchimbaji iliyokuwa ikijulikana
kama African Barrick Gold Mining, ni wafanyakazi 10 tu pekee ambao walipimwa afya
na Wizara kupitia OSHA.Je, ni nini hatma ya wafanyakazi 69 ambao mpaka leo
hawajapimwa? Ni nini hatma ya wafanyakazi wote 79 ambao wanaendelea kupata
madhara pamoja na ahadi ya Serikali ya kuwapima wafanyaazi hao na kuhakikisha
wanapata haki zao kwa mujibu wa Sheria?
Mheshimiwa Spika,
Wakati Serikali ikiwa busy kuandaa mikutano na semina kwa wenye viwanda mbalimbali
nchini, inasahau kuwa baadhi ya viwanda na mahali pa kazi hawatekelezi Sheria
kwa kiwango kinachotakiwa. Leo hii Serikali inaeleza kuwa imefanikiwa kufanya
kaguzi za kushtukiza sehemu za kazi huku ni ukweli usiopingikiza kuwa baadhi za
makampuni na viwanda yana ulinzi mkali na iwapo maofisa wa OSHA watafanya
ukaguzi, vikwazo vya ulinzi pekee vinatosha kumuandaa muajiri kukwepa wajibu
wake na kujiandaa na ukaguzi kwa kuficha mapungufu yaliyopo mahali pa kazi.
MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni katika kipindi chote cha miaka mitano tumeshauri
mambo yafuatayo kuhusiana na mifuko ya hifadhi ya jamii hapa nchini;
1.Kuunganisha mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii na kubaki chini ya usimamizi wa Wizara ya
Kazi na Ajira lengo likiwa ni
kuirahisishia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi za Jamii katika kutekeleza Sheria moja nakuunda
vifungu sawa vya kisheria vitakavyosimamia utekelezaji na uendeshaji wa mifuko
hii. Tulipendekeza PPF na NSSF iunganishwe na kuwa mfuko mmoja kwa ajili ya
Sekta Binafsi vilevile LAPF, PSPF na GEPF iunganishwe na kuwa mfuko mmoja kwa
ajili ya Sekta ya Umma.
2. Tumeitaka serikali kuwa na jitihada za haraka kunusuru uhai wa Mifuko
ya Hifadhi ya jamii kwa kulipa fedha walizochota kwa ajili ya uwekezaji katika
miradi mikubwa kama ambavyo imeonyeshwa katika Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2012/2013, 2013/2014 lakini ripoti ya CAG
ambayo imetolewa hivi karibuni ya 2014/2015.
Mheshimiwa Spika,
Ni kweli kuwa sikio la kufa halisikii dawa. Madeni sugu ya serikali
yanatishia uhai wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini huku Mamlaka ya Usimamizi ya
Mifuko hiyo (SSRA) ikitoa angalizo kwa serikali kuhusiana na hali hiyo kufuatia
kuidai Sh. trilioni 8.43 kuwa hali hiyo inaweza kukwamisha mifuko hiyo kuwalipa
mafao wanachama wake, kujiendesha yenyewe na kuwekeza katika miradi mbali
mbali. Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka alitoa tahadhari hiyo Oktoba mwaka jana
mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa
kuwakutanisha wakurugenzi wa mifuko ya hifadhi ya jamii, Wizara ya Fedha, Ofisi
ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali, SSRA na Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo alieleza kuwa iwapo serikali itaendelea kukopa na
kutopeleka michango ya wanachama wake, mifuko hiyo itaathirika kiasi cha
kushindwa kulipa mafao kwa wanachama wake.
‘’ tuliyonayo, mifuko yetu ni ya pensheni, hasara
ni ya mifuko. Mwanachama hatamsamehe mwenye mfuko kwa kushindwa kumlipia, kadri
deni linavyoongezeka ndivyo Mfuko unaumia na baadaye kushindwa kulipa mafao
yanayotakiwa,”
Mheshimiwa Spika,
Kauli hii ni ya msimamizi mkuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii ambaye
ndiye mwenye dhamana ya uhai wa mifuko hii. Mara kadhaa Kambi ya upinzani
imeelezea na kuonya jinsi ambavyo madeni haya ambayo ni pamoja na PPF (bilioni
192), NHIF ( bilioni 107), NSSF ( bilioni 467), PSPF ( bilioni 4.29), LAPF (
bilioni 170) na GEPF (bilioni 6.86) yanavyohatarisha uhai wa mifuko hii. Si
Raisi Kikwete wala viongozi waandamizi wa CCM wenye kuelewa kuwa, hili ni bomu
litakapolipuka muda wowote. Ieleweke kuwa hakuna mpinzani yeyote anayepinga
miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa chuo kikuu cha Dodoma (UDOM).
Tunachokipinga ni kitendo cha Serikali kutumia fedha za wachangiaji wa mifuko
kwa miradi yake ambayo ingeweza kutekeleza ipasavyo kwa kutumia fedha nyingine
na kama ingefuta misamaha ya kodi,
ingepigana ipasavyo kuzuia ufisadi na ubadhirifu kama wa ESCROW, EPA, RICHMOND-
DOWANS na/ au kama ingeweza kupunguza matumizi makubwa ya serikali.
Mheshimiwa Spika,
Huwezi kuukataa ukweli kuwa utawala wa awamu ya nne umeshindwa kuipa
wizara ya fedha uwezo wa kitaasisi wa kukusanya kodi matokeo yake, serikali
inakuwa inakodolea macho fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii na hii ni dhambi
ambayo haitafutika machoni pa watanzania. Na sasa tunaelewa ni kwa nini serikali
ilikuwa inaishinikiza wachangiaji wa mifuko wasichukue pensheni zao mpaka
wafikishe umri wa kustaafu ambao ni miaka 60, kwa kuwa wanajua umri wa maisha
ya wa watanzania ni miaka 52. Hatuwezi kuwa na serikali ambayo ina trade-off na
ustawi wa maisha ya watu wake, hii ni aibu kubwa!
MFUKO
WA TAIFA WA HIFADHI YA JAMII (NSSF)
Mheshimiwa Spika,
mfuko wa hifadhi ya jamii, NSSF, ni mojawapo ya mifuko ambayo mbali ya kutoa
mafao ya kustaafu na huduma zingine kwa kadri dira na dhima yake lakini bado inajishughulisha katika uwekezaji
kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo ni kwamba mbali ya kuwekeza kwenye ujenzi wa
majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma na Daraja la Kigamboni, pia NSSF ina miradi
ifuatayo ya ujenzi wa nyumba;
i.
Nyumba 300 za Mtoni Kijichi (PHASE I &II) –Nyumba hizo zilikwisha
uzwa tayari
ii.
Nyumba
800-Flats 500 na Villas 300 (PHASE III) ambao umegharimu shilingi bilioni 137.
iii.
Mradi
wa AZIMIO SATELITE -Kigamboni wenye
Nyumba 7160 (Flats &Villas) –Utagharimu shilingi bilioni 871
iv.
Mradi
wa Dungu Farm-Kigamboni (Flats 568) Utagharimu
shilingi bilioni 140
v.
Mradi
wa MZIZIMA TOWER nyumba ya Ghorofa 32 unaotarajiwa kumalizika Juni 2017, ambao
utagharimu shilingi bilioni 233. Lakini hadi sasa bado mradi haujaanza.
Mheshimiwa
Spika,
Kambi Rasmi sio kama inapinga uwekezaji unaofanywa na NSSF, je uwekezaji huo
unafanywa kwa kuangalia kipindi ambacho miradi hiyo itarejesha faida za
uwekezaji (return on investment)?
Aidha, kwa mujibu wa
kifungu cha 3.12 cha mwongozo wa
Msimamizi wa Mifuko ya Hifadhi(SSRA) wa mwaka 2003, pamoja na kanuni
zake kuhusu uwekezaji salama wa mifuko
na marejeo yake ya mwaka 2012 ni kwamba, mifuko inatakiwa kuwekeza asilimiai 70
ya mali zake kwenye dhamana (T-Bills) na
hati fungani ( T-Bonds), asilimia 25 ya mali zake kwenye Miundombinu, asilimia
30 ya mali zake kwenye mali isiyohamishika (Real Estates). Je, ni kwa kiasi
gani NSSF imefuata Sheria na kanuni kuhusu uwekezaji wake mpaka sasa kwa
kufuatia mgawanyo uliotajwa?
Mheshimiwa
Spika, NSSF
walinunua majengo ya Manji (EPZ-Project) kwa jumla ya shilingi bilioni 47.5
mwaka 2006, kwa mujibu wa taarifa mbalimbali , ni kuwa majengo hayo hayakuwa na
thamani hiyo wakati NSSF inayanunua. Pamoja na hayo, mradi huu unasemekana
mpaka sasa kutorudisha thamani ya uwekezaji kwa muda. Kambi ya Upinzani Bungeni
inahusisha upandishaji huo wa thamani isiyo halisi kuwa ni mojawapo ya mianya
ya watendaji wa NSSF kujipatia 10% kwa miradi isiyo na tija. Aidha, kodi ya
mwaka ya Jengo hilo inayotokana na upangaji, haijaweza kuakisi marejesho ya
faida ya uwekezaji huo kwa kuwa mradi huo mpaka sasa umeshindwa kurudisha hata
nusu ya fedha zilizowekezwa na hivyo kuhatarisha uwezo wa mfuko kutoa marejesho
kwa wanachama wake.
Kwa mujibu wa sheria
ya SSRA, Benki Kuu ndio mamlaka ya kuhakikisha mifuko inafanya uwekezaji
makini, je kwa uwekezaji huu ambao taarifa ya CAG ilisema kuwa unauweka mfuko
katika hali ya kuweza kufilisika na hivyo wanachama kukosa mafao, Wizara ya
Fedha inatoa majibu gani?
Mheshimiwa
Spika,
kuonesha kuwa uwekezaji wa NSSF umekuwa ukiongozwa na matakwa ya watu binafsi,
kuna jengo la ghorofa 4 lililojengwa Kigoma kwa gharama ya shilingi Bilioni 7
na limekamilika sasa ni miaka 2, lakini hadi muda huu halijapata mpangaji.
Kambi ya Upinzani inahitaji kupata majibu ya uhakika kuhusu uwekezaji huu usio
na tija ni nini hatma ikiwemo uwajibikaji wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Hifadhi kwa kushindwa kuusimamia mfuko ipasavyo?
Mheshimiwa
Spika,
NSSF imenunua ardhi mikoa kadhaa kwa bei ambayo ni zaidi ya ile ya soko
(Inflated price) na mwishowe viwanja hivyo vinakosa wanunuzi. Kambi Rasmi ya
Upinzani inaona kuwa NSSF kukataa kuwekeza kwenye dhamana za Serikali na
kuwekeza kwenye majengo ni wa kutia shaka na ni mwanya wa watendaji wake
kupokea rushwa au makampuni yanayopewa kandarasi za ujenzi ni makampuni yao na
hivyo uwekezaji huo kuwanufaisha wao binafsi na si wanachama wa mfuko.
Kambi
ya Upinzani Bungeni, inataka
majibu ya kina kutoka kwa Wizara juu ya uwekezaji mzima unaofanywa na NSSF bila
kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo kwa kuwa ni dhahiri kuwa uwekezaji
mkubwa usio na tija unaofanywa na NSSF
unahatarisha kwa kiwango kikubwa uhai wa mfuko huu.
PENSHENI KWA WAZEE.
Mheshimiwa Spika,
Wazee nchini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokupata matibabu
bure,kupoteza mali zao na haki ya kurithi,kuuwawa kwa imani za kishirikina ikiwemo wazee 2,866 waliouwawa katika mikoa
10 kwa kipindi cha miaka 5 iliyopita sawa na wastani wa wazee 573 kila mwaka au
takribani mzee mmoja anauwawa kila siku. Tumeendelea kushuhudia wazee katika
nchi hii kupuuzwa, kunyanyasika na kudharauliwa huku wakijisahau kuwa na wao
pia ni wazee watarajiwa. Ikumbukwe kuwa ilikua ni ahadi ya uchaguzi ya Rais
Kikwete kuwa wazee watalipwa pensheni.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa sensa ya Watu na Makazi, 2012 wazee nchini ni milioni
2,507,568 sawa na asilimia 5.6 ya idadi yote ya watanzania. Ongezeko la wazee
nchini na duniani ni jambo lisilowezwa kupuuzwa tena kwani mtu mmoja katika
watu tisa ni mzee, hata hivyo idadi hii inategemewa kuongezeka hadi kufikia
mzee mmoja katika watu watano ifikapo 2050.
Katika hotuba zetu za miaka mitano mfululizo Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni tumeendelea kusisitiza umuhimu wa wazee kupewa pensheni, na Serikali
imekua ikitoa kauli kuwa utoaji wa pensheni kwa wazee unafanyiwa utafiti ama
uko katika hatua za mwisho. Aidha, kauli za Serikali kuwa wazee wapatiwe
matibabu bure imekua ni changa la macho kwa kuwa wazee wengi wamepata usumbufu katika
kupata huduma za afya na wengine wameshindwa kabisa kupata huduma hizo. Kwa
kuwa kauli ya kuwapa wazee pensheni ilitumiwa na CCM katika uchaguzi,
tunawataka wazee kuwa makini kwa kuwa CCM hawa hawa, watarudi tena na kauli ya
kuwalipa pensheni kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa nia ya kuwaomba kura.Tunapenda
kuwakumbusha wazee wetu kuwa ‘zimwi
likujualo halikuli likakishwa’. Na iwapo itatokea CCM kuwafata kuomba kura
wasisahau kuwakumbusha CCM kuwa ‘baniani
mbaya kiatu chake dawa’.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni naomba
kuwasilisha.
……………………………..
CECILIA DANIEL
PARESSO (MB)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
WIZARA YA KAZI NA AJIRA
25.05.2015
No comments:
Post a Comment