Tuesday, May 26, 2015

HOTUBA YA MHESHIMIWA SALUM KHALFAN BARWANY (MB) MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016. (Inatolewa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013).

UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge, Kanuni ya 99 (9) naomba kuwasilisha maoni ya Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha wa 2015/2016 ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuwasilisha hotuba hii, napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Kambi ya Upinzani Bungeni kuungana na wananchi wa Burundi na wapenda amani duniani kote kulaani mauaji ya Kiongozi wa Upinzani huko Burundi Zedi Feruzi, mkuu wa Chama cha Umoja wa Amani na Demokrasia UPD-Zigamibanga aliyeuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mjini Bujumbura huku machafuko yakiendelea nchini humo. Kiongozi huyo aliuawa Jumamosi usiku alipokuwa akiingia nyumbani kwake katika eneo la Ngagara. Mlinzi wake pia ameuawa katika tukio hilo. Kambi ya Upinzani Bungeni inalaani mauaji haya kwa kuwa ni mwendelezo wa vyama tawala kudhuru na hata kutoa uhai wa wapinzani wao pale wanapoona wameshindwa ama hawakubaliki tena kwa wananchi. Ni wajibu wetu wapinzani kusemea haya kwa kuwa hata nchini kwetu Tanzania, hatupo salama na tunaamini kuwa Mungu atatusimamia. Na ikiwa damu yetu itamwagika katika dhuluma na haki, vizazi vyetu vitasimama na kupaza sauti zao dhidi ya tawala dhalimu. Mwenyezi Mungu azilaze roho za wahanga wote wa dhuluma za kisiasa mahali pema peponi.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Kivuli wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Salum Barwany, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na kuendelea kunisimamia katika maisha yangu. Napenda kuchukua fursa hii pia kuwashukuru, ndugu, jamaa, marafiki na familia ya Mheshimiwa Barwany kwa kuendelea kuwa pamoja naye kwa hali na mali. Niwashukuru vilevile wananchi wa Lindi mjini kwa kumpa ushirikiano mkubwa mbunge wao na napenda kuwahakikishia kwa niaba yake kuwa Oktoba 2015, ataendelea kuwatumikia kama mwakilishi wao kwa ushindi wa kishindo.
Aidha, napenda kuchukua fursa kuwashukuru wabunge wote wa Kambi ya Upinzani na watendaji wake kwa ushirikiano mkubwa,  viongozi na wanachama wa vyama vinavyounda UKAWA kwa nia yao ya dhati ya kuwakomboa watanzania hasa kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.
Mheshimiwa Spika, Mwanaharakati wa Haki za Kiraia na Mkulima maarufu wa Marekani Cesar Chavez aliwahi kusema ;
“ Hatuwezi kutaka mafanikio kwa ajili yetu tu na kusahau maendeleo na ustawi wa jamii yetu... Malengo yetu ni lazima yawe makubwa kiasi ili kujumuisha matarijio na mahitaji ya wengine kwa ajili yao na kwa ajili yetu pia”.
Hii ni tafsiri ya maneno ya Cesar Chavez kwa nukuu ya lugha ya kiingereza ni kama ifuatavyo;
“We cannot seek achievement for ourselves and forget about progress and prosperity for our community... Our ambitions must be broad enough to include the aspirations and needs of others, for their sakes and for our own”
Mheshimiwa Spika, ikiwa tumebakiza miezi michache takribani miezi minne mpaka ufanyike uchaguzi mkuu ni dhahiri kuwa tutasikia kauli nyingi zenye kulenga kuwaaminisha watanzania kuwa Serikali ya CCM itaenda kutekeleza matarajio ya watanzania waliyokuwa nayo chini ya utawala wa Raisi Jakaya Mrisho Kikwete yalitolewa wakati wa Uchaguzi wa mwaka 2005 na pia uchaguzi Mkuu wa 2010.
Mheshimiwa Spika, labda tuikumbushe Serikali ya CCM usemi kuwa ‘Mla ndizi husahau ila si mtupa maganda’. Pamoja na kuwa Serikali ya CCM ilitoa ahadi kemkem zikiwemo za kuinua maisha ya watanzania kwa kauli ya maisha bora kwa kila mtanzania, mpaka kufikia leo mwaka 2015, hali za watanzania zimeendelea kuwa duni tangu kuanza kwa utawala wa awamu ya nne hasa wenye sekta ya maendeleo ya jamii , jinsia na watoto.


 Inaendelea.........


 Mheshimiwa Spika,ni wajibu wetu kuwakumbusha wanaoachia madaraka kuwa watanzania ambao kwao ni watupa maganda, hawajasahau ulaghai na ahadi zilizotolewa kwao mwaka 2005 na 2010  kwa kuzingatia yafuatayo;
MAENDELEO YA JAMII
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kwa hali iliyopo sasa, Taifa letu limekumbwa na mporomoko mkubwa wa maadili unaoochangiwa na kasi kubwa ya utandawazi.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni moja kati ya mataifa ya Afrika yenye uwezo wa kutumia historia na utamaduni wake katika kukuza maadili na jamii yenye staha. Lakini katika miaka ya karibuni, taifa letu limeshuhudia vitendo vya kuporomoka kwa maadili ambavyo vimechangia kukithiri kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti, wizi na ujambazi, mauaji, biashara ya ngono, ulevi, ngoma na sherehe zisizo  na staha, waathirika wa madawa ya kulevya na ongezeko kubwa la maambukizi ya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa.
Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Kambi ya Upinzani Bungeni imekua ikiitaka Serikali kuhakikisha kuwa masuala ya kimkakati ya kuzuia ama kupunguza mmomonyoko wa maadili kwa kuvipa uwezo vyuo vya maendeleo ya jamii pamoja na vya maendeleo ya wananchi ili kuongeza idadi ya wataalamu na kuwatumia wataalamu hao kwa maendeleo ya jamii nchini. Ni dhahiri kuwa vyuo vilivyopo vya maendeleo ya na vyuo vya wananchi havikidhi ongezeko la watu nchini na pia havipewi kipaumbele katika kuviwezesha kutoa elimu na ujuzi unaofaa kwa wataalamu wa maendeleo ya jamii nchini kwa kuwa Serikali imeendelea kutenga bajeti finyu. Vyuo vingi vimeendelea kuwepo katika majengo ambayo ni chakavu, yenye ukosefu wa miundombinu bora na ambavyo haviwezi kuendelea kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.
Upungufu wa Maafisa Maendeleo ya Jamii Nchini
Mheshimiwa Spika, tukiwa tunajadili bajeti ya mwaka ujao wa 2015/2016 huku randama ya Wizara hii ikionesha kuwa maafisa wa maendeleo ya jamii nchini wanakadiriwa kufikia asilimia 29 tu, huku Sera ya Maendeleo ya Jamii ikitaka kuwepo kwa mtaalamu ama afisa maendeleo ya jamii kwa kila kata nchini. Hii ni mojawapo ya sababu inazofanya jamii ya Kitanzania kukumbana na changamoto kama nilivyoorodhesha awali. Ni jambo la kushangaza kuwa pamoja na kuwa na vyuo vya maendeleo ya jamii ambavyo kwa mwaka 2014/2015 pekee vilikadiriwa kudaili jumla ya wanafunzi 3594 lakini bado kuna upungufu wa maafisa maendeleo ya jamii nchini. Ikiwa Serikali inajivunia ongezeko la wanafunzi katika vituo hivi, je ni nini kinachowashinda Serikali kuajiri wahitimu wa vyuo hivi ili kukabiliana na upungufu wa maafisa wa maendeleo ya jamii nchini?
Mheshimiwa Spika, maslahi duni katika fani za maendeleo ya jamii na wananchi ni mojawapo ya sababu zinazosababisha kuwe na uhaba wa wataalamu hao hasa katika ngazi za kata. Baadhi ya wahitimu wameshindwa kujiunga na kazi zinazohusiana na fani hii na kukimbilia katika kada nyengine ili waweze kujikwamua kiuchumi. Hii ni mojawapo ya sababu zinazofanya Serikali ya CCM isiwe na tija kwa muda wa miaka 10 ya kipindi cha awamu ya nne.
Mheshimiwa Spika, kumbukumbu rasmi za Bunge lako zinaonesha kuwa kwa kipindi cha miaka mitano toka kuanza kwa Mkutano Wa Kumi (10), Kambi ya Upinzani katika kila mjadala wa bajeti imekua ikiishauri Serikali kuajiri wahitimu wa vyuo vya maendeleo ya jamii mojakwamoja na kuwapangia vituo katika kata mbalimbali nchini. Lakini kwa kuwa Serikali imeendelea kupuuza maoni yetu ya Kambi ya Upinzani Bungeni, ni dhahiri kuwa Serikali imeshindwa kutekeleza jukumu lake la kuwa mlezi wa jamii zetu nchini.
Mheshimiwa Spika, ni jambo la aibu kubwa kwa Serikali ya CCM ambayo toka utawala wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere, haijaviendeleza hata vyuo vilivyoanzishwa na kujengwa kati ya miaka 1950 na 1963. Ni aibu kwa Serikali inayojivunia mafanikio, kujivunia kuchakaza majengo ya vyuo vilivyoanzishwa kwa nguvu za Baba wa Taifa na kusababisha uchakavu mkubwa. Leo CCM inaposema inamuenzi Mwalimu Nyerere, je inamuenzi kwa kuchakaza juhudi zake na kugeuza vyuo hivyo magofu? Ikiwa Serikali ya CCM imeweza kuacha kutumia magari ya zamani chakavu na kununua mashangingi kwa ajili ya viongozi wa Serikali, inashindwaje kuvipa hadhi vyuo vilivyojengwa toka enzi za Mwalimu? Hii ni aibu kubwa.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kukithiri kwa vitendo kama kangamoko, vigodoro, singo n.k (ambavyo pamoja na Kambi ya Upinzani kushauri kuvipiga marufuku na kuwatia hatiani wahusika), vitendo hivi vinaelekea kuota mizizi na kusababisha mmomonyoko wa maadili kutokana na Serikali kushindwa kutatua changamoto za maendeleo ya jamii nchini! Ni imani yetu kuwa wananchi wamekua mashahidi wa jinsi tulivyojitahidi kusimamia bajeti za Serikali ikiwemo mapendekezo ya kuinua na kuipa hadhi sekta ya maendeleo ya jamii kwa muda mrefu lakini tumepuuzwa. Ni kwa imani hiyo ambayo watanzania wanayo kwetu UKAWA, tunaamini kuwa mwaka  2016/2017 tutatoa vipaumbele wa kutatua changamoto za maendeleo ya jamii ikiwemo ufinyu wa bajeti, uhaba wa waalimu na wataalamu wa vyuo vya maendeleo ya jamii na vyuo vya maendeleo ya wananchi vyenye kuleta mabadiliko chanya kwa watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa matumizi makubwa ya Serikali na misamaha ya kodi isiyo na tija kwa taifa, imekua chanzo kikubwa cha kudumaza Taifa. UKAWA inajipanga kukabiliana na matumizi makubwa ya Serikali pamoja na kupunguza misamaha ya kodi ili kujenga vyuo vya maendeleo pamoja na kuvikarabati vyuo chakavu kwa mustakabali wa Taifa letu na vizazi vyetu.

Maendeleo ya Jinsia Nchini
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kuwa ili kuendeleza jamii yoyote kuwa jamii bora na yenye maendeleo basi kipaumbele kikubwa kiwe kuhusisha masuala ya wanawake katika mikakati ya kisera na ujumuishaji wake katika shughuli mbalimbali za maendeleo.  Pamoja na kuwa na ongezeko la wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwemo ongezeko la majaji, mawaziri na wakuu wa wilaya pamoja na wabunge ni dhahiri kuna changamoto kubwa katika kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi hizo kutokana na sifa. Aidha, changamoto kubwa pia ipo katika ngazi muhimu hasa katika ngazi za chini ambazo zinamuathiri mwanamke moja kwa moja. Ngazi hizi za maamuzi ni pamoja na ngazi za familia na vijijini ambapo mwanamke anaonekana kama mzigo ama chombo kisicho na umuhimu katika maamuzi.
Mheshimiwa Spika, ongezeko la ukatili dhidi ya wanawake nchini ni mojawapo wa viashiria kuwa, ongezeko la viongozi wanawake katika ngazi za juu hakujamkomboa mwanamke hasa wanaotoka katika mazingira duni kwa namna yoyote ile.
Uwezeshaji wa Kiuchumi
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sensa iliyofanyika mwaka 2012 inaonesha kuwa kati ya watanzania milioni 45, wanawake ni milioni 23. Pamoja na kuwa kundi hili la wanawake limechanganywa na watu walio chini ya miaka 18, inaleta taswira kuwa idadi ya wanawake nchini ni kubwa na hivyo takwimu za uwezeshaji kwa kundi la wanawake zinazotolewa na Serikali , zinaacha kundi kubwa la wanawake likiwa halijafikiwa na mafunzo na mikopo ya uwezeshaji.
Kwa mfano , kwa mujibu wa takwimu za Wizara hii zinaoesha kuwa ni wanawake 11350 tu walioweza kufikiwa na Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) ambao kwa mujibu wa taarifa hii ni sawa na asilimia 87%  na wanaume 1642 sawa na asilimia 13 kati ya mwaka 2009 na 2014. Hiki ni kiini macho cha mchana kweupe kwa kuwa ikiwa kwa mujibu wa Sensa;  wanawake na wanaume wenye umri juu ya miaka 15 ni takribani 25,200,000, basi kwa muda wa miaka 5,  Benki hii imeweza kunufaisha asilimia 0.49% ya wanawake na wanaume wa Tanzania nzima kwa miaka 5.
Ukatikili wa Kijinsia
Mheshimiwa Spika, Kama ilivyoandikwa katika Mwongozo wa Sera ya Ukatili wa Kijinsia (MOHSW 2011), ukatili wa kijinsia (GBV) ni tatizo kubwa ambalo linawanyima uhuru wanaume, wanawake na watoto kufurahia haki za msingi za binadamu na kufanya wapendavyo. Licha ya tatizo hilo kuwepo katika nchi nyingi duniani lakini halipewi kipaumbele wala halishughulikiwi ipasavyo. Ukatili wa kijinsia unatokana na tofauti za kijinsia na baadhi ya mila na desturi potofu ambazo mara nyingi zinasababisha kuwepo kwa tofauti za kijinsia katika ngazi mbalimbali za jamii. Wanawake kutothaminiwa katika familia, hali duni ya uchumi na kutofahamu sheria kunawafanya washindwe kupata msaada pindi kunapotokea ukatili wa kijinsia.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa asilimia 45 ya wanawake wametendewa ukatili wa kijinsia. Pia, kwamba wasichana watatu kati ya 10 wametendewa angalau tendo moja la ukatili wa kijinsia kabla ya kufikia umri wa miaka 18. Vilevile, zaidi ya asilimia 13 ya watoto wa kiume wenye umri ule ule wamefanyiwa matendo ya ukatili kabla ya kufikisha umri wa miaka 18. Leo Serikali inapoongelea kuhusu kufanikiwa kudhibiti ukatili wa kijinsia, unazungumzia kufanikiwa katika kuyalinda makundi haya ama katika kuandaa semina na warsha zinazowanufaisha watu wachache?
Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha hata kuona na kusikia Waziri mwenye dhamana akifurahia kujengea kamati ya Kitaifa uwezo wa kukabiliana na ukatili wakati huu ambao ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake majumbani na sehemu za kazi umeendelea kuongezeka, kati ya wanawake watatu, wawili wanatendewa ukatili wa kijinsia na wanaume.
Mheshimiwa Spika, ni aibu kuona Serikali ya CCM inajivunia kuwa mtetezi wa wanawake na watoto wakati kama nchi, bado tuna changamoto kwenye sheria za urithi na ndoa ambazo zinarudisha nyuma juhudi za kupigania usawa wa kijinsia.
Mimba za Utotoni
Mheshimiwa Spika, Kutokana na taarifa ya umaskini na maendeleo ya watu ya 2011, mimba za utotoni zilifikia 1,056 kwa mwaka mmoja tu. Wasichana wote hawa waliacha shule. Leo hii tukimaliza miaka kumi ya utawala wa Rais Kikwete, tunamaliza na maumivu ya kauli yake aliyoitoa mwaka 2010 akiwa katika ziara mkoani Mwanza akisema kuwa matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababishwa na viherehere vya wanafunzi wenyewe.
Mheshimiwa Spika, kwa Rais kutoa kauli inayowatupia lawama wanafunzi wa kike bila uchambuzi, kunaenda kinyume na azma ya   Serikali kuwajibika kwa wananchi kuhusu kufanyia kazi matatizo ya msingi yanayosababisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za Serikali kupata ujauzito. Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, mpango wa Serikali kuhusu shule za sekondari za kata ulilenga shule hizo zijengwe karibu na makazi ya wananchi ili watoto waweze kutoka nyumbani na kwenda shuleni na kurudi nyumbani kwa urahisi kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wengi wanapata elimu nzuri na bora zaidi. Lakini kwa asilimia kubwa utekelezaji wa mpango huo haujafanyika kama ilivyokusudiwa kwa sababu kuna maeneo mengi nchini ambapo wanafunzi wengi tena wenye umri mdogo chini ya miaka 17, bado wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita kumi kila siku kwenda shuleni huku wakipita katikati ya mapori, mabonde na milima yenye hatari mbalimbali kwa maisha yao ukiwemo ubakaji.
Mheshimiwa Spika, ni wanafunzi hawa wanaopata mimba za utotoni ambao wanakaa katika maeneo ambayo yanashida za maji na hivyo kulazimika kutembea umbali mrefu baada ya masomo ili kupata maji kwa matumizi ya majumbani mwao. Kushindwa kwa sera za Serikali ya CCM ndio kumepelekea watoto wa kike kukumbwa na mimba za utotoni. Kushindwa kwa Serikali kusimamia utekelezaji wa ahadi zake za kipindi cha uchaguzi ndizo zinazosababisha ongezeko la mimba za utotoni, hivyo kauli ya Raisi Kikwete si iliwaumiza waathirika wa mimba za utotoni bali pia iliwadhalilisha wazazi masikini wa kitanzania.
Kambi ya Upinzani Bungeni, inaelewa kuwa kuna baadhi ya mimba za utotoni zinazosababishwa na kuporomoka kwa maadili kwa baadhi ya watoto wa kike lakini asilimia kubwa ya wasichana waliopata mimba za utotoni, wanahitaji nafasi kwa ajili ya kurekebisha makosa. Mtoto akinyea mkono, ‘hauukati’ ni kauli ambayo sisi wazazi tunatumia katika kurekebisha watoto wetu, hivyo kulitenga kundi hili na kutolipa kipaumbele ni kuongeza mzigo katika taifa hasa watoto wa mitaani. Ni rai yetu kwa watoto wote wa kike nchini, kutumia nafasi finyu waliyopewa katika elimu ili kujikwamua. Sisi UKAWA tunaamini kuwa, kufanya kosa si kosa bali kosa ni kurudia kosa. Tunawataka wazazi wote nchini kuwa walezi na marafiki nambari moja wa watoto wao ili kujenga jamii yenye kuwajibika ili kuondokana na umasikini na matusi ya viongozi wasio na uchungu na maisha yao.
Maendeleo ya Watoto Nchini
Mheshimiwa Spika, tafiti mbalimbali zilizofanyika zinazohusu watoto hapa nchini, zimeonesha kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, wakati watoto yatima wakifikia milioni 2.4. Katika tafiti hizo, zimeonesha kuwa, tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi limeonekana Mijini na Vijijini na zaidi kwenye Miji mikubwa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Tanga, Moshi, Dodoma na Mbeya. Idadi ya watoto wanaoishi mitaani imeendelea kuongezeka kutoka 1,579 mwaka 2007 hadi 2,010 mwaka 2011, wakati watoto 11,216 wanaoishi katika Vituo vya Kulelea Watoto kati yao 6,089 ni wavulana na 5,127 ni wasichana. Aidha, idadi ya Watoto Yatima waliopo nchi nzima wamefikia 2,400,000 kati ya hao Wasichana ni 1,055,000 na Wavulana ni 1,345,000, ambapo idadi ya watoto 2,700 kati ya miaka 0-14 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini.[1]
Mheshimiwa Spika, takwimu hizo zinatoa viashiria na taswira pana juu ya watoto wanaoishi katika Mazingira hatarishi hali ambayo inachangia kwa ongezeko la watoto mitaani pamoja na kukithiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Katika taarifa ya jumla ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali juu ya ufanisi kwa mwaka 2014, inaonesha kua mfumo wa udhibiti takwimu na taarifa za watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ni dhaifu na haukidhi matakwa ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi[2]
Ongezeko la Watoto wa Mitaani na Athari zake katika Taifa
Mheshimiwa Spika, wakati piramidi ya Idadi ya Watu nchini Tanzania inaonesha kuwa idadi kubwa ya watu nchini Tanzania ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 na vijana. Asilimia 44 ya watu wote hapa nchini ni watoto wenye umri chini ya miaka 15, ambapo ongezeko la watoto wa mtaani limeendelea kuwa na athari huku sababu mbalimbali kama umasikini katika familia, mifarakano na ukosefu wa amani kwenye familia na Wazazi kutowajibika katika malezi na makuzi ya watoto wao vikipelekea watoto hao kuishi katika mazingira hatarishi. Sababu nyingine ni vitendo vya ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji wa watoto kutoka kwa familia na jamii kwa ujumla, nyingine ni kufariki kwa wazazi hasa kutokana na magonjwa mbalimbali, pia huchangiwa na ndoa za umri mdogo pamoja na mimba zisizotarajiwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni imenuia kujenga  mfumo wa utambuzi wa miji inayoongoza kwa watoto wa mitaani na kuwaweka watoto hawa wa mitaani chini ya uangalizi wa walezi watakaokuwa wakiwezeshwa  na Serikali (Foster Parents) ili kupunguza idadi ya watoto wa mitaani. Aidha, Kambi ya Upinzani imejiandaa kuhakikisha kuwa vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi hasa yatima, wanaweka mfumo wa kumbukumbu na taarifa kamili ili kufuatilia maendeleo yao popote walipo nchini Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya watoto kwa kuwa vituo vingi vimeendeshwa bila kuwanufaisha watoto hasa wanaoishi katika vituo hivyo na kwenye mazingira hatarishi.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya masikitiko napenda kuzungumzia hali ya maendeleo ya watoto wenye ulemavu mbalimbali hapa nchini. Pamoja na kuwa Wizara imepewa dhamana ya kuhakikisha maendeleo ya watoto wenye ulemavu ni endelevu, bado mikakati ya Serikali imeendelea kuweka kundi hili la watoto katika hatari kubwa. Kundi hili la watoto wenye uhitaji maalumu kama walemavu wa viungo, macho, usikivu na ngozi hajawekewa uzito wa kutosha na hivyo kuwafanya wanyonge na washindwe kuendelea kwa kasi ile ile kama watoto wengine.
Mheshimiwa Spika, wakati wa mawasilisho ya hotuba ya Bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Barwany ambaye ni waziri kivuli wa maendeleo ya jamii, jinsia na watoto lakini akiwa ni mlemavu wa ngozi alionesha wasiwasi wake juu ya dhamira ya Serikali katika kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi. Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge Mheshimiwa Jestina Mhagama alisimama na kutoa maelezo kuwa Serikali imeandaa utaratibu wa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuwaandalia tracking devices system (mfumo wa kutambua mienendo ya mlengwa) ambayo inafanywa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa watu wenye ulemavu wa ngozi na masuala ya usalama. Mhe. Barwany hakuridhishwa na kauli ile kwa kuwa yeye pia ni mmoja wa watu wanaoishi kwa wasiwasi kwenye taifa hili.
Mheshimiwa Spika, zikiwa zimepita siku mbili toka Mhe. Barwany kuonesha wasiwasi wake juu ya mfumo wa ulinzi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Mwanamama Remi Luchoma alikatwa mkono na watu wasiojulikana mkoani Katavi. Hii ni aibu kubwa kwa Serikali na ni dhahiri kuwa imeshindwa kuwalinda watu wenye ulemavu kwa kuwa kwa masikitiko na uchungu mkubwa, miezi mitatu (3) iliyopita  mwili wa mtoto Yohana Bahati aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja ambaye alikuwa ni mlemavu wa ngozi maarufu kama Albino, ambaye alitekwa siku ya Jumapili Februari 15, 2015 ulipatikana akiwa ameuawa katika eneo la Shilabela Mapinduzi kilomita kadhaa kutoka nyumbani kwao kijiji cha Ilelema.
Mheshimiwa Spika, nayazungumza haya leo kwa kuwa tunapozungumzia maendeleo ya jamii, jinsia na watoto, huwezi kuepuka kuzungumzia wanawake na watoto ambao wana ulemavu na hasa uliosababishwa na vitendo vya Kikatili. Huwezi kuacha kuzungumzia matukio ya kikatili na ya kutisha yanayoelekezwa kwa kundi hili muhimu katika jamii. Natoa maelezo haya nikiwa na masikitiko makubwa na huzuni nyingi na huku nikiwa natafakari hatma ya watu wenye ulemavu nchini kwetu wenyewe. Je, waikimbie Tanzania? Je ni nani atamfunga paka kengele? Ni nani atawasaka na kuwazuia watekaji, watesaji na wauaji wa watu wenye ulemavu hasa wa ngozi? Napinga kwa nguvu zangu zote na kuendelea kusikitishwa na vitendo vya kikatili vinavyoendelea dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Waziri Jenista Mhagama kueleza kuwa jambo la ulinzi wa watu wenye ulemavu wa ngozi haliwezi kuzungumzwa hadharani kwa kuwa Serikali ipo katika Mkakati, je leo hii anaweza kujibu ni idadi ya watu wangapi wenye ulemavu wa ngozi wauwawe ili mfumo huo uanze kufanya kazi? Anawaambia nini watu wenye ulemavu kuhusu kitendo cha kikatili cha ukataji wa kiungo cha mwanamke mwenzake kilichotokea siku mbili tu baada ya yeye kama waziri mwanamke kuhakikisha kuwa Serikali inawalinda watu wenye ulemavu wa ngozi?
Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuiomba jamii kubadilika na kuachana na imani potofu ambazo zinahatarisha maisha na usalama wa watu wengine na ambazo zinarudisha nyuma jitihada zinazofanywa za kupiga vita ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, wanawake na watoto. Hali kadhalika, tunawataka wananchi wote, kuwafichua wale wote wanaojishughulisha na vitendo hivyo na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola na mamlaka sahihi ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, nitoe wito kwa watanzania wote kutowabagua watu wenye ulemavu wa ngozi na kuchukua jukumu la kwanza la kuwa walinzi wa haki ya walemavu wa ngozi kuishi kwa kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kuwazuia wauaji na watesi wa watu wenye ulemavu.
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
Mheshimiwa Spika, Serikali ya CCM imeendelea kuuma na kupuliza kuhusu usimamizi wa mashirika yasiyo ya Kiserikali. Ni Serikali hii ambayo kwa miaka kadhaa imekua ikiyapa usajili mashirika yasiyo ya Kiserikali lakini Serikali hiyohiyo ikashindwa kuyafuatilia utendaji wake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria. Ni kweli kuwa kuna baadhi ya mashirika yasiyo ya Kiserikali ambayo yamelenga kutumia mwanya uliopo kufanya kazi kinyume na utaratibu ulioekwa lakini ni ukweli usiopingika kuwa mashirika ambayo yamegeuka kuwa mwiba kwa Serikali hasa kwa kufichua uozo na uovu wa Serikali hii ndiyo yamekuwa walengwa wa mkakati wa Serikali wa kuyafuta kwa kuwa yanafanya kazi bila kufuata mashinikizo ya CCM.
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuamini kuwa Serikali inatekeleza mpango wa kuyafutia mashirika yasiyo ya Kiserikali hasa kutokana na hofu ya kazi inayofanywa na mashirika hayo kutoa elimu kwa umma na hasa tunapoelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba. Ni jambo la kushangaza kuwa Serikali inaeleza changamoto mojawapo za mashirika yasiyo ya Kiserikali ni kujikita mijini na sio vijijini kwenye wananchi wengi wenye huhitaji, ikiwa nayo inashindwa kutekeleza wajibu na majukumu yake ya kuhakikisha maendeleo ya jamii yananufaisha vijiji na si miji peke yake inawezaje kuyafuta mashirika haya? Ni nini kinachoifanya Serikali ya CCM ifute mashirika kwa kushindwa kujikita vijijini na nini kitaizua UKAWA kuifuta CCM ambayo imeshindwa kutimiza wajibu wake kwa watanzania? Tunapenda kuikumbusha CCM kuwa, ‘mwenzako akinyolewa upara, nawe tia maji kichwa chako’.
Aidha, ni jambo la kushangaza kuona kuwa taarifa ya Wizara ya utekelezaji unaelezea changamoto kuwa mashirika haya yanategemea ufadhili wa wa nje katika kutimiza majukumu yao, Je, si Serikali hii hii ya CCM ambayo inategemea fedha za nje kuendesha miradi ya maendeleo nchini? CCM imechoka na hii ndio lala salama yao. Amkani si shwari ‘No Longer at Ease’!
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, ni katika kadhia hizi ndipo tunaamini kuwa, kwa kuwa ushauri wetu kwa miaka mingi umepuuzwa; Serikali ya CCM ijiandae kuachia ngazi ifikapo Oktoba 2015 kwa kuwa Serikali itakayoongozwa na vyama vinavyoundwa UKAWA imepanga na inatarajia kurudisha maendeleo ya jamii katika ngazi ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alitarajia kutufikisha watanzania. Nimalizie kwa kunukuu maneno ya Baba wa Taifa aliyowahi kusema
‘Uhuru na Maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana; uhusiano wao ni sawa na uhusiano baina ya kuku na yai! Bila ya kuku hupati mayai; na bila mayai kuku watakwisha. Vile vile, bila ya uhuru hupati maendeleo, na bila ya maendeleo ni dhahiri kwamba uhuru wako utapotea’
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba kuwasilisha.

                        .....................................................
Khalfan Barwany Salum (MB)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO.
25 MEI 2015.
[1] Ripoti ya “Ukatili Dhidi ya Watoto Tanzania. Matokeo ya Utaļ¬ ti wa  Kitaifa, 2009: Muhtasari wa Kuenea kwa Ukatili wa Kijinsia, Kimwili na Kiakili, Muktadha wa matukio ya Ukatili wa Kijinsia, Afya na Athari ya Tabia ya Ukatili iliyotokea utotoni, Dar es Salaam, Tanzania”, UNICEF Tanzania
[2] Ripoti Ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali Hadi Machi 2014 ukurasa  wa 11

No comments:

Post a Comment