Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Serengeti, kimezindua mpango maalumu wa kuchangia fedha chama hicho utakaojulikana kwa jina la ‘Changia Chadema Kanda ya Serengeti ili Kushinda Uchaguzi 2015.
Mpango huo unalenga kukusanya fedha zitakazotumika kusaidia kampeni za wagombea wa ubunge na udiwani katika Kanda hiyo ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Bariadi mkoani Simiyu, mara baada ya uzinduzi wa mpango huo uliofanywa na Mwanasheria Mkuu wa Chama, Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Raslimali wa Chadema Kanda ya Serengeti, Samuel Mbise, alisema mpango huo unawahusu wananchi wote.
Mbise alisema kuwa, Chadema na vyama washirika wenza katika UKAWA imedhamiria kushinda udiwani na ubunge katika majimbo yote ya mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga.
Uchangiaji wa fedha hizo utafanyika kwa kutumia simu za mikononi na fomu maalumu.
“Mpango huu utatumika kwa njia ya simu za mikononi kwa kutumia tigo pesa, M-pesa na airtel money. Tunahitaji kuiondoa CCM kwa njia ya kura kwa sababu imechoka na haiwezi tena kuleta maendeleo kwa wananchi.
“Pia zipo fomu maalumu zilizoandaliwa ambapo mtu yeyote anaruhusiwa kuchangia ili kufanikisha kuiangusha CCM katika Uchaguzi Mkuu hapo Oktoba mwaka huu,” alisema Mbise.
Naye mmoja wa wanasheria wa chama katika kanda hiyo, Wakili Ngwilimi Simba, aliyetangaza kugombea Ubunge Jimbo la Bariadi Magharibi linaloongozwa kwa sasa na Andrew Chenge, aliwaomba Watanzania kuichagua Chadema na vyama washirika wa UKAWA katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
“Ndugu zangu wananchi, tunahitaji kushinda mwaka huu ili Chadema iwasaidie kupata maendeleo. Msidanganyike tena na propaganda za CCM zikiwemo danganya toto zao za kofia, tisheti, kanga na chumvi. Ichagueni Chadema muone neema ya maendeleo,” alisema Simba.
Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapigakura wakati zoezi hilo litakapoanza Bariadi, ili waweze kutimiza wajibu na haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kuwachagua wagombea wa Chadema na UKAWA na kukiondoa CCM madarakani.
No comments:
Post a Comment