Thursday, May 28, 2015

HOTUBA YA MHESHIMIWA FELIX FRANCIS MKOSAMALI (MB) MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI-WIZARA YA UJENZI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016


1.  UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa kanuni ya 99(9) ya Kanuni za kudumu za Bunge, toleo la mwaka 2013 naomba kuwasilisha maoni ya kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya wizara ya ujenzi kwa mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, kwa unyenyekevu mkubwa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu na uwezo wa kusimama mbele ya Bunge lako tukufu kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa sekta nzima ya ujenzi. Sekta ambayo kibajeti inachukua asilimia kubwa ya bajeti lakini kihalisia ni sekta yenye madeni makubwa sana toka kwa wakandarasi na washauri.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwapongeza viongozi wetu wakuu wa vyama vinavyounda ushirikiano wa UKAWA kwa kusikiliza kilio cha miaka mingi ya wananchi juu ya kuunganisha nguvu ili kuiondoa Serikali ya CCM ambayo imeondoka kwenye misingi yake ya awali ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi na kuwa chama cha kukumbatia wala rushwa, mafisadi na mabwanyeye  na wahujumu wakubwa wa rasilimali za watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu wa kipekee ni kwapongeza wananchi wa Jimbo la Muhambwe kwa ushirikiano wanaonipatia katika kuhakikisha ninafanya vyema kazi yangu ya uwakilishi niwapo nje na ndani ya Bunge. Nasema asanteni sana, na ninasema sasa Daftari la Kudumu la Wapiga kura linaloendelea Kigoma, tuhamasishane kuhakikisha kila mwenye sifa anajiandikisha kwani hilo ndilo litaondoa utawala wa Serikali ya CCM uliolewa madaraka kwa kudhani kuwa watanzania wana macho lakini hawaoni matendo maovu yanayofanywa na wanachama na  watendaji wao.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi, kutokana na muundo wake wa kiutawala, ina majukumu yafuatayo: kusimamia sekta ya ujenzi ambayo inajumuisha Barabara Kuu na Barabara za Mikoa, Vivuko, Nyumba na Majengo ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, Aidha, Wizara ina jukumu la kusimamia Taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta ya Ujenzi, taasisi hizo ni pamoja na wakala wa Barabara, wakala wa majengo ya Serikali, wakala wa ufundi umeme, bodi ya mfuko wa barabara, baraza la taifa la ujenzi, bodi ya usajili makandarasi, bodi ya usajili wa wahandisi, bodi ya usajili wa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi. Pia wizara inasimamia chuo cha ujenzi Morogoro na chuo cha Matumizi stahiki ya nguvukazi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa utangulizo huo sasa, hotuba yetu itajikita zaidi katika maeneo ambayo tunaona bado yana matatizo makubwa.
2.  MADENI MAKUBWA YA WAKANDARASI
Mheshimiwa Spika, katika mawasilisho ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha Bungeni aliliambia Bunge lako tukufu kwamba kulikuwa na kikosi kazi cha kuhakiki madeni ambayo wizara mbalimbali zinadaiwa na wazabuni. Moja ya Wizara ambazo zinadaiwa na wazabuni na wakandarasi ni wizara hii.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi alieleze Bunge kwamba, kile kikosi kazi kilichoundwa na Wizara ya fedha ili kuhakiki uhalali wa madeni ya wizara yake. Kimebaini Wizara ya ujenzi inadaiwa kiasi gani na Wakandarasi pamoja na Wazabuni wengine?

Endelea.......


Mheshimiwa Spika, Wizara ya ujenzi ni wizara ambayo imekuwa ikitengewa fedha nyingi  za miradi ya maendeleo katika bajeti kuliko wizara zingine. Kwa mwaka wa fedha 2011/12 zilitengwa shilingi 1,155,976,936,000/-, Je madeni yalikuwa ni kiasi gani na fedha za zilizoenda kwenye ujenzi zilikuwa ni kiasi gani? Mwaka 2012/13 zilitengwa shilingi 693,948,272,000/-, Je, madeni ya wakandarasi na washauri yalikuwa kiasi gani na fedha zilizoelekezwa kwenye ujenzi zilikuwa ni kiasi gani? Mwaka 2013/14 fedha zilizotengwa ni shilingi 845,225,979,000/- Je madeni ya wakandarasi na washauri yalikuwa ni kiasi gani na fedha zilizoelekezwa kwenye ujenzi zilikuwa ni kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imetaka kuelewa madeni yaliyokuwa inadaiwa Wizara ili kuona kweli kilometa za Barabara anazosema Mhe Dr. Magufuli John Pombe ni halisia au ni ngonjera tu?

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, wizara ya ujenzi imetengewa jumla ya shilling bilioni 662,234,027,000.00 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Hadi kufikia Januari, 2014 madeni ya makandarasi na washauri yalikua ni shilingi bilioni 663,870,970,636.26

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi mpaka sasa inadaiwa zaidi ya Billion 800 na hakuna majibu juu ya ulipwaji wa madei hayo. Licha ya uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara hii kuwa na kelele na mbwembwe nyingi ukweli ni kwamba madeni ya Wizara yanazidi fedha za maendeleo tunazaopitisha na Bunge lako Tukufu.  Mfano mzuri ni Bajeti ya 2014/2015 Wizara ilikuwa na madeni yaliyofikia shilingi Billioni 760. Huku bajeti ya maendeleo kwa wizara na taasisi zake ikiwa ni bilioni 762. Ni dhahiri kabisa kuwa Wizara hii haikuwa na fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri kulieleza ukweli Bunge lako tukufu kwamba kwenye Bajeti ya 2014/2015  ni fedha kiasi gani zimelipa madeni na fedha kiasi gani  zimekwenda kwenye miradi ya Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri kuacha mbwembwe nyingi bali aeleze kuwa madeni hayo ya Billioni zaidi ya 800 yanatoka kwenye barabara zipi? Yatalipwaje? Na riba ni kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, hata kwa mwaka huu wa fedha, Bajaeti ya maendeleo ni Billion 890,572,000.00 kwa Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara huku madeni yakiwa zaidi ya Bilioni 800.  Hivyo hakuna uhalisia kati ya fedha za maendeleo zinazoombwa na madeni husika.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatakuelewa kwa undani suala hili, kutokana na kilio kilichotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakandarasi (CRB) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Contractors Association of Tanzania(CAT), Mhandisi Bi.Consolata Ngimbwa  kwenye Mkutano wa Mashauriano na Maonyesho uliofanyika tarehe 14 MEI,2015 kwenye ukumbi wa Mlimani City.

Mheshimiwa Spika, Kwa uchungu mkubwa Mhandisi huyo aliueleza umma kwamba wakandarasi watatu wamekufa kutokana na msongo wa kudaiwa na watu waliokuwa wanatoa huduma katika Kampuni zao, hii ni kutokana na Serikali kutowalipa madeni yao pale wanapomaliza kazi. Hii ni hasara kubwa kupoteza waandisi ambao tunaamini kama taifa bado tunauhitaji mkubwa wa watu hao.

3.  AHADI ZA UONGO ZA CCM KATIKA UTENGENEZAJI WA BARABARA
Mheshimiwa Spika, kila inapofika mwaka wa uchaguzi CCM imekuwa ikiahidi kujenga barabara kwa lengo la kupata kura tu,  lakini haitimizi   ujenzi wa barabara  walizoahidi.
Mifano ya Barabara ambazo Serikali ya CCM iliahidi kwenye  ilani yake na nyingine  akaahidi Mgombea wa Urais na hazijajengwa ni pamoja na:-
1.   Barabara ya Nyakanazi, Kibondo, Kasulu kidahwe Km 310 hii ni ahadi ya Serikali  ya awamu ya Tatu na ya awamu ya nne hivyo wananchi wa Nyakanazi, Kakonko, Kibondo, Kasulu na Kigoma kwa ujumla n,k hatupaswi kuchagua CCM kwa  kuwa imeahidi uongo zaidi ya miaka 20.

2.  Barabara ya Karatu – Mang’ola – Matala, barabara hii iliahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami lakini mpaka sasa haijajengwa hivyo CCM iliahidi 2010 uongo na wananchi wanaendelea kula vumbi tu.

3.  Barabara ya Karatu – Mbulu KM 77 iliahidiwa 2010 kwenye ilani ya CCM lakini. Barabara hii nayo iliahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami mpaka sasa wananhi wanaendelea kula vumbi tu.

4.  Aidha katika ukurasa wa 76 wa ilani ya CCM, iliahidi uongo kujenga  barabara ya Arusha – Moshi – Himo – Holili KM 140 mpaka sasa ni vumbi tu bado haijajengwa.

5.  Barabara ya Bunda – Kisorya – Nansio KM 93.  Hii nayo iliahidiwa na bado jaijajengwa hata KM 1.  Tazama ukurasa wa 74 wa ilani ya CCM 2010.

6.  Barabara kilombelo – Ifakara – Mahenge bado haijajengwa wakati ni ahadi ya kutafuta kura za Morogoro.

7.  Barabara ya Mpemba - Isongole yenye urefu wa km 51.5 haijajengwa ni ahadi katika Ilani yenu, hivyo wananchi wa Ileje mjihadhari na uongo wa CCM.
8.  Kolandoto –Meatu-Mto Sibiti-Singida nayo haijajengwa kama ilivyoahidiwa, hata upembuzi yakinifu bado haujafanyika, na barabara nyingine nyingi hiyo ni mifano michache tu.

Aidha zipo  ahadi mbalimbali za uongo zilizotolewa na  Rais Kikwete mpaka sasa hazijajengwa katika miji midogo mbalimbali nchini .  Mifano ya Ahadi za kutafutia kura na hazijatekelezwa ni pamoja na:-
1.  Ujenzi wa KM 2 mjini Karatu
2.  Ujenzi wa KM 1 ½  Kibondo Mjini
3.  Ujenzi wa lami mjini kondoa na Mbunge wake amekua akilia kila siku hapa Bungeni, na ahadi nyingine lukuki hiyo ni mifano tu.
Mheshimiwa Spika, pia yapo madaraja mbalimbali yaliyoahidiwa kwa mbwembwe nyingi kwa lengo la kutafuta kula tu  lakini hayajajengwa mpaka sasa mfano wa madaraja hayo ni daraja la mto sibiti ambalo mwaka 2014/15 ilitengewa shilingi bilioni 3 lakini fedha hizo hazikutolewa na Hazina. Mwaka huu wa fedha Wizara haijatenga chochote kuhusiana na daraja hilo na Mkandaraji ameondoka site.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka ufafanuzi juu ya daraja hili.

Mheshimiwa Spika, daraja lingine ni daraja la Kigamboni, ambapo Rais Kikwete aliahidi mwaka jana alipotembelea ujenzi wa daraja hilo kwamba litakamilika mwezi wa sita mwaka huu, kwa hali ilivyo inaonesha kuwa ahadi hiyo haitekelezeki.

4.  UNUNUZI WA KIVUKO CHA DAR – BAGAMOYO
Mheshimiwa Spika, kivuko hiki, kimenunuliwa kwa takribani Bilion nane fedha za kitanzania, kivuko hiki kinabeba abiria 300 na pia kinatumia masaa matatu kutoka Dar kwenda Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, ni jambo la ajabu kununua kivuko chakizamani au chakavu chenye spidi ndogo. Azam Bakhresa ana Meli inayotoka Dar kwenda Zanzibar kwa muda wa dakika 90 tu na kinabeba abiria 500 na kwa taarifa tulizonazo kinauzwa kati ya Bilioni 4 na Bilioni 5 tu.

Kambi Rasmi ya Upinzni Bungeni inaombaBunge lako kuunda Tume kwenda kuchunguza ununuzi wa kivuko hiki kibovu na cha kizamani kilichonunuliwa kwa bei kubwa huku kwa siku kikiweza kwenda Dar es Salaam mara moja tu na kurudi Bagamoyo mara moja tu, Aidha kivuko hiki kimekosa abiria kwani wananchi wanaona bora kupanda daladala kuliko kupanda kivuko kinchotumia masaa matatu.

Hivyo mbwembe na kelele za Magufuli kwamba watanunua meli kusaidi kupunguza foleni zimegonga mwamba kwa kununua kivuko kibovu na cha kizamani kinachokosa abiria.

5.  UANDISHI WA HOTUBA ZA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI KUANDIKWA KISANII
Mheshimiwa Spika, Wizara ya ujenzi imekuwa ikiandika hotuba ndefu  kuwachanganya Wabunge.  Wizara hii inaandika barabara zilizojengwa miaka ya 80 na miaka ya 90 kama vile zimejengwa hivi karibuni.
Aidha Wizara hii haina ufafanuzi unaoridhisha juu ya fedha zinazotengwa na KM zinazojengwa, mfano ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam = Chalinze – Morogoro KM 200, Sehemu ya Dar es S alaam Chalinze imetengewe Billion 2.45.  Lakini hakuna ufafanuzi kwani kilometa 100 haziwezi kujengwa kwa Billioni mbili tu.
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Dr. Waziri alieleze Bunge hili tukufu, hizo fedha zilizotengwa shilingi bilioni 2.45 kwa ajili ya kujenga kipande cha Dar es Salaam hadi Chalinze zitajenga kilometa ngapi kati ya hizo kilometa 100 anazotuambia?

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Usagara – Geita – Kyamyorwa KM 424 sehemu ya Uyovu – Bwanga – Biharamulo KM 112 imetengewa Billioni 4.97 lakini hakuna ufafanuzi fedha hizo zinakwenda kujenga KM ngapi kati ya KM 424?

Mheshimiwa Spika, Barabara ya IBANDA-ITUNGI/KAJUNJUMELE-KIWIRA PORT  (KM 26): Shilingi Milioni 405 kwa mwaka wa fedha 2015/16 lengo la Serikali ni kufanya ukarabati wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Hoja hapa ni je kilometa hizo 26 ukarabati huo utakuwa ni wa aina gani?

Mheshimiwa Spika, barabara ya NZEGA-TABORA (KM 114.7): shilingi milioni 5,336 au shilingi bilioni 5.336 kati ya hizo shilingi bilioni 2.623 ni kulipa deni la Mkandarasi kwa sehemu ya Puge –Tabora –KM 56.1 na KM 58.6 Nzega-Puge ujenzi bado unaendelea na zimetengwa shilingi bilioni 2.713. Je, fedha hizi zilizooneshwa hapa ni kulipa deni la huyo mkandarasi anayejenga Nzega-Puge ni kiasi gani? Na zinabakia kiasi gani kwa ajili ya ujenzi wa hizo Kilometa?

Mheshimiwa Spika, barabara ya SUMBAWANGA-MPANDA-KIDAHWE (KM 438): shilingi milioni 11,692,000/- lengo ni kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwa mwaka wa fedha 2015/16. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 3.586 fedha za ndani ni kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa sehemu ya Sumbawanga-Kanazi, shilingi bilioni 3.586 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa sehemu ya Kanazi-Kizi-Kibaoni. Shilingi bilioni 2.681 kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya Kizi-Sitalike-Mpanda. Je, hapa madeni ni kiasi gani na fedha halisi za ujenzi ni kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, kwa eneo jipya la Kizi-Sitalike-Mpanda ni kilometa ngapi na kiasi hicho cha shilingi bilioni 2.681 kazi gani zinakwenda kufanyika?

Mheshimiwa Spika, kiasi cha shilingi bilioni 1.839 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa sehemu ya Mpanda-Mishamo kilometa 100. Kama tulivyohoji hapo awali fedha hizi fedha kiasi gani ni kulipa wakandarasi waliokuwa wamesimamisha ujenzi (madeni) na ni kiasi gani kwa ajili ya ujenzi?

Mheshimiwa Spika, waheshimiwa wabunge tutaweza kuelewa vyema mahesabu ya Mheshimiwa Dr.Magufuli John Pombe, pale tutakapoelewa ni kiasi gani cha fedha kinajenga kilometa moja ya barabara kwa kiwango cha lami. Hivyo tunamtaka alieleze Bunge lako tukufu ni Shilingi ngapi zinajenga kilometa moja ya barabara kwa kiwango cha lami? Kinyume cha hapo ni kupeana matumaini yasiyokuwepo katika uhalisia kwa maeneo husika.

6.  BARABARA ZILIZOJENGWA NI CHINI YA KIWANGO

Mheshimiwa Spika, licha ya kwamba Wizara na hata Waziri Mkuu wanajigamba kujenga KM 13,000 za lami katika awamu ya nne ambacho ni kiwango kidogo sana ikilinganishwa na zaidi ya kilometa 86000 zinazopaswa kujengwa kwa lami. Kambi Rasmi ya Upinzani inaelewa vizuri mtandao wa Barabara ni kutoka Dar es Salaam hadi Kagera, Dar es Salaam hadi Kigoma, Dar es Salaam hadi Songea, Dar es Salaam hadi Tunduma Dar es Salaam hadi Masasi n.k. Mitandao yote hiyo wakati Serikali ya Mkapa inamaliza muda wake barabara hizo zilikuwa za lami na zingine zilikuwa zimebakiza vipande vichache vya kuunganishwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Dr. Magufuli John Jombe alieleze Bunge hizo kilometa 13,000 wanazosema kuwa Serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete imezijenga. Ziko wapi?, azitaje hizo barabara, urefu wa kila moja? na zina hali gani kwa sasa, wakati atakapohitimisha hoja yake.

Mheshimiwa Spika, hata hizo barabara ambazo zinasemwa, zimejengwa chini ya viwango na zinabomoka na  kuharibika miezi sita au pungufu au mwaka mmoja baada  ya matengenezo. Hii inaonesha kuna rushwa na parcent katika ujenzi wa Barabara za lami. Mifano ya barabara zilizojengwa na kubomoka kwa muda mfupi ni:-
1.  Barabara ya Dar es Salaam hadi Dodoma hii imebonyea upande wa kushoto na inatengenezwa kila wakati lakini inaharibika.
2.  Barabara ya Bagamoyo Msata imeanza kuharibika hata kabla haijakabidhiwa.
3.  Barabara ya Dodoma Iringa nayo imejaa mashimo kwenye maeneo kadhaa, maana yake ni kwamba imejengwa chini ya kiwango.
4.  Barabara ya Dodoma- Mwanza hasa maeneo ya mlima wa Sekenke ilibomoka muda mfupi mara tu ya kukabidhiwa Serikalini

Mheshimiwa Spika, hoja hii ya barabara kujengwa chini ya kiwango imepata nguvu zaidi kutokana na majibu ya Mhe.Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi alipolieleza Bunge kuwa kuongezeko kwa ajali za barabarani kunachangiwa na ubovu wa miundombinu kwa asilimia 7 katika ajali zote za barabarani. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza hivi barabara zilizojengwa chini ya viwango mnazipokea je kutoka kwa wakandarasi?

7.  BARABARA MBOVU KATIKA MIJI YETU
Mheshimiwa Spika, ifahamike kwamba jiji la Dar es Salaam halina planning na mara ya mwisho limepimwa mwaka 1979. Kutokana na Serikali ya CCM kushindwa kuwa na mipango ya muda mrefu hali inazidi kuwa tete katika jiji la Dar es Salaam.  Ikumbukwe kwamba kama Wizara ya Ardhi haiwezi kupima maeneo ya Miji na kufahamu barabara zitapita wapi ni dhahiri, kwamba ujenzi wa barabara utakuwa mgumu sana.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inazidi kutupa lawama kwa Serikali hii ya CCM kujenga Daraja la Jangwani kwa mabilioni ya shilingi lakini mvua zilizonyesha hivi karibuni zimepelekea maji kupita juu ya daraja hilo na hivyo njia hiyo kufungwa kwa muda. Aidha ujenzi wa Mradi wa mabasi yaendayo kasi yaani DART umesababisha adha kubwa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

8.  KUPUNGUZA MSONGAMANO KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika, kabla ya kusema chochote naomba ninukuu, sehemu ya hotuba ya Mhe.Waziri wa Ujenzi aliyoitoa Bungeni mwaka 2011/12 kuhusiana na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam, “MIRADI YA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAGARI KATIKA JIJI LA DSM.  Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na mpango wa kujenga Fyovers ili kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam. Usanifu wa Flyover eneo la makutano ya Barabara ya Mandela na Barabara ya Nyerere eneo la TAZARA umekamilika chini ya ufadhili wa JICA, mradi wa Mwenge-Tegeta unaendelea. Sehemu ya Mwenge-Morocco usanifu umekamilika na ujenzi utaanza mwaka 2012/2013 chini ya ufadhili wa JICA na mradi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni unaendelea.”

Mheshimiwa Spika, Kama tulivyosisitiza mwaka jana Kambi ya Upinzani Bungeni tunaamini juu ya ujenzi wa Flyovers  ili kuepusha kero kubwa kwenye jiji la Dar es Salaam maeneo ya TAZARA, MOROCO, UBUNGO, MAGOMENI, SURRENDER BRIDGE n.k. Serikali haina nia ya dhati kwa hilo, kwani bajeti ya 2011/12 kama ilivyonukuliwa inaonesha kuwa angalau kwa sasa tungekuwa na Fly over moja imekamilika lakini hakuna dalili zozote. Hii inaonesha kuwa Bajeti za Mhe Dr. Magufuli John Pombe (Mb) ni story za kuwafurahisha wabunge na watanzania tu. Leo anatuambia tenda za ujenzi wa fly over ya TAZARA itafunguliwa mwezi wa sita nchini Japan.

Mheshimiwa Spika, Aidha Kambi Upinzani inaamini kwamba planning za Serikali ya CCM ni finyu mno kwani flyovers zinapaswa kujengwa miji yote mikubwa kama Arusha, Mwanza, Mbeya, Iringa, Tanga n.k.  Pia hata Mikoani na Miji mingine inayokua.

9.  WAKALA WA BARABARA VIJIJINI
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mwaka  juzi na mwaka jana tuliishauri Serikali kuanzisha wakala wa Barabara vijijini, nanukuu tulichokisema, “Mheshimiwa Spika, tunatambua barabara vijijini zinasimamiwa na Halmashauri zetu ambazo nyingi hazina uwezo mkubwa wa kifedha na pia hutengewa fedha kidogo na mfuko wa barabara kulingana na kazi kubwa wanayotakiwa kufanya ya kuhakikisha kuwa barabara zinapitika katika kipindi chote cha mwaka mzima, Aidha wana ukosefu mkubwa wa nyenzo na wataalam. Kutokana na umuhimu wa barabara hizi kwa uchumi wa wananchi wetu ambao wanaishi vijijini, kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuishauri Serikali na kupendekeza kuwepo na WAKALA WA BARABARA VIJIJINI (RURAL ROADS AGENCY) kwa ajili ya usimamizi, ufanisi na ujenzi wa barabara bora vijijini”.
Mheshimiwa Spika, hoja ya Kambi Rasmi ya kuanzishwa kwa Wakala wa Barabara Vijijini ni uwepo wa umuhimu wa kusimamia matumizi ya mabilioni ya fedha zinazotolewa kila mwaka lakini hazionyeshi kama zinafanya kazi kulingana na thamani ya fedha zinazotolewa. Aidha aina ya barabara na madaraja vinavyojengwa haviendani na fedha zinazotengwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kuwanzisha wakala hii ili kusimamia barabara zinazojengwa na Halmashauri, Serikali ijayo ya UKAWA itahakikisha inaanzisha WAKALA WA BARABARA VIJIJINI ili kusimamia ubora wa barabara na madaraja yanayojengwa kwa fedha za Halmashauri.

10.              WAKALA WA UFUNDI NA UMEME-TEMESA

Mheshimiwa Spika, Majukumu ya TEMESA ni kushughulikia matengenezo ya magari, mitambo,pikipiki, mifumo ya umeme,majokofu,viyoyozi na elektroniki kwa Serikali na sekta binafsi. Aidha, Wakala unaendesha na kusimamia vivuko vya Serikali na ukodishaji wa magari na mitambo ya kusaga kokoto (Stone Crushers) na kutoa ushauri wa kitaalamu katika Nyanja mbalimbali za kihandisi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri kueleza kwanini magari ya Serikali yanatengenezwa kwenye kalakana binafsi kwa gharama kubwa  wakati wakala huyu yupo?

11.              MAGARI YANAYOZIDISHA UZITO, MIZANI NA UHARIBIFU WA BARABARA
Mheshimiwa Spika, Matakwa ya sheria  Sheria Na. 30 ya 1973 na kanuni Namba 30 ya 2001 iliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali tangazo Namba 30 la tarehe 9 Februari , 2001 iliyoanza kutumika tarehe 24 Januari 2001 inafafanua uzito wa magari unaotakiwa. Kipengele cha saba cha sheria hiyo pamoja na kanuni ya 7(3) ninaeleza magari yote yenye uzito kuanzia tani 3.5 na kuendelea na aina ya makosa ya uzidishaji uzito, ambapo kifungu cha 2, 3 na 4 vinafafanua matumizi ya uzito uliozidi asilimia tano.

Mheshimiwa Spika, Waziri wa ujenzi Mhe. Magufuli aliwahi kunukuliwa akisema ataendelea kusimamia sheria ya barabara namba 30 ya mwaka 1973, hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari ambayo yanazidisha uzito na kuharibu barabara. Namnukuu Mhe. Dr. John Pombe Magufuli“Nchini Ujerumani, uzito wa magari yote ni tani 40, Uingereza tani 40, Ufaransa tani 40, Urusi tani 38 lakini Tanzania tani 56, wakati mwingine tunakamata hadi tani 96,” alisema,Magufuli.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maeleza ikiwa uzito unaokubalika kwa barabara za Ulaya ni chini ya ule unaotakiwa hapa kwetu, na tunaamini barabara za Ulaya zina ubora zaidi ya ubora wa barabara zetu. Je anasimamia nini hasa kama uzito anaoruhusu ni mkubwa kwa uhai wa barabara zetu?
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kupinga kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ya kuruhusu malori yanayozidisha uzito kuendelea  kuharibu barabara zetu. Sambamba na hilo ni kuitaka Wizara ya Ujenzi kitengo cha mizani kuwa na mizani ambayo inauwezo wa kupima uhalisia wa uzito wa gari kinyume na ilivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.


…………………………………….
Felix Francis Mkosamali (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Ujenzi.

27.05.2015

No comments:

Post a Comment