Wananchi wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wametakiwa kubadilisha utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili kufaidi rasilimali alizonazo.
Rai hiyo ilitolewa na Katibu Mwenezi Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila, wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi Wilaya ya Buhigwe, mkoani hapa.
Aidha, aliwataka wananchi hao waunganishe nguvu zao pamoja na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ili wabadilishe utawala wa CCM.
Alisema CCM imekaa madarakani miaka 50 lakini matatizo yako palepale.
Aliwataka wananchi hao watubu kwa kosa la kumchagua mbunge wa Jimbo la Manyovu kupitia CCM, kuwa hawatarudia tena.
Alisema kwa sasa vyama vya upinzani vitachagua mgombea mmoja ambaye atasimama kwa niaba ya upinzani ili mbunge wa jimbo la Manyovu apumzike.
Alisema wakija watu wengine kuleta chama chao ambacho kiko nje ya Ukawa, wawaambie Ukawa ndiyo mpango mzima.
Alisema upungufu wa madawati Tanzania nzima ni 145,000, kila dawati moja ni Sh. 100,000 maana yake wanahitaji Sh. bilioni 14.5 lakini serikali inadai haina fedha, wakati zinaliwa na wachache.
"Pale Benki kuu watu wanagawana fedha za Escrow bilioni 306," alisema.
Alisema dunia nzima yenye nchi 193 Tanzania peke yake ni nchi ya 11 kwa mito mingi yenye maji ujazo wa kilomita za ujazo milioni 5.8 maana yake asilimia 17 ya maji ya kunywa duniani yanapatikana Ziwa Tanganyika.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi Taifa, Ambar Khamis, aliwataka wananchi kukikataa CCM ili waweze kupata maendeleo.
“Kama wewe ni mwanacha wa CCM njoo kwanza Ukawa uje ukuze maslahi yako na mafanikio yako tuko pamoja, Ukawa tumejipanga kauli ya umma ni kauli ya Mungu na mkataa wengi ni mchawi msikubali kuwa wachawi sisi wapemba tulikataa CCM sasa hivi tuna maendeleo na ninyi ikataeni ili mpate maendeleo,” alisema.
No comments:
Post a Comment