Saturday, April 4, 2015

Chadema wasafiri kwa chopa kusaka majimbo Kanda ya Ziwa

Mwanza. Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Ziwa Magharibi, kimeanzisha operesheni maalumu kwa ajili ya kusaka ubunge katika majimbo yote yaliyoko kwenye kanda hiyo ambayo yanashikiliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Operesheni hiyo inayojulikana kama ‘tigitigi’, ilianza juzi kwa kutumia usafiri wa helikopta katika majimbo kadhaa, ikiwamo Jimbo la Sengerema linaloshikiliwa na mbunge wa sasa, William Ngeleja.

Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Geita Alphonce Mawazo ni miongoni mwa makada wa chama hicho waliofika katika jimbo la Sengerema juzi, wakiambatana na kada wa chama hicho anayetaka kutangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo, Hamis Tabasamu.

Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji tofauti kwa muda wa dakika 30 katika kila kijiji, Mawazo alisema wameanzisha operesheni hiyo kwa lengo la kushinda ubunge kwenye majimbo yote yaliyoko kwenye kanda hiyo ili kuleta ukombozi wa kweli kwa wananchi.

“Wananchi naomba niwambie tumeanza na Jimbo la Sengerema, tutapambana hadi hatua ya mwisho ili kulikomboa jimbo hili. Tunataka Kanda ya Ziwa iwe ya mfano, tutazunguka kata zote na vijiji vyote katika mikoa ya Geita, Simiyu, Mwanza, Tabora, Shinyanga na Mara kuelimisha wananchi,” alisema Mawazo na kuongeza’

“Pia naomba wananchi mjitokeze kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili tuweze kupata nafasi ya kufanya mabadiliko ya kweli mwezi Oktoba. Ndugu zangu mapambano yameanza hakuna kulala, huu ni wakati wetu Chadema,” alisema.

Naye mtangaza nia wa jimbo hilo, Hamis Tabasamu ambaye aliwahi kuwa diwani wa Sengerema, alisema kuwa watafungua ofisi 78 za Chadema kwenye jimbo hilo ili wananchi waweze kuwa na sehemu za kutoa malalamiko yao kwa viongozi na kuhudumiwa.

Alisema muda uliopo sasa ni wa kufanya mabadiliko na kwamba kazi ya kutafuta ukombozi Sengerema imeanza, hivyo ni jukumu la wananchi wa eneo kuunga mkono jitihada za chama hicho za kuwaletea maendeleo endelevu.

“Mimi ni mtangaza nia wa jimbo hili nipo tayari kushirikiana na nyie kuleta mabadiliko ya kweli Sengerema. Tutafungua ofisi 78 hapa na kazi zitafanyika kila kona ya jimbo hili ili tuweze kuing’oa CCM hapa. Nia na sababu ya kuing’oa CCM tunazo kwa kuwa ni ukweli kwamba haijafanya kitu chochote katika uongozi wake eneo hilo,”alisema Tabasamu.

No comments:

Post a Comment