Wednesday, April 29, 2015

Chadema: Wanyimeni kura mafisadi.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewataka wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, kuachana na woga wa kushindwa kuwaadabisha viongozi mafisadi kwa kuwanyima kura wakati wa uchaguzi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Shinyanga juzi, Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylivester Kasulumbai (pichani), alisema wananchi wa ukanda huo wanatakiwa kuwawajibisha viongozi mafisadi kwa kutowapigia kura katika uchaguzi mkuu na kuachana na woga.

Alisema asilimia kubwa ya matatizo nchini yamekuwa yakisababishwa na wananchi wenyewe kwa kuuza utu wao kwa fulana, khanga, chumvi, sabuni na fedha ndogo ndogo kwa kuchagua viongozi wasiyo na uzalendo na matokeo yake nchi inakosa mwelekeo.

Hata hivyo, viongozi hao wa Chadema wakizungumza katika mkutano huo wa hadhara kwa nyakati tofauti, waliwataka wananchi hao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kupigiakura litakapofika mkoani Shinyanga, ikiwa ni silaha pekee ya kuukataa umaskini kwa kutowachagua viongozi wasio wazalendo.

Awali, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema wananchi wanatakiwa kuacha kuwasikiliza viongozi wasaliti kwa lengo la kujitengenezea nafasi ya kuangalia viongozi bora.

Lema alisema asilimia kubwa ya wananchi hawana ‘kitu’ hivyo ili kupata kitu, ni lazima kuangalia mfumo wa uongozi wa vyama ili kujipatia maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (Bavicha), Patrobas Katambi, alisema ni wakati kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.

No comments:

Post a Comment