Wednesday, April 29, 2015

Ukawa wajipanga kuimarisha nguvu

Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameendelea na ziara zao katika maeneo kadhaa nchini huku wakiibua mambo muhimu yanayoikabili nchi kwa sasa.

LISSU: TUSHIKAMANE KUING’OA CCM
Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amewataka Ukawa unaoundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kushikamana na kuongeza nguvu katika juhudi za kikiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akihutubia umati wa wananchi waliojitokeza katika uwanja wa Mashujaa mkoani Mtwara juzi, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa singida Mashariki, alisema vyama hivyo bila kuungana havitakuwa na uwezo wa kuing’oa CCM kutokana na takwimu za matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010.

Alisema katika uchaguzi huo uliokuwa na majimbo 239 nchi nzima, Chadema walisimamisha wagombea 179 na kujikuta wakishinda majimbo 24 pekee huku CUF ambao walikuwa na wagombea wa ubunge 189 Tanzania Bara wakiambulia majimbo mawili ya Lindi Mjini na Kilwa Kusini.

Alisema NCCR- Mageuzi mwaka 2010 waliweka wagombea 67 kati ya majimbo 239 na majimbo 172 waliwaachia CCM na kupata majimbo manne.

“Mtu anayefikiria kwamba sisi Chadema bila Ukawa tutaiweza CCM huyo mtu ni mjinga, mtu wa CUF anayesema CUF tunaweza huyo naye ni mjinga na mwambie usitupotezee muda,” alisema.

Aliongeza kuwa mfano nzuri wa umuhimu wa Ukawa ni katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana, katika Manispaa ya Mtwara Mikindani walifanya vizuri kuliko CCM ambako katika kata zote 18 wagombea wa Ukawa waliongoza, jambo ambalo linatoa mwanga wa kufanya vizuri pia katika uchaguzi ujao katika nafasi za udiwani.

Lissu alisema kwa jimbo lote la Mtwara mjini, kura zilizopigwa kwa Ukawa ni 12,724 na zile za CCM zilikuwa 8,960 na kuwafanya kuwa na matumaini makubwa kuelekea katika uchaguzi wa wabunge kwa kuwa na mtaji wa kuanzia wa kura hizo huku wapinzani wao wakiwa na mtaji mdogo wakiwazidi kwa kura zaidi ya 3,000.

“Kwa hiyo kwa matokeo haya, tukienda kama Ukawa, ubunge tutashinda na udiwani tutashinda kata zote. Tabia ya wapigakura kote duniani huwa hawabadiliki kama hawajaudhiwa, kwa hiyo msipowaudhi wapiga kura hawa kwa ushahidi huu basi Mtwara CCM hakuna,” alisema.

PROF. LIPUMBA AIVAA NEC
CUF kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuacha kutumia fedha za umma vibaya kwa kulazimisha katiba inayopendekezwa ipigiwe kura ya maoni mwaka huu, badala yake fedha hizo zielekezwe kwenye uandikishaji wa daftari la wapigakura.

Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliokuwa ukihamasisha wanachama wa chama hicho na wakazi wa Kata ya Mikindani, mkoani Mtwara kujiandikisha katika daftari la wapigakura.

Alisema tume hiyo inapaswa kufanya kazi yake pasipo kuingiliwa, vinginevyo kutasababisha migogoro na mikanganyiko isiyo ya lazima.

Prof. Lipumba alisema mshikamano wa kitaifa utapatikana endapo watu wote wataona hakuna anayebaguliwa.

Alisema kama nchi inahitaji kujenga umoja wa kitaifa, ihakikishe mikoa iliyoachwa nyuma kimaendeleo hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili nayo inufaike na kusonga mbele kimaendeleo.

Alibainisha kuwa wananchi wa mikoa ya kusini hawana ubaguzi, bali wanahitaji serikali inayotenda haki kwa kuhakikisha rasilimali zinazowazunguka zinawanufaisha na hilo sio kosa.

Kwa upande wake, Mbunge Viti Maalum, Kuruthumu Mchuchuri, aliwataka wanawake na vijana kujiandikisha kwa wingi katika daftari hilo ili muda utakapofika wafanye maamuzi ya busara kwa kuchagua viongozi kutoka CUF.

KAFULILA: UKAWA TUIONDOE CCM
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, amesema ili kuondoa utawala mbovu, ni lazima wananchi waunganishe nguvu kupitia Ukawa ili kukiondoa CCM madarakani.

Kafulila alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika Kijiji cha Mtego wa Noti, Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma.
Aliwataka wananchi kuhakikisha wanajiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura ili kuubadilisha utawala wa CCM kwa sanduku la kura.

Kafulila alisema Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza inaongozwa na Ukawa na kwamba wananchi wanapashwa kuhakikisha inaendelea kuwa chini ya umoja huo kwa kuandaa wagombea bora wa udiwani na ubunge ili kuhakikisha uchaguzi mkuu wanashinda.

Pia, aliitaka serikali kuhakikisha watendaji wote walioshtakiwa kwa makosa ya ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escow waachie ofisi zao mpaka Mahakama itakapotoa hukumu.

Alisema: “Inashangaza chombo cha serikali kama Takukuru inafikisha watumishi wa serikali mahakamani kwa makosa ya ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi za serikali, lakini bado wanaendela kukalia ofisi badala ya kusimamishwa hadi hapo Mahakama itakapotoa hukumu dhidi ya makosa yanayowakabili.”

Aidha, alisema utamaduni huo wa serikali kuendelea kuwabeba vigogo wa serikali haukuanza leo kwenye sakata la Escow na kwamba baadhi wameshtakiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mahakamani, lakini wanaendelea kukalia ofisi za umma.

Kafulila alisema inasikitisha kuona serikalini mtumishi kama mkuu wa wilaya anafanya ufisadi wilaya moja na kuhamishiwa wilaya nyingine na kwamba huko ni kulinda uozo.

No comments:

Post a Comment