Thursday, April 16, 2015

Chadema: Serikali iwajibike

SUZAN Lyimo-Waziri kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ameitaka Serikali iwajibike kwa kushindwa kuwalipa wazabuni wanaosambaza chakula katika shule za umma badala ya inawabebesha lawama wakuu wa shule, zilizofungwa ili kunusuru wanafunzi wasife njaa. 

Kauli ya Suzan ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum- Chadema, inakuja siku chache baada ya serikali kutengua likizo za baadhi ya wakuu wa shule, ikisema kuwa halmashauri zao zina fungu kwa ajili ya kuwalipa wazabuni hao. Badala yake serikali kupitia Wizara ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imeagiza wakuu hao wa shule wachukuliwe hatua kwa kufunga shule kwa madai ya kukosa chakula cha wanafunzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Lyimo amesema maamuzi hayo ya walimu kuwaongezea wanafunzi muda wa likizo yalitokana na serikali kushindwa kuwalipa wazabuni na hivyo hawakuweza kununua chakula kwa ajili ya wanafunzi.

“Hii ni aibu kubwa sana kwa serikali, na kama mdau wa elimu imenisikitisha sana. Natambua kuwa kuna baadhi ya wazabuni ni wazalendo na wengine hata wanakopa kwa ajili ya kulisha wanafunzi hao lakini wamefikia kikomo,” amesema Lyimo.

Amesema kuwa shule mbalimbali nchini zikiwemo Malangali, Mpwapwa, Chanwe, Ihungo, Rugambwa na nyingine nyingi zimeendelea na likizo ya Pasaka ili kusubiri uwepo wa chakula shuleni.

“Jana nilimwona Katibu Mkuu Tamisemi, akiongelea jambo hili na kuzitaka halmashauri zenye shule husika kufuatilia na wanafunzi warejee mara moja shuleni. Suala la kujiuliza ni; je, serikali yetu inaendeshwaje? Ni kweli kuwa Katibu mkuu wa Tamisemi hakuwa na taarifa za madai ya wazabuni? Amehoji Lyimo

Katika hatua nyingine, Lyimo amezungumzia kuhusu ajira za waalimu jambo alilosema ni kilio cha muda mrefu nchini, hususani maeneo ya pembezoni na hata mijini.

“Waziri wa Utumishi wa Umma, Celina Kombani amewahi kusema Tanzania haina tatizo kabisa la walimu wa masomo ya Sayansi za jamii (arts)- wakati sio kweli. Leo ni Aprili, zaidi ya wahitimu wa ualimu 34,000 waliomaliza katika vyuo mbalimbali nchini kawana ajira,” amesema Lyimo.

Ameitaka serikali kutekeleza wajibu wake kwa wanafunzi na kuacha kufanya maamuzi mabovu hususani katika kipindi hiki ambacho mitihani ya kidato cha sita inakaribia

No comments:

Post a Comment