Na Bryceson Mathias, Morogoro.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tawi la Mbigiri wilayani kilosa, kimesema kitamng’oa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Hemed Ibrahim Salim, kama ataendelea kutoitisha vikao kwa kisingizio cha kuogopa kukataliwa kwa kukosa taarifa ya makabidhiano.
Akizungumza na Tanzania Daima, Mwenyekiti wa Chadema Tawi hilo, Maftaha Hamis, alimtuhuhu, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho kwamba, alichapisha Vitabu vya Risiti za Michango kwa ajili ya ufuatiliaji wa Mgogoro wa Wakulima na Wafugaji, ikidaiwa fedha hizo zilizokusanywa; Zimetafunwa.
Awali ilifahamika kwamba, Mwenyekiti Salum anabanwa kuhusu taarifa ya makabidhiano ya Serikali ya Kijiji hicho kwa sababu, kabla ya kuchaguliwa Desemba 14, mwaka jana kwenye uchaguzi wa Serikali mitaa, kwa kuwa alikuwa mwenyekiti wa Mpito, baada ya aliyekuwa mwenyekiti kujiuzulu.
Hamisi alisema, “Kuna risiti feki alizochapisha na kugonga Mhuri wa Halmashauri kisiri, ambapo Wakulima waliopo kijijini mbigiri, walichangishwa Sh. 2,000/-, na Wakulima wa Mbigiri wanaoishi Morogoro Mjini walichangia Sh.5,000/-, lakini kwa masikitiko, fedha hizo zilitafunwa”.
Mbali ya fedha zenye risiti feki kutafunwa, Mwenyekiti Hamis wa Chadema, alidai sababu nyingine za kumng’oa Mwenyekiti wa CCM, Salim, ni pamoja na sintofahamu ya ziliko fedha za Ruzuku ya Kijiji Sh. Milioni 15/-, na Mifuko Saruji 50 za Mfuko wa Maendeleo wa Rais (TASAF), ambazo hazijulikani ziliko.
Aidha Hamis aliongeza kutoa madai kwamba, bado kuna sintofahamu kuhusu Shule ya Sekondari ya Mazoezi ya Mbigiri, ambayo imekuwa haifahamiki kama imesajiriwa au laa, kwa sababu tayari imetumia fedha nyingi kuikarabati, na wananchi wamechangia nguvu zao kwa kiwango kikubwa.
Awali, Mwenyekiti Salim alipohojiwa dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake, alikanusha vikali, na kudai, kuhusu mifuko 50 ya Saruji, anatakiwa ahojiwe aliyekuwa mwenyekiti kabla yake, ili kujua waliitumiaje na aliyekuwa Mkandarasi wa Sekondari ya Magore, na kuhusu Sh. Mil. 15/-, alisema zilipopelekwa kijijini hapo, zilipokelewa zikiwa na Maagizo ya Wilaya ya Kilosa, ya nini zifanye.
No comments:
Post a Comment