Monday, March 9, 2015

Mipango kumdhuru Dk. Slaa yafichuka.

Mlinzi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa (pichani), Khalid Kangezi, anahojiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, kwa tuhuma za kushiriki katika mipango ya kukihujumu chama hicho na kutaka kumdhuru Dk. Slaa.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Camillius Wambura, alithibitisha jana Kangezi kufikishwa katika kituo cha polisi Oysterbay na kwamba, hadi jana jioni alikuwa akiendelea kuhojiwa.

Taarifa za awali zilizotolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, zilieleza kuwa Kangezi amekuwa akitumiwa na maofisa 22 wa vyombo vya usalama katika miaka miwili iliyopita kufanya mipango hiyo dhidi ya chama hicho.

Alidai Kangezi amekuwa akitumiwa na maofisa usalama wa vyombo hivyo kupata taarifa nyingi za Chadema na kuwasilishwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Marando alidai mipango hiyo imegunduliwa na kitengo cha usalama cha Chadema kupitia simu za Kangezi na kwamba, ililenga kuiumiza Chadema kisiasa.

Alidai katika hujuma hizo, Kangezi amekuwa akiwasiliana na mmoja wa vigogo wa ngazi ya taifa wa CCM.

Marando alidai kuanzia Desemba, mwaka jana hadi wiki iliyopita, Kangezi alikuwa amekwishafadhiliwa Sh. milioni saba kwa ajili ya matumizi ya mawasiliano ya simu kufanikisha upatikanaji wa taarifa za Chadema kupitia vikao vyake mbalimbali, ikiwamo kamati kuu.

Alidai alipohojiwa na chama, Kangezi aliwapa kitabu chake cha kutunza kumbukumbu, ambacho kinaonyesha mawasiliano kati yake na baadhi ya maofisa wa vyombo vya usalama, aliowataja kwa majina na namba za simu zao za mikononi.

“Huyu kijana ilibidi atuandikie statement (andishi) kwa mkono wake mwenyewe. Na pamoja na mambo mengine juu ya mheshimiwa (kigogo wa CCM-anamtaja jina). ‘Mzee (anamtaja jina) mwenye simu namba (anaitaja) mimi nilimpigia mara tatu, amenitumia fedha za vocha mara mbili kiasi cha Sh. 50,000 siku ya Jumatatu tarehe 14/7/2014 na pia 150,000 tarehe 4 Desemba, 2014 siku ya Alhamisi kwa madhumuni ya kunishawishi kumpatia taarifa za siri za chama na pia kumpigia simu katika vikao mbalimbali,” alidai Marando.

Alidai kuwa wataalamu wa Chadema wamefanikiwa kuingia katika simu mbili zinazomilikiwa na Kangezi na kugundua mawasiliano aliyoongea kwa zaidi ya saa mbili au tatu katika siku, ambazo rekodi zinaonyesha kuwa zilikuwa ni za vikao vya chama.

Marando alidai wataalamu hao waligundua kuwa aliyekuwa akipigiwa simu na Kangezi kumpa taarifa za chama ni mmoja wa vigogo wa moja ya vyombo vya usalama katika wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Alidai kigogo huyo wa usalama alionekana kuwa na mawasiliano ya karibu na vigogo wawili CCM ngazi ya taifa.

“Sasa kilichotushtua zaidi, huyu kijana ametuambia katika hili andishi lake kwamba, katika siku za karibuni amekuwa akielekezwa hata uwezekano wa kutoa maisha ya Katibu Mkuu wa chama chetu, Dk. Willibrod Slaa,” alidai Marando.

Kutokana na hali hiyo, Marando alilaani suala hilo na kusema chama kilitarajia kumpeleka Kangezi polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Alipoulizwa jana na NIPASHE, Kamanda Wambura alisema Kangezi alifikishwa katika kituo cha polisi Oysterbay saa 8.14 mchana na kwamba, muda huo watu waliompeleka walikuwa wakiendelea kuandika maelezo kituoni.

Alisema Kangezi alipelekwa katika kituo hicho cha polisi na mmoja wa mawakili wa Chadema.

Kangezi alipotafutwa na NIPASHE kuzungumzia tuhuma hizo, hakupatikana na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.

Hadi tunakwenda mitamboni,Wambura alisema Kangezi alikuwa akiendelea kuhojiwa katika kituo hicho.

No comments:

Post a Comment