Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema mchakato wa uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura mkoani Njombe utakamilika Aprili 12.
Kwa mujibu wa taarifa ya NEC kwa vyombo vya habari, mashine za kielektroniki za Biometric Voters Registration (BVR), zinazotumika katika uandikishaji huo zina uwezo wa kuandikisha wapigakura kati ya 80 na 160 kwa siku.
Wakati uandikishaji huo ulioanza Februari 23 mwaka huu ukikamilika, kitendawili kinabaki kwa Nec kama itakamilisha uandikishaji kwa wakati kabla ya Aprili 30 mwaka huu ili kutoa fursa kwa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa kufanyika.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva amekuwa akikaririwa mara kadhaa akisema ili kura ya maoni iweze kufanyika ni lazima watu wote wenye sifa wawe wameandikishwa.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema jana kuwa: “Kura ya maoni kufanyika Aprili 30 ni kitendawili kwani muda uliobaki, kwa Tume haiwezi kumaliza kuandikisha nchi nzima.”
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Nec ilisema, baada ya kukamilika kwa uandikishaji itatoa ratiba ya mikoa mingine kuanza mchakato huo.
Kwa mjibu wa ratiba hiyo inaonyesha kuwa, Machi 3 uandikishaji ulianza Kata ya Kitandililo na utamalizika Machi 9. Kata ya Mahongole na Utengule utaanza Machi 11 hadi Machi 17. Machi 16 hadi Aprili 12 uandikishaji huo utaendelea Wilaya za Njombe, Makete, Ludewa na Wanging’ombe.
“Uandikishaji katika Kata tisa za Halmashauri ya Mji wa Makambako ulifanyika kwa ufanisi na mafanikio makubwa kutokana na kuvuka malengo kwa kuandikisha wapigakura 46,709 tofauti na tulivyopanga kuandikisha watu 32,370.”
“Tunawaomba viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyombo vya habari kuhamasisha wananchi wote wenye sifa za kujiandikisha katika Wilaya za Njombe, Makete, Ludewa na Wanging’ombe kujitokeza kwa wingi kujiandikisha,” ilisema taarifa hiyo ya tume.
Iliongeza: “Tangu uandikishaji uanze katika Halmashauri ya Mji wa Makambako na kumalizika, wananchi wameonyesha mwamko mkubwa wa kujiandikisha.”
Taarifa ya tume ilisema, mashine nyingi za kielektroniki za Biometric Voters Registration (BVR) zilifanya kazi kwa ufanisi mkubwa kutokana na kuandikisha wapigakura kati ya 80 na 160 kwa siku.
No comments:
Post a Comment