Friday, March 13, 2015

Dk. Slaa afichua mauaji dhidi yake; awataka TISS, Kikwete waachie ngazi

KIONGOZI mkuu wa upinzani nchini, Dk. Willibroad Slaa, amekoleza moto kuhusu madai ya kutokomeza maisha yake.

Katibu mkuu huyo wa Chadema, ameiambia MwanaHALISI Online, muda mfupi baada ya kusajili maelezo yake kituo cha Polisi cha Kati, “Mungu bado ananipenda na anakipenda Chadema.”

Alisema, “Tumepata ushahidi usio na shaka kuhusu mpango wa kutaka kuniua. Kumekuwa na mawasiliano mazito sana kati ya maafisa usalama, viongozi wakuu wa CCM na mlinzi wangu. Mawasiliano haya yalilenga kudhuru maisha yangu.”

Amesema, “Tumebaini kwamba Idara ya Usalama wa Taifa walikuwa wanafanya ujasusi dhidi ya Chadema. Walikuwa wanatoa fedha kwa mlinzi wangu binafsi ili kumshawishi kuvujisha siri za chama. Jambo hili ni kinyume cha sheria ya kuanzishwa idara ya usalama wa taifa.

Amesema, kutaka kufanya au kutishia kuua, ni kosa la jinai, hivyo analitaka jeshi la polisi kuhakikisha mhalifu huyo, anakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Taarifa zinasema, aliyekuwa anashirikiana na TISS na viongozi wa CCM kutokomeza maisha ya Dk. Slaa, ametajwa kuwa ni Khalid Kagenzi.

Kwa mujibu wa mawasiliano katika simu ya Kagenzi, aliyekiri kushiriki njama za kumuua Dk. Slaa, waliokuwa wanawasiliana na Kagenzi, ni pamoja na Philiph Mangula, makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara; Gwamaka Mwang’onda na wengine kadhaa, ambao watachapishwa katika mtandao huu katika toleo lake la Jumamosi.

Akizungumza kwa uchungu na mwandishi wa gazeti hili, Dk. Slaa amesema, “Idara ya usalama wa taifa imepoteza heshima katika jamii na kuwataka viongozi wake wajiuzulu.”

Ametoa mfano wa nchini Marekani, kwamba “…ilipothibitika Rais Nixon na chama chake cha Republican walikuwa wamefanya ujasusi dhidi ya chama cha democrats, Rais Nixon alilazimika kujiuzulu. Hata CCM na idara yao ya usalama wa taifa wanafanya kosa kama hilo.”

Mwenyekiti wa CCM na ambaye ni Rais wa Jamhuri, ni Jakaya Kikwete.

Dk. Slaa amesema yeye alifika polisi kama mlalamikaji. Alitoa maelezo yake ili kuwawezesha kufanya kazi yao ya uchunguzi.

Amesema, “Sikuhojiwa kama baadhi ya watu wanavyofikiri. Mimi sio mtuhumiwa. Mimi ni mlalamikaji.”

Amesema haki zake zote zimezingatiwa alipokuwa polisi. Aliongozana na wanasheria watatu wa Chadema, Prof. Abdallah Safari, Nyaronyo Kicheere na John Mallya.

Prof. Safari, pia ni makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara.

Zoezi la kuandika maelezo yake, lilitanguliwa na majadiliano kati yake na polisi ili kujenga picha ya pamoja kuhusu jambo litakalo andikwa.

Anasema, polisi waliuliza kama nataka waandike maelezo yangu wao au nataka kuyaandika mwenyewe. Nilichagua kuyaandika mwenyewe. Sheria inaruhusu hili pia.

Malalamiko yake yana kurasa tisa.

Akizungumzia wanachama watatu wa Chadema wanaoshikiliwa na polisi, Ahmed Sabula, Benson Mramba na Jacob Boniface (Diwani wa Ubungo), Dk. Slaa amesema, “Ni jambo la kusikitisha, muuaji yuko nje na waliozuia mauaji ndiyo wanaoshikiliwa.”

Habari ambazo zimepatikana baadaye zinasema, jeshi la polisi limeahidi kuwapa dhamana “makachero” hao wa Chadema kesho.


Chanzo : Mwanahalisi Online

No comments:

Post a Comment