Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ametakiwa kujitathimini kwanza katika utendaji wake wa kazi kuliko kuwaongezea hasira Watanzania kutokana na kutumia pesa za umma kufanya ziara wakati anakabiliwa na kashfa ya fedha kuchotwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara jijini Mwanza juzi, naibu katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Salum Mwalimu, alisema ni wakati wa Profesa Muhongo kuacha kuzunguka mikoani akitumia pesa za umma wakati anafahamu alichofanya kwenye Escrow.
“Kwanza tunashangazwa na Rais Jakaya Kikwete, kushindwa kumtolea maamuzi magumu Profesa Muhongo, amemchukulia hatua Profesa Anna Tibaijuka na kumuacha waziri huyu ambaye anatumia pesa za umma kuzungukia mikoani akidai atawapa Watanzania umeme ,” alisema Mwalimu.
Aidha akizungumzia uboreshaji wa daftari la wapigakura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR), alisema haitakiwi wanajeshi wasimamie zoezi hilo.
Mwalimu alisema kutumia wanajeshi kusimamia uandikishaji na uchaguzi mkuu mwaka huu, ni kuwatisha wananchi ambao wanahitaji kufanya uchaguzi kwa amani bila vitisho vya wanajeshi.
Akiwa wilayani Ukerewe katika kisiwa cha Ukara, Mwalimu aliwapongeza wananchi wa kisiwa hicho kwa kuipa Chadema ushindi wa vijiji saba kati ya nane ikilinganishwa na hapo awali ilikuwa na uongozi katika vijiji viwili kabla ya uchaguzi mwezi uliopita.
Alisema Watanzania hawatakiwi kurudi nyuma badala yake waongeze umoja na mshikamano walioonyesha katika uchaguzi wa serikali za vijiji na mitaa ili kuing'oa CCM madarakani, huku mwenyekiti wa Chadema wilayani humo, Jacob Munyaga pamoja na mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli, wakieleza mikakati ya chama hicho kupata ushindi wa kishindo.
No comments:
Post a Comment