Saturday, January 10, 2015

Msigwa ataka Ukawa kutolipiza visasi kwa CCM

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter msigwa (Chadema) amewataka viongozi walioshinda uchaguzi wa serikali za mitaa kupitia vuguvugu la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutolipiza visasi dhidi ya wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioshindwa.

Alisema hatua yoyote ya kulipiza visasi inaweza kupoteza imani ya wananchi dhidi ya Ukawa hasa katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Mchungaji Msigwa, aliyasema hayo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.

Mkutano huo ulilenga kuwashukuru wakazi wa jijini humo kuwachagua wagombea wengi wa upinzani kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka jana.

“Mlioaminiwa na wananchi mkachaguliwa kupitia Ukawa, hamna sababu ya kulipiza visasi kwa yale yote mliyofanyiwa na viongozi wa CCM, badala yake elekezeni nguvu zenu katika kuleta maendeleo ya wananchi,” alisema na kuongeza:

“Kama mkijielekeza kwenye visasi, wananchi watapoteza imani na nyie, hivyo malengo yetu ya kuing’oa CCM madarakani hayatafanikiwa.”

Alisema kuwa licha ya upinzani kupitia Ukawa kupata ushindi huo, kila chama cha upinzani hususani Chadema na Watanzania, wana kazi nzito ya kuhakikisha wanafanya mabadaliko ndani ya taifa kwa kuiondoa CCM madarakani.

Asema kuwa bila mabadaliko ya kiutawala, taifa litaangamia hivyo akawataka watanzania kuikabidhi nchi kwa wapinzani ili walete mabadiliko katika elimu, afya, uchumi na kurejesha heshima kwa usalama wa taifa.

Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, alisema chanzo cha vurugu na migomo inayoibuka katika maeneo mbalimbali hususani kwenye majiji ni askari Polisi na mgambo kutumiwa vibaya na watawala.

Alisema, Chadema ikishinda na kupata madiwani wengi kwenye Uchaguzi Mkuu ujao itavunja kitengo cha mgambo ili wananchi waishi kwa amani ndani ya jiji hilo.

“Chadema tukishika halmashauri ya Mbeya, kitu cha kwanza kukiondoa kitengo cha mgambo wa jiji kwani wanatumika vibaya na ndio chanzo cha vurugu kati yao, machinga na mama ntilie,’ alisema.

Kwa upande wake, Mwanamuziki wa muziki wa kizazi kipya ambaye pia ni kada wa Chadema, Joseph Haule maarufu kwa jina la ‘Professa Jay’, pamoja na kushiriki harakati za kupigania haki za raia kupitia muziki, sasa amejikita katika akiwa siasa mwanachama wa Chadema.

“Mimi ni mkazi wa pale Mikumi Morogoro, nimeingia kwenye siasa ili kupigania haki kwa watanzania wote, nimetangaza nia ya Ubunge….. na pale Mikumi ilikuwa kichaka cha CCM lakini sasa tumekisambaratisha na kuizika kabisa CCM,” alisema.

No comments:

Post a Comment