Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amemkalia kooni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akieleza kuwa endapo Rais Jakaya Kikwete hatamwajibisha, anakusudia kupeleka hoja bungeni ya kushughulikia uongo, udhaifu na utendaji mbovu katika wizara hiyo.
Mnyika , anakuwa mbunge wa pili kuahidi kutumia Bunge kumng’oa Mhongo akitanguliwa na mbunge wa Simanjiro (CCM) Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, aliyesema endapo Rais hatamuwajibisha atapaleka hoja binafsi bungeni ya kutokuwa na imani na viongozi hao.
Sendeka alisema hayo juzi katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wachimbaji wadogo na wamiliki wa migodi, uliofanyika mjini Mererani.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana, Mnyika alisema kuwa, kiporo cha Kikwete kuhusu Muhongo kinaendelea kuleta athari ndani ya wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapo tuhuma za kujipendelea kwenye uteuzi wa viongozi wanaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya wizara hiyo.
Mbunge huyo alisema anazo taarifa za ndani za wizara kuwa Shirika la Umeme (Tanesco), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Taasisi ya Uchunguzi wa Madini (MRI) kutumika kuficha udhaifu na ufisadi ukiwamo uteuzi wa watendaji.
Alisema zipo tuhuma mbalimbali alizipata kuhusu teuzi zilizofanywa kabla na baada ya kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow , ambako zaidi ya Shilingi bilioni 300 zilichotwa na kusababisha taharuki na chuki.
Alisema anakusudia kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge kupata ushahidi wa uteuzi uliofanyika.
“Kabla ya uteuzi huo, Profesa Muhongo alitangaza kwamba timu za wataalamu zimeundwa kuchambua mabadiliko ya muundo wa Tanesco, TPDC na MRI na kufanya uteuzi wa watendaji kwa ushindani.
Mnyika alisema kuna tuhuma za upendeleo katika mashirika na taasisi hizo zote tatu za wizara hiyo.
“Nitatoa kauli na kuchukua hatua baada ya kupata maelezo na vielelezo vyote kupitia vikao vya kamati za bunge hilo vinavyoanza kesho na mkutano wa Bunge unaotarajia kuanza Januari 27, mwaka huu,” alisema na kuongeza:
Wakati Mnyika akiyasema hayo, yapo madai kuwa, wajumbe wa bodi ya Tanesco iliyoteuliwa wiki iliyopita ina wajumbe wengi kutoka ukanda mmoja wa Tanzania.
Wajumbe wa bodi hiyo iliyoteuliwa na Profesa Muhongo ni Kissa Kilindu, Juma Mkobya, Dk. Haji Semboja, Shabaan Kayungilo, Dk. Mutesigwa Maingu, Boniface Muhegi, Felix Kibodya na Dk. Nyamajeje Weggoro.
Kadhalika kuna madai ya kuteuliwa kwa Mkurugenzi wa taasisi moja ya wizara kwa upendeleo akitoka kanda hiyo.
Kutokana na madai hayo, NIPASHE ilimtafuta Naibu Waziri, Charles Kitwanga, ambaye alishangaa Watanzania kuhoji ukabila badala ya vigezo walivyonavyo wateule hao.
“Karne ya 21 bado tunahoji ukabila, nilitegemea watu wangeuliza watu hawa waliopewa nafasi hizi wanavigezo gani, wengine hapa wameingia kwa vyeo vyao,” alisema.
No comments:
Post a Comment