Wakati Jeshi la Polisi likiwa kwenye operesheni ya kuwasaka watu wanaovamia, kuteka vituo vya polisi na kupora silaha, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, amemgeukia Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, Paul Chagonja, akisema anahusika katika kupanga mkakati wa kutekeleza vitendo hivyo vya uhalifu.
Amesema mkakati huo umepangwa na Kamishna Chagonja kwa nia mbaya ya kumhujumu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, ili kuchafua taswira ya uongozi wake mbele ya macho ya jamii.
Lema alisema hayo wakati akichangia mjadala kuhusu taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe, bungeni juzi.
Alisema kutokana na nchi kufikia kuwa mithili ya 'gheto', ambamo kila anayeishi humo ana uhuru wa kufanya anavyotaka, katika Jeshi la Polisi, Chagonja haamini kama Rais Jakaya Kikwete amekwishafanya uteuzi wa IGP na hivyo, kujiamulia kufanya mambo anavyotaka.
Lema alisema hali hiyo ni uthibitisho dhahiri wa taarifa alizonazo kwamba, jeshi hilo limepasuka vipande viwili, ambavyo kila upande unafanya unavyotaka.
"Na mimi nikiwaambia na nimelichunguza. Jeshi la Polisi limepasuka. Ma-RPC (makamanda wa polisi wa mkoa) wanalalamika. Chagonja haamini kama Rais ameshafanya uteuzi wa IGP," alisema Lema.
Aliongeza: "Na mimi nasema hata hizi bunduki zinaoibwa inaweza ikawa mkakati wa Chagonja ku-subotege (kumhujumu) IGP."
Alisema hata Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, pamoja na watu wote duniani wanaujua mkakati huo wa Chagonja, lakini wote wanashindwa kupaza sauti kuueleza.
"Hii nchi ni kama gheto, yaani nchi ni kama gheto kabisa. Hujui serikali iko wapi. Na tukiongea humu kuwashawishi wananchi wawe imara tunasemwa tunachochea vurugu," alisema Lema.
No comments:
Post a Comment