Saturday, January 31, 2015

Mdee amvaa Chenge

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, ametaka wabunge wachunguzwe kuhusiana na kashfa ya ufisadi wa mabilioni ya shilingi za umma unaodaiwa kufanywa na baadhi ya vigogo, na wa kwanza kuchunguzwa awe Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge (pichani).

Mdee alitoa pendekezo hilo wakati akichangia mjadala kuhusu taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), bungeni jana.

Alisema Chenge, ambaye ni mwanasheria mkuu mstaafu wa serikali, amekuwapo katika kashfa mbalimbali za ufisadi, kuanzia ile inayohusu mikataba mibovu.

Kashfa nyingine za ufisadi, ambazo alisema Chenge ameshiriki ni pamoja na inayohusu kampuni ya kufua umeme ya Independent Tanzania Limited (IPTL).

Nyingine alisema ni ya hivi karibuni, ambayo alipata mgawo wa Sh bilioni 1.6 zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

"Tuanze kuchunguzana wabunge, tuanze na Chenge," alisema Mdee.

Kauli hiyo ilionyesha kumkera Chenge, ambaye alisimama bungeni kusema amelazimika kufanya hivyo baada ya kumvumilia Mdee.

Hivyo, akasema kama Mdee ana ushahidi wa tuhuma anazozielekeza kwake, aupeleke bungeni kama kanuni za Bunge zinavyotaka.

"Mheshimiwa mwenyekiti, mimi ningelipenda Bunge hili liendelee kuwa na heshima yake. Pili, naomba sana hayo wanayoyasema wawe na ujasiri wa kwenda kuyasema nje ya ukumbi huu wa Bunge, wasijifichie katika immunity (kinga) ya Bunge," alisema Chenge.

Alisema anayo mengi ya kusema, lakini kwa sababu alisimama kuhusu utaratibu, kumtaja yeye kwa jina moja kwa moja, anaomba aweke ushahidi mezani.

Akijibu hoja hiyo, baada ya kutakiwa na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, Halima alisema kuna utaratibu wa kikanuni, hivyo kama utafuatwa na Chenge na akatakiwa na apeleke vielelezo, atavipeleka kwa kuwa hilo halina shida.

Alisema kilichokuwa kikijadiliwa jana kinahusu matumizi mabovu, mikataba mibovu na wizi wa mali za umma.

"Mzee wangu (Chenge) ni rafiki yangu, lakini leo nimeamua nimfungukie kwa sababu haya mambo yana mwisho. Kwa hiyo, mimi hiyo hoja nimeimaliza," alisema Mdee.

Awali, Mdee alisema kama vigogo wote wanaohusika na ufisadi wa fedha za umma wakichapwa barabarani, watashika adabu.
Alisema kashfa inayolikabili Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) linazuiwa kujadiliwa na Bunge kwa vile wakubwa wako nyuma yake.

No comments:

Post a Comment