Wednesday, May 28, 2014

SALAAM ZA RAMBIRAMBI KIFO CHA MWANDISHI MAXIMILIAN JOHN NGUBE

Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha mmoja wa waandishi wa habari za picha (mpiga picha) mwandamizi nchini, Maximillian John Ngube aliyefariki siku ya Ijumaa baada ya kuugua muda mfupi.

Kwa masikitiko makubwa kurugenzi, kwa niaba ya chama, inatuma salaam za pole kwa familia ya marehemu Maximilian kwa kuondokewa na baba na mpendwa wao, katika wakati ambao tunaamini walikuwa bado wakimhitaji sana kama moja ya nguzo za familia.

Kurugenzi pia inatoa salaamu za pole kwa wafanyakazi wa Mlimani Media House, (inayomiliki Mlimani Tv, Radio Mlimani na Gazeti la The Hill Observer), ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma, ambako Maximilian alifanya kazi na kutimiza wajibu wake kwa jamii kama mwandishi wa habari, hadi mauti yalipomkuta.

Salaam hizi za rambirambi pia zinatolewa kwa waandishi wa habari nchini, kwa kumpoteza mwandishi mwenzao, mmoja wa wapiga picha wakongwe, katika wakati ambao uhodari wake na utayari wa kujituma kwa ajili ya ubora wa kazi yake na chombo chake, hatimaye tasnia nzima ya upashanaji habari, ulikuwa bado ukihitajika kweli kweli.

Tunajumuika pamoja na familia, waandishi wa habari nchini na wengine wote waliowahi kufanya kazi naye, bila kusahau Watanzania wote walioguswa na kifo cha Maxi (kama alivyojulikana kwa watu wengi), ambao tunajua hata kama hawakuwa wakimjua Maxi kwa sura, lakini wamenufaika na matunda ya kazi zake nzuri katika vyombo vya habari mbalimbali nchini alivyowahi kuvifanyia kazi.

Kifo cha Maxi, si kwamba kimeacha pengo kubwa kwa familia yake na kazini kwake pekee, bali kwa tasnia nzima ya uandishi wa habari nchini.

Maxi alijulikana sana miongoni mwa waandishi na ‘sources’ wake na hatimaye jamii nzima, atakumbukwa zaidi kwa mambo matatu, uhodari (ubora) wa kazi zake, ucheshi na alivyokuwa mwalimu wa vijana wengi ambao kwa kupitia mikononi mwake, wamekuwa watangazaji wa habari au wapiga picha wazuri na hodari kama alivyokuwa Maxi, ambao wamesambaa kwenye vyombo mbalimbali nchini.

Hakuna mtu aliyemjua Maxi asiujue ucheshi wake! Hakuna mtu aliyewahi kumshuhudia Maxi akiwa kazini, ambaye asingejua ndani ya muda mfupi kuwa yule aliyekuwa mbele yake, akihangaika huku na kule, hapa na pale, kutafuta ‘angle’ au ‘shot’ nzuri, alikuwa ni mwandishi anayeipenda taaluma na kuithamini kazi yake.

Kwa watu waliofanya kazi na Maxi katika majukumu yake, kama waandishi au vyanzo vya habari au waliomfahamu kupitia maisha yake ya kawaida, hakuna maneno yatatosha kumalinza simanzi ya ghafla waliyoipata kwa kuondokewa na ‘mpiganaji’ huyu, ambaye pamoja na kufa kimwili, sifa na matendo yake katika tasnia ya habari yataendelea kudumu.

Tunawaombea wote walioguswa na msiba huu, Mwenyezi Mungu awatie nguvu na kuwapatia moyo wa subira wakati huu wa majonzi mazito ya kuondokewa na mpendwa, Maxi.
Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi Maxi.

Imetolewa leo Jumamosi, Mei 24, 2014 na

Tumaini Makene-Ofisa Habari Mwandamizi

Kny; Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano- CHADEMA

1 comment:

  1. Mnashindwa hata kuandika kifo cha mama yake Zitto, ama kweli
    Chadema mmejishusha thamani sana mbele ya macho ya wananchi. Huyu mama alikuwa mjumbe wa kamati kuu yenu. Au asie kuwepo.......Kumbukeni Chadema inajengwa na watu sio wanyama na ukiona mwenzio ananyolewa ...............

    ReplyDelete