0.1 UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, napenda
kuchuku nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema na kwa kunitumia
kama chombo cha mabadiliko hasa katika kutetea haki za wanahabari, vijana,
wanamichezo na wasanii. Namshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mhe.
Freeman A. Mbowe kwa kuendelea kuwa na imani nami katika kuisimamia Serikali katika
wizara hii. Aidha, napongeza hatua ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuungana
kwa pamoja kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania. Napongeza UKAWA kwa kazi nzuri
wanayoifanya ya kuwaelimisha wananchi nchi nzima. Napenda kuchukua nafasi hii
kutoa salamu za rambirambi kwa wasanii nchini kwa vifo vya waigizaji Adam
Kuambiana na Rachel Haule vilivyotokea hivi karibuni. Mungu azilaze Roho za
Marehemu mahali pema peponi. Amen.
Mheshimiwa Spika naomba
kuanza hotuba hii kwa kumnukuu kwa kirefu mmoja wa viongozi wetu ambao
wamejipambanua kwa namna ambayo wanastahili sifa za kuitwa ‘statesmen’, mtu
huyu si mwingine bali ni Jaji Mark Bomani, ambaye hivi karibuni wakati akitoa
hotuba kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo Duniani, alinukuliwa na vyombo vya
habari akisema;
“Inasikitisha kuona kuwa hali
ya Mtanzania inazidi kudidimia au kubaki pale pale katika sehemu nyingi hasa
vijijini katika kipindi cha miaka 40 iliyopita kwa kukosa fursa muhimu za
maendeleo na viongozi hawalioni hilo.”
Vyombo vya habari vilimnukuu
zaidi Jaji Bomani akisema “nchi itaendeshwa kwa kusimamia haki na ukweli na
kuwataka wanahabari wasichoke kuisimamia haki na uhuru wa nchi yao bila woga
kwani bila kufanya hivyo nchi itaongozwa kiimla.
“Ni aibu kuona mswaada wa
sheria ya habari umekwama kwa zaidi ya miaka 10 kwa sababu ambazo hadi leo
hazijaeleweka.”
Akawataka waandishi wa habari,
Akawataka waandishi wa habari,
“wasikate tamaa na badala
yake waendelee na kupambana kuhakikisha kwamba harakati za kupata Sheria ya
Haki ya Kujua inafanikiwa ili kupunguza matukio ya manyanyaso, kupigwa,
kuteswa, kufungwa kwa vyombo vya habari na kuuwawa.”
“Haki haiombwi simamieni haki zenu na songeni mbele.”
“Haki haiombwi simamieni haki zenu na songeni mbele.”
2.0
MAENDELEO YA SEKTA YA HABARI NCHINI
2.1
Miaka 10 ya mapambano na ahadi za uongo uliofika ngazi ya kimataifa
Mheshimiwa
Spika,
naomba kuchukua nafasi hii kuzungumzia vyombo vya habari. Kwanza napenda
kuvishukuru kwa kazi kubwa inayofanywa na ‘mhimili’ huu usio rasmi katika kuimarisha
demokrasia na kupigania umuhimu wa uongozi nchini kwetu.
Vyombo vya habari vimekuwa
mstari wa mbele kuibua na kuweka bayana vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali
ya umma na matumizi mabaya ya madaraka licha ya sheria mbaya na kandamizi
ambazo zinaendelea kuminya uhuru wa habari na haki ya kupata habari kwa
wanahabari na wananchi kwa ujumla.
Mheshmiwa
Spika, kwa muda
mrefu sasa Kambi ya Upinzani Bungeni tumezungumza kwa kirefu, tukishauri, kutoa
angalizo, kuonya na kuelekeza kwa mapana na marefu kuhusu kufuta sheria kandamizi
zilizopo zinazominya uhuru wa habari na kupata taarifa na badala yake zitungwe sheria
zingine ambazo zitaimarisha uhuru huo na kusaidia kukomaza demokrasia nchini. Mapambano
haya ya wananchi kupigania uwepo wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na
Haki ya Kupata Habari si ya leo. Yameanza tangu mwaka 2007.
Mheshimiwa
Spika,
katika namna ya kipekee ambayo ilipaswa kuungwa mkono na serikali hii kama ingelikuwa
ni sikivu, wadau wa habari kwa jitihada za kulisaidia taifa lao, walichukua
jukumu la kukusanya mawazo na mapendekezo ya wadau mbalimbali wa habari kuhusu
namna ya kuboresha miswada ambayo ilikuwa imeandaliwa na serikali. Mapendekezo
hayo yaliwasilishwa serikalini tangu mwaka 2007 kwa sheria ya Haki ya Kupata
habari na 2008 kwa sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.
Hatuna haja ya kurudia kusema
juu ya danadana ambazo Serikali hii ya CCM imezifanya tangu wakati huo hadi
sasa nchi imeshindwa kuwa na sheria nzuri kama ilivyopendekezwa na wadau. Mwaka jana wananchi walifarijika walipomsikia
Rais Jakaya Kikwete akitoa ahadi kwa maneno mazito mbele ya mkutano wa
kimataifa kuwa serikali ingeleta muswada wa Sheria wa Haki ya kupata Taarifa ifikapo
mwezi Aprili mwaka huu!
Mheshimiwa
Spika, Rais
Kikwete alikuwa akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Serikali Uwazi ulioitishwa
na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroun ambao ulijadili masuala mbalimbali
ikiwa ni pamoja na uwazi katika manunuzi ya umma, uwazi
katika mikataba, haki ya kupata habari, uwazi katika ukaguzi wa fedha za umma,
uwazi wa Serikali na vyombo vya habari, uwazi katika mikataba ya maliasili,
uwazi katika maendeleo ya nchi zinazoendelea.
Akizungumza kwenye
mkutano huo Alhamis ya Oktoba 31, Rais Kikwete si tu kwamba aliwaahidi
Watanzania bali pia alitumia jukwaa hilo la kimataifa kuitangazia dunia nzima
kuwa Serikali yake tayari inafanyia kazi utungaji wa Sheria ya Kupata Taarifa,
kwa ajili ya kuwapatia wananchi haki ya kupata taarifa kutoka serikalini.
Vyombo vya habari
mbalimbali, vya ndani na nje ya nchi, vilimnukuu Rais Kikwete akitoa ahadi
hiyo, kwa kusema;
"Kama watu wanataka kupata taarifa kuhusu
namna gani dawa zinagawanywa, kama wanataka kupata taarifa kuhusu bajeti za
shule zao za msingi, wanastahili kuwa na haki ya kuzipata. Kama watu wanataka
kupata taarifa kuhusu lini watasambaziwa maji wanapaswa kuwa na haki hiyo. Pale
watu wanapotaka kupata taarifa, haipaswi kuonekana kuwa wanaingia mahali ambapo
hapawahusu.”
Gazeti la The
Guardian likiandika kuhusu ahadi hiyo ya Serikali ya CCM, lilisema hivi;
“Ahadi hii inawakilisha moja ya hatua kubwa
kuelekea haki ya kupata taarifa na suala la Serikali Uwazi nchini Tanzania.
Hata hivyo, kama ilivyo ada siku zote, jaribio halisi litakuwa ni katika
utekelezaji (wa ahadi hiyo).”
Watu wengi hawajui
kuwa kabla ya kutoa ahadi hiyo nchini Uingereza ambako Rais Kikwete
aliitangazia dunia kuwa Tanzania itatunga sheria ya uhuru wa habari na kupata
taarifa yenye viwango vya kimataifa, pia aliwahi kutoa ahadi ya namna hiyo hiyo
kwenye mkutano kama huo, nchini Brazil mwaka mmoja kabla ambako alisema hivi;
“Ninaahidi kuwa tutafanya kadri
ya uwezo wetu wote kutimiza matarajio ya ushirikiano huu ili kuhamasisha uwazi
na uwajibikaji wa serikali yetu kwa wananchi wa Tanzania. Napenda
kuwahakikishia kwamba utashi wetu wa kisiasa kufanikisha malengo ya OGP
hayatakwama kwa sababu dhana ya Serikali Uwazi iko kwenye moyo wa mkataba kati
ya dola na wananchi.”
Mwandishi katika
Gazeti hilo la The Guardian akamalizia kwa kusema
“Je
Tanzania inaweza kusimama imara kutekeleza maneno haya mazito?”
Swali hilo linaweza
kujibiwa na viongozi wa Serikali hii ya CCM ambao sasa si kwamba wanaweza kutoa
ahadi za papo kwa papo za kuwahadaa Watanzania pekee, bali sasa wamevuka mipaka
ya nchi na kutoa ahadi za uongo dunia nzima ikiwasikiliza. Si tu kwamba hawaoni tatizo kuahidi, bali sasa
hawaoni shida hata kutotekeleza kila wanachoahidi. Hii ni dalili ya wazi ya
ukosefu wa dhamira na uwezo wa kukidhi matarajio ya watu.
Mheshimiwa
Spika, katika hali ambayo kwa kweli wadau wa habari
nchin wanapaswa kuanza kumjua adui yao halisi kwenye mapambano ya kupata sheria
hizi mbili muhimu, ni kitendo cha CCM kupitia kwenye vikao vyake vya ndani
kutoa maelekezo kwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na chama hicho
na washirika wake, ambayo kwa ujumla yanapingana na dhana nzima ya uwepo wa
sheria hizo.
Katika waraka wake
wa siri ambao umeripotiwa mara kadhaa na vyombo mbalimbali vya habari, CCM
imeamua kujiandikia rasimu nyingine ambayo chama hicho ndiyo kinataka eti
Katiba Mpya ya nchi. Katika nyaraka hiyo, vikao vya CCM ambavyo vinaongozwa na
Mwenyekii wake Jakaya Kikwete, kimepinga dhana za uwazi, uadilifu na
uwajibikaji kama ambavyo zimependekezwa na wananchi ili ziwe sehemu ya tunu za
taifa ndani ya katiba.
Mheshimiwa
Spika, hali hii si tu kwamba inawachanganya wananchi,
lakini inaibua munkari wa kuhoji iwapo Rais Kikwete kupitia serikali yake,
wanayo dhamira ya kuheshimu na kutambua mchango wa vyombo vya habari na umuhimu
wa wananchi kuwa na taarifa juu ya namna nchi yao inavyoendeshwa! Ni suala
linalochanganya na kuibua maswali mengi yasiyokuwa na majibu kuona Rais Kikwete
anatoa ahadi kimataifa kuhusu kukuza uwazi na uwajibikaji kwa kuimarisha uhuru
wa habari na kupata taarifa, lakini wakati huo huo akiwa hapa nchini bali ya
serikali yake kushindwa kutimiza ahadi hiyo, anasimamia vikao vya chama chake
ambacho kinapinga maoni ya Watanzania wanaotaka Katiba Mpya izingatie uwazi,
uadilifu na uwajibikaji!
Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia majibu ya Serikali yaliyotolewa
hapa bungeni kwenye mkutano huu wa 15 kikao cha 16 kuhusu miswada ya sheria
hizi mbili na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Ubungo John Mnyika na Serikali
ikashindwa kutoa majibu ya kuridhisha, inazidi kudhihirisha kuwa hakuna dhamira
ya dhati kutekeleza jambo hili. Sasa maelezo ya Mheshimiwa waziri wa Sheria na
Katiba, Dr. Asha Rose Migiro katika hotuba ya Makadirio ya wizara yake ni kuwa waraka
wa kupeleka kwenye Baraza la Mawaziri wa kupendekeza kutungwa kwa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa
umeandaliwa.
Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni ilitarajia Serikali ya CCM kutambua umuhimu wa kutekeleza ahadi zake
hapa bungeni kwa miaka 7 lakini zaidi ya hapo kutimiza ahadi iliyotolewa na
Rais Kikwete ili kumwokoa na aibu ya kusema uongo kwenye mkutano mkubwa wa
kimataifa wa Open Government Partnership, mjini London. Tulitarajia Serikali
hii ingelikuwa sikivu, ingetambua kuwa sheria hizo ni mtambuka na inahusu
wananchi wote katika haki ya kupata na kutoa taarifa kama ilivyoelekezwa na
Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Mheshimiwa
Spika, Kambi
ya Upinzani inalaani kwa nguvu zote, sheria kandamizi zinazonyima vyombo vya
habari uhuru wa kufanyakazi zake kwa ufanisi, za kufichua maovu kama rushwa,
ubadhirifu wa mali za umma na hujuma za raslimali za taifa. Sheria hizo
zinatishia uhuru wa uhariri na kuleta woga wa kushtakiwa kwa makosa ya jinai.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imekuwa ikitoa ahadi ya kuleta Bungeni muswada wa sheria ya Huduma za Vyombo
vya Habari ambazo zitasimamia utendaji kazi wa vyombo vya habari nchini. Wote tunafahamu
kuwa sheria zilizopo zinazosimamia vyombo vya habari ni mbaya, ni kandamizi na
hazina nafasi katika nchi inayojinadi kuwa ni ya kidemokrasia. Sheria hizi zinavifanya vyombo vya habari na
wanahabari kutekeleza majukumu yao katika mazingira magumu. Katika vikao vya
bunge kwa takriban miaka saba sasa, tumekuwa tukisikia ahadi za serikali ya
kubadilisha sheria hizi kandamizi ambazo kwa kiasi kikubwa zinakiuka Ibara ya
18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa
Spika, tunawasiwasi
mkubwa wa nia ya serikali ya kufanya mabadiliko stahiki. Tunaona hakuna dhamira
ya dhati ya kuleta sheria bora. Hili limedhihirishwa na hatua ya serikali ya
mwezi Novemba mwaka 2013 ya kuleta mabadiliko ya sheria mbalimbali
(Miscellaneous Ammendement Act) ambayo ndani yake ilikuwa na mapendekezo ya
Sheria ya Magazeti 1976, Sheria ya Filamu na Michezo ya Jukwaa na Sheria ya
Kanuni za Adhabu ambazo zilikuwa na lengo ya kuongeza adhabu kubwa kwa makosa
ya kitaaluma.
Ni
muhimu sana kwa Serikali kuacha kutoa ahadi hewa hapa Bungeni na kwingineko na
badala yake tudhihirishe utashi wetu kwa kutekeleza kwa vitendo. Ahadi
zinazotolewa na mawaziri miaka nenda miaka rudi hapa Bungeni bila kutekelezwa
zinashusha hadhi ya Bunge na Taifa letu machoni mwa watanzania na dunia kwa
ujumla. Ni jambo lisilopendeza na ni la aibu kwa kweli kwani inaonyesha dhahiri
kuwa ama utendaji kazi ni hafifu sana katika serikali hii au la basi Serikali hii
haina nia njema ya kufanya marekebisho ya kimfumo ili tuwe na sera na sheria
nzuri ambazo zitastawisha demokrasia, uwazi na uwajibikaji.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani Bungeni inawataka mawaziri husika wawe jasiri na watimize
ahadi walizotoa kwenye Bunge hili tukufu za kuleta miswada ya sheria za Haki ya
Kupata Taarifa na ule wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari. Wadau wa habari wameshafanya kazi kubwa kwa
kutoa mapendekezo yao serikalini. Wayatumie mapendekezo hayo kuandika miswada
hiyo na kuileta hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika,
wenzetu wadau wa habari wamejipanga kuboresha na kuinua hali ya uwajibikaji na
maadili katika vyombo vya habari. Tuwaunge mkono kwa dhati kwenye hilo. Kupitia
Baraza lao la habari wamepitisha Azimio la Dar es Salaam ambalo linazungumzia
haki na wajibu wa vyombo vya habari katika kuimarisha weledi, maadili na uhuru
wa uhariri.
Napenda
niongeze kwa lengo ya kuweka msisitizo kuwa Haki ya Kupata Taarifa ni muhimu na
ya msingi sana, kwani ni sheria mtambuka na inahusu haki ya
msingi ya kupata habari ambayo ni haki inayolindwa kikatiba. Ni ukweli wa
uhakika kuwa utawala ulioshamiri katika mila za usiri
ndio ulioifikisha Tanzania yetu mahali hapa pabaya. Ndio chanzo cha mikataba
mibovu na kushindwa kwa uwajibikaji kwa sababu tu watendaji wabovu wanaweza
kujificha katika kinga ya usiri. Kambi Rasmi ya Upinzani tunaitaka Serikali kuleta
Bungeni muswada wa sheria ya Haki ya Kupata Habari ndani ya mwaka huu kama
alivyoahidi Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inasisitiza tena kuwa uwepo wa sheria nzuri za
vyombo vya habari ambayo itakuwa kwa manufaa ya wananchi na serikali. Wakati
wananchi wanasubiri sheria mpya ya Huduma za Vyombo vya Habari, Kambi ya
Upinzani inaitaka Serikali kuleta Bungeni Muswada wa kufuta Sheria ya Magazeti
ya mwaka 1976 pamoja na kufanyia marekebisho sheria nyingine 17 zenye vipengele
kandamizi kwa vyombo vya habari kwa kuwa sheria hizo ni kinyume na Katiba ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Pia sheria hizo zinaendeleza utamaduni
wa usiri ambao kama nilivyosema awali unasaidia sana kufanya viongozi
wasiwajibike ipasavyo na kufanya mambo yasiyostahili kwa kujificha kwenye kinga
ya usiri.
2.2 Uhuru wa uhariri, vitisho kwa
waandishi wa habari na utatu hatarishi
Mheshimiwa
Spika, katika hali ambayo imezidi kudhihirisha kuwa Serikali ya CCM
inawalazimisha Watanzania kuendelea kuishi ‘zama za mawe’, Mwezi Septemba mwaka
jana, tasnia ya habari ilipata dhahama kubwa baada ya Serikali kupitia wizara
husika na Habari Maelezo, katika hali ambayo hadi sasa haijulikani ilikuwa kwa
maslahi ya nani, iliamua kufungia magazeti mawili ya Mtanzania na Mwananchi. Tunasema
ni zama za mawe kwa sababu, vitendo vya kufungia vyombo vya habari kwa namna
ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali ya CCM ikitumia sheria zilizopitwa na
wakati, ikiwa ni sehemu ya kubana uhuru wa maoni na utoaji wa fikra mbadala, vilifanywa
enzi zile ambapo dunia ilikuwa inaaminishwa kuwa ina muundo wa meza.
Mheshimiwa Spika,
Kwa namna ambayo iliendelea kutuanika namna tunavyokumbatia ‘ukoloni na
ukaburu’, Serikali ya CCM ilijigeuza mlalamikaji, polisi (mkamataji), mwendesha
mashtaka, hakimu na kisha askari magereza (mfugaji) kisha kulifungia Gazeti la
Mtanzania siku 90 na Mwananchi siku 14. Kambi ya Upinzani Bungeni inataka kujua
kupitia kauli ya serikali hapa bungeni, mtindo huu wa udikteta unaofanywa na
serikali hii inayojiita sikivu inayoshughulikia vyombo vya habari, utaendelea
hadi lini?
Mheshimiwa Spika,
kwa sasa zipo fikra miongoni mwa wadau wa vyombo vya habari kwamba uhuru wa
habari nchini unazidi ‘kuwambwa msalabani’ kwa sababu ya utatu wa hatari ambao
umetengenezwa na Serikali ya CCM, kwenye Wizara ya Habari, Vijana, Michezo na
Utamaduni. Utatu huu hatari unaundwa na waziri mwenyewe Dk. Fenela Mkangara
ambaye mbali ya kwamba si mwanahabari, si mwanasanaa, si mwanamziki wala si
mwanamichezo, taarifa zinaonesha kuwa amekuwa na dhamira ya kupambana na vyombo
vya habari, ambao ni wadau wake, tangu alipoteuliwa.
Mheshimiwa Spika,
Akiandika kwenye safu yake, mmoja wa waandishi waandamizi nchini, alikuwa na
haya ya kusema juu ya Dk. Mukangara;
“Waziri
mwenye dhamana Dk. Fenella Mukangara kwa muda mrefu amekuwa na nia ovu dhidi ya
vyombo vya habari. Julai mwaka jana (akimaanisha 2012) tukiwa Hotelki ya Dodoma
mjini Dodoma, wakati tunafanya mazungumzo rasmi na Waziri Mukangara, walikuwepo
Theophil Makunga, Pili Mutambalike, Neville Meena na marehemu Alfred Mbogola na
wengine, Dk. Mukangara alitoa kauli iliyotushtua wengi na sasa ndipo tunaona
inatekelezeka kwa vitendo.”
Mwandishi huyo aliongeza kwa kunukuu
maneno ya Waziri Mukangara ambaye amenukuliwa akisema;
“Nikipata fursa Mwananchi nitalifuta,
mimi linanikera sana. Tena na Nipashe nao naona wanakuja, ikibidi nitawafungia
tu, mimi siogopi kitu.” Hayo ni maneno ya Waziri anayetakiwa kuwa mlezi wa
vyombo vya habari!
Mwandishi huyo katika makala yake
akaendelea kuandika hivi;
“Baada ya kauli hii tuliendelea na
mazungumzo mengine, lakini Meena akatwambia kuwa Dk. Mukangara aliwahi kutoa
kauli kama hii ofisini kwake walipokwenda akina Jesse Kwayu, Meena na Absalom Kibanda
kuomba Gazeti la Mwanahalisi lifunguliwe. Mwanahalisi alilifungia kwa muda
usiojulikana…”.
Mheshimiwa
Spika, si Waziri
Mukangara mwenyewe wala mtu mwingine yeyote kwa niaba yake, amewahi kukanusha
maneno hayo aliyonukuliwa akiyasema hadharani mbele ya wadau ambao yeye
anapaswa kuwa kiongozi na mlezi wao. Kutokana
na mwenendo wa Waziri Mukangara wa kupamabana na vyombo vya habari, unaofumbiwa
macho na mamlaka iliyomteua, labda kwa bahati mbaya au sehemu ya mkakati wa
serikali hii ya CCM. Uhusiano wa waziri na vyombo vya habari ulifikia hatua
mbaya zaidi, baada ya wadau wa habari waliokutana Oktoba 9 mwaka jana, kufikia
maazimio kadhaa, ikiwemo lile linalosema;
“Kusitisha kuandika, kutangaza na kupiga
picha shughuli zozote zitakazowahusisha au kuratibiwa na Mheshimiwa Fenella
Mukangara na Assah Mwambene hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo. Adhabu hiyo
inaanza mara moja kuanzia leo.”
Mheshimiwa
Spika, hapo juu
kwenye moja ya maazimio ya wadau wa habari, ametajwa Assah Mwambene, huyu ni
Mkurugenzi wa Habari Maelezo. Mkurugenzi huyu ambaye amewahi kufanya kazi
kwenye vyombo vya habari kama mwandishi, pamoja na kwamba kwa majukumu yake
hayo alipaswa kuwa mtu wa karibu kama mwelekezi na kiongozi kwa wadau wake, kwa
kushirikiana na Waziri Fenella Mukangara, amekuwa ni mwiba kwa utendaji wa
vyombo hivi, akihusika kuuweka uhuru wa habari na uhariri katika sintofahamu
kubwa.
Mheshimiwa
Spika, kitendo
cha Mkurugenzi wa Habari Maelezo kufanya maamuzi makubwa ya kuyatisha magazeti
ya Mwananchi na Rai, kutimiza wajibu wa kuendelea kuhabarisha, kwanza bila kuwa
na msingi wowote wa kisheria na pili bila kuwasiliana na wakubwa wake wala
wasaidizi wake, kama ilivyotamkwa na aliyekuwa Naibu Waziri Amos Makala, ni
jambo ambalo linathibitisha jinsi alivyo sehemu ya utatu huu tunaozungumza
hapa.
Mheshimiwa
Spika, anayekamilisha
utatu unaoweka uhuru wa habari na uhariri kwenye hati hati ni Naibu Waziri Juma
Nkamia. Kwa kauli zake mwenyewe hapa hapa bungeni akisikiwa na Watanzania wote,
wakiwemo wadau wa habari, alithibitisha jinsi alivyo na chuki dhidi ya
waandishi wa habari.
2.3
Kauli za Dharau Dhidi ya Wanahabari
Mheshimiwa
Spika,
wakati katibu mkuu kiongozi anataja mabadiliko ya baraza la mawaziri Ikulu
tarehe 19 Januari Mwaka huu, akiwa amezungukwa na wanahabari kutoka vyombo
mbalimbali vya habari, wakati akitaja jina la Naibu waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Mhe. Juma Nkamia, wanahabari hao waliguna na kucheka ikiwa
ni ishara ya kutoridhishwa na uteuzi huo. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inaungana na wana habari wote kwa kuguna na kuchekeshwa na uteuzi wa Mhe. Juma
Nkamia ambaye ni dhahiri hana maslahi na wana habari bali ameitumia tasnia ya
habari kama daraja lake la kufanikisha maslahi yake binafsi ya kisiasa.
Mheshimiwa
Spika, tarehe
17 Novemba mwaka 2013, Baraza la Habari la Tanzania lilioneshwa kusikitishwa na
kauli za Mhe. Nkamia ambaye alitoa kauli ya kulikashifu baraza hilo wakati
akiwa katika vikao vya Bunge wakati yeye akiwa ni mmoja watu walionufaika na
Baraza hilo. Akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Mhe. Nkamia alitamka kuwa , MCT(Baraza la Habari Tanzania) na TEF
(Jukwaa la wahariri Tanzania) ni sawa na asasi zisizo za Kiserikali (NGOs)
lakini zimekuwa zikijipa kazi ya kusimamia waandishi wa habari nchini.
Mheshimiwa
Spika, ni
wazi kuwa kauli ya Mhe. Nkamia ilikua ni ya dharau dhidi ya wana habari, dharau
dhidi ya tasnia ya habari na dharau dhidi ya vyombo hivyo ambavyo kwa nyakati
tofauti, kabla na hata baada ya kupata ubunge, Naibu Waziri alikua akizitambua
na kushirikiana nazo. Na kwa kumbukumbu rasmi, ni kuwa MCT na TEF ndizo taasisi
zinazoendelea kupigania maslahi ya wana habari dhidi ya uonevu unaofanywa na
Serikali hasa kwa wale ambao wana misimamo na misingi ya uadilifu kwani vyombo
hivyo ndivyo vilivyounda timu maalum ya
uchunguzi kuchunguza mazingira yaliyopelekea kuuawa kwa mwandishi wa habari
Daudi Mwangosi Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo, wilaya ya Mufindi,
mkoani Iringa ambapo ripoti yake ilifichua kuwepo kwa mahusiano mabaya baina ya waandishi wa habari
na aliyekua kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa ambaye aliulizwa maswali magumu
na Marehemu Mwangosi ikiwemo ni kwanini chama tawala cha CCM kiko huru kufanya
mikutano ya kisiasa wakati chama cha upinzani kama Chadema kinawekewa vikwazo
na polisi kila wakati.
Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri amesahau kuwa anazoziita asasi
zisizo za kiserikali, ndizo zilizochangia kwa mapinduzi katika sekta ya habari
nchini kwa kufanikisha mambo muhimu ikiwemo kusimamia maadili ya waandishi wa
habari, kuandaa mitaala ya kufundishia waandishi wa habari ambayo imepitishwa
na Baraza la Elimu la Taifa (NACTE) na pia kutumiwa na viongozi wakuu wa
Serikali na wanasiasa kama aliyekua Makamu wa Rais, Dkt. Omar Ali Juma,
mawaziri wakuu waliopita Edward Lowassa na Fredrick Sumaye katika kusululuhisha
migogoro inayohusiana na tasnia ya habari, inakuaje yeye binafsi avipuuze
vyombo hivyo muhimu? Na ndio maana kuteuliwa kwake kuwa Naibu Waziri
kuliwashangaza wanahabari na wadau wa habari.
Mheshimiwa Spika, aidha kwa nyakati tofauti Naibu waziri amekua
akiwaita waandishi wa habari kuwa ni waandishi makanjanja na yeye kujinasibu
kuwa ni mwandishi mwenye weledi na taaluma. Kambi rasmi ya Upinzani, ina
ushahidi kuwa Mhe. Nkamia amelidanganya bunge na taifa kwa ujumla kwa
kutuaminisha kuwa yeye alikua ni mfanyakazi mwajiriwa wa Shirika la Habari La
Uingereza BBC, kitengo cha Propaganga wakati Bwana Tido Mhando ambaye amefanya
kazi na Shirika hilo kwa takribani miaka 20, alikana kujua uwepo wa kitengo
hicho katika Shirika hilo na zaidi kueleza kuwa Mhe. Nkamia hakua muajiriwa wa
Shirika hilo bali aliitwa ili kwenda kusoma taarifa za habari tu kama kibarua
jaambo ambalo hajawahi kusema hadharani. Hivyo mbwembwe zote za Naibu waziri
zilikua ni kumuhadaa Rais Kikwete ili apate uongozi kwa sifa asizostahili.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inauliza, je wakiitwa waandishi makanjanja,
Kiranja wao ama mwalimu wao mkuu ni nani?
3.0
MAENDELEO YA VIJANA
3.1
Baraza la Vijana la Taifa, Benki ya Vijana na Mustakabali wa Maendeleo ya
Vijana Nchini
Mheshimiwa
Spika; Kifungu
6002 Idara ya Maendeleo ya Vijana ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
katika mwaka wa fedha 2014/2015 inaombewa jumla ya Sh. 995, 234,000 kwa ajili
ya matumizi ya kawaida. Fedha hizo kwa kiwango kikubwa ni za matumizi yasiyo ya
lazima yanayohusiana na Mbio za Mwenge yasiyokuwa na uhusiano moja kwa moja na
maendeleo ya vijana nchini. Ikumbukwe
kwamba siku chache zilizopita tarehe 27 Mei 2014 katika kikao cha kumi na tisa
kwenye Mkutano huu wa Bunge, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
ilijibu kwa mfano mwaka 2012 Jumla ya Tsh 650,000,000 zilitengwa kwa ajili ya
kuadhimisha Uzinduzi na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Hali hii inajidhihirisha
katika uchambuzi wa kasma za idara hii ya maendeleo ya vijana ambapo kwenye
matumizi ya kawaida kasma 210314 kumetengwa posho za vikao Sh 20,100,000 katika
mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya “vikao vya uanzishwaji wa Baraza la
Vijana, Benki ya Vijana pamoja na tathmini ya Mbio za Mwenge wa Uhuru”.
Mheshimiwa
Spika; Hali
hii inadhihirisha Wizara haiweki kipaumbele katika kazi muhimu zinazohusu
uanzishaji uanzishwaji wa vyombo viwili muhimu kwa ajili ya vijana: Baraza la
Vijana la Taifa na Benki ya Vijana ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani imehoji kwa
nyakati mbalimbali kutaka utekelezaji uharakishwe. Kitendo cha kutenga
rasilimali kidogo kwa ajili ya kazi hizo, huku rasilimali hizo zikielekezwa
katika posho za vikao na vikao hivyo
vikiwa na ajenda nyingi nyingine zikiwa tofauti na masuala ya msingi ya
maendeleo ya vijana kinaashiria udhaifu mkubwa wa Serikali inayoongozwa na CCM
katika masuala yanayohusu vijana.
Mheshimiwa Spika, kwa
vyovyote vile, chini ya makada wa CCM posho hizo zitatumika kujadili kuhusu
mbio za Mwenge kuliko masuala ya msingi ya uanzishwaji wa Baraza la Vijana la
Taifa na Benki ya Vijana kwa kuzingatia namna Serikali ya CCM ilivyojibu
bungeni kubariki Mwenge huo kutumika kwa ajili ya propaganda potofu za Serikali
mbili kuelekea kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba. Hivyo, Kambi Rasmi ya
Upinzani inatoa mwito kwa uongozi wa Bunge na Wabunge katika mjadala wa
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hii kuhakikisha mamlaka na madaraka
ya wabunge kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya Katiba ya Nchi yanatumika vizuri zaidi
kuwezesha kuharakishwa kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa na Benki ya Vijana
kwa ajili ya Maendeleo ya Vijana nchini.
Mheshimiwa
Spika; Katika
Mkutano wa 14 Kikao cha 15 tarehe 21 Disemba 2013 ulisomwa Bungeni Muswada
Binafsi wa Mbunge wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013. Baada
ya muswada huo, Bunge lilielezwa pia na Mheshimiwa Spika,
“ Waheshimiwa wabunge, muswada binafsi wa
Mheshimiwa Zitto Kabwe sasa utaanza kuwepo kwenye website ya Bunge na utakuwa
public mpaka utakapopangiwa tarehe ya kujadiliwa na utapelekwa kwenye kamati
zitakazohusika wakati muafaka”.
Kambi Rasmi ya Upinzani
inatoa mwito kwa Spika: Mosi, kuweka kumbukumbu sawa kwa kulieleza Bunge kwamba
muswada binafsi wa mbunge uliwasilishwa na Mheshimiwa John Mnyika; Pili,
kulieleza Bunge sababu ya maelekezo yake ya muswada huo kuwepo kwenye tovuti ya
bunge kwa ajili ya kuwa wazi kwa umma mpaka sasa kutokutekelezwa, Tatu, ni lini
muswada huo utapangiwa tarehe ya kujadiliwa; Nne, ni kwanini mpaka sasa muswada
huo haujapelekwa kwenye kamati zinazohusika;
Tano, ni upi wakati muafaka alioutaja kwenye maelezo yake.
Mheshimiwa
Spika; Kambi
Rasmi ya Upinzani inawahimiza wabunge kuzingatia kwamba kutokuwepo kwa chombo
kinachowaunganisha vijana wote bila kujadili itikadi kufuatilia masuala ya
maendeleo ya vijana kunafanya Wizara mbalimbali za kisekta kutokuzingatia
masuala yaliyokipaumbele kwa maendeleo ya vijana. Mathalani, katika Mkutano huu
wa Bunge katika Fungu la 65 la Wizara ya Kazi na Ajira Kitabu cha Nne Cha
Miradi ya Maendeleo Kifungu cha 2002, pamoja na wabunge na vijana kupewa
matumaini kwamba zimepitishwa bilioni tatu kwa ajili ya mikopo na mitaji kwa
vijana ukweli ni kwamba fedha hizo zimepangiwa matumizi ambayo kusipokuwa na
chombo cha kuyafuatilia kutakuwa na udhaifu, ufisadi na ubadhirifu kama
ilivyojitokeza katika fedha za mifuko ya maendeleo ya vijana kati ya mwaka 1993/1994 mpaka 2013/2014.
Mheshimiwa
Spika; Kwa
mujibu wa Kasma za Kifungu hicho cha 2002 cha Bajeti iliyopitishwa ya Fungu 65
Wizara ya Kazi na Ajira, fedha hizo zinazopaswa kuwa za mikopo na mitaji kwa
vijana zitatumika milioni 700 kwa ajili ya kulipia utaalamu elekezi
(consultancy fees) kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana 200 tu; milioni 150
zitatumika kununulia magari Wizarani, milioni 60 zitatumika kwenye matangazo na
orodha ndefu nyingine ya matumizi yasiyo
ya lazima ambayo kutokana na ufinyu wa muda sitaendelea kuyataja. Aidha, katika mjadala wa bajeti hiyo wabunge
waliweka bayana kwamba kiwango kinachotengwa katika Mifuko ya Maendeleo ya
Vijana iwe ni kwa Serikali Kuu na hata Halmashauri ni kidogo ukilinganisha na
uwezo wa nchi, mahitaji ya vijana na mafungu mengine yasiyo na matumizi muhimu
yanavyotengewa fedha nyingi katika baadhi ya Wizara.
Mheshimiwa
Spika;
Hivyo, ili Baraza la Vijana la Taifa na Benki ya Vijana ambavyo ni vyombo
muhimu kwa maendeleo ya vijana viweze kuanzishwa kwa wakati, Kambi Rasmi ya
Upinzani inatoa mwito kwa Spika wa Bunge kuelekeza muswada binafsi uliokwisha
wasilishwa kwa Bunge kwa kamati zinazohusika kwa ajili ya kuanza kuujadili. Aidha, Spika arejea ratiba ya
Bunge ambapo imetajwa bayana kwamba kati ya tarehe 5 Juni 2014 na 11 Juni 2014
ratiba ya Bunge haitahusu uwasilishaji wa Bajeti za Serikali. Ratiba imetaja
bayana kwamba “Shughuli nyingine yoyote kama itavyokuwa imeelekezwa na Spika”
inaweza kuingizwa kwenye ratiba; hivyo, fursa hiyo itumike kuleta muswada huu
Bunge kusomwa kwa mara ya pili.
Mheshimiwa
Spika; Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka Bunge kuingilia kati suala hili na kuisimamia
Serikali kwa kuzingatia kwamba katika majumuisho ya Bajeti ya Wizara hii kwa
mwaka 2013/2014 tarehe 21 Mei 2013 mkutano wa 11 kikao cha 30; Serikali
ilitumia kisingizio kwamba ‘ni bunge la bajeti’ kukwepa kuwasilishwa kwa muswda
Bunge. Hata hivyo, ahadi ya Serikali ya kuwasilisha muswada haikutekelezwa
kwenye mikutano mitatu uliyofuatia ya 12, 13 na 14; hivyo mkutano huu wa 15 ni
muafaka kuwezesha maamuzi kufanyika kwa ajili ya maendeleo ya vijana nchini.
Mheshimiwa
Spika; Kambi
Rasmi ya Upinzani inaikumbusha Serikali na wabunge kwamba Sera ya zamani ya
maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa
katika Sera mpya ya mwaka 2007; hata hivyo Serikali imekuwa ikikwepa
kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa pamoja na kuwa
suala hilo linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani inakumbusha pia kwamba katika ilani za uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010 vyama mbalimbali viliahidi kuhakikisha kwamba Baraza la Vijana la Taifa
linaundwa. Ili kuwahadaa na kujipatia
kura za vijana CCM kwa kupitia ilani yake katika kipengele 80 (k) inasema
“Kuhamasisha ushiriki wa
vijana katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwa ni pamoja na kukamilisha
uanzishaji wa Baraza la Vijana”.
Mheshimiwa
Spika;
Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inatarajia kwamba wabunge wa pande zote katika
suala hili la kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa kuungana kuwa kitu kimoja
kuisimamia Serikali na kutumia madaraka ya
Bunge kutunga sheria wakati wa Mkutano huu wa Bunge unaoendelea.
Serikali na wabunge mzingatie kwamba
zaidi ya miaka 18 ahadi za kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa
baraza la Vijana la Taifa; bila utekelezaji
kamili na wa haraka. Baraza la Vijana litawezesha vijana kuanzia kwenye
vijiji/mitaa mpaka taifa kuweza kuwa na vyombo vya kuwaunganisha vijana kwa
kike na wa kiume kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa.
Mheshimiwa
Spika;
Aidha, Baraza hilo litafuatilia pia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya
maendeleo ya vijana kwenye Halmashauri, Serikali kuu, katika vyombo mbalimbali
vya maendeleo na wadau wa maendeleo. Pia, Baraza la Vijana litafuatilia kwa
karibu utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuhakikisha kwamba fedha
zinatengwa za kutosha na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana kujiajiri,
kukuza vipaji vyao na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla.
Mheshimiwa
Spika, aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji ni kwa
nini kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 Jumla ya fedha zilizopelekwa kwenye
vikundi mbalimbali kwa kupitia mfuko wa vijana ni shilingi milioni 172.6 tu sawa na asilimia 2.8 tu, kati ya Shilingi Bilioni 6.1 ambazo Serikali mwaka jana iliwadanganya vijana kuwa
itatenga, huku taarifa ya wizara ikionesha kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 2 sawa na asilimia 32.7 pekee ndizo zilizokua zimepokelewa hadi kufikia April
2014. Je, kiasi cha shilingi milioni 827.4,
zimetumikaje tumikaje? Je, Serikali itaacha lini kuwahadaa vijana kuwa
wanatenga mabilioni ili kuwanyamazisha katika kudai haki zao huku ikijua kuwa
haiwezi kuwasaidia hata kwa kile wanachostahili?
4.0
UTAMADUNI
4.1
UTAMADUNI:
KIELELEZO CHA HISTORIA YA TAIFA
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imekua ikishauri
Serikali juu ya umuhimu wa kutunza maeneo na majengo ya kale ili kuweza
kuonesha urithi wa utamaduni wa taifa letu. Ni dhahiri kuwa maeneo mengi ya
kihistoria yameachwa na kuwa magofu na mengine yanaendelea kubomolewa kwa
ujenzi mpya hali inayofanya historia ipotee, jambo ambalo pia linalikosesha
taifa mapato yanayotokana na utalii. Kambi Rasmi ya Upinzani, inataka kujua
mikakati ya wizara kuhakikisha kuwa maeneo na majengo ya kale yanahifadhiwa na
kuachwa katika hali yake kwa mwaka huu wa fedha wa 2014/2015.
4.2 BARAZA LA SANAA
TANZANIA (BASATA)
Mheshimiwa Spika, Baraza la Sanaa nchini lina dhamana kubwa
kuhakikisha kuwa sanaa ya mtanzania haipoki wala kudhalilisha maadili pamoja na
kuiendeleza sanaa hapa nchini. Ni jambo la kushangaza kuona kuwa Baraza hili
hufanya kazi kwa kuzinduka tu usingizini huku athari za uporomokaji wa maadili
kwa kupitia sanaa katika jamii zinakua kubwa.
Mheshimiwa Spika, ngoma ya Kigodoro haikua maarufu katika sehemu
kubwa za nchi kutokana na ngoma hiyo kuchezwa katika sehemu chache. Lakini,
baada ya kutolewa kwa filamu ya Kidogoro ambayo kwa kiasi kikubwa ilihamasisha
jamii kutaka kujua maana ya kidogoro na hivyo ngoma hiyo kuzidi kupata umaarufu
katika sehemu kubwa ya jamii ya watanzania hata kwa watanzania wanaoishi nje ya
nchi. Mara baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuelezea athari za ngoma
hii katika maadili ya watanzania BASATA ghafla ikazinduka usingizini na kupiga
marufuku ngoma hiyo, huku filamu ya Kigodoro ikiwemo katika soko la filamu na
ikiendelea kuuzwa huku ikiambatana na ujumbe ambao si tu unahamasisha uvunjifu
wa maadili ya kitanzania bali unatoa taswira ya jamii isiyostaarabika. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka wizara hii kuisimamia BASATA ipasavyo
pamoja na kuipa uwezo wa kifedha ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kuutunza
na kuutangaza utamaduni wa mtanzania kwa kupitia kazi za sanaa. Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka BASATA kuacha uvivu na kutekeleza majukumu
yake kwa ubunifu ili kulinda na kuutangaza utamaduni wa Mtanzania ili hatimaye
navyo vitoe mchango katika taifa kutokana na mapato yanayotokana na mauzo ya
kazi za sanaa na utamaduni.
4.3 WASANII NA
HARAKATI MBALIMBALI
Mheshimiwa Spika, katika mapambano ya kudai haki za wasanii
duniani popote, wasanii huongozwa na dhamira ya kutumia sanaa zao ili kuleta
mabadiliko ya kweli na si kukubali kutumika kuwa faraja kwa watu wengine
kufanikisha malengo yao na mwishowe haki wanazozipigania kuonekana kama kelele
za chura.
Mheshimiwa Spika, kila mtu ana uhuru wa kufanya maamuzi yake
hasa maamuzi ya msimamo wa kisiasa. Ila kwa muda mrefu sasa, wasanii wa
Kitanzania tumeshindwa kuwa mabalozi wa kweli wa haki katika kuhakikisha kuwa tunatumia
kazi zetu za sanaa tunapigania haki na usawa ili kulikomboa taifa. Matokeo
yake, baadhi ya wasanii wamekua wakitumika kama chambo na baadhi ya wanasiasa
ili kuweza kutimiza maslahi ya wanasiasa, ambayo kwa kifupi baada ya kutumika,
hata maslahi ya wasanii ambayo wanapigania huwa hayapewi kipaumbele. Mfano
mzuri kwetu wasanii ni jinsi ambavyo tumetumika sana katika harakati za kisiasa
lakini katika mchakato wa katiba, tumesahulika. This is a wake up call kwa
wasanii wote ambao wamekubali kutumika kwa maslahi ya muda mfupi bila kuangalia
mustakabali wa sekta ya sanaa katika taifa letu. Kambi rasmi ya upinzani
Bungeni, inawataka wasanii kuacha kutumika na kujenga umoja imara utakaotetea
maslahi yao kwa ujumla bila ya kufuata mashinikizo ya kisiasa ili kuleta
mapinduzi ya kweli katika sanaa.
4.3.1SANAA NA WASANII KUTUMIKA KWENYE UFISADI NA
UFICHAJI WA MGONGANO WA MASLAHI
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yetu kwa hoja hii ya mwaka jana,
Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu ilizungumzia kwa kirefu jinsi
ambavyo Serikali hii ya CCM imeshindwa kulinda haki za wasanii licha ya kuwepo
kwa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki tangu mwaka 1999. Tulielezea jnsi
ambavyo, licha ya masharti ya Sheria hiyo na licha ya kuwepo kwa Chama cha
Hakimiliki Tanzania (COSOTA) tangu mwaka 2007, nyimbo za wasanii nchini
zimeendelea kutumiwa kwenye matangazo ya vyombo vya habari, hasa vya Serikali
kama vile Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1 na TBC2) bila wasanii
waliozitunga au kuziimba nyimbo hizo kupata malipo yoyote.
Mheshimiwa Spika, Ni haki na wajibu
kwa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kupiga kelele dhidi ya
unyonyaji huu wa wasanii wetu, hasa wanamuziki vijana wa kizazi kipya ambao
wanajihangaikia kutafuta maisha na kuendeleza vipaji vyao. Kwa sababu hiyo,
Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inawaahidi wasanii wetu kwamba
itaendelea kutimiza wajibu wake kwa kutetea haki na maslahi yao hadi
watakapotendewa haki.
Hata
hivyo, Mheshimiwa Spika, ni haki na wajibu kwa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge
lako tukufu kuwakemea na kuwakosoa vijana pale wanapojiingiza katika vitendo
vinavyochafua sanaa na sifa zao kama wasanii na wa-Tanzania. Kama
inavyofahamika na wananchi na hata kwa Bunge lako tukufu, wasanii kadhaa wa
ki-Tanzania wamekamatwa katika nchi za nje wakiwa na madawa ya kulevya. Wasanii
wa aina hii, wanaokubali kutumiwa kama punda wa mizigo ya madawa ya kulevya na
mitandao haramu ya biashara hiyo, hawastahili chochote kutoka kwa wa-Tanzania
zaidi ya dharau na adhabu kali zilizowekwa na sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Kutumia
umaarufu wao ili kuficha ushiriki wao katika biashara haramu ya madawa ya
kulevya sio tatizo pekee la baadhi ya wasanii wetu. Sasa limejitokeza tatizo la
baadhi ya wasanii wetu, hasa wanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, kujiingiza –
kwa kujua au kwa kutumiwa na wajanja bila ya wao kujua – kwenye ‘dili’ za
kifisadi za kuiba fedha za umma. Wajanja hao hujificha katika kivuli cha
makampuni yanayotajwa kuwa na malengo ya kuendeleza wasanii na sanaa kumbe ni
vichaka vya kuficha ufisadi, mgongano wa kimaslahi na matumizi mabaya ya
madaraka ya baadhi ya viongozi wa umma dhidi ya fedha za umma wanazopaswa
kuzisimamia.
Utaratibu
unaotumika kutekeleza dili hizi za kifisadi unafanana kwa kiasi kikubwa na
utaratibu uliotumika kuiba mamia ya mabilioni ya fedha za umma kutoka kwenye
akaunti ya madeni ya nje ya Benki Kuu ya Tanzania (EPA) mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, Tarehe
13 Agosti, 2012, Msajili Msaidizi wa Makampuni katika Wakala wa Usajili wa
Makampuni na Leseni (BRELA) alitoa Hati ya Usajili (Certificate iof Incorporation) kwa kampuni inayoitwa Leka Dutigite
Limited. Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, Leka Dutigite Ltd. ina ofisi zake
katika ghorofa ya kwanza ya jengo la City House lililoko katika Mtaa wa Mkwepu,
Dar es SalaaM. Mheshimiwa Spika,
Katiba,
yaani Memorandum and Articles of
Association, ya kampuni ya Leka Dutigite Ltd. iliyosajiliwa BRELA tarehe 13
Agosti, 2012 inaonyesha kwamba mwenye hisa nyingi katika kampuni hiyo ni
kampuni nyingine inayoitwa Gombe
Advisors Ltd. ya Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa taarifa za kibenki ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako
tukufu imezipata, mnamo tarehe 10 Desemba, 2012, Hifadhi ya Taifa ya Saadani
ilihamisha jumla ya shilingi 12,200,000 kwenda kwenye akaunti na. 0150357447800
iliyoko CRDB Bank tawi la Pugu Road, Dar es Salaam, inayomilikiwa na Leka
Dutigite Ltd. Hifadhi ya Taifa ya Saadani inamilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi za
Taifa (TANAPA), ambayo ni shirika la umma. Siku moja baadae, fedha hizo
zilitolewa kwa pesa taslimu kutoka kwenye akaunti hiyo.
Baada
ya hapo, kati ya tarehe 14 Januari na 7 Februari, 2013, akaunti ya Leka
Dutigite Ltd. iliingiziwa jumla ya shilingi 28,600,000. Fedha hizi zote
ziliingizwa kama fedha taslimu na mtu aitwaye Mchange (shilingi 3,600,000
tarehe 14 Januari, 2013) na Leka Dutigite (shilingi 25,000,000 tarehe 23
Januari na 7 Februari, 2013). Kufikia tarehe 7 Februari, 2013, fedha hizo zote zilikwishatolewa
benki.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 28 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd. iliingiziwa shilingi
32,367,000 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Kwa mujibu wa taarifa
za kibenki, siku hiyo hiyo, fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo. Siku nne
baadae, yaani tarehe 4 Machi, 2013, NSSF ilifanya malipo mengine kwenye akaunti
ya Leka Dutigite Ltd., kwa mikupuo miwili, ya jumla ya shilingi 46,663,000.
Siku hiyo hiyo, fedha hizo nazo zilitolewa kutoka kwenye akaunti hiyo kwa mikupuo
miwili. Kwa hiyo, katika kipindi cha miezi mitatu katika ya tarehe 10 Desemba,
2012 na 4 Machi, 2013, Leka Dutigite Ltd. ililipwa shilingi 119,930,000 kwa
utaratibu huo huo wa ingiza na toa fasta. Kati ya fedha hizo, shilingi
12,200,000 zililipwa na TANAPA na shilingi 79,027,000 zililipwa na NSSF.
Mheshimiwa Spika, Katika
mazingira ya kawaida, sio kitu cha ajabu kwa mashirika ya umma kama NSSF na
TANAPA kufanya biashara na watu au taasisi mbali mbali kama makampuni binafsi.
Ukweli ni kwamba, kwa upande wa malipo yaliyofanywa na TANAPA, Kambi Rasmi ya
Upinzani ya Bunge lako tukufu imeweza kupata nakala ya mkataba unaohusu Maandalizi ya Filamu (Documentary) kwa Ajili
ya Kuhamasisha Shughuli za Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa
Kutumia Wasanii Kutoka Kigoma. Mkataba huo umesainiwa tarehe 5 Desemba,
2012, kati ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Leka Dutigite Ltd. na una thamani
ya shilingi 12,200,000, kiasi kile kile kilicholipwa na Hifadhi hiyo.
Hata
hivyo, Mheshimiwa Spika, mazingira ya malipo haya sio ya kawaida. Hii ni kwa
sababu ya uwepo wa kampuni ya Gombe Advisors Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka za
BRELA, kampuni hii ilisajiliwa tarehe 24 Novemba, 2011. Kwa mujibu wa nyaraka
hizo, ofisi za Gombe Advisors Ltd. ziko kwenye jengo la City House, Mtaa wa
Mkwepu, Dar es Salaam, ziliko ofisi za Leka Dutigite Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka
hizo, wakurugenzi wa Gombe Advisors Ltd. ni Zitto Zuberi Kabwe ambaye kazi yake
inatajwa kuwa ‘mchumi’, na Raphael Ongangi ambaye anatajwa kuwa ‘mchambuzi wa
fedha na vitega uchumi’ (Financial and Investment Analyst). Bwana Ongangi
aliwahi kutajwa na gazeti la kila wiki la Mawio la tarehe 26 Desemba 2013 kuwa
ni mmoja wa washauri wa Zitto Zuberi Kabwe na anasemekana kuwa msaidizi
wake.
Mheshimiwa Spika,
Zitto Zuberi Kabwe sio ‘mchumi’ anayetajwa katika nyaraka za BRELA zinazoihusu
kampuni ya Gombe Advisors Ltd. pekee, bali pia ni Mbunge, tangu mwaka 2005, wa
Bunge lako tukufu. Kama Mbunge, Mheshimiwa Zitto Kabwe ni ‘kiongozi wa umma’
kwa mujibu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, 1995. Sheria hii inawalazimu
viongozi wa umma, wanapokuwa madarakani, kuwa “waadilifu, wenye huruma, utulivu, umakini na watakaoendeleza viwango
vya juu vya maadili ili kujenga na kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa
Serikali.”
Aidha, viongozi wa umma “... watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa
umma na kuendesha shughuli zao binafsi kwa namna ambayo itaonekana na
kuthibitika kuwa ni wazi kwa umma na haitatosheleza kwao kutekeleza wajibu wao
kwa kufuata sheria tu.” Vile vile, kuhusiana na maslahi binafsi, Sheria hii
inaelekeza kwamba “... viongozi wa umma
hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali
wanayoshiriki katika kuyafanya.”
Mwisho, kuhusiana na maslahi
ya umma, viongozi wa umma wanatakiwa, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa,
kupanga masuala yao “kwa namna
itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi, iliyojificha au inayoonekana kuwepo
na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati ya maslahi binafsi na maslahi ya
umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma.” Kwa kadri ya
ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, Mheshimiwa Zitto Kabwe
hajawahi kutangaza maslahi aliyonayo kwenye mikataba ya Gombe Advisors Ltd. na
Leka Dutigite Ltd. na NSSF na TANAPA.
Mheshimiwa
Spika,
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe sio tu ni Mbunge anayebanwa na masharti ya Sheria
ya Maadili ya Viongozi wa Umma, bali pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Fedha za Serikali (PAC). Kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza
ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu, mojawapo ya majukumu ya PAC
ni kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma
katika Wizara na Mashirika ya Umma yaliyoainishwa katika taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. NSSF na TANAPA ni baadhi tu ya Mashirika ya
Umma yaliyo chini ya usimamizi wa kibunge wa PAC.
Kwa maana hiyo, Mheshimiwa
Spika, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwa kutumia makampuni yake ya Leka Dutigite Ltd.
na Gombe Advisors Ltd., amefanya biashara na TANAPA, shirika la umma analolisimamia
kama Mbunge na Mwenyekiti wa PAC. Mheshimiwa Zitto Kabwe na wanamuziki
washirika wake, kwa kutumia makampuni ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite
Ltd., wamelipwa fedha za umma za TANAPA na NSSF.
Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kutoa maelezo juu ya madai ya ukiukwaji wa Sheria uliofanywa
na viongozi wa umma na mashirika ya umma katika kashfa hii. Pamoja na maelezo
yatayotolewa , Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa na
TANAPA na NSSF; msukumo uliofanya fedha hizo zitolewe na matumizi ya fedha hizo
kwa kuzingatia masharti yanayosimamia
fedha za umma na utawala bora katika usimamizi wa fedha za umma. Aidha, Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ifanye uchunguzi juu ya malipo na
matumizi husika kwa kurejea masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma
na Sheria nyingine zinazohusika. Kwa
upande mwingine, kwa kuwa suala hili linahusu mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge inayohusika na usimamizi wa fedha za umma, Kamati ya Kinga, Haki na
Madaraka ya Bunge nayo ifanye uchunguzi wake juu ya madai ya masharti ya Katiba
ya Nchi, Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kanuni za Bunge juu ya
maadili ya kiongozi wa umma ikiwemo yahusuyo utangazaji wa maslahi.
Mheshimiwa
Spika;
Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inatoa rai kwa wanamuziki
na wasanii wengine wote nchini kuwa waangalifu na watu wanaotaka kutumia
umaarufu wao kama wanamuziki na wasanii kwa lengo la kufanikisha dili za
kifisadi. Bila kuchukua tahadhari ya kutosha, wasanii hao wanaweza kujikuta
wakipoteza sifa na umaarufu wao ambao wameujenga kwa jitihada zao wenyewe.
4.4 MCHAKATO BUTU WA
VAZI LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, wakati
huo chini ya Waziri Dk. Emmanuel Nchimbi, ilifanya uteuzi wa wajumbe wa Kamati
ya Kubuni Vazi la Taifa mwezi Desemba 15, 2011.Kamati hiyo iliyokuwa na watu
wanane, Mwenyekiti ni Joseph Kusaga na Katibu ni Angela Ngowi, pamoja na
wajumbe wa kamati hiyo ni Habib Gunze, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali,
Makwaia Kuhenga, Ndesambuka Merinyo na Absalom Kibanda, ambaye baadaye
alitangaza kujiweka kando. Desemba
22, 2011, kamati hiyo ikazinduliwa rasmi na aliyekuwa Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Mhe. Emmanuel Nchimbi, tayari kuanza kazi ya kubuni Vazi
la Taifa, mchakato ambao ulipaswa kukamilika ndani ya siku 75 tangu siku ya
kuzinduliwa kwake. Mhe.Nchimbi
aliahidi kuwa mara baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi hiyo ikiwamo kuainisha
mapendekezo mbalimbali ya vitambaa vinavyoweza kufaa, Watanzania watakuwa
wamepata Vazi la Taifa. Siku hiyo
Waziri Nchimbi alisema kazi ya kamati hiyo si kuanza mchakato mpya wa Vazi la
Taifa, bali ni kumalizia mchakato wa kupata vazi la mwanamume na mwanamke
ulioanza mwaka 2004. Hata hivyo, baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri,
tarehe Septemba 10, 2012,
Kamati ya Vazi la Taifa chini ya Ndugu Kusaga ilikabidhi ripoti kwa Waziri
Mukangara aliyekuwa na naibu wake, Amos Makalla. Uwasilishaji wa ripoti hiyo ulifanywa
na Katibu wa Kamati ya Vazi la Taifa Angela Ngowi, akiwa na wajumbe wa kamati
hiyo, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali na Ndesambuka Merinyo. Angela akasema katika mchakato wa kupata vazi hilo, walipokea zaidi ya
michoro 200 kutoka kwa wasanii 88 na kupitisha michoro sita iliyokuwa imekidhi
vigezo na kuikabidhi kwa wataalamu wa vitambaa kwa ajili ya kutoa uamuzi wao. Waziri Mukangara alionesha shauku yake ya
kuona vazi hilo linapatikana haraka na kwamba lingevaliwa katika maadhimisho ya
miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika ya Desemba 9, mwaka 2012.
Mheshimiwa Spika, ikiwa inakaribia kuwa miaka
takribani miwili sasa tangu Waziri Mukangara apokee ripoti hiyo, hakuna vazi
lililopatikana wala maelezo mapya juu ya hatima ya vazi hilo. Kwa vile vazi la
taifa limekuwa likisubiriwa kwa shauku kubwa na Watanzania tangu mchakato huo
ulipoanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inataka maelezo ya kina kutoka kwa Waziri ni nini kimeukwamisha mchakato huo?
4.5
SANAA NA USANII KUTAMBULIWA KAMA SEKTA YA KIUCHUMI NA ULINZI WA MILIKI BUNIFU
KUBORESHWA KUINUA VIPATO VYA WASANII NA MAPATO KWA NCHI
Mheshimiwa
Spika; Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa juu ya maoni ambayo Wasanii
waliyawasilisha mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na baadaye kwa baadhi ya
wabunge ikiwemo wa upinzani kutaka wasanii watambuliwe kama kundi maalum katika
katiba mpya kama ilivyo kwa wafugaji, wakulima na fani au tasnia nyingine.
Aidha, wasanii wamependekeza kwamba rasimu ya katiba mpya itaje miliki bunifu
(intellectual property).
Mheshimiwa
Spika;
Kutokana na umuhimu wa mapendekezo ya wasanii hao waliyoyatoa kupitia
mashirikisho yao manne Shirikisho la Filamu, Shirikisho la Muziki, Shirikisho
la Sanaa za maonyesho na Shirikisho la Sanaa za ufundi, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inatoa maoni kwa Serikali kwamba haipaswi kusubiri mpaka mchakato wa
mabadiliko ya katiba bali marekebisho ya
msingi ya kisheria yapaswa kuharakishwa kuwezesha sanaa na usanii kuchangia
katika kuongeza ajira, kuboresha maisha ya wasanii na kuchangia kwa kiwango
kikubwa katika mapato ya Serikali na Uchumi wa Nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa
Spika;
Serikali imekuwa ikitazama sanaa kama suala la burudani zaidi badala ya
kuitazama kama ni sekta muhimu ya kiuchumi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kuzingatia kwamba Wasanii sio wanamuziki tu, wasanii wapo karibu
katika kila kaya Tanzania. Wafinyanzi, wasusi, wapambaji, wanamuziki waigizaji,
mafundi mbalimbali wa ushonaji ujenzi na kadhalika, wako wengi wala hata wao
hawajitambui kama ni wasanii kutokana na mazingira waliyomo.
Mheshimiwa
Spika;
Katika ripoti mojawapo ya BASATA ya mwaka 2006, idadi ya wasanii nchini wakati
huo ilikuwa ni milioni 6, ni wazi kuwa idadi hiyo kwa sasa itakuwa
imepanda. Katika miaka ya karibuni
vijana wengi wamekuwa wanaongezeka kujiunga na kundi hili kwani katika sanaa
kumekuwa na uwezekano wa kujipatia ajira, tena isiyokuwa na ukomo. Na hivyo
sanaa kwa sasa si utamaduni peke yake bali ni sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania.
Mheshimiwa
Spika;
Wasanii ni sehemu muhimu katika sekta ya Hakimiliki, takwimu za ripoti ya
WIPO(World Intellectual Property Organisation) ya mwaka 2010, kuhusu mchango wa
sekta ya hakimiliki katika uchumi wa Tanzania, inaonaonyesha kuwa sekta hii, kati ya 2007-2010 ilichangia
kati ya asilimia 3-4.6% ya gross domestic product(GDP). Na kiasi cha kati ya
TSH 38.930 bilioni na 86.686 billion kilipatikana kama kipato cha walioajiriwa
katika sekta hiyo.
Mheshimiwa
Spika; Kati
ya watu 28, 202 na 44, 331 waliajiriwa rasmi, na hiyo ilikuwa kati ya asilimia
4.5 na 5.2% ya kundi zima la waajiriwa wa Taifa hili. Kwa kipimo cha GDP, sekta
hii ilikuwa zaidi ya sekta ya madini, ambayo wote ni mashahidi imekuwa katika
mazungumzo kila kona ya nchi. Na katika ajira sekta hii ilikuwa juu zaidi ya
sekta nyingi zikiwemo madini, usafirishaji, mawasiliano, afya na ustawi wa
jamii, maji, gesi, na hata ujenzi. Kwa mchango wa sekta hii wa 3.2% katika GDP
kwa mwaka 2009 , umeweka sekta hii kuwa bora kuliko sekta za aina yake katika
nchi kama Croatia 3%, Singapore 2.9%,
Latvia 2.9%, Lebanon 2.5%, Kenya 2.3%. Na katika mchango wa ajira sekta hii
ilikuwa juu ya Romania, Bulgaria, Lebanon, Jamaica, Colombia, Kenya na Ukraine.
Mheshimiwa
Spika; kwa
upande wa Tanzania, Takwimu hizi hazijionyeshi katika takwimu za Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kuwa sanaa bado inaonekana ni burudani
tu, na thamani yake katika uchumi haitiliwi uzito. Kutambuliwa kwa kundi hili
kutawezesha kutungwa sheria na taratibu za kuwezesha Wasanii kuongeza ajira na
mapato, na Taifa kufaidika na uchumi wa
raslimali hii.
Mheshimiwa
Spika; Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka marekebisho makubwa kwenye sheria za nchi yetu
kuwezesha kutajwa kwa miliki bunifu katika sanaa, usanii na sekta zote nyingine
muhimu za kiuchumi. Ni muhimu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na
Serikali kwa ujumla ikazingatia kwamba mali ziko za aina tatu. Kuna mali
zinazohamishika, mali zisizohamishika na mali zitokanazo na ubunifu. Aina mbili
za kwanza zimetajwa katika katiba na ulinzi wake hujulikana na ni wa jadi.
Lakini hii aina ya tatu ya mali huwa ni ngumu kuilinda kutokana na mfumo wake
kuwa haushikiki hivyo sheria maalumu hutungwa kulinda aina hii ya mali (IP
Laws).
Mheshimiwa
Spika; Mali
zitokanazo na ubunifu kwa sasa ndio mali zenye kipa umbele duniani. Uvumbuzi wa
teknolojia mbalimbali, ugunduzi wa njia mbalimbali za kuboresha maisha, sanaa
na mengi yanayolindwa na milikibunifu, vimeweza kutoa ajira kubwa na kutoa
mchango mkubwa wa kipato kwa wagunduzi na nchi ambazo wagunduzi hao wamekuwa
wakiishi au kuzisajili kazi zao. Kama wasanii, haki zetu katika milikibunifu
zinajulikana kama Hakimiliki, lakini kama Watanzania tunaona ni muhimu kulinda
haki zote za Milikibunifu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa
Spika; Nchi
zote ambazo zimeweka taratibu imara za kulinda Milikibunifu duniani,
zimewezesha wabunifu wake kubuni mambo ambayo yameweza kubadilisha maisha ya
binadamu wengine duniani kote. Marekani iliweka kipengele cha Ulinzi wa hakimiliki
katika katiba yake tangu mwaka Agosti 1787, na kazi za wagunduzi wa Marekani
tunaziona kila wakati katika kazi za sanaa na teknolojia. Korea kusini
ilinakiri sehemu ya katiba ya Marekani kuhusu ulinzi wa Milikibunifu kuanzia
mwaka 1948, kwa wakati huu wote ni mashahidi wa bidhaa kama Samsung, Ld Daewoo,
Hyundai na kadhalika.
Mheshimiwa
Spika;
Milikibunifu pamoja na kulinda haki katika kazi za sanaa ambazo picha ndogo ya
mapato yake zimetajwa hapo juu, Milikibunifu italinda haki za wabunifu wetu, tafiti
za wasomi wetu, ugunduzi mbalimbali, taratibu mbalimbali za mambo yetu ya
kiasili, dawa za asili za miti yetu, na taratibu za matumizi ya dawa hizo, na
mali asili zetu nyingine nyingi tunazozifahamu na ambazo bado hatujazifahamu .
Mheshimiwa
Spika; Kuna
hasara nyingi ambazo hupatikana kama nchi haina ulinzi wa Milikibunifu, mifano
michache hapa Tanzania, ni kupoteza kwa Milikibunifu ya jina Tanzanite, ambayo
licha ya kuwa inachimbwa Tanzania tu lakini jina linamilikiwa na kampuni ya
Afrika ya Kusini. Vazi la kikoi, pamoja kuwa ni la asili ya Tanzania,
milikibunifu imesajiliwa Kenya, staili ya michoro maarufu ya Tingatinga
milikibunifu yake iko Japan. Na haya ni machache ambayo yameshtukiwa
Milikibunifu ikifuatiwa vizuri ndipo haswa ukubwa wa tatizo utakapojulikana.
Kuna ulazima mkubwa wa kutaja Milikibunifu katika sheria zote muhimu na
kuanisha ulazima wa kulinda kuendeleza na kwezesha wabunifu wan chi kwa manufaa
ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.
6.0 SEKTA YA MICHEZO
NCHINI
6.1 UENDELEZAJI WA VIWANJA
VYA MICHEZO NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
imeendelea kuona umuhimu wa taifa kuwekeza katika viwanja vya michezo ili
kuweza kupanua wigo wa taifa kujitangaza na kukusanya mapato yanayotokana na
viwanja vya michezo nchini. Labda, wizara mpaka sasa haijaweza kujua hasara
ambazo kama taifa tunapata kutokana na kutotumia nafasi zinazotokea na
kutowekeza vya kutosha katika kuboresha michezo nchini.
Mheshimiwa Spika, enzi za chama kimoja, majengo na maeneo yote ya
umma yalikuwa chini ya Serikali. Ujenzi na uendelezaji wa maeneo hayo ulifanya
na Serikali kupitia kodi za wananchi, michango, fedha za wafadhili na wahisani
mbalimbali. Hata baada ya uwepo wa vyama vingi, uendelezaji wa miradi yote
iliyokuwa chini ya Chama kimoja ilifanywa kuwa ni jambo la kitaifa. Kwa namna
isiyoeleweka baadhi ya maeneo ambayo CCM imeshindwa kuyarudisha kwa wananchi na
kuwa mali ya umma na kuyafanya ni mali ya chama ni pamoja na Uwanja wa CCM
Kirumba (Mwanza), Samora (Iringa), Sokoine (Mbeya), Sheikh Amri Abeid (Arusha),
Majimaji (Songea), Kaitaba (Kagera) n.k.
Mheshimiwa Spika, pamoja na CCM kuendelea kuhodhi viwanja hivi
imeshindwa kuviendeleza na matokeo yake kuwanyima fursa wananchi wa maeneo
husika kushuhudia michezo mbalimbali kwa kuwa viwanja hivyo huwa havikidhi
viwango vya ubora vya michezo hali inayofanya michezo mingi mikubwa ikiwemo ya
kimataifa kufanyika Dar Es Salaam pekee.
Kambi rasmi ya upinzani inarudia tena kuitaka Serikali kuvirudisha
viwanja vyote vilivyohodhiwa na CCM kwa wananchi ili viendelezwe kwa kupitia
Mamlaka ya Viwanja vya Michezo nchini kama tulivyopendekeza mwaka jana.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Mechi ya Taifa Stars na Zimbabwe
kuhamishwa kutoka uwanja wa Sokoine Mbeya tarehe 18 Mei na kuhamishiwa uwanja
wa Taifa Dar Es Salaam, kwanza kimewavunja moyo mashabiki wa mpira na wakazi wa
Mbeya ambao walijiandaa kuonesha uzalendo kwa taifa lao. Kutokana na kitendo
cha mechi hii kuhamishwa, Wanambeya walikoseshwa fursa za kujitangaza kiutalii
na hatimaye kuchangia katika uchumi kulikosababishwa na Serikali ya CCM
kuendelea kuhodhi viwanja vya michezo nchini. Rudisheni viwanja vya wananchi
ili viendelezwe na kuwanufaisha wananchi.
6.2 KASUMBA YA MPIRA
WA MIGUU KUWA MCHEZO PEKEE WA KIPAUMBELE.
Mheshimiwa Spika, kama Waziri kivuli mwenye dhamana ya kuisimamia
Serikali katika masuala ya habari, vijana, utamaduni na michezo. Lakini ni
dhahiri kuwa Wizara hii imeshindwa kusimamiwa ipasavyo katika sekta ya
michezo,huku soka peke yake ikifanywa kuwa ni mchezo unaopewa kila aina ya
msaada na kuidharau michezo mengine. Kwa kifupi ni kuwa, Tanzania ina hazina
kubwa ya wanamichezo ambao hawajatumika ipasavyo na wala Serikali haijawekeza
vya kutosha katika kuhakikisha kuwa aina nyengine za michezo zinapewa
kipaumbele. Kwa mfano, Filbert Bayi ni mwanariadha wa Tanzania ambaye
alililetea taifa sifa kubwa kwa kushinda medali ya dhahabu mwaka 1974, tunaye
mchezaji wa mpira wa kikapu nchini Marekani Hasheem Thabit anayechezea NBA.
Mheshimiwa Spika, kama taifa kushindwa kuwa na orodha ya wana
michezo ambao wamefanya vizuri katika medani ya michezo duniani na kuweza
kuwahesabu kwa uchache wao, kunazua maswali mengi sana si kwetu tu bali hata
kwa wadau wa michezo nchini ikiwa Serikali ina nia ya dhati ya kuendeleza
michezo kwa ujumla.
6.3
MAKOCHA WA KIGENI NA MUSTAKABALI WA MICHEZO NCHINI
Mheshimiwa
Spika, kwa
muda mrefu tumekua tukionesha wasiwasi kwa uamuzi wa Serikali kuendelea
kuwaabudu makocha wa kigeni katika
michezo. Hali hii si tu kuwa inadumaza soka, bali pia inavunja nguvu makocha
wazawa pamoja na kuwakatisha tamaa vijana ambao wamekua na ndoto za kuwa
makocha hapa nchini. Hii imekua ni Kasumba ambayo ina athari katika maendeleo
ya michezo hapa nchini. Pamoja na makocha wa kigeni kuabudiwa na baadhi ya
viongozi wa michezo na wa kitaifa , makocha hawa wamekuwa na dharau kwa makocha wa nyumbani hali ambayo
inadumaza maendeleo haya ya michezo. Imekuwa ni kawaida hata kwa baadhi ya
viongozi wa soka wa klabu zetu na hata timu ya taifa kuwathamini na
kuwatetemekea makocha kutoka nje pamoja na kwamba tuna zaidi ya miaka 15 sasa
na mlolongo mrefu wa makocha wa kigeni, lakini hawajaweza kuleta mafanikio
makubwa yanayostahili majina makubwa ya klabu zetu na timu zetu za taifa.
Mheshimiwa
Spika,
umeshuhudia mara nyingi makocha kutoka nje wakiletwa nchini na kupokelewa na
maandamano na shangwe na wanachama na wapenzi wa klabu husika kukifuatwa na
kupewa mishahara minono, usafiri wa uhakika na nyumba za kisasa za kuishi. Kuna
kocha wa timu mojawapo kubwa ya Tanzania alitaka nyumba atakayopewa kuishi
lazima iwe na bwawa la kuogelea, na akapewa. Hii ni sawa na kuwa mtumwa ndani
ya nyumba yako mwenyewe. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji ni nini
ambacho makocha wa kigeni wanancho ambacho makocha wazawa hawana kinachofanya
Serikali itenge kiasi cha shilingi Bilioni
1.6 kwa ajili ya malipo ya makocha wa kigeni kwa timu za taifa na matumizi
ya kawaida ya BMT bila mchanganuo? Je, kwanini Serikali inaendelea kuajiri
makocha wa kigeni wakati nchi kuna makocha wenye uwezo wa kufundisha timu za taifa?
Je, ni kwanini serikali na wizara hii inasita kuwafadhili
kimasomo makocha wazawa nje ya nchi ili waweze kutumikia taifa lao pindi
wakimaliza masomo na mafunzo yao?
6.4
MWENENDO WA MCHEZO WA RIADHA
Mheshimiwa
Spika; Tanzania imewahi kupata heshima
kubwa kimataifa kutokana na mchezo wa riadha.Hata hivyo, katika mchezo huu pia
nchi yetu iko katika ‘chumba cha wagonjwa mahututi’. Hali hiyo, inachangiwa na udhaifu wa
kiuongozi, kisera, kimikakati na kioganizesheni kwenye mchezo wa riadha nchini
kuanzia ngazi za chini mpaka taifa.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini
kwamba taifa letu linaweza kutolewa ‘kimasomaso’ na mchezo huu iwapo katika
mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2013/2014 na makadirio ya mapato na
matumizi kwa mwaka 2014/2015 riadha itapewa kipaumbele katika mjadala.
Mheshimiwa
Spika; Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo imekuwa ikitoa maelezo bungeni kwamba riadha nchini inaendelezwa
kupitia wadau mbalimbali ikiwemo Chama Cha Riadha Tanzania (RT). Hata hivyo,
Wizara haijawahi kutoa majibu kamili bungeni namna inavyoshughulikia migogoro
na matatizo ya kiuongozi na kiutendaji katika chama tajwa hali ambayo inaathiri
mustakabali mwema wa mchezo wa riadha nchini.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataarifa kwamba
kabla na hata baada ya uchaguzi wa Chama Cha Riadha Tanzania (RT) uliofanyika
Morogoro tarehe 20 Mei 2012 kwa nyakati mbalimbali kumekuwepo malalamiko ya
wadau wa mchezo huo juu ya uhalali wa uchaguzi huo pamoja na hali tete ya
maendeleo ya mchezo huu. Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ujibu bungeni maswali muhimu yafuatayo
kuhusu mustakabali mwema wa riadha nchini:
Mheshimiwa
Spika; Mosi, Baada ya kufanya vibaya
katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika London 2012 zilitolewa kauli na
ahadi mbalimbali na Wizara na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ya kufanya
maandalizi bora kuelekea 2016 Rio De Janeiro Olympics; Wizara na Baraza la
Michezo Tanzania (BMT) wanalihakikishia vipi bunge kwamba maandalizi
yamekamilika kuondoa ‘ukame’ wa medali na ‘aibu’ kwa taifa?
Mheshimiwa
Spika; Pili, Kambi Rasmi ya Upinzani
inafahamu kwamba kama sehemu ya diplomasia ya michezo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa alilieleza bunge kwamba kwa kushirikiana na Wizara ya
Habari, Vijana na Michezo ilipeleka vijana 50 pamoja na walimu wao kwenye
makambi ya mafunzo katika nchi mbalimbali ikiwemo New Zeland. Baadhi ya vyombo
vya habari viliripoti kwamba mwanariadha Atson Mbugi na Kocha Samwel Tupa nao
wapo nchini New Zeland kwenye mazoezi. Hata hivyo, taarifa zilizoifikia Kambi
Rasmi ya Upinzani ni kwamba wapo Tanga na Arusha. Je, ni kwanini wameachwa,
wakina nani wamepelekwa badala yao na ni kwanini taarifa za uongo zilitolewa
kwenye vyombo vya habari? Ni muhimu kwa Bunge kupewa taarifa kwa kuzingatia
kuwa kwa nyakati mbalimbali zimekuwepo kashfa za wanamichezo wasio na viwango kupewa nafasi za
wenye vipaji na hatimaye kwenda kulisababishia aibu taifa. Aidha zimekuwepo pia
kashfa za wengine kupenyezwa kwenye misafara ya wanamichezo kwa ajili ya kubeba
biashara haramu yakiwemo madawa ya kulevya.
Tatu; Wizara na Baraza la Michezo
Tanzania (BMT) walichukua hatua gani baada kupokea tahadhari ya wanariadha na wataalamu wa riadha juu ya
madai ya uchaguzi wa chama hicho kuelekea kufanyika kinyume na Sheria na. 12 ya
Baraza la Michezo ya mwaka 1967 kabla ya Mwenyekiti wa BMT Dionis Malinzi na
Mkurugenzi wa Michezo Leonard Thedeo kwenda kusimamia Uchaguzi huo?
Mheshimiwa
Spika; Nne; mara baada ya uchaguzi huo
yapo malalamiko ambayo yaliwasilishwa kwa Waziri yenye kuwasilisha maelezo na
vielelezo kuhusu namna uchaguzi huo ulivyokiuka sheria; je, ni sababu zipi
zilizoifanya Wizara kutokutoa majibu yoyote juu ya madai hayo?
Tano; Inadaiwa kwamba viongozi wa
Chama cha Riadha Tanzania (RT) walisaini Makubaliano ya Maelewano (MOU) mbele
ya Viongozi wa Wizara na BMT kwamba marekebisho bora ya katiba ya chama hicho
yangefanyika ndani ya siku tisini ambazo zilimalizika tarehe 20 Agosti 2012.
Hata hivyo, taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani imeelezwa ni kwamba
marekebisho hayo yaliyopaswa kuwezesha mustakabali mwema wa riadha nchini
hayajafanyika. Je, Wizara imechukua hatua gani kwa chama hicho na viongozi wake
kwa kwenda kinyume na makubaliano hayo?
Mheshimiwa
Spika; Sita; Chama Cha Riadha Tanzania
(RT) kimekuwa kikipokea fedha za maendeleo ya mchezo wa riadha kutoka
Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kwa ajili ya mashindano ya kitaifa na
kimataifa. Aidha, Kamati ya Olimpiki (TOC) nayo imekuwa ikipokea fedha kutoka
vyanzo mbalimbali kwa ajili ya pamoja na mambo mengine maandalizi ya wanariadha
kwa ajili ya mashindano hayo. Kwa ujumla riadha imekuwa pia ikichangiwa kwa
ajili ya maandalizi ya All African Games. Hata hivyo, pamoja na vyanzo hivyo,
RT imeburuzwa katika mahakama ya Temeke kwa deni la milioni ishirini ambalo
maelezo yake yana utata. Hali hii inaacha maswali kuhusu mapato na matumizi
katika RT na TOC. Je, Wizara na BMT wako tayari kuwasilisha nakala ya taarifa
zote za mapato na matumizi
yaliyokaguliwa ya RT na TOC ya miaka ya fedha 2012/2013 na 2013/2014?
Mheshimiwa
Spika; Kwa hali hiyo tete na tata ya
kifedha ambayo inasababisha hata wakati mwingine wanariadha wa Tanzania kukosa
vifaa vinavyostahili, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo kutoka kwa Wizara
na BMT, ni nini kilisababisha udhamini wa kampuni ya Lining ya China kwa RT na
wanariadha wetu wa toka mwaka 2007 kusitishwa? Je, uamuzi wa TOC kuingia
mkataba mwingine na PUMA bila kujadili masharti ya mkataba mwingine uliokuwepo
uliathiri vipi mkataba wa awali kwa kuzingatia kwamba yapo madai ya baadhi ya
wadau wa riadha kwamba ilikuwa mikataba ya ‘mtaka yote mkosa yote’?
Mheshimiwa
Spika; Kwa kuzingatia uzito wa maswali
hayo, pamoja na majibu yatakayotolewa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo katika majumuisho; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ifanye uchunguzi wa masuala haya na
mengine yanayohusu RT na TOC ili kuwezesha mustakabali mwema wa mchezo wa
riadha nchini. Hata hii italiwezesha bunge kupokea taarifa na kupitisha
maazimio yatakayorudisha heshima ya taifa letu kimataifa katika mchezo wa
riadha.
7.0 MBIO ZA MWENGE
Mheshimiwa Spika, kwa mufa mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
imekua ikipingana na utumiaji wa fedha za walipa kodi na kitendo cha Serikali
kuendelea kuwatoza wananchi kwa mashinikizo bila ridhaa zao kuchangia shughuli
za mbio za Mwenge wa Uhuru. Ni kweli kuwa Mwenge wa uhuru ni hazina kwa taifa
letu jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana nalo na kwa muda
mrefu tumependekeza Mwenge wa uhuru uwekwe katika makumbusho ya taifa ili
kuweza kuwapatia fursa wananchi kuweza kujifunza hapo.
Mheshimiwa Spika, Suala la kuenzi utamaduni wa Taifa ni la lazima
lakini kuendelea kutumia gharama kubwa kwa jambo hili wakati Watanzania wengi
hawana huduma muhimu ni dharau kubwa. Aidha, katika kipindi hiki ambacho mwenge
wa uhuru unapitishwa katika sehemu mbalimbali za nchi, chama tawala nacho
kinapita katika maeneo mbalimbali ya nchi kuangalia utekelezaji wa ilani yake
pamoja na kuzindua miradi ya maendeleo ya wananchi. Huu ni usanii mkubwa
unaofanywa na Serikali ya CCM kwa dhumuni la kuwanyonya watanzania masikini kwa
kigezo cha kuwa wanachangia shughuli za maendeleo wakati ukweli ni kuwa
watanzania wanachangishwa mpaka fedha kwa ajili ya malazi na chakula kwa
wakimbiza mwenge kama alivyojibu Waziri Mkuu. Na kwa kuwa kumekua na malalamiko
kutoka wa wafanyabiashara, wafanyakazi wa Serikali na hasa walimu sehemu
mbalimbali nchini kuwa wanalazimishwa kuchangia mwenge bila ridhaa yao. Na kama
CCM inataka bado mambo ya mbio za mwenge basi wagharamie wenyewe kwa asilimia 100 na si kuwalazimisha wananchi
kuchangia hasa ukizingatia kuwa Waziri Mkuu alitoa kauli wiki hii kuwa
kuchangia mbio za mwenge wa uhuru ni hiyari. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaendelea kusisitiza kuwa sasa ni wakati muafaka mwenge wa uhuru
kupelekwa jumba la Makumbusho ya Taifa.
8.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, napenda kuhitimisha hoja za Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na michezo kwa
kulitaka Bunge lako tukufu kuishinikiza Wizara kutekeleza maoni ya Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni ambayo Wizara imekua ikiyakubali kwa muda wa miaka mitatu
mfululizo.
Aluta Continua.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha
…………………………………………..
Joseph Osmund Mbilinyi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya
Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo.
29.05.2013
No comments:
Post a Comment