Tuesday, May 6, 2014

Mnyika: Tutaandamana kudai maji Ikulu

Mbunge  wa Ubungo John Mnyika,  amesema endapo Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, hatachukua hatua  na kutoa majibu yanayoeleweka  katika Bunge la Bajeti juu ya tatizo la maji jijini Dar es Salaam, ataungana na wananchi kuandamana hadi Ikulu.
Mnyika alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema baada ya kuona hakuna majibu ya ufumbuzi wa tatizo hilo kutoka kwa viongozi husika aliamua kumuandikia barua Rais Jakaya Kikwete yakumtaka aitishe kikao cha kuzungumzia tatizo hilo, lakini hadi sasa hamna majibu yaliyotolewa.
Aidha, alisema atakwenda katika Bunge la Bajeti kupambana na Profesa Maghembe ampe majibu yanayoeleweka na kuhakikisha anachukua hatua bila hivyo ataungana na wananchi kwenda Ikulu kumtaka Rais Kikwete kuingilia kati tatizo hilo kwa sababu linawatesa sana wananchi.
Mnyika alisema katika ziara aliyofanya jimboni kwake tatizo la maji ni kubwa na baadhi ya kata hazijapata maji kwa kipindi cha miezi mitatu sasa pamoja na kwamba wananchi wamelalamika kwa mamlaka husika, lakini hakuna jitihada zozote zinazofanyika kutatua kero hiyo sugu.

1 comment:

  1. Mnyika kaza buti.Siku ya maandamano tutakwenda na ndoo zetu kuteka maji ikulu.

    ReplyDelete