Friday, May 9, 2014

Mbowe atoboa CCM ilivyohodhi wabunge 201 Bunge la Katiba

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimehodhi Bunge Maalum la Katiba kwa kuingiza makada wake 160 kati ya wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais.

Kadhalika, kambi hiyo imesema wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hawatarejea ndani ya Bunge la Katiba na wataendelea na harakati za kudai Katiba mpya nje ya Bunge.

Kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe, akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2014/15, alisema Ukawa wataendelea na harakati zao za kudai Katiba mpya yenye kujibu haja, matakwa na matumaini ya Watanzania walio wengi nje ya Bunge Maalum kwa kuwa limetekwa nyara na CCM.

Alisema utafiti uliofanywa na kambi hiyo umebaini kuwa kati ya wajumbe 201, wajumbe 160 ni wanachama na viongozi wa CCM waliochomekwa kwenye Bunge hilo kwa kutumia kivuli cha waganga wa kienyeji, taasisi za kidini, asasi za kiraia, taasisi za kitaalamu, watu wenye malengo yanayofanana na hivyo kuweka msingi mbaya katika Bunge hilo.

“CCM iliendelea kufanya hila za kuchakachua kanuni za Bunge Maalum ili kupitisha hoja zao kirahisi na ziliposhindwa walitumia mabavu ya wazi kwa kulazimisha Mwenyekiti wake Taifa, Kikwete kutumia kivuli cha Urais kusisitiza msimamo wa CCM na kutisha wajumbe wa Bunge hilo kwamba wakipitisha muundo wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume basi Jeshi la Wananchi litapindua serikali,” alisema.

Mbowe alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itaendeleza harakati nje ya Bunge Maalum zitakazowezesha kubadilishwa kwa muundo wa Muungano kwa kuivua Tanganyika koti la Muungano, kuipitia Zanzibar mamlaka kamili ndani ya Muungano na kujenga mahusiano ya hadhi na haki sawa baina ya Tanganyika na Zanzibar.

“Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuweka wazi msimamo wake na wanachama wa Ukawa kwamba haitakuwa busara kuendelea na mjadala wa Bunge Maalum wenye lengo la kupitisha mapendekezo ya kundi la viongozi wa CCM, hatutashiriki Bunge lililojaa kauli za kibaguzi, kashfa, vijembe na matusi dhidi ya wajumbe wa Ukawa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Mbowe.

Alisema Ukawa wamekataa kuwa sehemu ya Bunge Maalum lililojaa vitisho, kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana na kushinikizana na kwamba hawatarejea hadi dhima halisi ya Bunge hilo itakapopatiwa ufumbuzi.

Mbowe alisema kwa sasa Rasimu ya Katiba mpya imewekwa kando na wajumbe wa kundi la walio wengi kujivika jukumu lililokuwa la Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakidai kupokea maoni mbadala ya wananchi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na ukiukwaji wa kiasi kikubwa wa haki ya wananchi ambao kwa ujumla wao walitoa maoni yao kwa Tume ya Katiba
MAPATO NA MATUMIZI
Mbowe alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, hadi kuahirishwa kwa Bunge hilo kiasi cha Sh.  blioni 27 zilitumika na kwamba kwa ujumla mchakato mzima kwa kipindi cha miaka miwili umetumia kiasi cha Sh. bilioni 102 na kwamba kiasi hicho ni kikubwa katika nchi ambayo maendeleo na huduma za jamii zenye umuhimu mkubwa kwa ustawi wa wananchi zimekwama kwa kukosa fedha.

Alisema fedha kwa ajili ya Bunge Maalum zilitakiwa kuidhinishwa na ama sheria ya matumizi ya serikali iliyotungwa mahususi na Bunge au sheria iliyotungwa kwa mujibu wa ibara ya 140 ya Katiba inayohusu mfuko wa matumizi ya dharura unaoanzishwa kwa ajili ya mambo ya haraka.

Aidha, Mbowe alihoji na kuitaka serikali kutoa majibu ya bajeti ya matumizi ya Bunge Maalum ni kiasi gani na kwa ajili ya matumizi gani, kiasi kilichotumika hadi sasa na kwa matumizi gani, nani aliyejadili na kupitisha bajeti hiyo, sheria gani iliyotungwa na Bunge lipi iliyoidhinisha matumizi ya fedha hizo na kwa waraka gani Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliidhinisha matumizi hayo.

Aidha, alisema majibu ya maswali hayo ni muhimu ili kuepusha Taifa na balaa la ufisadi na wizi mkubwa wa fedha za umma kama ilivyotokea mwaka 2005 kwa mabilioni ya fedha yaliibwa kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  kwa ajili ya kugharimia uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

KAULI ZA CCM KUHUSU SUK
Mbowe alisema CCM nje ya Bunge hilo wameendelea na kauli za uchochezi na kibaguzi zinazoweza kuvunja amani na kwamba katika mkutano wa hadhara uliofanyika Zanzibar Jumapili iliyopita, baadhi yaviongozi wake walisema wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi ili kuwapa nafasi wananchi waulizwe iwapo wanataka kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar iliyoundwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Alisema madhumuni ya mchakato huo ni kuvunja SUK ambayo iliamuriwa iwepo na kura ya maoni ya Wanzanzibari wote na imesaidia kuleta amani na utulivu Zanzibar.

KAULI ZA KIBAGUZI
Alisema kauli ya Makamu wa Pili wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, katika mkutano wa CCM, alisema Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Ismail Jussa Ladhu, ambaye pia ni Mwakilishi wa Mji Mkogwe si raia wa Zanzibar ni kauli ya kibaguzi, kichochezi na yenye kupandikiza chuki dhidi ya watu wenye asili ya Kihindi.

“Ni kauli inayopaswa kulaaniwa na kila mpenda amani popote alipo,” alisisitiza. Alisema viongozi wa serikali wanawajibika kukemea kauli hizo, lakini hawafanyi hivyo na badala yake kuonekana ama kuzitoa, kuzikoleza au kuzishabikia bila kutathmini nafasi na wajibu wao wa kuliunganisha Taifa.

UCHAGUZI MKUU/MITAA 

Alisema iwapo Tanzania itakwenda katika uchaguzi mkuu bila Katiba mpya Taifa litaingia katika mgogoro mkubwa wa kikatiba ambao utakuwa rahisi kuzaa machafuko haswa kipindi cha uchaguzi.

Alisema Katiba inatumika sasa ina mapungufu mengi na haiwezi kuwa jawabu la uchaguzi ulio huru na wa haki katika mazingira ya sasa yanayojengwa na uzoefu wa chaguzi zilizopita chini ya mfumo wa vyama vingi na kwamba upo uwezekano wa chaguzi za serikali za mitaa kufanyika bila Katiba mpya kama ambavyo serikali imeshasema na kuanza maandalizi ya uchaguzi huo Oktoba mwaka huu.

Aidha, alisema Kambi hiyo inaishauri serikali kuweka utaratibu wa mpito kushughulikia masuala yote ya uchaguzi na kwamba Taifa haliwezi kuingia kwenye uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa kwa utaratibu uliopo sasa na uchaguzi mkuu mwakani.

No comments:

Post a Comment