CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimesema kuwa kimepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za
msiba wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, Bi. Shida Salum ambaye ameaga dunia leo
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya chama,
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe amesema kuwa Bi. Shida ambaye pia
hadi anafariki alikuwa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ameacha pengo kubwa
kutokana na utumishi wake wa muda mrefu ndani ya chama.
“Kwa niaba yangu,viongozi wa wenzangu
ndani ya chama, wanachama, wapenzi, mashabiki na wafuasi wetu nchi nzima, kwa
masikitiko makubwa natoa salamu za rambirambi kwa familia ya Mama Shida Salum.
“Tunaungana na familia hiyo, ndugu,
jamaa na marafiki na watu wote walioguswa na msiba huu katika wakati huu mgumu.
Tunaomba sana Mwenyezi Mungu awatie nguvu na kuwapatia moyo wa subira kuukabili
wakati huu wa msiba wa kuondokewa na mpendwa Mama Shida Salum,” amesema
Mwenyekiti Mbowe.
Ameongeza kusema kuwa CHADEMA taarifa
hizo za kushtua za kuondokewa na Mjumbe wa Kamati Kuu, zimewakuta viongozi
mbalimbali wa chama hicho wakiwa wametawanyika katika maeneo mbalimbali nchini
kwa majukumu ya kichama.
Mwenyekiti Mbowe ameongeza kusema kuwa kutokana
na hali ya uharaka wa chama kushiriki kikamilifu katika mazishi ya Bi. Shida
Salum yanayotarajiwa kufanyia kesho Jumatatu mkoani Kigoma, amemteua Mjumbe wa
Kamati Kuu ya CHADEMA, Ezekiel Wenje (MB) ambaye pia ni Waziri Kivuli katika
Kambi ya Upinzani Bungeni, kukiwakilisha chama, huku viongozi wengine nao
wakijaribu kutafuta njia ya kuweza kuwahi mazishi hayo.
“Tayari tumepata ndege ya kukodi ambayo
Wenje ataitumia kwenda Kigoma kuwahi mazishi ya Bi. Shida Salum. Wenje alikuwa
mmoja wa viongozi waliokuwepo Dar es Salaam. Hadi Mama Shida anaaga dunia leo,
Wenje alikuwepo hospitalini akituwakilisha kumjulia hali mama,” amesema
Mwenyekiti Mbowe.
Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa Mama
Shida daima atakumbukwa kwa namna alivyokipigania chama chake, familia yake na alivyokuwa
mtetezi wa makundi maalum katika jamii, kwa muda mrefu wa maisha yake hapa
duniani.
Imetolewa leo Juni 1, 2014 na
Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano
Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA)
No comments:
Post a Comment