Tuesday, May 13, 2014

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE MCH ISRAEL NATSE (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS MAZINGIRA KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015

(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99 (9), ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Mwaka 2013)
  1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali la Majukumu ya Wizara (Assignment of Ministerial Responsibilities Notice), la mwezi Januari, Mwaka 2011, majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais yameainishwa kwa ifuatavyo:-
Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Sera na Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Kufuatilia na kuratibu Shughuli za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (National Environment Management Council-NEMC).
Aidha, kutatua changamoto zinazohusiana na uharibifu wa Mazingira ili kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali na maliasili.

 Mheshimiwa Spika,
Serikali iliunda Sera ya Taifa ya Mazingira mwaka 1997, sera ilibaini matatizo makuu sita ya kimazingira yaliyopo nchini ambayo ni:
1.       Uharibifu wa ardhi;
2.       Kutokupatikana kwa maji safi na salama kwa wakazi wa mijini na vijijini
3.       Uchafuzi wa Mazingira
4.       Upotevu wa Makazi ya Wanyamapori na bioanuai;
5.       Uharibifu wa makazi na viumbe wa majini; na
6.       Ukataji wa misitu.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kubaini matatizo hayo yakawekwa malengo ya sera ili kukabiliana na madhara hayo:
1.      Kuhakikisha, udumishaji,usalama na  matumizi sawa ya raslimali kwa msingi wa sasa na vizazi vijavyo bila ya kuharibu mazingira au kuhatarisha afya na usalama,
2.      Kuzuia na kudhibiti uharibifu wa ardhi, maji, mimea na hewa ambayo ndiyo mfumo wa uhai wetu,
3.      Kuhifadhi na kuendeleza urithi wetu na ule uliotengenezwa na binadamu, ikiwa ni pamoja na maisha ya viumbe wa aina mbalimbali na wa kipekee nchini Tanzania;
4.      Kung’amua na kufahamu mahusiano muhimu kati ya mazingira na maendeleo na kuhimiza ushirikiano wa mtu binafsi na jamii katika kuhifadhi mazingira;
UHARIBIFU WA ARDHI
Mheshimiwa Spika,
Ardhi ndio msingi mkuu katika utunzaji wa mazingira na pia ndio msingi mkuu katika kuchangia mabadiliko ya tabia nchi. Hivyo basi matumizi mabaya ya ardhi ni kupelekea uharibifu wa mazingira na hivyo kuzidisha au kuharakisha mabadiliko ya Tabia nchi.
Ni ukweli kwamba kama ardhi imeharibika maana yake ni kwamba hakuna mmea utakaopandwa na kuota bila ya kutumia mbolea, na hapa hoja ni je wananchi wetu wanauwezo kiasi gani kuendelea kununua mbolea za viwandani kwa ajili ya kuotesha miti ambayo mpaka ni kuivuna inachukua muda wa kuanzia miaka saba?

Mheshimiwa Spika,
Matumizi makubwa  ya muda mrefu na yasiyoratibiwa vyema ya mbolea za chumvi chumvi za viwandani ni sababu tosha inayochangia uharibifu wa ardhi. Hivi sasa nyanda za juu kusini kilimo cha aina yoyote hakiwezi kufanyika bila ya kutumia mbolea za viwandani.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa tuna wataalam wengi na wazuri wa udongo na pia wataalam wa mazingira, na tatizo hili sio kwamba limetokea leo bali ni la siku nyingi.

Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kama sera ya Mazingira ya mwaka 1997 inavyosema kuwa wao ndio wasimamizi wa sheria ya uhifadhi wa mazingira ya mwaka 2004. Je, ni ushauri gani wamekwisha utoa kwa taasisi au wizara husika juu ya kupunguza au kusitisha matumizi ya mbolea za chumvi chumvi za viwandani kwa wakulima hasa wa mikoa ya Iringa, Njombe, Songea, Mbeya, Rukwa na Katavi?

Mheshimiwa Spika,
Tunahoji hilo kwa sababu sheria ya Mazingira ndiyo sheria iliyokuwa juu ya sheria zingine zote linapotokea suala la kuhifadhi mazingira.




  1. MABADILIKO YA TABIANCHI

Mheshimiwa Spika,
Tanzania tayari imeathirika kwa uwepo wa mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo pamoja na ukame wa muda mrefu unaojirudia rudia ambao unaambatana na athari kubwa katika kilimo,usafirishaji, nishati, biashara na sekta mbalimbali za uchumi kwa jamii. Hivi sasa zaidi ya asilimia 70 ya majanga yote ya asili katika Tanzania yanahusika na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame na mafuriko.
Mheshimiwa Spika,
Wakati wa majanga hayo, kilimo katika maeneo husika kinadorora au kusimama, mifugo mingi na wanyama wa porini wanakufa kwa kukosa chakula na maji, na wakati mwingine kusombwa na mkondo wa maji yaliyofurika.
Mheshimiwa Spika,
Baadhi ya viashiria vya uwepo wa mabadiliko ya tabianchi katika nchi yetu ni pamoja na vifo vya mifugo vilivyokithiri kutokana na ukame, hasa maeneo ya kaskazini mwa Tanzania kama vile Monduli na Longido. Wastani wa mvua kwa mwaka umepungua kwa asilimia 25. Utokeaji wa mafuriko unaosababishwa na ongezeko la mvua zisizotabirika katika maeneo makame yasiyo na mimea na hivyo maji kutiririka kwa kasi zaidi na kusababisha madhara maeneo yanapoelekea.
Mheshimiwa Spika,
Ongezeko la joto duniani linasababisha ongezeko hatari na utokeaji wa magonjwa mapya kwa mamilioni ya watu, hasa yale yanayoenezwa na vimelea na bacteria kwa maeneo ambayo kwa asili hayakuwepo. Tafiti mbalimbali zinazohusu mwelekeo wa joto wa muda mrefu katika ziwa Viktoria,Tanganyika na Nyasa zinaonesha ongezeko la joto katika maji ya kina kirefu kati ya nyuzi za sentigredi 0.2 mpaka 0.7 kuanzia mwanzoni mwa  miaka ya 1900( Taarifa za Serikali ya mwaka 2009).
Mheshimiwa Spika,
Kwa asili tulizoea watu kuhama au kuwa wakimbizi kutokana na mapigano ya vita, lakini kwa sasa wahamiaji wengi wanatokana na mabadiliko ya tabianchi na kwa lugha iliyozoeleka ni “environmental refugees”. Hili limekuwa tatizo sana kwani kutokana na watu kuhama maeneo yao ya asili kwa ajili ya ukweli kwamba maeneo hayo hayawezi tena kuwezesha kuishi kwao na hivyo inawalazimu kuhamia maeneo mengine ili kuendelea na maisha yao. Hili limetokea sana kwa wafugaji na wakulima.
Mheshimiwa Spika,
Kiutalaam, mabadidiko ya tabianchi yamechangiwa na  Kuongezeka kwa shughuli mbalimbali katika uso wa dunia, hasa zile zinazofanywa na binadamu. Shughuli hizo baadhi zikiwa za kimaendeleo na zisizo za kimaendeleo zimechangia kuzalisha hewa chafu (green house gases) ambazo huchangia katika ongezeko la joto duniani (global warming). Kwa ufupi ni kwamba shughuli zote ambazo zinaongeza hewa ukaa angani ndio chanzo kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Spika,
Baadhi ya shughuli hizo kwa uchache ni kama vile ongezeko la viwanda hasa katika nchi za ulaya na Asia, ukataji miti na uchomaji misitu, uzalishaji na utupaji wa taka ovyo, ufugaji usiozingatia idadi ya mifugo hasa ng'ombe, mbuzi , kondoo na wanyama wengine wanaoharibu mazingira kwa kuangamiza mimea, uchimbaji madini, matumizi mabaya ya mashine/mitambo na magari yaliyochoka yanayozalisha hewa ya ukaa, utumiaji wa vyombo chakavu kama majokofu, computer, Tv na vitu vingine na ongezeko la shughuli za kivita sehemu mbalimbali duniani ambazo huchangia kuzalisha hewa chafu kwa kulipua mabomu.
Mheshimiwa Spika,
Kuna ushahidi mwingi sana kuthibitisha uwepo wa “mabadiliko ya tabia nchi”. Miongoni wa ushahidi huo ni kuwepo kwa hali mbaya ya hewa, kama vile: ukame, mvua isiyotabirika, mafuriko, mkondo wa joto kali na kuongezeka kwa vimbunga, ongezeko la joto, magonjwa ambayo hapo mwanzo hayakuwepo katika baadhi ya maeneo, kuongezeka kwa kasi ya kuyeyuka kwa barafu na kubadilika kwa uoto na maumbile asilia duniani.
Mheshimiwa Spika,
Tanzania na watanzania wa maeneo mbalimbali ni wahanga wa Mabadiliko ya Tabia nchi, kwa ushahidi uliotolewa hapo awali. Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mpango kazi  wake bado haujawa na tija kwa taifa.
Mheshimiwa Spika,
Ni ukweli kwamba madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kila mwananchi katika kila nchi, hili limepelekea uwepo wa maslahi binafsi yanayokinzana kimataifa na hivyo suala hilo kuwa gumu kufikia maridhiano  katika historia ya dunia. Masuala ya mabadiliko ya tabianchi yanashughulikiwa kwa kuzingatia sayansi na ujuzi wa masuala ya asili na hali ya hewa. Kwa sasa siasa za kimataifa wakati mwingine maslahi binafsi ya taifa na itikadi yake vinakuwa juu ya sababu zingine zozote za kuongoza maamuzi ikiwemo hata ile ya sayansi na utaalaum unavyotaka[1].
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya Utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/14 na makadirio ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2014/15, sehemu ya iv, mojawapo ya malengo ya Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira  kwa mwaka huu wa fedha katika Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, ni kuunda/kuanzisha Idara/sehemu ya Mabadiliko ya Tabianchi.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya Tabianchi hapa kwetu, kila mtu anaona bila ya hata kuambiwa.Kwa masikitiko makubwa ni kwamba hata Idara rasmi katika Wizara hii haikuwepo, bali watendaji wamekuwa wanakwenda kuhudhuria mikutano na makongamano ya kimataifa tu. Hoja ni je ni kwa vipi ujuzi na uzoefu wao katika makongamano ya nje na ndani umekuwa ukiisaidia nchi yetu kukabiliana na matatizo yaletwayo na mabadiliko ya Tabianchi?
Mheshimiwa Spika,
Ni dhahiri kwamba bila ya kuwepo kwa idara ambayo ipo chini ya mtu maalum basi uwajibikaji hauwezi kupimwa, na kwa hili la Mabadiliko ya Tabianchi, swali ni nani anahitajika kuwajibika? Je Wizara nzima ambayo ni Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira? Kufanya hivyo ni kuto-itendea haki kwani Ofisi hiyo inatakiwa iwe na Idara na Kurugenzi tafauti za kiutendaji kulingana na upana wa sekta ya mazingira.
Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira katika Mradi Na. 5306-(Mainstreaming Environment and Climate Change Adaptation in the Implementation of National Policies and Development Plans) zimetengwa shilingi 800,825,000.00. Wizara haina idara inayoshughulika na mambo ya Mabadiliko ya Tabianchi, pili ukiangalia matumzi yaliyowekwa kwa ajili ya fedha hizo zaidi ya asilimia 8 ni vikao tu, na kuandaa mfumo wa kitaasisi katika usimamizi wa mabadiliko ya Tabianchi.

Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa hakuna mfumo wa kitaasisi kama Serikali inavyokiri katika Randama na mabadiliko ya Tabianchi ni tatizo ambalo liko nje ya mipaka ya Tanzania. Hivyo basi bila ya kuwa na mfumo wa kiutendaji unaoeleweka fedha nyingi zinaendelea kuletwa na wahisani, kama mwaka huu zinaingia shilingi 720,825,000.00 na fedha hizo hazitatumika kuilinda nchi yetu na madhara yanayotokana na mabadiliko ya Tabianchi.
Mheshimiwa Spika,
Mradi namba(…..)?: Climate Change Adaptation Programmes Sh. 1,892,755,000.00. Kwa mujibu wa Randama inaonyesha kwamba kiasi cha shilingi 2,893,755,000.00 zinaombwa kwa ajili ya kutekeleza kazi za mradi huu. Mheshimiwa Spika, sijui kulikuwa na makosa ya kiuchapaji au ndio ilivyokusudiwa kwa ongezeko la shilingi bilioni 1.
Kwa kuwa mradi wenyewe unaoombewa fedha hizo haioneshi ni mradi namba ngapi, na katika kuhakiki tarakimu ni dhahiri kuwa si makosa ya kiuandishi bali kuna jambo ambalo Kambi Rasmi inahitaji ufafanuzi wa utofauti wa fedha hizo za mradi tajwa wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Mheshimiwa Spika,
Sera inatoa suluhisho la ushirikishwaji wa wananchi katika ngazi zote katika kupambana na mabadiliko ya Tabianchi, wakati huohuo Sera ikijenga mazingira ya wananchi kunufaika na fursa zilizomo katika mabadiliko ya tabianchi katika ngazi zao zote za jamii.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa Serikali ya CCM haina Sera kwa ajili ya Mabadiliko ya Tabianchi, ni dhahiri kwamba hakuna suluhisho lolote zaidi ya matumizi yasiyo na tija ya fedha za walipa kodi, kuhusiana na tatizo hili la mabadiliko ya Tabianchi.
Mheshimiwa Spika,
Katika kufanya uchambuzi wa bajeti ya ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, inaonyesha kwamba japokuwa ofisi hiyo imetengewa fedha kidogo kwa kulinganisha na majukumu hasa ya kulinda na kiuhifadhi mazingira katika dhana pana.
Mheshimiwa Spika,
Ofisi hii imetenga jumla ya shilini milioni 126.32 kwa ajili ya mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa ajili ya watumishi wake kwa idara mbalimbali kwenye Wizara hiyo. Ni ukweli uliowazi kwamba kuna wahitimu wengi sana wenye sifa mitaani na kuna wanafunzi wengi sana ambao wanakosa mikopo na hawana kazi.
Mheshimiwa Spika,
Kwa hali ya kawaida tu, ni kwa vipi Serikali inaweza kutumia kiasi kikubwa cha fedha kusomesha watu ambao tayari wanakazi na wanauwezo wa kulipia masomo yao? na mbaya zaidi wanaendelea kulipwa stahili zao kama watumishi.  Kambi Rasmi ya Upinzani inaliona hili kuwa ni njia mojawapo ya kuwanyima fursa wale wote wanaohitaji zaidi msaada wa Serikali.

  1. TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa rasmi za Bunge za tarehe 19 April 2013 ni kwamba “Takribani zaidi ya tani milioni moja ya mkaa hutumiwa kwa mwaka hapa nchini huku Dar es Salaam pekee ikitumia zaidi ya asilimia 50% ya mkaa wote unaozalishwa na kutumika hapa nchini. Magunia zaidi ya elfu ishirini na nane (28,000) yenye kilo kati ya 60 hadi 80 huingizwa Dar es Salaam kila siku. Hii ina maana kuwa, Dar es Salaam pekee huingiza wastani wa zaidi ya magunia milioni 10.2 kwa mwaka. Kiasi hiki kinaifanya Tanzania kushika nafasi ya nne na kuwa miongoni mwa nchi kumi duniani zinazoongoza kuzalisha mkaa kwa wingi kuliko nchi zote ambapo Tanzania pekee inazalisha asilimia 3% ya mkaa wote unaozalishwa duniani. Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa Tanzania hutumia zaidi ya tani 2,650 za mkaa kila siku.
Mheshimiwa Spika, Ili kuzalisha tani moja ya mkaa kwa njia ya jadi kama inavyofanyika hapa nchini, zaidi ya tani 10 hadi 12 za miti au kuni huhitajika. Hii ina maana kuwa kuzalisha magunia 15 huhitajika tani 10 hadi 12 za miti au kuni hivyo kuhitaji ekari 846 za miti kila siku ili kuvunwa kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya mkaa kwa watumiaji. Takwimu zinaonyesha kuwa matumizi ya mkaa tangu mwaka 1960 yamekuwa yakiongezeka kila siku. Itambulike kuwa eneo la misitu Tanzania ni kilomita za mraba 344,326 sawa na asilimia 38.9% ya ardhi yote”.
Mheshimiwa Spika,
Imetubidi kunukuu maneno hayo kwa sababu kubwa kwamba, Ofisi ya Makamu wa Rais ndio yenye mamlaka na jukumu la msingi la kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa salama. Kwa uvunaji wa miti na uchomaji wa mkaa kiasi hicho, hoja hapa ni kwa jinsi gani tunaweza kuepukana na jangwa kwa miaka ijayo kama takwimu za matumizi ya mkaa kwa mkoa mmoja wa Dar es Salaam yako hivyo, je na kwa mikoa mingine zaidi ya Dar es Salaam takwimu zikoje?
Mheshimiwa Spika,
Aidha, ni ukweli kuwa matumizi ya mkaa na kuni kwa maeneo ya vijiji ni makubwa lakini si kama ambavyo mkaa unatumika mijini. Na kwa mwaka jana ukweli ni kwamba Serikali haikutoa mwelekeo tunakwendaje mbele katika kuhakikisha matumizi ya mkaa kwa mijini yanapungua.
Mheshimiwa Spika,
Kwa sasa tumejaaliwa kuwa na gesi, lakini kwa masikitiko makubwa makampuni yanayoingiza gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani ndiyo yanazidi kuongezeka. Jambo hili linatoa hisia kwamba sekta hii ya gesi ya kupikia ndio sababisho la kwanza kuzuia gesi yetu ya asili isichakatwe kwa ajili ya matumizi ya majumbani. Kambi Rasmi ya Upinzani ina hoji, Je Ofisi hii ya Makumu wa Rais inachukua hatua gani katika mchakato huu wa kuhakikisha matumizi ya mkaa yanapungua na uharakishaji wa matumizi ya gesi asilia kwa matumizi ya majumbani unafanikiwa haraka?
Mheshimiwa Spika,
Ni dhahiri kwamba bila ya kuwepo matumizi mbadala ya mkaa ambayo ni gesi, achilia mbali umeme ambao bei yake haiwezekaniki kwa mtanzania wa kawaida. Vinginevyo suala la kukata miti haliepukiki kutokana na kutokuwepo kwa mbadala wa uhakika kwa watanzania.

  1. UJENZI HOLELA MIJINI
Mheshimiwa Spika,
Miradi yote hapa nchini kabla ya kuanza utekelezaji wake ni lazima kwanza ufanyiwe tathmini (Environmental Impact Assessment-EIA) na kupata cheti cha kuuwezesha uendelee kama ulivyokuwa umepangwa. Jambo la kushangaza ni kwamba miradi ambayo inamilikiwa na Serikali imekuwa haipati cheti cha Tathmini na hivyo imekuwa ikileta usumbufu mkubwa sana kwa watumiaji na hivyo kuwa kero kwa Serikali yenyewe.


Mheshimiwa Spika,
Hoja hii inatokana na ukweli kwamba, Ofisi ya Kampuni inayojenga miundombinu ya mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam (Strabag) imepewa Hati na Serikali ya kumiliki eneo hilo la Jangwani na hivyo tayari wamejenga ofisi zao za Kudumu.  Mbali na kuhoji utolewaji wa hati kwa Kampuni hiyo, je tathmini ya mazingira imefanyika? kwani eneo hilo miaka yote linakumbwa na mafuriko. Kitendo cha kujenga hapo ni kurudisha maji kwa maeneo jirani na kuzidisha maafa. Aidha, kama Kampuni hiyo imepewa hati miliki ni kwanini waliokuwa wamejenga eneo hilo walihamishwa na kupelekwa nje ya mji?
Mheshimiwa Spika,
Moja ya tatizo kubwa mijini ni ujenzi holela wa makazi na viwanda, jambo ambalo linaleta usumbufu mkubwa hasa kwa kipindi hiki ambacho Dunia imekabiliwa na tatizo kubwa la mabadiliko ya tabianchi. Jiji la Dar es Salaam lina mabonde ambayo ndiyo njia kuu ya maji kutoka nchi kavu kuelekea baharini, hivyo basi ujenzi holela unazuia mkondo wa maji ni matatizo makubwa sana kwa majirani.
Mheshimiwa Spika,
Wale wote ambao wamefanya hivyo ni watu ambao wanahadhi katika jamii, Mhe Mbunge Getrude Rwakatare amelalamikiwa sana  kwani amezuia mto Ndumbwi kwa kuziba  mkondo wa maji na hivyo kusababisha mafuriko  na daraja kuvunjika na kuleta madhara makubwa  kwa wakazi wa eneo jirani na hilo. Aidha, kuna mtu mwingine anayeitwa Mzamili Katunzi,amejenga na anaendelea na ujenzi katikati ya mto na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. Je Serikali iko wapi? Au iko likizo?  Serikali itoe kauli kutokana na ukiukwaji huu wa sheria unaofanywa kwa makusudi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani ina hoji kama Serikali iko likizo kutokana na ukweli kwamba watumishi wa NEMC wametishiwa maisha kwa kupigwa wakiwa kazini, lakini hakuna hatua zozote zimechuliwa kwa wahusika. Tunaitaka Serikali kutoa maelezo kuhusiana na suala hili.

  1. UCHAFUZI WA MAZINGIRA
Mheshimiwa Spika,
Katika mwendelezo huo huo wa uchafuzi wa mazingira, malalamiko ni makubwa kwa viwanda, na makampuni ya madini kutokufuata sheria zinazohusiana na uhifadhi wa mazingira. Mojawapo ya kiwanda kinachoharibu mazingira ni kiwanda cha 21-Century kilichopo mkoani Morogoro- kinatiririsha maji machafu kwenye mto Ngerengere mto ambao unaungana na mto Ruvu ambao ndio chanzo kikuu cha maji yanayotumiwa na wakazi wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika,
Mbali ya taka hizo zenye sumu kuingia katika chanzo cha maji yanayotumiwa na wakazi wengi, pia kiwanda hicho inakadiriwa kwa siku kutumia kuni tani 50 kwa ajili ya uendeshaji wake. Hii ni teknolojia iliyopitwa na wakati. Kuni hizo au magogo hayo ni kutoka kwenye miti ya asili.
Mheshimiwa Spika,
Mbali na Kiwanda hicho cha 21-Century kuna Kampuni ya Barrick inayochimba dhahabu katika mgodi wa Nyamongo-Tarime, hadi sasa bado maji taka yenye sumu yana tiririka katika mto Tigite na hakuna hatua zilizochukuliwa na Serikali kwa kampuni ya Barick kwani uchafuzi bado uko pale pale.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kumbukumbu zilizopo ni kwamba Bunge la Tisa lilikwisha unda kamati ndogo kwa ajili ya kuchunguza tatizo hilo, lakini kwa masikitiko makubwa taarifa yake haijawahi kuletwa hapa Bungeni ili Bunge zima liijadili na kutoa maazimio. Huu kwa njia mojawapo unaweza kuwa ni uzembe au muendelezo wa Bunge letu kwa kutokutaka kujadili taarifa za kamati ndogo zinazopoundwa kuangalia matatizo yanayozikabili jamii- (Kwa mfano: Uchunguzi Loliondo-Wananchi kuchomewa nyumba na Tarime- uchafuzi wa maji yanayoingia mto Mara).
Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza kwa hili NEMC iko wapi? Uwajibikaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais uko wapi?
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa sheria ya Usimamizi na Mazingira ya mwaka 2004, inasema kuwa makampuni yanayojihusisha na uchimbaji wa madini, pindi wanapomaliza shughuli zao ni lazima warudishie ardhi katika hali ilivyokuwa kabla ya kuanza uchimbaji.
Mheshimiwa Spika,
Makampuni ya Lesolute iliyokuwa inafanya shughuli zake Wilaya ya Nzenga na Kampuni ya Barick Gold Mine iliyokuwa inamiliki mgodi wa Tulawaka uliokuwa Wilaya ya Biharamulo imemaliza kazi na kuiuzia mgodi huo STAMICO lakini haikutimiza kazi yake ya kuhakikisha mazingira yanarejshwa katika hali yake ya uhalisia. Kambi Rasmi ya Upinzani inaliona kuwa mzigo mkubwa umerudishwa kwa Wananchi kupitia kampuni ya STAMICO japokuwa kampuni hiyo bado ni change. Je Serikali inatoa kauli gani kwa ulaghai huo?

  1. BARAZA LA USIMAMIZI WA MAZINGIRA-NEMC
Mheshimiwa Spika,
Baraza la usimamizi wa mazingira ndicho chombo kikuu chenye dhamana ya kuhakikisha sheria ya mazingira inafuatwa kwa ukamilifu wake, lakini kwa bahati mbaya ni kwamba fedha inayotengewa kwa ajili ya kutimiza majukumu yake ni kidogo sana kiasi kwamba  Baraza linashindwa kufanya kazi muhimu ya ufuatiliaji.
Mheshimiwa Spika,
Randama ya Wizara inaonyesha kuwa Bajeti ya ruzuku kwa Baraza  kwa mwaka wa fedha 2013/14 ilikuwa shilingi bilioni 1.96, kwa mwaka huu wa fedha ruzuku kwa Baraza zimetengwa shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. Aidha, Baraza linakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo kukosa ofisi inayojitosheleza kwa shughuli zote ikiwemo maabara na vitendea kazi kama inavyohitajika.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi inaitaka Serikali katika kukabiliana na matatizo ya wakosaji/ wavunjaji wa sheria ya Mazingira kujificha katika mahakama, kuwepo na Kitengo cha Mahakama kinachohusika na  Mazingira (Environmental Appeal Tribunal) ambacho kitakuwa kinahusika kuwachukulia hatua wale wote ambao kwa makusudi wanakiuka sheria ya mazingira/au wanaokaida amri halali ya Baraza.
Aidha, katika kupambana na ujenzi holela ni muhimu kila ofisi ya  Mipango miji NEMC ihusishwe ili mtaalam wa Mazingira atoe ushauri wake, kwa njia hii matatizo yanayojitokeza sasa kwa kiasi kikubwa tutayapunguza.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
…………………………….
Mch. Israel Y.Natse (Mb)
Msemaji Mkuu Kambi Rasmi ya Upinzani- Ofisi ya Makamu wa Rais,Mazingira.
12.05.2014



[1] Sera ya CHADEMA mabadiliko ya Tabianchi-toleo la kwanza 2013

No comments:

Post a Comment