(Inatolewa chini ya Kanuni
ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
1.0
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Frank Herbert aliwahi kusema
“Utawala bora, kamwe hautegemei Sheria bali
sifa binafsi za wale wanaotawala. Vyombo vya Serikali mara zote vipo chini ya
wale wanaowaongoza. Kwa hiyo sifa muhimu ya Serikali ni namna ya
kuteua/kuchagua viongozi”
Serikali ya awamu ya
nne, imeshindwa kuwajenga viongozi wake katika misingi bora na ndio maana pamoja
na matatizo ya kimfumo, wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kubadilisha
viongozi na matokeo ya ufanisi wake yamekua ni kioja na dhihaka katika
utendaji.
2.0
UTEKELEZAJI
WA MAAZIMIO 16 YA BUNGE
Mheshimiwa Spika, kamati
ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilileta Bungeni taarifa
yake tarehe 20 Disemba 2013 liyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Mhe. James
Lembeli kuhusu uchunguzi wa matatizo katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Ujangili, iliyokua na maazimio kumi na sita (16). Taarifa hiyo ndiyo
iliyomuondoa aliyekua Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na
mawaziri wengine.
Mheshimiwa Spika, mojawapo
ya maazimio ya Bunge, yaliyoongezwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni pamoja kuundwa
kwa Tume ya Uchunguzi wa Kimahakama. Aidha, ni takribani miezi zaidi ya mitano
kupita tangu Serikali iahidi Desemba mwaka jana, kuahidi, kupitia kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuunda tume maalumu ya kuchunguza kilichotokea
wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili. Katika makujukumu yake, Tume hiyo
imepewa kazi zifuatazo;
a)
Kuchunguza na
kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa;
b)
Kuchunguza na
kubaini iwapo sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea zilifuatwa na watu
waliotekeleza operesheni hiyo.
c)
Kuchunguza na kubaini
kama kuna mtu aliyekiuka sheria, taratibu na hadidu za rejea wakati wa
operesheni;
d)
Kuchunguza
na kubaini kama kuna watu ambao walikiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji
wa operesheni hiyo na kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao
zilikuwa stahiki;
e)
Kupendekeza hatua
zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu ambaye itabainika alikiuka sheria,
taratibu na hadidu za rejea pamoja na kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati
wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na kuundwa kwa Tume hii lakini Serikali haikupaswa tena kuipa tume kazi
mpya katika maeneo yote bali yale yaliyohitaji ushahidi
wa ziada wa kijinai, hii ni kwa sababu makosa mengine yako wazi ambayo Serikali
ilipaswa iwe imeshachukua hatua badala ya kusingizia inasubiri taarifa ya tume.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, sasa inaitaka Serikali iwasilishe taarifa ya
utekelezaji wa maazimio ya Bunge wakati wa Majumuisho ya Bajeti ya Wizara ili
maazimio ya Bunge hili yasiishie kabatini kama ilivyokuwa kwa mengine ya miaka
ya nyuma na ilivyozoeleka sasa.
Endelea....
2.1
Uwajibishwaji
Wa Watendaji Kutokana Na Maazimio Ya Bunge
Mheshimiwa Spika,
aidha katika azimio namba Saba (7), Bunge liliazimia pia kumwajibisha
Mkurugenzi wa Wanyamapori Prof. Alexander Songorwa kwa kutoa taarifa zisizo
sahihi kwenye vyombo vya habari na kuudanganya umma kuhusu mazingira na kifo
cha Emiliana Marrow wa Babati.
Mheshimiwa Spika, katika
hali ya kushangaza Waziri wa Maliasili na Utalii wa sasa, Mhe. Lazaro Nyalandu
ambaye akiwa katika nafasi yake ya unaibu waziri, kipindi kifupi tu kabla ya uteuzi wake, kwa
kasi ya ajabu aliandaa mikutano mingi na ziara mbalimbali huku akiandamana na
lundo la vyombo vya habari kama kumbikumbi,na kutoa matamko makali dhidi ya
ujangili na watumishi wasio waaminifu. Akiwa katika ziara hizo, aliwahi
kuikandia sana Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi na Maliasili iliyoongozwa na Mhe.
James Lembeli, huku akidai kuwa ilikuwa ya uwongo mtupu. Lakini baada ya
kubanwa zaidi, alikana kutoa kauli za kuikosoa ripoti hiyo ya kamati. Sababu za
kwanini akanushe maneno aliyoyasema zaidi ya mara nne, inabakia kuwa siri yake
mwenyewe.
Mheshimiwa Spika, Waziri
Nyalandu alitoa taarifa za kuwavua nyadhifa zao Mkurugenzi Mkuu wa Wanyamapori
na Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Matumizi
Endelevu ya Wanyamapori nyadhifa zao. Nyalandu anadai kuwa moja ya sababu za
kuwaondoa, ni kutekeleza maazimio ya Kamati ya Lembeli kutokana na kutowajibika
wakati wa Operesheni Tokomeza. Jambo
la kujiuliza, kama aliwahi kusema kuwa taarifa ya kamati ni uongo mtupu, je ni
lini amethibitisha kuwa kile alichodai kwamba ni uwongo, ulikuwa ukweli? Cha
ajabu, aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya ukurugenzi, Paul Sarakikya aliyekuwa
kiongozi wa utekelezaji wa operesheni tokomeza na aliyehusika moja kwa moja na
kinachodaiwa kuwa uvunjifu wa haki za binadamu, ndiye amepewa nafasi ya kukaimu
ukurugenzi! Wote tunafahamu ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na
ukatili uliofanywa katika operesheni tokomeza kiasi cha kusababisha mawaziri
wanne kuwajibishwa kwa kutenguliwa nafasi zao.
Mheshimiwa Spika,
aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ilitumia vigezo gani
kumteua Sarakikya kukaimu nafasi ya Ukurugenzi wa Wanyamapori huku ikijua
alivyoshindwa kutokomeza ujangili hapa nchini na jinsi aliyoendesha operesheni
tokomeza ujangili iliyokuwa imejaa dhuluma, uporaji, utesaji na udhalilishaji
dhini ya wananchi. Jambo ambalo liliishangaza zaidi Kambi Rasmi ya Upinzani ni
kitendo cha Waziri Nyalandu kumteua Ndugu Sarakikya kukaimu nafasi ya
Mkurugenzi wa Wanyamapori huku akijua kuwa Sarakikya alifanya makosa mengi
katika utendaji wake wa kazi katika
idara hiyo ya Wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe
pia kuwa Ndg. Sarakikya ndiye aliyeongoza kikosi cha kuzuia ujangili hata kabla
ya operesheni tokomeza. Katika kipindi hicho, Tanzania ilishika nafasi ya
kwanza kati ya nchi nane duniani zilizoongoza kwa matukio ya ujangili. Aidha,
ili kuonyesha kwamba Serikali hii haizingatii weledi katika utendaji,
alietuliwa tena kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili.
2.2 Kauli Tata
Za Serikali Juu ya Kufukuzwa Kazi kwa Wakurugenzi
Mheshimiwa Spika, mara
baada ya waziri kutangaza kuwavua nyadhifa zao wakurugenzi hao tarehe 24
Februari 2014, Katibu Mkuu wa wizara hii Bi. Maimuna Tarishi aliwarudisha
kazini wakurugenzi hao huku Serikali nayo kwa kupitia kurugenzi ya habari
maelezo,ikitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa taarifa za kufukuzwa kwa
wakurugenzi hao si sahihi. Pia, Ikulu kwa kupitia Katibu Kiongozi Balozi Ombeni
Sefue, ilitoa tamko la kuitaka Wizara kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za
utumishi wa umma za kumfukuza mtumishi kazi.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002, Kifungu cha IV (23) (2)
inayozungumzia mamlaka ya Rais kumwondoa mtumishi aliyemteua kazini, amri ya
kumfukuza mtumishi wa umma itatekelezwa iwapo;
(a)hati
ya mashtaka imeandikwa dhidi yake (b)mtumishi wa umma amepewa nafasi ya kujibu
mashtaka hayo
(c)Maombi
yametolewa kwenye hati ya mashtaka kwa mujibu wa taratibu zilizo chini ya
kifungu namba 34.
Swali
la kumuuliza Waziri Nyalandu, je, hatua hizi zilifuatwa katika kuwasimamisha
kazi wakurugenzi hawa? Na je, maamuzi yake ya kumfukuza Prof. Songoro katika
vikao vya kamati na kumdhalilisha hata baada ya Ikulu kutoa maagizo ya Wizara
kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za kufukuza watumishi kazi ni utawala bora?
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali na Wizara kuhakikisha kuwa, uamuzi
wowote uliofanywa na kuendelea kufanywa katika kutekeleza maazimio ya Bunge
katika kuwawajibisha watumishi hao uzingatie sheria, taratibu na kanuni kwa
kuwa Sheria na Kanuni hizo zinaeleza wazi hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Vilevile, tunasikitishwa na mvutano baina ya waziri na katibu mkuu wa wizara,
hali ambayo inaonesha kuwa kuna mgongano aidha wa kimaslahi na hivyo
kuthibitisha kuwa Serikali ni dhaifu kwa kuwa, Waziri na Katibu Mkuu wa wizara
moja wanafanya kazi bila kushirikiana na kila mmoja akionekana kumvizia
mwenzake hadharani badala ya kukaa kwa pamoja kutekeleza maazimio ya Bunge lako
tukufu.
Aidha,
mvutano huu pia ni ishara kuwa, maazimio ya Bunge yanaendelea kupuuzwa na
Serikali kwa kigezo cha kuzingatia sheria na kanuni huku zikiwaacha watumishi
wenye tuhuma wakihamishwa vitengo na idara na kuendelezea urasimu uleule hata
uko wanapohamishwa.
Mheshimiwa Spika,
ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote hamfichi mnafiki na debe tupu
haliachi kutika (si maneno yangu, bali ya wahenga). Si mara ya kwanza, kwa
Kambi Rasmi ya Upinzani kuhoji juu ya usafi wa Lazaro Nyalandu, Waziri wa
Maliasili na Utalii, na mara kadhaa tumeonesha kwa kiasi kikubwa udhaifu wake na
kutoa vielelezo mbalimbali vinavyotilia
shaka utendaji wake kabla na hata baada ya kukabidhiwa wizara hii nyeti!
3.0 TASWIRA YA TAIFA
KATIKA JUMUIA ZA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika,
kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani imeendelea kutoa taarifa kwa Serikali
juu ya mtandao wa kimataifa wa ujangili ambao pia unahusisha viongozi
waandamizi wa Serikali, maafisa usalama wa taifa, wanajeshi wafanyabiashara
wakubwa, polisi, wanasiasa, Ikulu na watumishi wa umma. Serikali ya CCM imekua
ikitoa kauli za kubeza pamoja na majibu mepesi ya tuhuma hizi huku tatizo la
ujangili likiendelea kulichafua taifa katika jumuia ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, katika
hali ya kushangaza baada ya gazeti la Mail on Sunday la nchini Uingereza kutoa
taarifa kuwa biashara ya ujangili inahusisha watu wa karibu na Rais wakiwemo wanasiasa, maafisa wa Serikali na wafanya
biashara wakubwa, Serikali ilitoa matamko mbalimbali pamoja na kulaani taarifa
ya gazeti hilo na hatimaye Waziri Nyalandu, alimwalika mwandishi wa gazeti hilo
kujionea mwenyewe shughuli za Serikali za kupambana na ujangili ikiwemo kutembembelea
ghala ya kuhifadhia pembe za ndovu zilizokamatwa. Mwaliko huo ilikua ni katika
kuthibitisha kuwa Serikali ya CCM haina la kuficha.
Lakini
katika hali ya kushangaza, uchunguzi na taarifa zaidi umeonesha kuwa ndani ya
miaka minane (8) Serikali ya CCM, imekua ikiomba kibali bila mafanikio kutoka
CITES (Convention on International Trade on Endangered Species) cha kuuza
shehena ya pembe za ndovu takribani 34,000 zenye uzito wa tani 125 zenye
thamani ya dola za kimarekani milioni 150 sawa na shilingi Bilioni 244.5 za
kitanzania (kwa wastani wa sh.1630 kwa dola 1).
Mheshimiwa Spika,
jumuia ya kimataifa imeshangazwa na kitendo cha Tanzania kuomba kibali cha
kuuza shehena iliyokamatwa ya pembe za ndovu kwa kuwa ni biashara haramu na kitendo
cha Serikali kuomba kuyauza ni sawa na kuchochea ujangili zaidi kwa kuwa hali
hii itaongeza uhitaji wa pembe za ndovu kwenye soko haramu nchini China. Jambo hili ni aibu kubwa kwa taifa kuomba
kufanya biashara haramu kwa kuwa imelidhalilisha taifa. Hii ni sawa na Serikali
ikamate madawa ya kulevya, halafu iamue kuyauza ili kupata fedha.
Mheshimiwa Spika, kitendo
cha waziri wa maliasili na utalii kumwalika nchini mwandishi aliyesemwa kuwa
ametoa taarifa za uongo na kulichafua taifa, ili ajithibitishie kuwa Tanzania
ni safi katika matukio ya ujangili, Bwana Martin Fletcher, na kumtembeza katika
sehemu mbalimbali nchini ikiwa na nia ya kumfunga mdomo(damage control),
haikusaidia bali ilivumbua uchafu mwingi na huu wote umewekwa wazi katika
vyombo vya habari vya kimataifa na kuendelea kuonesha uozo wa Serikali katika
kushughulikia tatizo la ujangili nchini.
Mheshimiwa Spika,
imeelezwa kuwa Raisi ameshindwa kusimamia suala hili vizuri kwa kuwa
wanaohusika na ujangili ni watu wake wa karibu ama rafiki zake. Aidha, taarifa
hizo zimeendelea kubana kauli za Waziri Nyalandu za kuwa anawafahamu majangili
kwa majina na kuwataka majangili hao kuacha ujangili ama watawachukulia hatua
za kisheria. Maswali yanayoulizwa, je, ni kwa nini waziri hawataji watu
wanahousika na ujangili? Pili, inakuaje waziri anawajua kwa majina na hata
sehemu wanazokaa, lakini anashindwa kuwachukulia hatua? Inakuaje waziri,
awabembeleze watuhumiwa wakati kuna sheria, kanuni na taratibu za kuwachukulia
hatua wahalifu? Ni nini kipo nyuma ya pazia katika kuwalinda na kuwaficha
watuhumiwa wa ujangili?
3.1 Kukosekana
kwa maafisa utalii katika balozi mbalimbali.
Mheshimiwa
Spika, kuna taarifa kuwa katika
balozi zetu mbalimbali na muhimu
ulimwenguni kumekuwa hakuna maafisa utalii ambao watakuwa na jukumu la
kuhakikisha kuwa wanaweza kuhakikisha kuwa tunapata watalii wa kutosha kwa
ajili ya kuinua pato la taifa letu.
Mheshimiwa
Spika, katika ubalozi wa Tanzania
–Berlin ni kati ya balozi kubwa ulimwenguni ambao hauna afisa utalii pamoja na
ukweli kuwa ubalozi huu unahudumia nchi nyingine za
Poland,Austria,Hungary,Frankfut,Uswis,Romania,Bulgaria ,Slovakia na Jamhuri ya
Czech , kwa kipindi kirefu sana ubalozi huu umeomba kupatiwa afisa utalii
kutoka wizara ya mambo ya nje lakini mpaka leo hawajaweza kupelekewa maafisa
hao kwa ajili ya kutekeleza kwa vitendo diplomasia ya uchumi ambayo ndio msingi
wetu wa diplomasia ya kimataifa .
Kambi ya
Upinzani, inataka kupata majibu ni
lini serikali itawapeleka wataalamu hao katika ubalozi huu kwa ajili ya
kuimarisha sekta ya utalii kwenye nchi zote muhimu ambazo zimekuwa mstari wa
mbele katika sekta ya utalii katika taifa letu. [1]
4.0
BIASHARA
HARAMU YA NYARA ZITOKANAZO NA WANYAMAPORI NA KUKITHIRI KWA TATIZO LA UJANGILI
NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Kumekuwa
na ongezeko kubwa na watu wanaojishughulisha na uwindaji na biashara ya nyara
za Serikali bila bila kuwa na kibali au leseni toka mamlaka zilizowekwa
kisheria. Kwa mujibu wa sheria ya
wanyapori kifungu cha 80(1) sehemu ya 10 “mtu yeyote haruhusiwi kujihusisha na
biashara ya nyara (trophies) bila kuwa na leseni ya biashara ya nyara (trophy
dealer license). Na kifungu cha 80(2) kinampa Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori mamlaka ya kutoa leseni ya
biashara ya nyara kwa mtu yeyote ambaye
ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupokea maombi kwenye fomu
maalum na kutimiza masharti yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kulipa ada
zilizopangwa.
Mheshimiwa
Spika, leseni ya biashara ya nyara
inayotolewa katika Kifungu hiki haimruhusu mhusika kuwinda, kuua au kupiga
picha mnyama yoyote, badala yake inamruhusu kukamata, kutengeneza bidhaa
inayotokana na nyara, kununua au kuuza nyara – 80(3)”[2].
Mheshimiwa Spika, licha
ya kuwepo kwa sheria hiyo, bado wanyama wetu wanaendelea kuuwawa kwa kasi ya
ajabu. Aidha, kumekuwepo kwa taarifa zinazoonyesha kuwepo kwa mtandao mpana wa
wahusika wa biashara ya wanyama pori na bidhaa za wanyamapori kutoka katika
nchi kadhaa kama vile, Kenya, Msumbiji, DRC, Namibia na Afrika ya Kusini.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu aliyoyatoa
mbele ya Waandishi wa Habari wakati
akiwa Naibu Waziri wa Wizara hii katika
Hoteli ya Mount Meru – Arusha mwaka jana, ni kwamba; kwa kipindi cha miaka
mitatu, iliyopita tembo 31348 sawa na
asilimia 42 walitoweka katika hifadhi ya Selous na Mikumi na kwamba kuna mtandao wa kijangili wa kimataifa (Sophisticated International
Syndicate) unaofanya kazi hapa nchini.
Aidha alitoa agizo kwa bodi ya wadhamini ya mamlaka ya hifadhi za taifa
(TANAPA) itoe maelezo ya kina kuhusu kuwepo watumishi wa ndani ya mamlaka ya
hifadhi wanaosadikiwa kushirikiana na majangili hao kuendesha ujangili ambao
unahatarisha hifadhi zetu na sifa ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Waziri Nyalandu aliirudia kauli hiyo mkoani Iringa, mwezi Juni, 2013 wakati wa kikao cha siku mbili cha wadau wa
ulinzi wa maliasili juu ya ujangili wa tembo katika mikoa ya Nyanda za juu
na kuahidi kwamba majina ya majangili yakiwemo ya vigogo wanaojihusisha na ujangili
wa tembo yatatangazwa hadharani, lakini mpaka sasa hakuna majina yoyote
yaliyotangazwa hadharani.
Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanywa na Tanzania
Wildlife Research Institute-TAWIRI katika mbuga ya hifadhi ya Selou na Mikumi
inaonyesha kuwa idadi ya Tembo imeshuka kutoka 74,900 mwaka 2006 hadi kufikia
43,552 mwaka 2009. Hii ikiwa na maana kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu
takribani asilimia 42 ambayo ni Tembo 31,348 katika hifadhi mbili tu waliuawa
na majangili[3].
Hii ni hatari kubwa sana na kwa kutilia maanani kuwa Tembo mmoja anapatikana
baada ya miaka miwili (yaani Tembo hubeba mimba kwa kipindi cha miaka miwili
ndipo azae)
Mheshimiwa Spika, biashara
haramu ya nyara zitokanzao na wanyamapori hususan tembo imechangia sana
ujangili wa kutisha wa tembo kiasi kwamba idadi ya tembo imepungua mno kiasi
cha kuwafanya tembo wawe miongoni mwa jamii ya viiumbe waliopo hatarini
kutoweka kabisa (endangered species). Nasema hivi kwa sababu idadi ya
tembo kwa uchache, waliokuwepo katika nchi za Kiafrika kwa miaka
ya sabini walikuwa ni takribani milioni moja
na laki mbili (1,200,000) lakini kwa sasa wamebakia
wasiozidi laki tano[4]
Mheshimiwa Spika, hali ya ujangili nchini imefika
pabaya na ina kiasharia kibaya kwa miaka michache ijayo. Takwimu zinaonesha
kuwa mwaka 2010, jumla ya tembo 10,000 waliuwawa Tanzania, ikiwa ni sawa na
wastani wa tembo 27 kwa siku. Mwaka 2012 pekee, tembo takribani 23,000
wameuwawa kwa mwaka ambayo ni sawa na tembo 63 kwa siku. Hii ni sawa na
ongezeko la 57% kwa kipindi cha miaka 2. Kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na
tembo kati ya 150,000 na 170,000.
Kutokana na takwimu hizi, ikiwa Tembo 63 wanauwawa kwa siku, ni dhahiri
kwamba kwa kipindi cha miaka 7
ijayo Tembo hawa watakuwa wameuawa wote.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa
Mataifa la kupamba na madawa ya kulevya na uhalifu (United Nation’s Office on
Drugs and Crime- UNODC-), inaonyesha kuwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la
Sahara na nchi za Kusini Mashariki mwa
Asia ni wasambazaji wakubwa wa bidhaa
haramu za wanyamapori kwenye soko la China, Marekani na baadhi ya nchi katika
bara la Ulaya. Bidhaa hizo za
wanyamapori ni pamoja na pembe za ndovu, pembe za faru, ngozi za chui na simba
na viungo mbalimbali vya wanyamapori. Kwa mujibu wa utafiti huo ni kwamba
mununuzi hulipa kiasi cha dolla za kimarekani 2,500 kwa kila pembe moja ya
faru.
Mheshimiwa Spika, tatizo la Ujangili limekuwa gumu
kumalizwa kabisa kwa kuna taarifa zinazohusisha askari wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi katika matukio ya
ujangili na biashara haramu ya nyara na taarifa hizo zimeripotiwa sana na
vyombo vya habari, lakini cha kusikitisha ni kwamba hakuna hatua
zilizochukuliwa dhidi ya askari wa majeshi hayo (yaani jeshi la polisi na jeshi
la wananchi wa Tanzania). Mpaka sasa Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania hawajakanusha taarifa hizo jambo linaloashiria kwamba pengine taarifa
hizo ni za kweli.
Mheshimiwa Spika, taarifa
za baadhi ya askari walioripotiwa na vyombo vya habari kuhusika na ujangili ni
kama ifuatavyo:
1. Mnamo
Tarehe 7 January 2013, Gazeti la habari leo lilitoa taarifa za askari wawili
kujihusisha na biashara ya meno ya tembo na kuhusishwa na mauaji ya faru katika
mbuga ya Serengeti na mpaka sasa hakuna taarifa rasmi kutoka Serikalini juu ya
hatua zilizochukuliwa dhidi ya askari hao.
2.
Mnamo Januari
20, 2013 Sajenti wa Jeshi la Wananchi Tanzania, Azizi Athuman Yusufu alikamatwa
mkoani Arusha akiwa na pembe mbili za ndovu na bunduki aina ya Riffle yenye
namba 458 huku akitumia gari ya mkufunzi wa kijeshi kutoka Zimbabwe
anayefundisha nchini.
3.
Tarehe 23 Julai, mwaka
2013, walikamatwa watu saba wanaodhaniwa kuwa ni majangili , wakiwamo askari
watatu wa Magereza Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara wakiwa na gari la Magereza aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili
STK 4394 lililokuwa limepakia nyara za
Serikali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 55. Nyara hizo zilikuwa ni
pamoja na Twiga wawili, Pundamilia wawili, Swala, Palapala majike wawili na
Mbuni wawili.
Mheshimiwa Spika, Biashara haramu ya
pembe za ndovu imevuka mipaka ya nchi na imeanza kushamiri katika ukanda wa
Afrika ya Mashariki jambo ambalo linatishia kutoweka kabisa kwa wanyama hao
ambao ni kivutio kikubwa cha utalii. Taarifa katika mtandao wa habari wa
“Annamiticus” (www.annamiticus.com)
zinasema kwamba mwaka 2012, makontena mawili kutoka Kenya na Tanzania
yalikamatwa huko HongKong yakiwa yamebeba tani 4 (Kilo 4,000) za pembe za
ndovu.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa
hiyo, kontena lililotoka Tanzania lilikuwa limeandikwa “plastic scrap”
ikimaanisha kuwa lilikuwa na vifaa ya plastiki lakini baada ya kufunguliwa
kulikuwa na vipande 972 vya pembe halisi za ndovu zenye uzito wa kilogramu
1,927 pamoja na kilo moja na nusu ya unga wa pembe za ndovu zilizosagwa.
Kontena lililotoka Kenya lilikuwa limeandikwa “roscoco beans” yaani maharage
aina ya roscoco, lakini lilipofunguliwa kulikuwa na vipande 237 vya pembe za
ndovu sawa na kilogramu 1,884.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa
hiyo, wingi wa pembe hizi za ndovu zilizokamatwa, unadhihirisha kwamba tembo takriban
600 kwa uchache waliuwawa.
Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili,2013
kontena lingine lilikamatwa likiwa limesheheni pembe za ndovu 113 huko
China zenye thamani ya Dola za Kimarekani 400,000.Kontena hili liliandikwa kwamba
limebeba vipuri (spareparts) toka Burundi. Kwa kuwa Burundi haina bandari, kuna
uwezekano mkubwa kwamba kontena hilo lilipitia bandari ya Tanzania, na hivyo
kuna uwezekano pia kwamba pembe hizo zinatokana na tembo waliouwawa Tanzania.
5.0
MAENDELEO
YA SEKTA YA WA WANYAMAPORI NCHINI
Mheshimiwa Spika, mchango
wa sekta ya wanyamapori katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu ni mkubwa sana.
Takwimu[5]
zinaonyesha kuwa uwindaji wa kitalii kwa miaka mitatu kati ya 2009 na 2012
uliingiza shilingi bilioni 91. Kwa sababu hiyo, Wizara ya Maliasili na Utalii
kupitia idara yake ya Wanyamapori inatakiwa kuilinda na kuiendeleza sekta hii
ili iendelee kuchangia zaidi katika uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika, katika
muktadha wa kuilinda na kuiendeleza sekta ya wanyamapori, Bunge lilitunga
Sheria ya Uhifadhi ya 2009, ambayo inatumika pamoja na
sera ya wanyamapori ya mwaka 2007 ili kuratibu na kudhibiti shughuli za
uwindaji wa wanyamapori kwa namna ambayo sekta ya wanyampaori inakuwa endelevu.
Mheshimiwa Spika, ulinzi
wa Sekta ya wanyamapori ni muhumu kwa kuwa sekta inachangia ukuaji wa uchumi
katika Nyanja mbalimbali. Kwa mfano wanyamapori ni kivutio kikubwa cha watalii
ambao hutoa fedha nyingi za kigeni wajapo kutalii hapa nchini kwa ajili ya
kutazama na kuwapiga picha wanyama hao. Aidha sekta ya wanyama pori inachangia
maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutoa ajira kwa wananchi na pia kukuza
soko la bidhaa za ndani.
Mheshimiwa Spika, licha
ya umuhimu wa sekta hii, Serikali imekuwa haifuatilii makampuni ya uwindaji
yenye leseni kuona kama wanafuata sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya 2009.
Matokeo ya udhaifu wa Serikali katika ufuatiliaji, kumekuwa na uvunjaji mkubwa
wa sheria jambo ambalo limesababisha uwindaji ufanyike kiholela. Kwa mfano,
Kampuni ya Uwindaji ya Green Miles Safaris Limited imekuwa ikiwakimbiza na
kuwakamata watoto wa wanyamapori pindi wanapozaliwa kinyume na kifungu cha
19(1) cha Sheria ya Wanyamapori ya 2009. Aidha Sheria hiyo inapendekeza adhabu
ya kifungo cha miaka mitano gerezani na au faini kati ya shilingi 500,000/=
hadi shilingi 2,000,000/=
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inataarifa kwamba Kampuni hii ya Green Miles Safaris Limited
ilishapewa zuio na Mahakama la kufanya uwindaji kutokana na uwindaji
usiozingatia sheria lakini Kampuni hiyo ilipita mlango wa nyuma na kuomba
kilbali cha uwindaji kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori na Mkurugenzi akatoa kibali na hivyo wote wawili wakapuuza
uamuzi wa Mahakama.
Mheshimiwa Spika, Kampuni
hii ya Green Miles Safaris Limited, pamoja na uhalifu mwingi inaoufanya katika
mbuga zetu wakati wa uwindaji, imekuwa ikilindwa na Serikali ndio maana Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni Upinzani Bungeni inashawishika kuamini kwamba
Serikali ndio chimbuko la tatizo la Ujangili na uwindaji haramu wa wanyamapori
hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo mbele ya bunge hili ni kwa
nini haijaichukulia Kampuni ya Uwindaji Green Miles kwa kufanya uwindaji haramu
hapa nchini?
Mheshimiwa Spika, Tatizo
kubwa la Maendeleo ya Sekta ya Wanyapori ni kwamba Serikali huwa haifuati hata
mapendekezo yanayotolewa na Kamati za zinazoudwa na Serikali yenyewe. Kwa
mfano, mwaka 2006, aliyekuwa Waziri
wa Maliasili na Utalii kwa wakati huo Mheshimiwa Anthony Mwandu Diallo (Mb),
aliunda Kamati ya Wataalam ambayo aliitaka ifanye uchambuzi wa kina wa shughuli
za uwindaji wa kitalii nchini. Uchambuzi huo ulitakiwa uzingatie utendaji kazi
katika shughuli za uwindaji wa kitalii, mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa na
matatizo yanayoikabili tasnia hiyo. Hatimaye, Kamati ilitakiwa kumshauri
Mheshimiwa Waziri namna ya kuleta mabadiliko ndani ya sekta hiyo kwa minajili
ya kulinda uhifadhi, kuwawezesha wananchi kushiriki katika uwindaji wa kitalii
kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika
kuondoa umaskini na kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, Hadidu
za rejea kamati hiyo ilizopewa ziliitaka Kamati:[6]
(i)
Ipitie utaratibu wa sasa wa uombaji na
ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii pamoja na chombo chake cha ugawaji
kuona kama havibagui wala havisababishi malalamiko kwa wadau mbalimbali;
(ii)
Ichambue kwa makini vigezo na masharti
yaliyopo yanayohusu ukaguzi wa uwezo wa Kampuni za Uwindaji zinazowasilisha
maombi kwa ajili ya Uwindaji wa Kitalii ili kuona kama yanafaa kwa mazingira ya
sasa;
(iii)
Ichambue Mikataba mbalimbali ya kampuni
za uwindaji; ya zamani na inayoendelea kwa lengo la kujiridhisha kama inafaa au
ina upungufu unaohitaji marekebisho ili kulinda uhifadhi na maslahi ya umma.
(iv)
Iangalie Kanuni za Uwindaji wa Kitalii
na zile za Utalii wa picha pamoja na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 1974 na
kushauri namna ya kuondoa migongano ambayo imejitokeza baada ya kuruhusu utalii
wa picha kwenye maeneo ya uwindaji wa kitalii.
(v)
Ichambue Sera na Sheria zinazohusiana na
Wanyamapori na Utalii, na Kanuni za Uwindaji wa Kitalii ili kuona kama Wananchi
wanafaidika na uwindaji huo wa kitalii.
(vi)
Ichambue utaratibu wa ukusanyaji mapato,
kubaini njia ambazo zitaongeza maduhuli ya Serikali, na kutathmini utaratibu wa
ugawaji vitalu kwa njia ya zabuni.
(vii)
Mwisho, Kamati iangalie uwezekano wa
Serikali kuwawezesha Wananchi kushiriki kikamilifu katika tasnia hii ya
uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo
ya Kamati hiyo yalikuwa ni kama ifuatavyo:
1. Kuboresha
utaratibu wa ugawaji wa vitalu kwa kuipa Kamati ya Ugawaji Vitalu nguvu za
kisheria na kwa kupanua uwakilishi wake.
2. Kuunda
Wakala wa Serikali wa kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii badala ya Idara
ya Wanyamapori.
3. Kuangalia
upya umiliki wa vitalu ili kuwawezesha wananchi kushiriki zaidi katika uwindaji
wa kitalii kwa njia ya ubia na baadaye kumilikishwa vitalu wakati wageni na
wananchi watafanya kazi ya kuwindisha.
4. Serikali
iwawezeshe Wawindaji Bingwa wa Kitanzania ili waweze kumiliki vitalu na kutumia
ujuzi na uzoefu walionao. Serikali inaweza kuwawezesha wananchi kwa kuzungumza
na mabenki ili wapunguze riba ya kukopa fedha benki na kuruhusu matumizi ya
vitalu kama dhamana. Pia wawindaji bingwa waanzishe bodi yao ya kitaalam.
5. Kuthamini
vitalu vya uwindaji wa kitalii na kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato
ili kuongeza mapato ya Serikali.
6. Kuweka
ukomo wa umiliki wa kitalu wa vipindi viwili vya miaka mitano ili ili kuruhusu
waombaji wapya.
7. Kuboresha
taarifa za sekta ya Wanyamapori kwa kuweka taarifa zote muhimu zinazohusu
shughuli za uwindaji wa kitalii kwenye Tovuti ya Idara.
8. Idara
iimarishe ufuatiliaji na tathmini ya vitalu kwa kuanzisha chombo huru cha
kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali kulieleza Bunge hili ni kwa
kiwango gani mapendekezo ya Kamati hiyo yametekelezwa na ni mangapi ambayo bado kutekelezwa na ni
kwanini?
6.0
UTALII NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA
Mheshimiwa
Spika,
Kwa eneo kubwa la
ardhi lililofunikwa na wingi wa misitu pamoja na aina mbalimbali za maua na
viumbe, Tanzania ni mojawapo ya vivutio
vikubwa vya utalii barani Afrika. Nchi yetu ina raslimali nyingi asilia ikiwemo
pamoja na maeneo mengi ya nyika za mapori yenye aina nyingi za banoai.
Mheshimiwa
Spika, Miongoni
mwa vivutio vya utalii ni pamoja na Mbuga za wanyama , hifadhi za taifa,
hifadhi zilizozuiliwa na maeneo ya
kihistoria. Hata hivyo kwa sababu ya ongezeko la joto, baadhi ya hivi vivutio
ikiwemo theluji katika kilele cha mlima Kilimanjaro iko katika hatari ya
kupotea. Na baadhi ya wanyama katika mbunga zenye ukame mkubwa wameanza
kupungua na kuathirika.
Mheshimiwa
Spika, Licha ya
kuwa na neema ya kuwa na vivutio vingi vya utalii, bado sekta ya utalii
inakabiliwa na chamgamoto kadhaa, zikiwa ni;
(i)
Uendelezaji
wa kazi zitakazohakikisha kuendelea kuwepo kwa vivutio mbalimbali vya utalii
kwa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi;
(ii)
Ukarabati
wa miundombinu kama vile barabara, madaraja, kambi za watalii na upatikanaji wa
umeme kwa ajili ya watalii wa mbugani;
(iii) Uwezo mdogo wa idara zinazohusika
kusimamia, kulinda vivutio vya utalii, kama vile kuendesha na kutangaza vivutio
vya utalii vilivyopo.
Mheshimiwa
Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani, inaamini kabisa tatizo la umeme katika vivutio vya utalii
vilivyopo mbugani, suluhisho ni kutumia umeme wa jua (solar energy), hili ni
rahisi katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa
Spika, kama
ambavyo nitaonyesha hapo baadae makusanyo yanayopatikana kutoka sekta ya utalii
hayana uwiano wa moja kwa moja na uwekezaji katika sekta hiii. Ndiyo sababu
kubwa ya mapato ya sekta kutokuakisi vivutio tulivyonavyo hapa nchini.
Mheshimiwa
Spika, uwekezaji
katika Sekta ya Utalii ni suala lenye tija kubwa katika uchumi wetu kwa kuwa
sekta hiyo imekuwa ikichangia katika uchumi wa Taifa licha ya uwekezaji mdogo
uliofanyika katika sekta hiyo.
Mheshimiwa
Spika, takwimu
zilizopo zinaonyesha kuwa katika maeneo
yote ya hifadhi zetu kwa sasa kuna kuna hoteli zenye uwezo wa kutoa huduma za
malazi (carrying capacity) kwa watu 6,681
ambapo kwa miaka mitano ijayo idadi hii itafikia uwezo wa kulaza watu 8,421.
Hiki ni kwango kidogo sana cha huduma za malazi kiasi kwamba tunapoteza fursa
ya kunufaika katika sekta ya utalii.
Mheshimiwa
Spika, japokuwa
uwekezaji katika sekta ya utalii ni mdogo lakini sekta imeendelea kuwa nguzo
muhimu katika uchumi wetu. Kwa mwaka 2011 utalii na usafiri wa kitalii
ulichangia asilimia 13 kwenye pato la taifa na kuchangia takriban asilimia 25
ya fedha za kigeni. Aidha, Mpango unaeleza kuwa lengo ni kuongeza wageni kwa asilimia
40 kutoka wageni 671,886 kwa sasa hadi 940,640
ifikap June 2016. Aidha Mpango unalenga pia kuzidisha siku za mtalii kutembelea
maeneo yenye vivutio vya kitalii nchini kutoka siku wastani wa siku 11 za sasa hadi
wastani wa siku 18[7].
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kutoa tathmini ya mpango huo ili wananchi wajue tumefanikiwa
kwa kiwango gani katiaka kuboresha sekta ya wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, miundombinu
ya usafiri na usafirishaji ya ndani ya nchi, uwekezaji katika ujenzi wa hotel
kwenye maeneo muhimu ya utalii kama vile kwenye hifadhi, mikoa inayozunguka
mlima Kilimanjaro kutasaidia sana kuvutia watalii. Hivyo Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kuboresha miundo mbinu ya usafiri hasa wa anga ili
na kujenga hoteli za viwango vya Kimataifa katika maeneo yenye vivutio vya
watalii ili kuvutia mashirika ya mengi ya ndege toka nje kuja hapa.
Ni
rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Serikali kwamba ifufue shirika letu la Ndege
la Taifa ili tuweze kumudu ushindani katika usafiri wa anga na hapohapo
kuongeza idadi ya watalii katika nchi yetu. Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro na
ule wa Julius Nyerere Dar es Salaam vikiboreshwa vinaweza kuwa ni kitovu cha
mashirika mengi ya kimataifa kubadilishia wasafiri kama kuna mkakati makini.
Mheshimiwa Spika, watalii toka nje wanapenda sana kupanda ndege za
nchi wanazotembelea zaidi kuliko kupanda ndege za kuunganisha. Kwa njia moja au
nyingine usafiri huo unawapunguzia gharama. Mfano mzuri ni miaka ya themanini
wakati Air-Tanzania ilipokuwa inafanya safari zake nchi za Ulaya, watalii wengi
walikuwa wanakuja kwa ndege zetu. Hoja ni kwamba Serikali ina mkakati gani wa
kufufua Shirika la Ndege la Taifa (ATC) Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza
Serikali kuingia ubia na makampuni binafsi kupitia mpango wa Private Public Pertnership
– ( PPP) ili kuboresha huduma za usafiri wa anga hapa nchini ambao unachoche
watalii wengi kuja kwa kuwa kuna usafiri wa moja kwa moja.
7.0
SEKTA
YA MISITU
Mheshimiwa Spika, misitu
ina nafasi muhimu ya kumeza hewa ukaa duniani wakati ikizuia uharibifu wa udongo/ardhi.
Ukataji miti na uondoaji misitu uliokithiri unachangia katika ongezeko la
uzalishaji wa hewa ukaa Tanzania. Kupitia misitu mingi tuliyonayo Tanzania
imeendelea kutoa huduma ya kumeza hewa ukaa duniani, bila ya kuwepo utaratibu
wowote wa kimataifa kutoa fidia yoyote.
Mheshimiwa Spika, mbali
ya kuwa na misitu mingi, kumekuwepo na changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya
misitu, nazo ni:
a) Kufanya
uendelezaji wa misitu kama raslimali ya kumeza hewa ukaa na kuinufaisha jamii
inayoizunguka;
b) Kuthibiti
ubora na uendelevu wa misitu
c) Jamii
inayoizunguka misitu kunufaika na biashara ya hewa ukaa duniani;
d) Ujenzi
wa uwezo wa kufanya tafiti za uendelezaji misitu nchini;
e) Uendelezaji
wa njia bora zinazowezesha jamii inayozunguka misitu kunufaika na raslimali
hiyo.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na changamoto hizo, zinazoikabili sekta hii ya misitu, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka kuhakikisha kwa kadri misitu ya Tanzania inavyoendelea kutoa huduma ya
kimataifa ya kumeza hewa ukaa duniani, hivyo ni lazima nchi na wananchi wetu
tunufaike kwa kupata kazi na teknolojia zinazochangia maendeleo endelevu.
Mheshimiwa Spika, sambamba
na hilo ni kwamba, ni muhimu Serikali kuhakikisha unajengwa uelewa kwa jamii na
wadau wa misitu juu ya uwepo wa fursa za kutumia uwezo wa misitu kumeza kumeza
hewa ukaa kama chanzo cha kunufaika na biashara ya hewa ukaa duniani.
Kuhamasisha ongezeko la matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati ya kupikia na
kuchemshia na kupunguza msongo kwenye misitu yetu kwa hitaji hilo.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inasema kuwa katika kuhamasisha hilo, ni muhimu kuwepo kwa
misitu mfano na miradi mfano katika ngazi za wilaya na vijiji ili wananchi
waone jinsi misitu inavyoweza kuwanufaisha wananchi wanaozunguka misitu mfano
hiyo. Hili linawezekana kama mipango na umakini katika utekelezaji wake
utakuwepo.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji
katika kilimo cha miti ni mojawapo ya kilimo ambacho kwa muda mrefu kinaweza
kuleta tija kubwa kwa wananchi hasa hapa nchini, uwekezaji huu unakabiliwa na
chamgamoto kubwa ya kukosekana kwa mikopo ya muda mrefu na ambayo inaweza
kuwa-accommodate wakulima ambao hawana dhamana ya kuweka zaidi ya umiliki wa
kimira wa ardhi husika, jjambo ambalo halikubaliwi na taasisi za fedha.
Mheshimiwa Spika, utaratibu
huu wa kilimo cha miti ni maarufu sana katika mikoa ya Iringa na Njombe, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni utaratibu gani hadi sasa
ambao wakulima wadogo hasa wa miti wanasaidiwa kupata mikopo ya muda mrefu
katika kukabiliana na tatizo hili la uwepo wa hewa ukaa na kuongeza kipato.
8.0
MAPITIO
YA BAJETI KWA IDARA NA VITENGO VYA WIZARA
Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2013/14 wizara ilitarajia kukusanya maduhuli ya jumla ya
shilingi bilioni 148.97 kutoka katika Idara na taasisi zilizo chini yake. Mwaka
huu wa fedha wizara inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 144.6,
ambayo ni pungufu ya shilingi bilioni 4.37 kwa kulinganisha na makadirio ya
mwaka 2013/14.
Mheshimiwa Spika, randama
inaonyesha kuwa Idara ya wanyamapori kwa kipindi cha mwaka 2013/14 ili kadiriwa
kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.65, Lakini hadi mwezi Machi,
2014 ilikuwa imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 8.92 ambayo ni sawa na
asilimia 31.13 ya malengo. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2014/15 Idara ya
Wanyamapori imepanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 15.55 kutoka kwenye
vyanzo vyake vilivyo chini ya idara. Makadirio haya ni pungufu ya shilingi
bilioni 13.1 kwa kulinganisha na mwaka 2013/14.
Mheshimiwa Spika, kwa
takwimu hizo ni kwamba Sekta ya
Maliasili na Utalii inashuka kimapato. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kueleza sababu zilizofanya mapato yatokanayo na makusanya ya maduhuli
kwa shuka kwa kiasi kikubwa namna hiyo. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Takwimu
zilizotolewa na taarifa ya uchunguzi maalum ni kwamba kwa kipindi cha kuanzia
mwaka 2009 hadi 2012 Idara ilikusanya shilingi bilioni 91 na hali halisi ni
kwamba uwezekano kukusanya zaidi ni mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu
matumizi ya kawaida, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 19.163 kwa
ajili ya matumizi ya Idara hiyo, ambayo ni sawa na asilimia 22.7 ya makusanyo
yake. Lakini hadi mwezi machi 2014, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni
9.161 tu. Swali hapa ni kwamba idara itawezaje kujiendesha ikiwa fedha
iliyotolewa ni kidogo namna hiyo? Ikumbukwe kwamba Idara hii inasimamia
taasisi/vyuo na wakala zipatazo sita ambazo ni TANAPA, NCAA, TAWIRI,CAWM-Mweka,
PWTI na CBCTC ambazo zinahitaji fedha za kutosha kuziendesha.
Mheshimiwa Spika, fedha
za maendeleo zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo kwenye sekta ya wanyamapori,
ni kwa miradi miwili tu ambayo ni mradi wa KILORWEMP unaotekelezwa kwa ushirika
kati ya Tanzania na Serikali ya Ubelgiji. Mwaka 2013/14 zilitengwa jumla ya
shilingi bilioni 1.82, lakini hadi Machi 2014 shilingi milioni 310 ambazo zilitoka
Serikali ya Ubelgiji.
Mheshimiwa Spika, mradi
wa pili ni ule wa Kulinda ushoroba wa Selous-Niassa, ambao unatekelezwa kwenye
wilaya za Namtumbo na Tunduru kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani. Kwa
mwaka jana hakuna fedha zilizotolewa.
Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2013/14 Idara ya Utalii ilikadiriwa kukusanya jumla ya shilingi
bilioni 16.896 lakini hadi mwezi mach, 2014 ilikuwa imekusanya shilingi bilioni
3.25 ambayo ni sawa na asilimia 19 tu ya matarajio kwa mwaka. Aidha, fedha
zilizoidhinishwa kwa ajili ya Matumizi ya kawaida kwa idara na Taasisi zilizo
chini yake ni shilingi bilioni 12.1, lakini hadi Machi, zilikuwa zimetolewa
shilingi bilioni 3.36.
Mheshimiwa Spika, mwaka
wa fedha 2014/15 idara hii ya Utalii inatarajia kukusanya jumla ya shilingi
bilioni 16.91. Aidha, kwa maendeleo Iadara hii imetengewa jumla ya shilingi
bilioni 1.2. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza inakuwaje Idara inakusanya
shilingi bilioni 16.91 lakini uwekezaji unakuwa wa shilingi bilioni 1.2, aidha
uwekezaji huo hauna matokeo ya moja kwa moja na ukuaji wa utalii. Je ni kwa
vipi katika Dunia hii ya ushindani katika sekta ya utalii inaweza kuleta tija
na kuinua uchumi?
9.0
HITIMISHO
Kambi
Rasmi ya Upinzani, haitochoka kuikosoa Serikali kwa kuwa, kwa muda mrefu sasa
katika Wizara hii tumekua tunatoa mapendekezo ambayo yanabezwa. Na kwa kuwa ni
wajibu wetu kuisimamia ipasavyo Serikali ya CCM, tunazidi kusisitiza kuwa ili
sekta ya maliasili na utalii iendelee kuna haja nzima ya kubadilisha mfumo wa
usimamizi, uendeshaji na utekelezaji wa Wizara, ambao utatoa fursa kwa viongozi
waandamizi wa Wizara pamoja na watumishi kutimiza na kutekeleza majukumu yake
bila mashinikizo ya kisiasa.
Ni
rai yetu kuwa, Serikali itayafanyia kazi mapungufu yote ambayo tumekua
tukiyasema kwa muda mrefu sasa na kuisimamia ipasavyo sekta hii hili iwe
mhimili wa uchumi kwa taifa kwa kuongeza mapato pamoja na kutoa nafasi za ajira
kwa wananchi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
naomba kuwasilisha.
..................................................
Mch.
Peter S. Msigwa (MB)
Msemaji
Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Maliasili na Utalii.
13.05.2014
[1]
ripoti ya CAG 2012/2013 pg
148.
[2] Sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009
[4]
Haken, J. (2011), “Transnational Crime in the Developing World” in the Global
Financial Integrity Journal of February, 2011.
[5]
Ripoti ya CAG-ukaguzi wa ufanisi na ukaguzi maalum kwa kipindi kinachoishia
tarehe 31 Machi, 2014
[6] Wizara ya
maliasili na utalii- Taarifa ya
kamati kuhusu uboreshaji wa
tasnia ya uwindaji wa
kitalii Tanzania, JUNI, 2006
[7]
Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka
Mitano 2011 - 2016
No comments:
Post a Comment